ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, July 1, 2022

MFANYAKAZI WA TANESCO AFARIKI AKIPUMZIKA NA MPENZI WAKE GESTI

 

Mtumishi wa Shirika la Umeme (TANESCO) anayefahamika kwa jina la Yahaya Abdul, mkazi wa Manispaa ya Mpanda mkoa wa katavi, amekutwa amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni alikoenda kujipumzisha na rafiki yake wa kike.


Tukio hilo limetokea mtaa wa Ikulu, Kata ya Kawajense, Mjumbe wa serikali ya mtaa huo George Kadesi, amesema baada ya kuona umati wa watu ukiwa umezungunguka gesti hiyo na alipofika alielezwa kuwa marehemu aliingia kwenye nyumba hiyo akiwa na rafiki yake wa kike.

Kwa upande wake mhudumu wa nyumba ya kulala wageni ameeleza kuwa marehemu alifika majira ya saa 7:00 mchana na mpenzi wake lakini ameshangazwa kuona pikipiki ya mtu huyo mpaka asubuhi ikiwa pale gesti.

Wednesday, June 29, 2022

MRADI WA MAJI UNAKUJA

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia) alipowasili katika Kijiji cha Bupigu Wilaya ya Ileje kukagua uwezekano wa kuwa na mradi wa kutoa maji kutoka Mto Bupigu
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akiwa ameambatana na Wahandisi wa RUWASA Mkoa wa Songwe wakielekea kwenye maeneo unapopita Mto Bupigu.
Wahandisi wa RUWASA Mkoa wa Songwe wakimuonyesha Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kushoto) maeneo ya milima ambayo Mto Bupigu unatiririsha maji yake.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga alipotembelea Kijiji cha Bupigu kukagua mtiririko wa Mto Bupigu.


Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema Serikali inatarajia kuwa na mradi mkubwa wa maji utakaohudumia miji mbalimbali katika Mkoa wa Songwe ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama.

 

Amesema hayo hivi karibuni alipotembelea eneo la Mto Bupigu, kijiji cha Bupigu Wilayani Ileje Mkoa wa Songwe kwa dhamira ya kukagua vyanzo toshelevu vya maji katika miji yenye changamoto ya huduma ya maji.

 

“Katika milima hii ndipo kuna chanzo tunachokitarajia kuchukua maji takriban kilomita 75 kutoka Bupigu kuelekea mji wa Tunduma. Ni mradi ambao tunautengeneza yaani  ‘project formulation’ ili  tutafute fedha za kuanza rasmi kujenga mradi,”  Mhandisi Sanga alisema.

 

Alisema Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa maeneo ya mijini mkoani humo na kwamba jitihada za makusudi zinaendelea kuchukuliwa ili kuwa na huduma toshelevu ya maji kwa wakazi wa miji hiyo.

 

“Kwa Mkoa huu wa Songwe, tunatambua changamoto kubwa ya maji ipo katika maeneo ya mijini, maeneo ya vijijini Serikali kupitia RUWASA imefanya kazi kubwa lakini mijini mathalan katika mji wa Tunduma mahitaji ni takriban lita milioni 17 kwa siku wakati maji yanayozalishwa ni chini ya lita milioni tano kwa siku,” Mhandisi Sanga alisema.

 

Alisema Serikali imelenga kutoa maji Mto Bupigu na kuyafikisha katika mji wa Ileje ambapo ndipo chanzo kilipo,  vijijini takriban 14 vipate maji kupitia mradi huo, makao makuu ya Mkoa wa Songwe yaani Vwawa, mji wa Tunduma, Mlowo na Mbozi.

 

Alifafanua kwamba matarajio ya Serikali ni kuhakikisha vyanzo toshelevu vya maji vinatumika kwa kuwa na miradi mikubwa ya maji ili kuwaondolea adha wananchi.

 

“Tunatarajia kutumia Mto Bupigu kujenga mradi mkubwa ambao utaondoa kabisa tatizo la maji katika mji wa Tunduma; ni ahadi ambayo tulikwishaitoa kupitia  viongozi mbalimbali wakitaifa ambao wamefika huku,” Mhandisi Sanga alibainisha.

