
MABINGWA watetezi, Al Ahly ya Misri usiku wa kuamkia leo wamefanikiwa kutinga Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Hilal ya Sudan Uwanja wa Cheikha Ould Boïdiya Jijini Nouakchott nchini Mauritania.
Shujaa wa Al Ahly, mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo ni kiungo Emam Ashour Metwally Abdelghany dakika ya 80 akimalizia kazi nzuri ya Farao mwenzake, mshambuliaji Taher Mohamed Ahmed Taher Mohamed Mahmoud.
Al Ahly wanakwenda Nusu Fainali kwa ushindi wa jumla wa 2-0 kufuatia kushinda 1-0 pia kwenye mchezo wa kwanza Aprili 1 bao la beki Mmisri, Mohamed Hany Gamal Eldemerdash Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo, Misri.
Ahly sasa itakutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambayo imeitoa Espérance ya Tunisia kwa kuichapa 1-0 nyumbani, Uwanja wa Venue Loftus Versfeld Jijini Pretoria, Tshwane kabla ya sare ya bila mabao jana Uwanja wa Olympique Hammadi-Agrebi mjini Radès, Tunisia.
Mechi nyingine ya marudiano ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika — Pyramids imekwenda Nusu Fainali licha ya kuchapwa 2-0 na wenyeji, FAR Rabat mabao ya washambuliaji, Mmoroco Youssef El Fahli dakika ya nane na Mkongo,
Joël Beya dakika ya 82 Uwanja wa D'Honneur mjini Miknas.
Hata hivyo, Pyramids inakwenda Nusu Fainali kwa ushindi wa jumla wa 4-3 kufuatia ushindi wa 4-1 kwenye mchezo wa kwanza Aprili 1 Uwanja wa Jeshi la Anga la Misri Juni 30 Jijini Cairo.
Siku hiyo, mabao ya Pyramids yalifungwa na mshambuliaji Mkongo wa zamani wa Yanga ya Tanzania, Fiston Kalala Mayele mawili, dakika ya pili na 12 na mengine mawili, kiungo Mmisri, Ibrahim Adel 38 na 67, wakati bao la FAR Rabat lilifungwa na kiungo Mmorocco, Abdelfattah Hadraf dakika ya 45.
Pyramids sasa itakutana na mshindi wa jumla kati ya wenyeji, Orlando Pirates na MC Alger ya Algeria zinazorudiana leo Uwanja wa Orlando Jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Ikumbukwe mechi ya kwanza Orlando Pirates iliichapa 1-0 MC Alger bao pekee la kiungo chipukizi wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Mohau Nkota dakika ya 65 Uwanja wa Julai 5, 1962 Jijini Algiers.