|
Maandamano Garissa. |
Wananchi wa mji wa Garissa nchini Kenya wamefanya maandamano kupinga vitendo vya kundi la Al Shabaab, lililoshambulia chuo kimoja kikuu mjini humo na kuwaua watu 147 wengi wao wakiwa wanafunzi hapo jana.
Waandamanaji pia wameelezea kutoridhika na vyombo vya usalama nchini humo wakisema havikuchukua hatua za kutosha kutoa ulinzi kwa waliouawa na kwa raia wengine kwa jumla.
Wazazi, jamaa na marafiki wa wanafunzi waliouawa katika chuo kikuu cha Garissa wamekuwa wakiendelea kuwasili katika eneo hilo kuitambua miili ya wapendwa wao.
Waliojeruhiwa wanaendelea kupata matibabu .
|
Garissa. |
Serikali ya Kenya imekuwa ikiwasafirisha manusura wa shambulio hilo kwa mabasi kuelekea makwao huku miili ya waliouawa ikisafirishwa mjini Nairobi.
Wakati huo huo rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamoud, amesema Somalia na Kenya zinafaa kuimarisha uhusiano wao katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Tamko hilo linajiri siku moja baada ya shambulio hilo la Alshaabab katika chuo kimoja kikuu mjini Garrisa.CHANZO: BBC SWAHILI