 

Alisema katika ngazi ya Wizara ya Maji kufika kwake hapo ni kuashiria kwamba mradi huo sasa upo katika hatua za kutengeneza ili uweze kuanza na kuwaondolea wakazi wa Tunduma na miji mengine Mkoani humo changamoto ya upatikanaji wa maji.

Tuesday, June 28, 2022

DC MOYO ATOA MASAA 48 RUWASA KUMLIPA MKARANDARASI FEDHA ZA MRADI WA NEGHABIHI NA IKENGEZA

 Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akitoa masaa 48 kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wanamlipa fedha zake mkandarasi wa mradi wa Neghabihi na Ikengeza unaotekelezwa kwa fedha za UVIKO19 wenye jumla ya gharama ya kiasi cha shilingi 643,792097,00.

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo ya matanki ya maji ambalo limejengwa katika kijiji cha Neghabihi kwa ajili ya kupeleka huduma ya maji kwa wananchi

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiwa na Mwenyekiti wa Halamshauri ya wilaya ya Iringa Mheshimiwa Stephen Mhapa wakilizisha kuanza kutoka kwa maji ambayo inaashiria kuwa mkandarasi anafanya kazi yake inavyotakiwa

 

Na Fredy Mgunda,Iringa.

 

MKUU wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo ametoa masaa 48 kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wanamlipa fedha zake mkandarasi wa mradi wa Neghabihi na Ikengeza unaotekelezwa kwa fedha za UVIKO19 wenye jumla ya gharama ya kiasi cha shilingi 643,792097,00.

 

Akiwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maji wilaya ya a Iringa, mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa kazi iliyofanywa na mkandarasi M/S GNMS Contractors kwa kiasi kikubwa imekamilika na kilichobakia ni mkandarasi kulipwa fedha zake.

 

Moyo alisema kuwa haiwezekani mkandarasi amemaliza kazi lakini mhasibu anachelewesha malipo hivyo alitoa maagizo kwa meneja wa RUWASA wilaya ya Iringa kumlipa fedha mkandarasi huyo.

 

Alimwagiza meneja amwambie mhasibu amlipe mkandarasi ndani ya masaa 48 kinyume cha hapo atamchukulia hatua za kisheria kwa kuwa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Iringa imeridhishwa na kazi iliyofanywa na mkandarasi huyo.

 

Moyo alisema kuwa mradi umefika asilimia 73 na hakuna malipo yoyote yale yaliyofanyika hivyo RUWASA wanapaswa kulipa haraka malipo ambayo mkandarasi anadai ili kumalizia kazi iliyobaki ili kufanikisha kuwatua ndoo wanawake.

 

Kwa upande wake meneja wa RUWASA wilaya ya Iringa Eng Masoud Samila alisema kuwa Mradi huyo ni  wa teknolojia ya msukumo kwa kutumia pampu ya umeme ambapo chanzo cha maji ni visima virefu kwa maeneo yote mawili ya Neghabihi na ikengeza.

 

Eng Samila alisema kuwa Lengo ni kuwapatia wananchi wa eneo husika maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 pamoja kupungunza mlipuko wa magonjwa mbalimbali yanayoweza kujitokeze kutokana na changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama.

 

Alisema kuwa mradi huo unarajiwa kuwanufaisha wananchi 4920 ambao walikuwa wanakosa maji safi na salama karibu nao hivyo kukamilika kwa mradi huo kutachochea kuongezeka shughuli za kiuchumi kwa wananchi waliopo maeneo ya mradi.

 

Eng Samila alimalizia kwa kusema kuwa wameyapokea maagizo yote ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Iringa na watayafanyia kazi haraka mno likiwepo swala la kumlipa mkandarasi fedha anazozidia kwa wakati kama walivyoagizwa na mkuu wa wilaya ya Iringa.

Monday, June 27, 2022

DC MOYO ATATUA MGOGORO WA KIJIJI CHA UFYAMBE NA WAWEKEZAJI WA ZAO LA PARACHICHI

 

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiongea na wananchi wakati wa kutatua mgogoro  wa ardhi wa zaidi ya hekari 110 uliokuwepo baina ya wawekezaji na wananchi wa Kijiji cha Ufyambe.

