Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema ambaye alikuwa mgeni rasmi wa uzinduzi wa Michuano ya Shule za Sekondari Nchini (UMESETA), akipiga dana dana wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam leo.
Wanafunzi wa shule za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema (kushoto), akikabidhi vifaa vya michezo kwa Shule ya Sekondari ya Azania vilivyotolewa na Kampuni ya Coca Cola. Kulia Ofisa kutoka kampuni ya Coca Cola wadhamini wakubwa wa michuano hiyo kwa mwaka 2016.
DC Mjema akisalimiana na mwamuzi wa mchezo kati ya timu ya Sekondari ya Tirav ya Yombo na Makongo uliopigwa katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam. Makongo ilishinda mabao 2-1.
DC Mjema akiwasalimia wachezaji wa timu ya Tirav.
DC Mjema akisalimiana na wachezaji wa timu ya Makongo Sekondari.
Mkuu wa Wilaya Sophia Mjema (kulia), akitoa nasaha zake kwa wachezaji hao kabla ya kuanza kucheza.
DC Mjema hapa akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa timu ya sekondari ya Tirav na viongozi mbalimbali.
DC Mjema hapa akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa timu ya sekondari ya Makongo na viongozi mbalimbali.
Hapa akiwa katika picha ya pamoja na waamuzi wa mchezo huo na viongozi mbalimbali.
Hapa mtanange ukiendelea.
Golikipa wa timu ya Tirav, Abdul Badi akiokoa moja ya hatari katika lango lake.
Wachezaji wa timu ya Makongo wakishangilia baada ya kupata bao lao la kwanza.
MKUU wa Wilaya ya Temeke Sophia Mjema amezindua michuano ya Shule za Sekondari Nchini (UMESETA) katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam huku akisisitiza kuwa yataendelea kuwaibua wachezaji wengi chipukizi.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mjema aliishukuru kampuni ya Cocacola kwa kudhamini mashindano hayo huku akiyaomba makampuni na wadau wengine kujitokeza kudhamini michezo mbalimbali.
Mashindano hayo yatashirikisha timu zaidi ya 40 katika mchezo wa mpira wa kikapu kwa vijana wa Shule za Sekondari kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini huku ikishirikiana na waandaaji wa michuano ya michezo ya Shule za Sekondari UMISETA katika kuhakikisha wanapata wachezaji wenye elimu kutoka mikoa yote hapa nchini.
Akizungumzia mashindano hayo Meneja wa Biashara wa Coca Cola Maurice Njowoka alisema wameamua kuongeza mchezo ili kupanua wigo wa mashindano hayo hapa nchini.
Aidha alisema lengo la kuungana na waandaaji hao, badala ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) pekee ni kutaka kupata wachezaji sahihi, kutoka mikoa yote, na ambao wako katika mashule ya Sekondari.
"Hii itatusaidia kupata wachezaji sahihi wenye elimu na ambao kweli wanasoma shule za sekondari,"alisema Njowoka.
Alisema tofauti na mwaka jana, tuliwatumia TFF pekee jambo ambalo tulipata wachezaji lakini katika mazingira magumu zaidi.
Alisema michuano ya mwaka huu wanaimani watapata wachezaji kiurahisi kwa sababu UMISETA ina rekodi ya wanafuzni wanaosoma katika shule za sekondari.
Njowoka alisema kwa kuanzia jijini Dar es Salaam, wametoa jezi na vifaa kwa shule za Sekondari zilizohudhuria katika mashindano hayo.
Alisema baada ya Dar es Salaam, wanaelekea Mwanza, Mbeya, Arusha na Moshi kwa ajili ya kuzindua rasmi michezo hiyo ambayo shule zinaanza kufanya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa.
Alisema katika udhamini wao watatumia kinywaji cha Coca Cola kwa upande wa soka, wakati Kikapu watatumia Sprite, lengo ni kufanikisha michuano hiyo safari hii kutokana na kuongeza idadi ya mchezo.