ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, December 28, 2025

SENEGAL NA DRC ZATOSHANA NGUVU, SARE 1-1 AFCON

 


TIMU za Senegal na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimetoa sare ya kufungana bao 1–1 katika mchezo wa Kundi D Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 usiku wa tarehe 27 Uwanja wa Tangier Grand mjini Tangier nchini Morocco.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na Refa Lahlou Benbraham wa Algeria, mshambuliaji wa Real Betis ya Hispania, Cédric Bakambu alianza kuifungia DRC dakika ya 61, kabla ya mshambuliaji mwingine, Sadio Mane wa Al-Nassr ya Saudi Arabia kuisawazishia Senegal dakika ya 69.

Kila timu inafikisha pointi nne bada ya kushinda mechi zao za kwanza za Kundi hilo, Senegal ikiichapa Botswana 3-0 na DRC ikiichapa Benin 1-0.
Baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Botswana leo, Benin inakaa nafasi ya tatu nyuma ya Senegal na DRC katika Kundi D kuelekea mechi za mwisho. 

TAIFA STARS YATOA SARE 1-1 NA UGANDA AFCON

 


TANZANIA na Uganda zimegawana pointi kwa sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa Kundi C Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) usiku wa Tarehe 27 Disemba 2025, huu Uwanja wa Al Medina Jijini Rabat nchini Morocco.

Mshambuliaji wa Al Talaba ya Iraq, Simon Happygod Msuva alianza kuifungia Taifa Stars kwa mkwaju wa penalti dakika ya 59, kabla ya mshambuliaji mwingine, Karl Anthony Uchechukwu Mubiru Ikpeazu wa St Johnstone ya Scotland kuisawazishia The Cranes dakika ya 80.

Karl Anthony Uchechukwu Mubiru Ikpeazu ni mzaliwa wa Harrow, England baba yake akiwa Mnigeria na mama yake Mganda.

Mshambuliaji wa Vipers SC ha kwao, Uganda Allan Okello alikosa penalti dakika ya 90 baada ya kupiga juu ya lango na kuzima matumaini ya The. Cranes kushinda mechi.

Kwa matokeo hayo, kila timu inaokota pointi ya kwanza baada ya kupoteza mechi zao za kwanza, Uganda ikifungwa 3-1 na Tunisia na Tanzania ikichapwa 2-1 na Nigeria.

Msuva amefikia rekodi ya Thuwein Ali Waziri kuifungia jumla mabao matatu Tanzania kwenye Fainali za AFCON akiwa amefikisha idadi hiyo katika Fainali tatu, 2019 Misri, 2023 Ivory Coast na za mwaka huu Ivory Coast.

Thuwein yeye alifunga mabao yake yote kwenye Fainali za mwaka 1980 nchini Nigeria.