ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, August 14, 2021

MBARONI KWA UHALIFU WA UTEKAJI, UBAKAJI NA KULAWITI WATOTO.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara Mark Njera.

 


Jeshi la polisi Mkoani Mtwara limemkamata Jabiri Bakari  kwa kosa la kujihusisha na uhalifu wa utekaji, ubakaji na kulawiti watoto wa kike wenye umri chini ya miaka kumi katika wilaya ya Mtwara.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara Mark Njera amewaambia waandishi wa habari leo kuwa mtuhumiwa huyo mwenye miaka 19 alikamatwa tarehe 12 August Mwaka huu  maeneo ya Mbae Manispaa ya Mtwara kufuatia msako wa jeshi la polisi uliofanywa.

Kamanda Njera amesema kabla ya kukamatwa na jeshi la polisi, mtuhumiwa aliwadanganya watoto wa kike watatu wenye umri wa miaka 8, 7 na mwingine mwenye miaka 9 ambao kwa nyakati tofauti aliwaiba sehemu mbalimbali kwa kuwalaghai kwa njia mbalimbali na kufanikiwa kuondoka nao kwenda kwenye maeneo na kuanzisha makazi ya mda akiwa na watoto hao.

Amesema mnamo tarehe 25 mwezi Juni mwaka huu mtuhumiwa alimlaghai mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 7 maeneo ya Mbae Mashariki wilaya ya Mtwara mtoto huyo akiwa anacheza na wenzake na baadae kuondoka naye ambapo mtoto huyo alipatikana baada ya siku tano akiwa amefanyiwa vitendo vya ukatili.

Mnamo tarehe 8 July maeneo ya Mbae, mtuhumiwa huyo alimchukua tena mtoto wa kike mwingine mwenye miaka 7 na kutoweka naye na kwenda kusikojulikana. Mtoto huyo alipatikana tarehe 24 Julya akiwa amefanyiwa vitendo vya kikatili.

Na mnamo tarehe 6 August mtuhumiwa huyo pia alimchukua mtoto mwenye umri wa miaka tisa ambaye pia alipelekwa kusikojulikana na mtuhumiwa huyohuyo na kufanyiwa vitendo vya ukatili. Kwa muhjibu wa kamanda Njera, mtoto huyo alipatikana tarehe 7 August kufuatia msako wa jeshi hilo.

Kamanda Njera ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mtwara kuhakikisha ulinzi na usalama kwa watoto na kutambua watu wanaojihusisha na vitendo vya ukatili kwa watoto na kutoa taarifa.

SIMBA YATAMBULISHA JEMBE LINGINE KUTOKA SENEGAL

 


RASMI kikosi cha Simba leo kimemtambulisha Pape Ousmane Sakho raia wa Senegal mwenye miaka 24.

Nyota huyo anakuwa ingizo jipya la nne ndani ya Simba baada ya jana Agosti 13 kumtambulisha Duncan Nyoni aliyeungana na Peter Banda pamoja na mzawa Yusuph Mhilu.

Nyota huyo anatajwa kuwa na uwezo mkubwa ndani ya uwanja pale anapopata nafasi akiwa ni kiungo mshambuliaji kinda aliyefanya vizuri kwenye ligi ya Senegal.  

Rekodi zinaonyesha kwamba alitupia mabao 8 na pasi 10 alitoa, pia ndiye mchezaji aliyeng'ara wakati timu ya Teungueth ikiitoa timu ya Raja Casablanca ya Morocco msimu ulioisha na kufuzu hatua ya makundi ya Caf Champions League.

Kwenye kambi nchini Morocco ambapo Simba wapo kwa sasa atajumuishwa na wengine ili kuendelea na maandalizi ya msimu ujao wa 2021/22.

Friday, August 13, 2021

YANGA YATAMBULISHA WAWILI - Djuma wa AS Vita NA Jesus Moloko

Shaban Djuma.

 

UONGOZI wa Yanga leo Agosti 13 umewatambulisha nyota wao wawili ambao watakuwa ndani ya kikoi hicho kwa msimu wa 2021/22.


Djuma ni beki ambaye anapewa nafasi ya kufanya vizuri msimu ujao kwa kuwa uzoefu wake unambeba na amecheza timu kubwa ya AS Vita ya Congo.

Ni Shaban Djuma ingizo jipya kutoka AS Vita pamoja na Jesus Moloko.

Jesus Moloko.


Moloko anakuwa mbadala wa Tuisila Kisinda ambaye anakwenda kujiunga na Klabu ya RS Berkane ya Morocco.

Moloko amebainisha kuwa hajawahi kufeli katika kazi ambazo huwa anafanya hivyo anaamini kwamba atafanya vizuri ndani ya kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi.

GARI LAKWAMISHA MBOWE KUPELEKWA MAHAKAMANI

 


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu, wameshindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kile kilichoelezwa ni changamoto ya usafiri wa gari la magereza.

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita yakiweno ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi, katika kesi ya Uhujumu Uchumi namba 63/2020.

Mashtaka mengine ni kula njama za kutenda makosa, kukutwa na silaha aina ya bastola, risasi pamoja na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kinyume cha sheria.

