ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, February 20, 2019

SAFARI YA MWISHO YA MWANAHABARI MARIA PHILBERT



HATIMAYE mwili wa aliyekuwa mwandishi wa habari mwakilishi wa Mwanza wa Radio Kwizera yenye makao yake makuu wilayani Ngara mkoani Kagera marehemu Maria Philbert, umezikwa leo katika makaburi ya Nyanshana Mabatini jijini Mwanza huku mamia ya waombolezaji wakijitokeza kuhudhuria safari hiyo ya mwisho kwa mwandishi huo.

Waombolezaji wakiwemo baadhi ya wafanyakazi wa Radio Kwizera na wanahabari wa mkoa wa Mwanza na maeneo jirani wamefurika kuanzia nyumbani kwao marehemu eneo la Mabatini wakishiriki ibada ya kuaga mwili wa mpendwa wao Maria Philbert (34) aliyefariki Februari 16, 2019.

Afisa uhusiano Radio Kwizera Padre Fredrick Meela amesema watumishi wenake wamempoteza mfanyakazi hodari mwenye kusema kweli na kwamba alihamamishiwa kituo cha Mwanza kwaajili ya kujiendeleza kitaaluma Chuo cha SAUT  jijini hapa.

Amesema marehemu alikuwa akijihusisha na uboreshaji huduma za kijamii hada utumiaji wa lishe bora kwa watoto na masuala ya jinsia, usalama na maendeleo hadi kujipatia tuzo huku akihusika na ushauri kwa wafanyakazi wenzake kujiendeleza kitaaluma.

Aidha ameongeza kuwa marehemu amefanya kazi kwa muda wa miaka sita na baada ya kuhamishiwa jijini Mwanza aliugua na kutoa taarifa kisha kushughulikia matibabu muda wa wiki mbili zilizopita akisumbuliwa na upele mdogo kichwani, lakini baada ya kufanyiwa upasuaji baadaye alizidiwa na kufariki.

Akisoma historia ya marehemu Maria, mmoja wa wanahabari wa mkoa wa Mwanza Fredrick Katulanda amesema marehemu alizaliwa 9 dec 1984 na kuanza elimu ya msingi katika Shule ya msingi Pamba mkoani Mwanza  pia kujiunga na elimu ya Sekondari mwaka 2005 mpaka 2008

Alianza masomo ya uandishi wa habari Chuo Cha Sengerema mkoani Mwanza na kufanya kazi kituo cha Redio Kwaneema Fm Mwanza hadi mwaka 2012 ambapo aliajiriwa na Redio Kwizera Ngara hadi mauti yalipomkuta, marehemu ameacha motto mmoja wa kiume.

‘BWANA AMETOA NA BWANA AMETWAA JINA LAKE LIHIMIDIWE’