Ndugu Waandishi wa habari, Tunapenda kutanguliza shukrani za dhati kwenu kwa kufika katika eneo hili kutusikiliza.Mbele yenu ni viongozi wa serikali za wanafunzi kutoka Vyuo vikuu mbalimbali vilivyopo mkoani Dodoma.Ndugu waandishi wa habari,si kawaida na wala mazoea kwa marais na viongozi wa serikali za wanafunzi kutoka vyuo tofauti kukutana kwa pamoja na kuzungumza na nyie wanahabari kama inavyotokea hii leo.
Ndugu wanahabari,siku ya Jumapili ya tarehe 22 mwezi huu wa 3,kundi la watu waliojitambulisha kama ni wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma walijikusanya nyumbani kwa mh; Lowasa na kutoa matamko mbalimbali ikiwa pamoja na kuutangazia uma wa watanzania kuwa sisi wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma tunamuunga mkono na tunahitaji Lowasa awe rais wetu sambamba kumchangia pesa.
Ndugu wanahabari,Tunapenda kukanusha kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma kwa ujumla wetu hatukuhusika na jambo lile na kama viongozi wa serikali za wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya mkoa huu wa Dodoma,Tunapinga na kulaani kitendo cha watu wachache kwenda kutuingiza sisi wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma katika jambo ambalo halituhusu na wala si lililotuleta hapa Dodoma.
Sisi kama wasomi ambao jamii inatutegemea kama kioo hatuwezi kuandamana na kujikusanya kwenye nyumba ya kiongozi na kumuomba agambee urais, wakati tunajua fika sisi hatuhusiki na uteuzi wa wagombea ndani ya taasisi yao.Kilichofanyika ni kuudanganya uma wa watanzania na taasiasi yake kupitia kivuli cha vijana wachache kutoka vyuo vya hapa Dodoma,waliolipwa pesa ili waweze kuwa kava la tukio lile.
Ndugu wanahabari,Mkoa wa Dodoma unavyuo vikuu visivyopungua 8,Na jumla ya wanafunzi wote tunaosoma katika vyuo vya Dodoma ni zaidi ya wanafunzi 35,000.Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) pekee yake kinawanafunzi wasiopungua 22,000.
Idadi ya watu waliojikusanya nyumbani kwa Mh: Lowasa siku ya tarehe 22-03-2015 haizidi watu 230 wakiwemo Wamachinga na Wenyeviti wa Jumuiya za wazazi, kama vyombo vya habari vilivyoripoti.
Ukiwatoa Wamachinga na Wenyeviti wa Jumuiya za wazazi waliotoka mikoa mbalimbali,idadi ya wanafunzi waliokuwepo kwenye tukio lile hawazidi 150.Idadi hii ni sawa na asilimia 0.4 ya wanafunzi wote wanaosoma vyuo vikuu vya Dodoma.Ndugu wanahabari,kwa akili ya kawaida kabisa asilimia 0.4 ya wanafunzi wa vyuo vikuu ndio waliokuwa pale.
Tunashangazwa na dhambi tusiyoitenda tunayobebeshwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma ambao kwa sasa tupo bize na msimu mpya ya masomo wenye changamoto mbalimbali.
Ndugu wanahabari,sisi kama vijana wasomi na watu tunaotegemewa na jamii zetu tutakusanyika katika kujadili na kuchambua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii yetu na sio kukusanyika kwa ajili ya mwanasiasa ambaye sifa zake na uhadilifu wake unatiliwa shaka katika jamii.
Tunaomba mlijulishe Taifa, kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma hatujahusika na tukio lile isipokuwa wanafunzi wachache walitumika kwa kupewa pesa na wahusika wa tukio lile.Tunataka Taifa lijue hatupo tayari kutumia elimu zetu kulitia upofu taifa letu.Waambieni mama zetu na baba zetu huku vijijini kwetu kuwa tumekuja kutafuta elimu ili ituwezeshe kuwakomboa wao na sio kutumika na Wanasiasa kwa malengo yao.
Tunatambua haki ya mwanafunzi kuamua na kufanya shughuli za kisiasa nje ya maeneo ya vyuo, lakini hatukubaliani na wanafunzi wachache kuchafua na kuwapaka matope maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma ambao hawajahusika na tukio lile.Hii sio haki na haikubaliki.
Vilevile tungependa kutumia fursa hii kuwaasa wanafunzi wenzetu popote pale nchini, makundi mbalimbali ya kijamii (wakulima, wafugaji, wavuvi, wamachinga, wasanii, n.k), zikiwemo taasisi za dini kwamba watu wachache kuzungumza kwa niaba ya makundi juu ya mambo yanayogusa maamuzi ya mtu binafsi.
Mwisho tunatoa wito kwa wanafunzi wenzetu wote kujitambua na kutumie muda wetu kwa mambo ya msingi na muhimu kwa ustawi wa Nchi yetu. Na kuonesha jinsi wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Dodoma walivyokasilishwa na jambo hili, Tamko hili limesainiwa na wanafunzi 7821 toka vyuo mbali mbali vya Dodoma.Majina ya sahihi za wanafunzi zimeambatanishwa. Tusikubali kutumika na wanasiasa wa aina hii..
Asanteni
Mungu ibariki Tanzania,Mungu vibariki vyuo vikuu vya Dodoma.
Kwa niaba ya wawakilishi wa serikali za Wanafunzi Chuo cha Mipango,Chuo cha Madini, Chuo cha Hombolo,Chuo kikuu cha Dodoma(UDOM) na CBE.
DANIEL DANIEL -Rais wa Saint Jonh’s University
26/03/2015