Mbali na Mbowe, ambaye ni mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo, wengine ni Halfan Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya.

SIMBA YATHIBITISHA CHAMA KUONDOKA.

 


Kaimu Afisa habari wa Simba SC Ezekiel Kamwaga amethibitisha kuwa Kiungo wa kimataifa wa Zambia Cloutous Chama (30) amejiunga na Club ya RS Berkane ya Morocco akisaini mkataba wa miaka mitatu.

Chama amesaini mkataba huo unaotajwa kuwa umeigharimu RS Berkane ada ya uhamisho ya Tsh Bilioni 1.5 kwenda Simba SC na kuongezewa mshahara mara nne ya aliokuwa analipwa Simba SC.

Chama ambae ameonekana kwenye mazoezi ya RS Berkane akiwa na Tuisila Kisinda wa Yanga, alijiunga na Simba SC mwaka 2018 akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia.

TANZANIA: UKATILI DHIDI YA WATOTO WAONGEZEKA, POLISI.

 

Ripoti ya jeshi la polisi nchini Tanzania inaonesha ongezeko la asilimia 25.95 la ukatili dhidi ya watoto. Katika mwaka 2020 visa 7388 viliripotiwa kote nchini tofauti na mwaka 2015 ambapo matukio 5,803 yaliripotiwa.

Watetezi wa masuala ya haki za watoto wametaja imani za kishirikina na utandawazi kuwa miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa matukio hayo. 

Ripoti hii ya Jeshi la Polisi inakuja katika kipindi hiki ambacho wazazi na walezi wengi wanatajwa kutokuwa karibu na watoto wao, wengi wakijihusisha na kusaka maisha bora ili kukidhi mahitaji ya msingi ya watoto huku wakiwapora haki ya kuwasikiliza.

Ripoti ya jeshi la polisi inataja miongoni mwa ukatili dhidi ya watoto ulioripotiwa kwa kiwango kikubwa kuwa dhuluma za kingono ambapo katika mwaka wa 2020 kuliripotiwa visa 7263 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo vilirikodiwa visa 5803, hii ikiwa ni sawa na visa 615 kwa mwezi jambo ambalo linatajwa kuwa linahatarisha mustakabali wa ustawi kwa watoto nchini humo.

Takwimu hizo zinarandana vilivyo na zile zilizotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania, katika ripoti yake ya hali ya haki nchini humo mapema mwaka huu, ambayo ilionesha kuongezeka kwa kiwango cha kutisha kwa matukio ya aina hiyo dhidi ya watoto.

Wanaharakati: Imani za kishirikina zachangia ukatili dhidi ya watoto Tanzania

Anna Henga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania, amesema ongezeko hilo ni kutokana na kukithiri kwa imani za kishirikina miongoni mwa wanajamii wanaotaka kusaka utajiri huku maeneo yaliyomulikwa zaidi ni upande wa Kanda ya Ziwa,

Aidha, ripoti zote mbili zimekwenda mbele zaidi na kuonesha kwa mwaka 2020 kulikuwa pia na wasiwasi juu ya ukatili juu ya watoto unaofanywa na watoto wenyewe, hasa matukio ya watoto kulawitiana katika shule za msingi na sekondari, matukio ambayo vyombo vya habari vilihusika kuyaripoti kwa asilimia 87.

Utandamazi na mmomonyoko wa maadili walaumiwa

Sophia Temba Afisa Program Jukwaa la Utu wa Mtoto, Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto. Amesema Mmomonyoko wa maadili na kutamalaki kwa utandawazi ndani ya jamii ni miongoni mwa sababu zinazoongeza kasi ya matukio hayo, lakini kuna haja ya kutengwa bajeti ya kutosha kutekeleza mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kunahitajika sasa.

Baadhi ya wazazi na walezi waliozungumza na JEMBE FM wanasema kwamba kuongezeka kwa rekodi ya matukio haya ni matokeo chanya, kwani ni kunatokana na kushamiri kwa elimu kwenye jamii ambapo hapo kabla yalitokea na watu waliyamaliza katika ngazi ya familia wakihofia sheria kuchukua mkondo wake, uhasama baina ya ndugu na visasi huku wakisahau afya za waathirika.

Thursday, August 12, 2021

HUU HAPA MCHONGO KWA WANAOTAMANI KUSOMA NJE YA NCHI.

 


Wengi hudhani ili mtu apate scholarships au nafasi ya kwenda kusoma nje ya nchi kwa mataifa kama Marekani, Ufaransa, Ubelgiji, Urusi, India na maeneo mengine ina kulazimu kuwa na fedha nyingi za mamilioni kwa mamilioni, lakini hivi unajua ukiwa na mtaji wa fedha kuanzia milioni mbili unaweza kwenda kusoma nchi yoyote unayotamani?

Ili kurahisisha upatikanaji na namna ya kujiunga na vyuo mbalimbali ulimwenguni Global link imeandaa orodha ya vyuo ambamo kuna fursa za kujiunga na masomo ya juu kwa wanafunzi kimataifa ndani ya nchi na nje ya nchi. Fuatilia mazungumzo haya kuzitambua fursa hizo na namna ya kuzifanyia kazi.