Mmoja ya wawekezaji akiongea na wananchi wakati wa kutatua mgogoro  wa ardhi wa zaidi ya hekari 110 uliokuwepo baina ya wawekezaji na wananchi wa Kijiji cha Ufyambe.Wawekezaji wakiongea na wananchi wakati wa kutatua mgogoro  wa ardhi wa zaidi ya hekari 110 uliokuwepo baina ya wawekezaji na wananchi wa Kijiji cha Ufyambe.Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiongea na wananchi wakati wa kutatua mgogoro  wa ardhi wa zaidi ya hekari 110 uliokuwepo baina ya wawekezaji na wananchi wa Kijiji cha Ufyambe.


Na Fredy Mgunda,Iringa.


MKUU wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo amefanikiwa kutatua mgogoro  wa ardhi wa zaidi ya hekari 110 uliokuwepo baina ya wawekezaji na wananchi wa Kijiji cha Ufyambe.

 

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara,mkuu wa wilaya Mohamed Hassan Moyo alisema kuwa alipokea malalamiko ya wananchi juu ya wawekezaji hao kuwa wamechukua eneo la ardhi bila ridhaa ya wananchi.

 

Moyo alisema kuwa kazi ya serikali ya wilaya ni kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto za wananchi pamoja na kuwasimamia katika maendeleo hivyo jukumu alilofanya alitimiza kama ambavyo inatakiwa iwe.

 

Alisema kuwa kitendo cha kuwaweka ndani viongozi wa serikali ya kijiji cha Ufyambe kilikuwa kitendo cha kutaka kupata ushahidi wa nini kinaendelea kwenye mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na wawekezaji.

 

Moyo alisema kuwa serikali lazima inafanye kazi kwa mjibu wa katiba na sheria za nchi katika kuwatumikia wananchi ndio maana wamefanikiwa kutatua mgogoro huo.

 

Alisema kuwa wawekezaji walikiuka baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yanaenda kinyume na kanuni za uwekezaji wa ardhi ya Kijiji hivyo baada ya kubaini hilo wawekezaji walifuata sheria zote.

 

Moyo aliwataka wawekezaji wote ambao wapo na wanataka kuwekeza katika ardhi ya wilaya ya Iringa wanatakiwa kufuata taratibu na sheria za uwekezaji ili wasibuguziwe.

 

Alisema kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji waliopo katika maeneo mbalimbali wanayazunguka ili kupata faida ya uwepo wa wawekezaji kama ambavyo wawekezaji wamekuwa wakichangia maendeleo kwenye miradi mbalimbali ya ujirani mwema.

 

Aidha Moyo alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anawakaribisha wawekezaji na anawapenda wawekezaji lakini anataka wawekezaji wafuate taratibu, sheria,kanuni na Katiba ya nchi.

 

John Lemomo,Baton Nsemwa na mchungaji Metili walisema kuwa walifanya kosa walipofika kuwekeza katika hatua za awali na kupeleka mgogoro ambao umetatuliwa na Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo.

 

Walisema kuwa wanamshukuru mkuu wa wilaya ya Iringa kwa kuwakumbusha kufuata taratibu na sheria za uwekezaji ili kuepukana na migogoro baina yao na wananchi wa maeneo husika.

 

Waliongeza kuwa wapo tayari kuwekeza katika Kijiji cha Ufyambe na wataendelea kutoa elimu kwa wawekezaji wengine ambao wanania ya kuwekeza ili wafuate taratibu na sheria za uwekezaji zinavyotaka.

 

Nao baadhi ya wananchi walisema kuwa wanakaribisha tena wawekezaji hao na wafanye uwekezaji wao kwa kufuata taratibu na sheria za uwekezaji ili kuepukana na migogoro baina ya wananchi wa Kijiji cha Ufyambe.

 

BALOZI WA UTALII LYDIA AMUUNGA MKONO RAIS SAMIA KWA KUANZISHA MBIO ZA MARANGU NATURE WALK RIDE&RUN

 

BALOZI wa Utalii nchini Lydia Lukaba akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza mbio za Marangu Nature Walk Ride&Run zenye lengo la kutangaza utalii wa ndani kulia ni Afisa Uhifadhi kutoka Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro Vitus Mgaya
BALOZI wa Utalii nchini Lydia Lukaba akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza mbio za Marangu Nature Walk Ride&Run zenye lengo la kutangaza utalii wa ndani kulia ni Afisa Uhifadhi kutoka Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro Vitus Mgaya na  kushoto ni Fredy Moshi kutoka Ndoro Water Fall
Afisa Uhifadhi kutoka Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro Vitus Mgaya akizungumza na waandishi wa habari kushoto ni Fredy Moshi kutoka Ndoro Water Fall
Fredy Moshi kutoka Ndoro Water Fall akizungumza
Meneja wa Hotel ya Hosea Inn Marangu Dues Masawe akizungumza


NA OSCAR ASSENGA,MOSHI.

