Mtendaji mkuu wa Dawasa Injnia Cyprian Luhemeja akizungumza katika ziara hiyo juu ya mikakati ambayo wamejiwekea katika kukabiliana na chanagamoto ya maji hasa katika kipindi cha miezi ya ukame.
Na Victor Masangu,Pwani
Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Dar es Salaam (DAWASA) katika kukabiliana na changamoto za ukosefu wa maji imeaanza kuweka mipango madhubuti na kuchukua hatua stahiki wakati wa ukame unapotokea kwa kujenga mabwawa mbali mbali kwa ajili ya kutunzia maji.
Kauli hiyo imetolewa na mtendaji mkuu wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja ambapo alisema kwamba Ujenzi wa mabwawa hayo yataweza kusaidia wananchi kuondokana na adha na kero waliyokuwa wakiipata.
Kuhemeja alifafanua kuwa kiwango kilichopo kwa sasa cha upatikanaji wa maji kitaweza kutuvusha katika kipindi kizima cha kiangazi na kwamba wananchi wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wasiwe na shaka yoyote.
Pia Luhemeja katika hatua nyingine amewataka wananchi wote kuhakikisha kwamba wanatunza na kulinda vyanzo vyote vya maji ili kuwepo na upatikanaji wa maji ya uhakika katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Mkoa wa Pwani.
“Itakumbukwa kwamba mnamo mwaka jana maeneo kadhaa ya Jiji la Dar es Salaam yalikumbwa na tatizo la uhaba wa maji nah ii ni kutokana na ukame uliosababishwa na kutokunyesha kwa mvua za vuli na ndio maana wakuu wa mikoa hii miwili wameweza kuungana kwa pamoja na kamati za ulinzi na usalama wakaona ni jambo la busara kuweza kutembelea na kujionea vyanzo vya maji,” alisema Luhemeja.
Kadhalika Luhemeja alisema kwamba mamlaka hiyo kwa sasa imeweka mipango madhubuti kwa ajili ya kuweza kuendelea kufanyabjitihada za makusudi za kuhakikisha kwamba kiasi cha maji kilichopo kwa sasa kinalindwa ili kuweza kudhibiti hali ya upotevu wa maji.
Kadhalika aliziomba kamati za ulinzi na usalama za mikoa yote miwili kushirikiana kwa dhati ili kuweza kuwadhibiti baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiyachepusha maji na kwamba ana imani kubwa bwawa ambalo wamelijenga kwa ajili ya kuhifadhia maji litakuwa ni mkombozi hasa katika kipindi chote cha ukame.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amosi Makala ametoa wito kwa wananchi pamoja na viongozi mbali mbali wa dini zote kuhakikisha wanafanya maombi kwa ajili ya kuombea mvua za vuli zinyeshe ili kusiweze kutokea tena majanga ya ukame kama ilivyoweza kutokea katika kipindi cha mwaka jana hali ambayo ilipelekea vyanzo vya maji kupungua na kusababisha wananchi kupata usumbufu.
Pia katika ziara hiyo Makala ameridhishwa na kazi amabzo zinafanywa na viongozi wa Dawasa na kuwahakikishia wakazi wa Mkoa huo kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa sasa ni nzuri hivyo wasiwe na shaka.
“Ndugu zangu waandishi wa habari mwaka jana kuliweza kutokea hali ya ukame wa maji kutokana na kutonyesha kwa mvua za vuli lakini nataka niwaambia kitu kikubwa ni kuomba Dua na maombi mvua zinyeshe na sio kuilaumu serikali kwani serikali haileti mvua na kwamba tutazidi kushirikiana na mamlaka husika lengo ikiwa hali ya maji iweze kupatikana katika kipindi chote,”alisema Makala.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amekemea tabia ya baadhi ya wananchi wenye tabia ya kuchepusha maji kutoka kwenye vyanzo vya maji na kuahidi kuwachukulia hatua kali kwa wale wote ambao watahusika kwani lengo la serikali ni kuwapelekea huduma ya maji safi na salama katika maeneo mbali mbali.
“Kitu kikubwa ninachowaomba wanachi kuhakikisha kwamba wanaachana mara moja na tabia ya kuchepusha maji katika vyanzo vya mto ruvu kwani wakifanya hivyo kunapelekea maji yapungue katika vyanzo vyetu vya maji”alisema Kunenge.
Ujio wa ziara hiyo ya siku moja ambayo imefanywa na wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani pamoja na wajumbe wa kamati za ulinzi na usalama wa mikoa miwili imeweza kusaidia kujionea chanzo cha maji Cha mto Ruvu pamoja na mitambo ya Ruvu juu na Ruvu chini.