STEVE NYERERE ALA SHAVU UBALOZI WA UVIKO -19

 


Msanii maarufu nchini na Mwenyekiti wa Jukwaa la Mama Ongea na Mwanao, Steven Mengele 'Steve Nyerere' ameteuliwa kuwa Balozi wa harakati za kupambana na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (Uviko 19).

Steve ameteuliwa leo Alhamisi Agosti 12 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, jijini Dar es Salaam.

Pamoja na Steve, wengine walioteuliwa ni Mwanaharakati wa Kutetea Haki za Wanawake nchini, Joyce Kiria na Mbunge wa Viti Maalumu, Neema.

Tangu janga la Uviko 19 liibuke tena nchini mwaka huu, Steve ameonyesha kupambana na janga hilo huku akihamasisha Watanzania kupata chanjo ili kujikinga dhidi ya ugonjwa huo hatari duniani.

PETER BANDA APEWA JEZI YA MIQUISSONE

 


Mchezaji mpya wa klabu ya Simba Peter Banda amekabidhiwa jezi namba 11 ambayo hapo awali ilikuwa ikitumiwa na Luis Miquissone ambaye anahusishwa kujiunga na miamba ya soka barani Afrika klabu ya Al Ahly ya huko Misri. 

Banda alijiunga na wekundu wa Msimbazi mwezi Agosti 3 mwaka huu akitokea Nyasa Big Bullets ya nchini Malawi kwa mkataba wa miaka mitatu.

 Mabingwa hao wa Tanzania hivi sasa wapo nchini Morocco ambako wameweka kambi yao kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya ujao.

MADIWANI HALMASHAURI YA WILAYA YA BABATI WALIA UBAKAJI, ULAWITI.



Na John Walter-Babati.

Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Babati mkoani Manyara, wamekemea vikali vitendo vya matukio ya ubakaji na ulawiti vinavyotokea  katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na kuitaka jamii kufichua watu wanaojihusisha na uovu huo.

Hayo yamejiri katika baraza la madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Babati, ambapo Diwani wa kata ya Dareda  Eluthery Joseph Burra amesema kuwa vitendo  hivyo vinapaswa kukemewa vikali kwani kwa hivi sasa vitendo hivyo vimekithiri katika kata yake.

Burra amesema katika kata yake ya Dareda na maeneo jirani sio watoto pekee yao hata wanaume  nao wanakumbwa na vitendo hivyo.

“Kwa Dareda sasaivi tuna kesi ambazo aidha zimeripotiwa polisi au ambazo zipo mafichoni,kuna kesi zaidi ya tatu ndani ya muda mfupi”alisema Burra

Amewataka maafisa ustawi wa jamii kufanya mikutano na wananchi mara kwa mara kutoa elimu kwani wamechoka kusikia malalamiko ya wananchi kuhusu ubakaji na ulawiti.

Diwani wa viti maalum Mariamu Kwimba  amesema Ukatili wa kijinsia umezidi kushika kasi haswa katika kata za Dareda,Dabil,Magugu na Galapo na linafanywa na wanaume ambapo wahanga ni watoto na wanawake huku watoto wa kiume wakilawitiwa.

Amesema wajibu wao kama viongozi  ni kutoa elimu katika maeneo yao kupitia vikao na mikutano ya hadhara ili kukomesha ukatili huo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Babati John Noya amesema mikutano ya hadhara itafanyika ka kushirikisha maafisa ustawi,viongozi wengine na  polisi kata wa eneo husika.

Amesema jamii ielimishwe juu ya athari ya vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia pamoja na kuwatumia wazee wa kimila katika kutokomeza vitendo hivyo.

RAIS WA MADAGASCAR ALIVUNJA BARAZA LA MAWAZIRI

 

 Rais wa Madagascar Andry Rajoelina amelivunjilia mbali baraza lake la mawaziri.

Ofisi yake haikutoa sababu, lakini Jumapili Bw Rajoelina alisema kutakuwa na hali ya kushindwa ndani ya serikali - "kama katika timu ya mpira wa miguu" - mabadiliko yangehitajika.

Kufutwa kwa baraza hilo kumekuja baada ya ripoti za njama iliyofeli ya kumuua rais ambaye ni kiongozi wa zamani wa mapinduzi huko Madagascar.

Zaidi ya washukiwa 20 - wakiwemo 12 kutoka kwenye jeshi - wamekamatwa. Bwana Rajoelina alikua rais wa kisiwa hicho miaka miwili iliyopita - baada ya mzozo wa kisheria uliogubika uchaguzi huo.

Tuesday, August 10, 2021

UTEUZI WA WANASHERIA WA KUSIKILIZA KESI YA DHULUMA ZA KINGONO DHIDI YA MSANII R.KELLY WAANZA.

 

Msanii wa R&B R. Kelly amefika mahakamani mjini New York,huku uteuzi wa wanasheria katika kesi ya dhulma za kingono dhidi yake ukianza.

Inajiri zaidi ya miaka miwili baada ya msanii huyo kushtakiwa kwa unyanyasaji wa wanawake na wasichana wadogo kwa karibu miongo miwili.