BALOZI wa Utalii nchini Lydia Lukaba ameunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu za kutangaza utalii nchini kwa kuanzisha mbio za Marangu Nature Walk Ride&Run zenye lengo la kutangaza utalii wa ndani

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Marangu Balozi Lydia alisema licha ya kuzitumia kutangaza utalii wa ndani lakini pia watachangia taulo za Kike kwa ajili ya watoto wa kike ambao hawana uwezo kwa kupatiwa msaada huo.

Alisema mbio hizo ambazo zitakwenda sambamba na matembezi zitakuwa endelevu na zitafanyika Julai 10 mwaka huu na zitaanzia Marangu Mtoni yatakuwa ya kilomita 50,21 mara mbili na kilomita 40 za baiskeli na Kilomita 5.

Balozi Lydia ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Conservation Marathon alisema mbio hizo zitapita eneo la Kinukamori Water fall na kilomita 10 zitakwenda Ndoro Water falls wakati zile za Kilomoita 21 zitaanza kinapa na kwenda Mandara na kumalizika Marangu mtoni kwa Hosea.

Alisema katika mbio hizo wanategemea kuwa na vyakula vya asili,vinywaji vya asili mbege na kwenye vituo vyao vitakuwa na vyakula vya kichaga ni wakati mzuri wa kupata uzoefu lengo mbali na kutangaza utalii na wameshirikisha shule mbalimbali za Msingi na sekondari .

Balozi huyo alisema wamefanya hivyo wakiamini kwenye utalii ni vizuri wakihusisha watoto wadogo waweze kujua utalii tokea wakiwa chini huku akiomba serikali iweze kuangalia suala hilo kwa kuanzia kufundisha utalii kuanzia shule za Msingi.

“Tumeona tutangaze utalii kupitia mbio kwani pia ni tiba na kumekuwa na mwamko mkubwa kwani watanzania hushiriki mbio mbalimbali kupitia hilo tunawakaribisha watanzania”Alisema ,

“Lakini pia lengo kuanzisha mbio hizo ni kuunga mkono juhudi ambazo zimeanzishwa na Rais Samia kwenye kampeni yake ya kutangaza vivutio vya utalii nchini”Alisema

Alisema Rais amefanya jambo kubwa na nzuri hivyo wao kama wadau wa utalii wameona watumie fursa ya kuanzisha mbio hizo kwa lengo la kuhakikisha wanakwenda sambamba na malengo ya Rais Samia.

Awali akingumza Afisa Uhifadhi kutoka Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro Vitus Mgaya alisema wameunga na Balozi wa Utalii Lydia ambaye amehamasisha kuandaa mbio za watu kutembelea ndani ya hifadhi kuendesha baiskeli na shughuli nyengine za utamadhu wao kama hifadhi wanamuunga mkono kwa juhudi zake na watamsaoti na watashirikisha watu wengine.

“Mbio hizo ni nzuri kwa sababu zitakuwa zinatangaza utalii na hivyo kuwafanya watanzania waweze kufahamu vivutio vyao na kuweza kutangaza utalii waje waungane Marangu tunawakabisha watanzania wote wajiandikishe”Alisisitiza.

Naye kwa upande wake Meneja wa Hotel ya Hosea Inn Marangu Dues Masawe alisema wazo aliloamua kulifanya Balozi Lydia kwa mbio hizo ni nzuri na watamuunga na kuwataka watanzania wamsapoti .

Hata hivyo kwa upande wake Fredy Moshi kutoka Ndoro Water Falls ambao wanaojishughulisha na uhifadhi wa mazingira na kuotesha miti alisema mbio hizo za zitapita kwenye eneo lao na wamejiandaa vizuri na wana mshukuru Lidya huku wakiwaomba wadau wengine wamsapoti wakiwemo Kinapa na Tanapa.

