ZAIDI ya wananchi 48,434 wa wilaya ya
Iringa wamefanikiwa kuchanja chanjo ya UVIKO 19 kwa lengo la kuendelea
kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Colona ambao umeshasababisha vifo vingi
vya wananchi wa wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa
kampeni ndogo ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kuchanja chanjo ya UVIKO 19,
Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa hadi kufikia tarehe
26/7/2022 walikuwa wamewafikia jumla ya wananchi 48,434 ambao wamepata chanjo ya
UVIKO 19 dozi ya pili ya chanjo ya Janssen ambayo ni sawa na asilimia 39.24 ya
walengwa 123,418.
Moyo alisema kuwa
lengo la kampeni hiyo ni kuhamasisha wananchi waliokuwa na miaka 18 na
kuendelea waweze kupata chanjo ya UVIKO 19 katika kipindi cha kampeni ndogo
inayoendelea hivi sasa katika wilaya ya Iringa.
Alisema kuwa kwa sasa
wilaya ya Iringa imetenge jumla ya vituo 79 vinavyotoa huduma za chanjo pamoja
na zoezi la uchanjaji katika vituo watoa huduma wanaotumia huduma za mkoba ili
kuwafikia wananchi popote walipo.
Moyo alisema kuwa
viongozi wa serikali, taasisi mbalimbali kama shule,vyuo, viongozi wa bajaji,
daladala,bodaboda,saluni,vikoba, viongozi wa dini,siasa wadau wa afya,wazee
mashuhuri na wazee wa kimila kuhakikisha wanashirikiana na serikali ya wilaya
ya Iringa kuhamasisha jamii ili iweze kupata chanjo ya UVIKO 19.
Alisema kuwa
wataalamu wa afya na jamii wanapaswa kupongezwa kwa namna ambavyo wamekuwa
wanalishughulikia suala la kitaifa kwa kuwa inaonyesha kwa namna gani
wanavyojitoa kutoa elimu kwa wananchi hadi wanachanja kwa hiyari chanjo ya
UVIKO 19.
Moyo alisema kuwa anatarajia wananchi
ambao hawajapata chanjo ya UVIKO-19 watashiriki kupata chanjo hiyo ambayo
inaendelea kutolewa na wataalamu wa afya.
“Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais
Dkt Philip Mpango na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa nyakati tofauti wamekuwa
wakiwaasa wananchi kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani maradhi hayo bado
yapo nchini hivyo tushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19,” amesema.
Moyo amesema baada ya maneno ya uongo na
dhana potofu kuonekana kuwa ni propaganda zisizo na maana yoyote, wananchi
wameamua kushiriki chanjo ya UVIKO-19 kwa manufaa yao.
“Mara nyingi kitu kigeni kikitokea kuna
baadhi ya watu wanapotosha na kuzungumza ndivyo sivyo juu ya jambo hilo
utadhani wanalitambua kumbe hawafahamu ila hili la UVIKO-19 wengi wao
wamelitambua na kulielewa ndiyo sababu wamejitokeza kwa wingi kuchanja,”
anasema Moyo
Mkazi wa kata ya Magulilwa John mwigane
anasema wataalamu wa afya wamekuwa wanafika hadi vijijini na kutoa elimu kwa
jamii kIsha kuwapatia chanjo hiyo ya UVIKO-19.
“Hadi hivi sasa elimu inaendelea kutolewa
kwa jamii huku vijijini na wanaitikia ushauri wa kupatiwa chanjo ya UVIKO-19
kwani wanatambua kuwa ukipata maradhi hayo bila kuchanja utapata matatizo
makubwa kwenye changamoto ya kupumua pindi ukiupata ugonjwa huo,” anasema.
Mkazi wa kijiji cha Ndiwili Hamisa Malima
anasema kuwa viongozi na wananchi wa Wilaya ya Iringa kwa pamoja wameungana
katika kuhakikisha wanapata chanjo ya UVIKO-19 ndiyo sababu ya wananchi
kujitokeza kuchanja chanjo ya UVIKO 19.
“Mtu anaona atapata maambukizi ya
UVIKO-19 yeye mwenyewe na hayo ni maradhi ambayo hayana matibabu hivyo ameona
hawezi kupata tatizo kisa kutochanjwa kwa kutosikiliza wataalamu wa afya na
kuwasilikiza wazushaji,” anaeleza
Hivi karibuni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu
akizungumza hivi karibuni kwenye tamasha la MZIKI MNENE lililofanyika uwanja wa
Nangwanda Mkoani Mtwara amesema imethibitika kuwa njia ambayo ni salama ya
kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19 ni kupata chanjo kwani ukichanja utakuwa umejikinga
na kuikinga jamii ya watanzania.
Waziri Ummy amesema Serikali inaendelea
kuwalinda wananchi wake katika maambuzi ya magonjwa mbalimbali kwa kutoa chanjo
ikiwemo ya UVIKO-19.
“Sisi kama Wizara ya Afya tutatumia mbinu
mbalimbali ambazo zitakazowafikia wananchi kama tunavyotumia matamasha haya
kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kupata huduma ya chanjo ya UVIKO-19,”
anamaliza kwa kusema Waziri Ummy.