Mwimbaji huyo aliyeshinda Tuzo ya Grammy anakabiliwa na mashtaka ya unyanasaji wa kingono dhidi ya watoto, ujambazi na rushwa. Amekanusha mashtaka

Wanasheria wanaotarajiwa kuongoza kesi hiyo wanahojiwa ikiwa wanaweza kuwa na mawazo huru katika kesi hiyo.

Baada ya majaji kuteuliwa, kesi inatarajiwa kuanza Agost18 na huenda ikaendelea kwa wiki kadhaa.Msanii huyo mwenye umri wa miaka 54 akipatikana na hatia huenda akafungwa jela kwa miongo kadhaa.

Kesi dhidi yake pia imewasilishwa katika mahakama ya Illinois na Minnesota.

Alipoulizwa jinsi anavyojihisi,wakili wa Kelly,Deveraux Cannick aliliambia shirika la Habari la AFP: "Ni sawa na Jumatatu nyingine."

Kelly, mmoja wa wasanii nyota wa miondoko ya R&B miaka ya1990, amekuwa akizuiliwa tangu Julai mwaka 2019.

Kesi ya New Yorki inamtuhumu mwimbaji huyo–ambaye jina lake halisi ni Robert Kelly –kwa kuongoza kundi la mameneja , walinzi wa kibinafsi na wengine ambao waliwaanda wanawake na wasichana kwa ajili ya kufanya ngono.

Waendesha mashtaka wanasema wahasiriwa waliteuliwa katika matamasha na maeneo mengine.

DEREVA ALIYEUWA WANAFUNZI WAWILI AAGIZWA KUJISALIMISHA.

 


Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limemtaka dereva aliyesababisha ajali iliyoua wanafunzi wawili katika barabara ya Bagamoyo, maeneo ya Afrikana stendi ya daladala, Wilaya ya Kinondoni kujisalimisha haraka iwezekanavyo kituo chochote cha Polisi kilichopo karibu naye.


Ajali hiyo iliyotokea leo Agosti 9, 2021, majira ya saa 11:15 alfajiri, ambapo gari yenye namba za usajili T 274 CBX liliwagonga wanfunzi waliofahamika kwa majina ya Collins Obed Ngowi (15) Mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya Sekondari Makongo na Salvina Odoro Otieno Mwanafunzi wa darasa saba Shule ya Msingi Mount Sery wote wawili walifariki dunia, huku mwanafunzi Ashura wa kidato cha tano shule ya Sekondari Al-haramain akipata majeraha sehemu za mwili na alikimbizwa hospitalini.


Jeshi la Polisi limeeleza kuwa dereva huyo alikimbia mara baada ya tukio kutokea hivyo kumtaka ajisalimishe kwani hana uwezo wa kujificha zaidi ya muda wa saa 48.


Hata hivyo chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa gari hilo lililohusika katika ajali.

SIMBA KUWEKA KAMBI MOROCCO

 


 Klabu ya Simba itakwea pipa kuelekea nchini Morocco kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya 2021/22
 

"Morocco ndio nchi ambayo mabingwa wa nchi tutaweka kambi kujiandaa na msimu mpya wa 2021/22" Simba SC

Simba na Yanga zote zitakuwa ndani ya Morocco kujiandaa na msimu mpya wa mashindano ya klabu bingwa na kuliwinda kombe la Ligi Kuu, Simba akitaka kuweka historia ya kunyakuwa kombe hilo mara 5 mfululizo na Yanga wenye hasira ya kulikosa kombe hilo mara 4 mfululizo.

KISA CHA KWANZA CHA KIRUSI CHA MARBURG CHAGUNDULIKA GUINEA.

 


Guinea imethibitisha kisa cha ugonjwa wa Marburg, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kirusi hicho hatari kinachohusiana na Ebola kutokea Afrika Magharibi. 
 
Kama tu ilivyo kwa ugonjwa wa COVID-19, kirusi hicho kinatoka kwa mnyama na kuingia kwa binaadamu. Shirika la Afya Ulimwenguni - WHO limesema kirusi hicho kinabebwa na popo na kina kiwango cha vifo cha hadi asilimia 88, kilipatikana kwenye sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa mgonjwa mmoja aliyefariki Agosti 2 katika eneo la kusini mwa Guinea la Gueckedou. 
 
Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika Matshidiso Moeti amesema uwezekano wa kirusi cha Marburg kusambaa hadi maeneo ya mbali una maana wanahitaji kukizuia mapema. 
 
Ugunduzi huo unakuja miezi miwili tu baada ya WHO kutangaza kumalizika kwa mripuko wa pili wa Ebola nchini Guinea, ambao ulianza mwaka jana na kuwauwa watu 12.

Wednesday, August 4, 2021

AHUKUMIWA KIFUNGO NA FAINI BAADA YA KUKUTWA NA SILAHA NZITO AINA YA KIFARU NYUMBANI KWAKE.

 

 Mstaafu mmoja nchini Ujerumani ametiwa hatiani kwa kosa la kumiliki silaha baada ya kubainika kuwa na silaha kubwa binafsi kikiwemo kifaru.

Mtuhumiwa huyo ,84, amehukumiwa kifungo cha miezi 14 na ameamriwa kulipa faini ya pauni 213,469.