RC MALIMA ASISITIZA VIWANGO BARABARA ZA TANGA

 



Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amemhimiza mkandarasi anayesimamia ujenzi wa Barabara ya Tanga-Pangani kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Km 50, kuzingatia viwango vyote vya ubora katika kukamilisha barabara hiyo ili iendane na fedha za Watanzania zilizotolewa kwa ajili hiyo.
 
Amesema barabara hiyo ni muhimu kwenye mfumo wa barabara za kitaifa na kimataifa si tu kwa ajili ya Tanga, kwani inaenda kuunganisha na Kenya.
 
Malima alisema hayo wakati akikagua barabara hiyo na nyingine za mkoa huo zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura).

“Kimsingi barabara hii inapunguza zaidi ya Km 120, inafupisha mtandao mzima wa kwenda hadi Mombasa (Kenya) kwa sababu matarajio ni babarabara hii kuingia hadi kwenye mtandao wa Afrika Mashariki.
 
“Kwa hiyo kukamilika kwa barabara hii ni muhimu sana lakini kwa bahati mbaya barabara hii imechelewa kwa sababu mbalimbali kwani ilikuwa Km hizo 50 ilikuwa zimalizike  Novemba mwaka jana lakini hapo katikati ikaingia corona, matatizo ya fidia kwa upande wa Tanga na migogoro mingine kwa hiyo ikachelewa ikapelekwa hadi Desemba mwaka huu,” alisema Malima.
 
Aidha, aliongeza kuwa bado inaonekana kwa asilimia zilizofikiwa maeneo ya lami yanaweza kufikiwa kama Km 30 hadi kufikia Desemba lakini kwa sasa tunaona kasi inakwenda vizuri zaidi kuliko ilivyokuwa kabla.
 
“Kwa hiyo niishukuru serikali kwani miezi kama sita iliyopita tulikuja kukagua na Waziri Mbarawa (Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi – Profesa Makame Mbarawa) tuliweka mkataba usio na maandishi baina ya serikali, Mkoa wa Tanga na wizara kwamba na sisi tutakuwa na utaratibu wa kupita na kukagua maendeleo ya pamoja na wahandisi wa mkoa, Tanroads, Kamati ya Usalama ya Mkoa na pale ambapo tunaona kuna ucheleweshaji wa jambo moja au jingine basi tutatumia fursa hiyo kumwambia waziri kwamba jamani kule barabara yetu mliyotuachia tufanye uangalizi na usimamizi kuna haya na haya.
 
“Hatua hii inatusaidia kujadili barabara ambazo tumeziona kwa macho katika Kikao cha Bodi ya Barabara na wakati tunapokea taarifa ya Tanroads na Tarura mkoa tunakuwa na uelewa wa barabara hizo kwa hiyo wakisema pale daraja sijui limefanya nini tunasema hapana tumeiona.
 
“Kwa mfano kama sasa msimamizi anakwamishwa kwa sababu kuna fedha zimechelewa kidogo kama bilioni tisa hivi ambazo zinamuweka kwenye hali ya kuchelewesha kazi na kupata kisingizio. Kwa hiyo changamoto zilizopo hapa tumeziona na tumepata taarifa kutoka kwa wahandisi,” alisema Malima.
 
 
Kwa upande wake Meneja wa Tanroads Mkoa wa Tanga, Mhandisi Eliazary Rweikiza alisema mradi huo unaosimamiwa na Mkandarasi Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Ltd. ya nchini China kwa gharama ya Sh bilioni 67.47 imefikia asilimia 37.6 ya utekelezaji na makubaliano na mkandarasi ni kwamba ikamilike Desemba 5, mwaka huu.
 
Alibainisha kuwa kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kulitokana na changamoto mbalimbali ikiwamo malipo kwani hadi kufikia Mei mwaka huu mkandarasi alikuwa anaidai serikali Sh bilioni 9.64.
 
“Aidha, changamoto za kuchelewa kulipa fidia kwa waliofuatwa na barabara ili kupisha mradi, matakwa ya fidia kutoka kwa wamiliki wa maeneo hayo, mkandarasi kuchelewa kulipwa malipo kwa wakati na upatikanaji wa maeneo mazuri ya changarawe na ugonjwa wa corona ambao ulisababisha wataalamu wa mkandarasi kuchelewa kuwasili eneo la kazi.
 