Maafisa walibaini kifaru na vifaa vingine vya kijeshi vya enzi ya vita vya pili vya dunia kwenye makazi ya mzee huyo katika mji wa Heikendorf mwaka 2015

Jeshi lilisaidia kuondoa vifaa hivyo.

Jumatatu, mahakama iliamuru kuwa mtuhumiwa huyo ambaye jina lake halikutajwa kwasababu ya sheria ya faragha ya Ujerumani, lazima auze au akigawe kifaru hicho na silaha ya kupambana na mashambulizi ya anga iwekwe kwenye makumbusho

Kwa mujibu wa wakili wa mtuhumiwa, idara ya makumbusho ya Marekaniina nia ya kununua kifaru.

Wanahistoria wengi wa Marekani wanasema kilikuwa kifaa bora zaidi kilichotumiwa na Ujerumani wakati wa vita vya pili vya dunia.

Mwanasheria amesema kuwa maafisa wanaokusanya vifaa vya kijeshi wa Ujerumani walitaka silaha nyingine kama vile bunduki na bastola, vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti.

Mamlaka za mji huo zilivamia makazi yake mwaka 2015 baada yakupata taarifa kuhusu vitu vinavyomilikiwa na mstaafu huyo, taarifa hiyo ilitolewa na wafanyakazi wenzao wa Berlin, ambao awali walifanya upekuzinyumbani kwake wakitafuta mchoro ulioibiwa baada ya enzi za Nazi.

Wanajeshi kama 20 hivi walitumia saa tisa kukiondoa kifaru hicho kutoka kwenye makazi ya mstaafu huyo

Vyombo vya habari vya huko viliripoti kwamba mtu huyo alikuwa ameonekana wakati mmoja wa baridi akitumia kifaru kama jembe la kuondolea barafu.

CHANJO ELFU TISINI ZATOLEWA MKOA KWA LENGO LA KUWAKINGA WANANCHI.

 


Na  Maridhia Ngemela

Mganga mfawizi wa hospitali ya rufaa Mkoa sekou toure Bahati Peter Msaki amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata chanjo na kuachana na maneno ambayo yanasemwa kwenye mtandao ya kijamii

Msaki ameeleza hayo wakati wa zoezi la uzinduzi wa chanjo ya kinga ya ugonjwa wa uviko 19 iliyozinduliwa leo mkoani hapa amesema zaidi ya watoa huduma 200wamejiandikisha kw lengo la kupata kinga huyo kwani ni kundi moja wapi ambalo limepewa kipaumbele kutokana na kazii inayowakutanisha na watu mbalimbali.
 
Bahati ameeleza kuwa kinga ni bora kuliko kusubiri kuungua ndio ukapate matibabu hivyo hakuna sababu ya kuendelea kudanganyana juu ya chanjo kuwa ina madhara mwilini.

Aidha amewataka wananchi kuendelea kujikinga kwa kuchukua hatadhali kwa kivaa barakoa,  kunawa mikono na kuepuka misongamano isiyokuwa ya lazima.

Kisali Simba ni mmoja kati ya waandishi wa habari aliyejitokeza kupata chanjo  ameeleza kuwa hakuna changamoto yeyote ambayo ameipata baada ya kupata kuchanjo  hiyo ya Uviko 19 .

"Nimefurahi kupata chanjo hii kwani kuanzia sasa niko imara kabsa sina hofu juu ya maambukizi ya ugonjwa huu" alisema kisali.


MABONDIA CLASS NA NASSIBU WAPIGWA PINI NA SUPER D BOXING PROMOTION

 


NA MWANDISHI WETU

PROMOTA wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' amewapiga pini mabondia Ibrahimu class na Nasibu Ramadhani kwa kuingia nao Mkataba wa kuzipiga Septemba 24 jijini Dar esa Salaam 

Akizungumza baada ya kuingia mkataba na mabondia hao uliotiwa saini mbele ya rais wa kamisheni ya ngumi za kulipwa TPBRC Agapeter Basili zilizopo keko Dar .

Super D amesema kuwa anapenda kufungua milango kwa wafadhili mbalimbali kujitokeza kudhamili mpambano uhu kwani mpambano ulikuwa unasubiliwa kwa hamu kubwa sana na mashabiki wa mchezo wa masumbwi kwa kuwa hii ni dabi ambayo ina kila kitu katika mchezo wa masumbwi mana mabondia wana uwelewa wa mchezo wa ngumi pamoja na kujulikana kimataifa zaidi.

aliongeza kwa kusema kuwa mchezo wa masumbwi sio uhadui kwani michezo ujenga urafiki pamoja na kujenga udugu, mabondia hawa ambao wamekuwa wakifanya kazi za uchambuzi wa mchezo wa ngumi katika TV. 

ata hivyo kwa sasa wanaingia katika vita ya kutafuta heshima katika mchezo wa ngumi ambao wanaupambania kila kukicha.

mbali na mabondia hao mabondia wengine waliokwisha saini mkataba kupitia kampuni tanzu ya kizalendo ya Super D Boxing Promotion ni Issa Nampepeche ambaye atavaana na Juma Choki katika mpambano wa kugombania ubingwa wa taifa.

MZUMBE WAJA NA MKAKATI KUWATAMBUA MASHUHURI WALIOHITIMU CHUONI KWAO.



 "Kwa muda mrefu tumekuwa na wahitimu wengi wenye sifa mbalimbali viongozi maarufu ndani na nje ya nchi, wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa waliofanya na wanaofanya makubwa kwa taifa hili, hii sasa itakuwa forum itakayo waunganisha kuweza kupata mrejesho toka kwenye soko "

Tuesday, August 3, 2021

OLIMPIKI TOKYO: MWANARIADHA MJERUMANI MWENYE ASILI YA TANZANIA ASHINDA DHAHABU



Raia wa Ujerumani mwenye asili ya Tanzania Malaika Mihambo, amelishindia taifa lake medali ya dhahabu katika mashindano ya michezo ya Olimpiki ya long Jump.

Mwanaridha huyo aliruka urefu wa mita saba ili kuchukua ushindi.

Awali Mihambo alikabiliwa na changamoto kadhaa kabla ya mashindano hayo lakini hatimaye alifanikiwa kuonesha umahiri wake.

Katika fainali ya mchezo huo iliofanyika hii leo Jumanne, bi Malaika hakuonesha ishara zozote za kuibuka mshindi.

Urefu wa mita saba alioruka katika jaribio la sita ulimwezesha kuipatia Ujerumani nishani yake ya kwanza ya dhahabu katika mchezo huo tangu Heike Drechsler aliposhinda mwaka 2000.

Nishani ya fedha ilimwendea mshindi mara nne wa mashindano ya dunia na Olimpiki yaliofanyika mjini London Brittney Reese wa Marekani baada ya kuruka mita 6.97 huku Ese Brume wa Nigeria akijinyakulia medali ya shaba na kuiongezea Afrika idadi ya medali katika michezo hiyo.

MTAKA: HALI SI NZURI DODOMA, CHUKUENI TAHADHARI DHIDI YA COVID -19

 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amewataka wakazi wa Dodoma kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona kwa sababu hali si nzuri mkoani humo.

Ameyasema hayo leo Jumanne Agosti 3, 2021 wakati akizungumza na askari wa usalama wa barabarani na viongozi wa masoko wa mkoa wa Dodoma.

Amewataka askari hao, viongozi wa masoko na wafanyabiashara kuhakikisha wanachukua hatua za kujikinga katika maeneo yao kwa kuvaa barakoa na kunawa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.

Pia amewataka askari wa usalama wa barabarani kuhakikisha watu wote wanakaa kwenye viti (level seat) kwenye daladala na bajaji na kwenye bodaboda kuhakikisha hawabebi abiria zaidi ya mmoja.

Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma, Boniface Mbao amesema watakapotoka katika kikao hicho wataenda kutekeleza maagizo hayo kwa kutoa elimu na ikibidi kwa ukali, ili kuhakikisha abiria wanakaa katika viti kwenye mabasi ya abiria.

Amesema hakuna gari litakalopita kwenye mkoa huu likiwa limejaza zaidi ya abiria waliokaa kwenye viti.

BABU WA LOLIONDO KUZIKWA KESHO SAMUNGE.

 


Mwili wa Mchungaji Ambikile Mwasapile maarufu Babu wa Loliondo unatarajiwa kuzikwa kesho katika Kijiji cha Samunge, wilaya ya Ngorongoro mkoa wa Arusha sehemu ambayo alikuwa akitoa tiba ya mitidawa maarufu kama kikombe cha Babu.

Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mwangwala amethibitisha taarifa hiyo akiliambia Gazeti la Mwananchi, familia imekubaliana mazishi ya Mchungaji Ambikile kuwa Samunge.

Babu wa Loliondo alifariki Julai 30 akiwa na umri wa miaka 86, aliugua nimonia kali ambayo ilimsababisha kupata changamoto ya upumuaji na kupeleka kifo chake.

WATATU WASIMAMISHWA KAZI, KAMATI YAUNDWA KUCHUNGUZA MOTO MSAMVU

 

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewasimamisha kazi wahandisi watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupisha uchunguzi baada ya Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme Msamvu kuungua moto na kusababisha hasara ya takribani shilingi Bilioni 2.

Aidha amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kheri Mahimbali kuunda kamati ya kuchunguza na kubaini chanzo halisi cha Moto huo na hasara iliyopatika ndani ya siku tano kuanzia leo (Agosti 3, 2021).


Katika ziara hiyo, Dkt. Kalemani aliambatana na Naibu  Katibu Mkuu wizara hiyo, Kheri Mahimbali, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt.Tito Mwinuka pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Wizara na TANESCO.

Sambamba na hilo aliiagiza Kampuni ya inayotekeleza Mradi wa Reli ya Umeme (SGR) kumchungumza mhandisi wake anayedaiwa kusababisha hitilafu hiyo kwa kukata waya wa umeme na kari la kuchimbua barabara wakati akitekeleza majukumu yake na kuchukuliwa hatua pindi itakapobainika.

Dkt. Kalemani alisema hayo, Mkoani Morogoro, Agosti 03, 2021 alipofanya ziara ya kukagua kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Msamvu kilichoungua moto Jana baada ya kutokea hitilafu na kusababisha wananchi kukosa Umeme.