“Lakini pia mwanzoni mwa mradi mkandarasi alikuwa na meneja wa mradi ambaye alikuwa hajui Kiswahili wala Kiingereza na kusababisha mawasiliano ya kiutendaji kuwa magumu. Changamoto hii kwa sasa haipo kwa kuwa meneja huyo aliondolewa na kuletwa mwingine ambaye anajua Kiingereza na ana ,ipango mizuri ya kazi,” alisema.

SERIKALI YASIKIA KILIO CHA MBUNGE MPINA UKOSEFU WA HUDUMA KWENYE ZAHANATI JIMBO LA KISESA

 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Innocent Bashungwa



WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Innocent Bashungwa amesikia kilio cha Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina aliyehoji sababu ya Serikali kutozifungua Zahanati 10 zilizojengwa na kukamilika kwa miaka mingi sasa huku wananchi wa vijiji hivyo wakilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma.

Akichangia bajeti ya Wizara ya Afya bungeni Dodoma Mei,2022, Mpina alisema upungufu wa watumishi wa kada ya Afya ngazi ya Zahanati ni tatizo ambalo halijapata suluhu kwa muda mrefu na wananchi wakiendelea kukosa huduma hitajika katika vijiji vingi vya Jimbo la Kisesa.

Mpina alisema Serikali ilipaswa kuweka utaratibu mzuri wa ajira na kutumia njia mbadala ya kuingia 4 mkataba na vijana waliohitimu mafunzo mbalimbali ya Afya ambao hawaja ajiriwa ili kusaidia utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Mheshimiwa Spika, Kwenye Jimbo langu la Kisesa nina Zahanati 10 zilizokamilika muda mrefu lakini huduma hazitolewi, Mfano Zahanati ya Kijiji cha Semu, Mwandu Kisesa, Makomangwa, Mwageni, Mwagayi, Isangijo, Ikigijo, Mwakisandu, Malwilo na Tindabuligi, lakini pia tuna maboma ya muda mrefu 10 ya Kijiji cha Inonelwa, Mwamhongo, Nzanza, Matale, Masanga, Mwakipugila, Ntobo, Ng’hanga, Mwakasumbi na Lubiga” alisema Mpina.

Hata hivyo kwa mujibu wa orodha ya majina ya watumishi wapya wa sekta ya Afya iliyotangazwa na Waziri Bashungwa Juni 26, 2022 kwa Jimbo la Kisesa zitafunguliwa Zanahati 6 kati ya 10 zilizokamilika ujenzi wake.

Waziri Bashungwa amezitaja Zahanati hizo mpya zilitakazofunguliwa rasmi kwa Jimbo la Kisesa na idadi ya watumishi wapya kwenye mabano kuwa ni Zahanati ya Kijiji cha Isangijo Kata ya Lubiga (3), Zahanati ya Kijiji cha Makomangwa Kata ya Mwandoya (3), Zahanati ya Kijiji cha Mwagayi Kata ya Itinje (3).

Pia Waziri Bashungwa amezitaja zahanati nyingine zitakazofunguliwa Jimbo la Kisesa kuwa ni Zahanati ya Mwageni Kata ya Isengwa (3), Zahanati ya Kijiji cha Mwasungura Mwageni B (2), Zahanati ya Kijiji cha Malwilo Mnadani Kata ya Tindabuligi (3), Zahanati ya Mwandu Kisesa Kata ya Kisesa (3).

Waziri Bashungwa amewataja watumishi hao na majina ya vituo vyao kwenye mabano kuwa kuwa ni Teodora Kalistus Chodota Muuguzi Daraja la II, Ayubu Gladwell Mwaibosi Muuguzi Daraja la II na Ramadhani Shabani Mrutu, Tabibu Daraja la II (Co) (Zahanati ya Isangijo).

Wengine ni Joseph Rashid Ghake, Muuguzi Daraja la II, Edomu Anania Mwakingwe, Muuguzi Daraja La II, Frank John Mandala Tabibu Daraja la II (Zahanati ya Makomangwa).