Dkt. Kalemani alifafanua kuwa wahandisi hao wa TANESCO, wamesimamishwa kwa kushindwa kubaini hitilafu iliyotokea katika mifumo ya kuendeshea mitambo kituoni hapo, na kusababisha harasa kubwa kwa taifa baada ya kituo hicho kuungua moto.

“Wahandisi waliokuwa zamu siku hiyo wasimamishwe kazi kuanzia Sasa kwa kushindwa kubaini mapema hitilafu iliyotokea katika mifumo na kusababisha hasara kubwa kwa Taifa, wakati walikuwepo kazini,pia matukio ya moto yamekuwa mengi lazima tuchunguze kufahamu kama kuna yeyote anahujumu miundombinu ya umeme”, alisema Dkt. Kalemani

Hata hivyo aliitaka TANESCO kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha umeme unarejea katika maeneo yote ndani ya saa 24 kuanzia leo,vilevile waongeze wataalam kutoka vituo vingine ili kuongeza nguvu kazi na kukamilisha kazi hiyo haraka.

Aidha Dkt. Kalemani aliwataka TANESCO kuharakisha manunuzi ya vifaa na miundombinu yoyote iliyoungua kwa kutumia mfumo wa dharura usioathiri taratibu za manunuzi ili kurejesha kituo hicho katika hali yake ya kawaida ndani ya kipindi kifupi.   

Vilevile aliwataka TANESCO kuhakikisha kuwa vituo vyote vya vilivyojengwa zamani vya kupoza na kusambaza umeme vinakuwa na mifumo maalum ya kubaini hitalafu ikitokea na namna ya kuidhibiti kabla ya madhara makubwa kutokea.

Pamoja na mambo mengine aliwaagiza kuweka alama katika maeneo yote ambayo miundombinu mikubwa ya umeme imepita chini ya ardhi hasa nyaya ili kutoa tahadhari kwa watakaokuwa wakifanya kazi au kupita maeneo hayo.

Pamoja na mambo mengine aliwataka wananchi ambao bado huduma ya umeme haijarejea kuendelea kuvuta subira wakati wataalam wakiendelea kufanya kazi zao, na kwamba tayari baadhi ya vifaa kutoka mkoani Singida viko njiani kuwasili eneo hilo ili kuhakikisha huduma ya umeme inarejea maeneo yote ndani ya muda mfupi.

Monday, August 2, 2021

WATAALAMU WA AFYA WAELEZA SABABU ZA WATOTO KUTOSHAMBULIWA KWA KIASI KIKUBWA NA UVIKO19

 


Wataalamu wa tiba za binadamu wamesema kuwa kufa na kuzaliwa kwa cell mara kwa mara kwa watoto ndio sababu inayopelekea watoto kutoshambuliwa na Virusi vya UVIKO 19 vinavyosababisha ugonjwa wa homa ya Mapafu.

Hayo yamebainishwa jijini Arusha na Mganga wa Hospitali ya Maunti Meru Dkt Sunday Wanyika wakati akitoa mada Kuhusu mlipuko wa Virusi vya UVIKO 19 kwenye mkutano wa wadau Kuhusu masuala ya msaada wa kisheria na upatikanaji haki kwa wananchi katika kipindi cha matumizi ya lugha ya kiswahili.

Mganga huyo ameeleza kuwa hali hiyo ndio imekuwa ikisababisha watoto kutoshambuliwa na Virusi hivyo maana vinapotaka kushambulia vinakuta cell zimekufa na kuanza kuzalishwa nyingine hivyo wao wakijikuta wanakuwa sugu na kuwa na uwezo wa kupokea na kuambukiza na kuathiri watu wazima.

"Zaidi ya aslimia 50 ya wagonjwa hawaonyeshi dalili na wanaongoza kwa kusambaza Virusi vya ugonjw huo hivyo wakati wa kujikinga usiwahofia ambao wameshaugua na kuonyesha dalili tu, muwe makini pia na kundi hilo, mpaka sasa watubmilioni 199 wameshapimwa na kukutw na maambukizi huku watu milioni 4 wakifariki na ugonjwa huo ulimwenguni,"amesema.

Ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanakuwa makini kwa kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo kwa kuchukua tahadhari zote ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanachoma chanjo ambalo ni lazima kutokana na hali halisi ilivyo sasa, kutokwenda kwenye mikusanyiko isiyo ya lazima na kutulia majumbani, kuvaa barakoa ambazo zinakinga, kutumia vitakasa mikono na kunawa maji tiririka.

"Simu za mkononi zinaongoz kwa mambukizi kutokana n kushikwa mara kwa Mara nawasii wannachi muwe nazo makini kw kutumia vitakasa mikono mara kwa Mara,"amesisitiza.

Akizungumzia Virusi vya UVIKO 19 awamu ya sasa amesema viko tofauti sana na vile vya awamu ya kwanza  vinasambaa kwa haraka zaidi na ni rahisi kusababisha kifo huku akitaja dalili namba moja kuwa ni kifua kuuma na kuwa kizito wakati awali ilikuwa ni kupta mfua, kukohoa na kushindwa kunusa.

Akifungua mkutano huo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Godfrey Mizengo Pinda amewataka mawakala wa sheria kwenye maeneo yao wapambanie afya za watu wao suala la chanjo ni muhimu Sana kwa maisha ya watanzania hivyo amewaasha washiriki wote wajitokeze kuchoma chanjo katika zoezi la uzinduzi wa chanjo litakalofanyika kesho jijini Arusha ili kujikinga.

SERIKALI YAIAGIZA TIPER KUTOA TAARIFA ZA UENDESHAJI KAMPUNI KWA WAKATI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali akizungumza na Waandishi wa Habari wakati alipotembelea Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) iliyopo jijini Dar-esalaam  tarehe 31 Julai, 2021 kujionea hali halisi ya uendeshaji wa kampuni hiyo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) Michael Mjinja wakati alipotembelea Kampuni hiyo iliyopo jijini Dar-esalaam tarehe 31 Julai, 2021 kujionea hali halisi ya uendeshaji wa kampuni hiyo.


 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) Michael Mjinja akitoa maelezo kuhusu utendaji wa Kampuni ya TIPER kufuatia ziara ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali kwenye kampuni hiyo tarehe 31 Julai, 2021.

 

Na Dorina G. Makaya – Dar-es-salaam


Serikali imeiagiza Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) kuhakikisha inatoa taarifa za uendeshaji wa kampuni hiyo kwa wakati, ili kuepusha changamoto ambazo zinaweza kujitokeza baadaye kutokana na kutokutoa taarifa kwa wakati.

Agizo hilo limetolewa jijini Dar-esalaam tarehe 31 Julai, 2021 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Kheri Mahimbali wakati wa ziara yake kwenye kampuni hiyo iliyolenga kujionea hali halisi ya uendeshaji wa kampuni ya TIPER.

Katika ziara yake, Naibu Katibu Mkuu Mahimbali, ametembelea kwenye maeneo mbalimbali ya kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na matenki ya kuhifadhia mafuta jambo ambalo ameonyesha kuridhishwa na utendaji kazi wa kampuni hiyo.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER) Michael Mjinja, ameishukuru Serikali kwa kufika katika eneo hilo ambapo wameweza kukubaliana masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupeana taarifa kwa wakati.

Amesema, licha ya mafanikio waliyonayo, bado kuna changamoto zinazowakabili huku kubwa ikiwa kuharibika kwa vifaa vya kusukuma mafuta pindi wanapoyatoa kwenye meli, vifaa ambavyo havipatikani nchini hadi viagizwe nje ya nchi.

Kufuatia hali hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali amesema, endapo taarifa hizo zitatolewa mapema, itakuwa mwarobaini wa changamoto hizo.

Ziara hiyo ni mwanzo wa ziara nyingine katika taasisi zote zenye ubia na Serikali katika Sekta ndogo ya Mafuta hapa nchini kwa lengo la kuboresha ufanisi na utendaji.

Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Kheri Mahimbali, aliambatana na baadhi ya viongozi na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Nchini Tanzania (EWURA) na Kampuni ya Serikali ya Uagizaji na Usambazaji wa Mafuta nchini (TANOIL).


Friday, July 30, 2021

TAARIFA YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CCM MAALUM ILIYOKETI JULAI 29,2021,Ikulu Jijini Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiongoza Kikao Maalum cha Kamati Kuu  ya Chama cha Mapinduzi CCM kilichokutana leo Julai 29,2021 Ikulu jijini Dar es salaam.



Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiongoza Kikao Maalum cha Kamati Kuu  ya Chama cha Mapinduzi CCM kilichokutana  Julai 29,2021 Ikulu jijini Dar es salaam.



 Wajumbe wa Kamati kuu wakifuatilia Kikao  Maalum cha Kamati Kuu  ya Chama cha Mapinduzi CCM kilichokutana  Julai 29,2021 Ikulu jijini Dar es salaam. (PICHA NA FAHADI SIRAJI WA CCM)

 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imekutana katika kikao maalumu Alhamisi 29 Julai, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan.


Pamoja na mambo mengine Kamati Kuu imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuruhusu chanjo ya virusi vya ugonjwa wa korona (UVIKO 19) Kutolewa nchini na yeye kuwa mfano wa  kukubali kuchanjwa ikiwa ni udhibitisho wa usalama wa chanjo hiyo. 

Uamuzi wake umetajwa kuwa ni kielelezo cha upendo na uzalendo mkubwa alionao katika kujali afya za watanzania na ni hatua nzuri ya Tanzania kuungana na dunia katika kukabiliana dhidi ya UVIKO-19, pia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 - 2025 Ibara ya 83(o) na 84.

Kamati Kuu imeelekeza kuanza kuchukuliwa hatua kwa wale wote wanaokiuka mienendo, taratibu na kanuni za maadili na uongozi kwa mujibu wa katiba ya Chama Cha Mapinduzi.

Aidha Kamati Kuu imefanya uteuzi wa makatibu wakuu wa Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi ambapo Ndugu Gilbert Kalima Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania na Dkt. Philis Nyimbi Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania  (UWT).


Shaka Hamdu Shaka
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
Itikadi na Uenezi
29 Julai, 2021.