Bashungwa amewataja wengine kuwa ni Nuru Daud Mwala , Muuguzi Daraja la II na Ernest Joseph Kachwele, Muuguzi Daraja la II (Zahanati ya Malwilo). Wengine ni Samwel Gelewa Simon, Muuguzi Daraja la II, Maryam Baraka Omar Female, Tabibu Daraja la II (CO) na Yohana Magori Magori, Muuguzi Daraja la II (Zahanati ya Mwagayi).

Wengine ni Azizi Poul Mgoboleni, Tabibu Daraja La II (Co), Johnson Joseph Kayombo, Muuguzi Daraja la II na Damian Emanuel Lyimo, Muuguzi Daraja la II (Zahanati ya Mwageni). Bertha Juvenary Nyamwiula, Muuguzi Daraja la II na Nkeshimana Jumanne Kasonga, Muuguzi Daraja la II (Zahanati ya Mwageni B- Mwasungura).

Wengine ni Kissile Nelson Mwakabago, Muuguzi Daraja la II, Eufransia Zacharia Mjuanga, Muuguzi Daraja la II na Ezekiel Christopher Mantyotyo, Tabibu Daraja la II (Co) (Zahanati ya Mwalilo Mnadani). Watumishi wengine ni Thereza Revocatus Lweyemaho, Muuguzi Daraja la II, Kasilda Gervas Nkembo, Tabibu Daraja la II (CO) (Zahanati ya Mwandu Kisesa).

WATUMISHI SEKTA YA MAJI WAPEWA MAELEKEZO

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kulia) akiwasikiliza watumishi Sekta ya Maji Mkoani Katavi (hawapo pichani).
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Mhandisi Mwajuma Waziri akizungumza na watumishi Sekta ya Maji Mkoani Rukwa (hawapo pichani). Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga.  

  Baadhi ya watumishi kutoka Ofisi za RUWASA Mkoa wa Katavi na Mamlaka ya Maji Mpanda wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (hayupo pichani)

Baadhi ya watumishi wa Sekta ya Maji Mkoani Rukwa wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (hayupo pichani)

Baadhi ya watumishi wa Sekta ya Maji Mkoani Songwe wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (hayupo pichani)

Katibu Mkuu Maji awafunda watumishi

Na Mohamed Saif

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amewaasa watumishi wote katika Sekta ya Maji kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni ili kufikia malengo ya kuwafikishia wananchi huduma toshelevu ya majisafi na salama.

Katibu Mkuu Sanga ametoa maelekezo hayo hivi karibuni kwa nyakati tofauti alipokutana na watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji katika Mikoa ya Katavi, Rukwa na Songwe.

“Sisi sote hapa ni watumishi wa umma; tunazo sheria, taratibu na kanuni za kiutumishi zinazotuongoza, ni muhimu kila mmojawetu akatimiza majukumu yake kwa kuzingatia haya mambo matatu,” alisisitiza Katibu Mkuu Sanga.

Mhandisi Sanga aliwaelekeza watumishi wote kwenye Sekta ya Maji kuepuka kuwa kero kwa wananchi na badala yake wawe ni wafumbuzi wa kero zinazowakabili wananchi hasa ikizingatiwa kwamba huduma ya maji haina mbadala na kwamba kila mwananchi anayo haki ya kupatiwa huduma bila kikwazo.

Aliwaasa watumishi hao kupenda kazi zao, kushirikiana, kuthaminiana, kupendana, kuheshimiana na kutambua jukumu la kila mmoja kwa jamii anayoihudumia ili kuepusha migongano isiyo ya lazima.

Alisema mwananchi anachohitaji ni kupata huduma ya maji haijalishi huduma hiyo anaipata kutoka kwenye Mamlaka ya Maji ama RUWASA na hivyo alizielekeza taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maji kushirikiana hasa ikizingatiwa jukumu la msingi la taasisi hizo ni kuhakikisha mwananchi anapata huduma toshelevu ya majisafi na salama.

“Wananchi wanatutegemea kuwafikishia huduma bora, toshelevu na ya uhakika, tusiwe kikwazo katika hili. Kila mmoja kwa nafasi alionayo na kwa taasisi aliyopo amsaidie mwenzake kufikia lengo hili na asiwe kikwazo kwa mwenzake,” alielekeza Mhandisi Sanga.

Aidha, watumishi hao walieleza changamoto zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi na pia walipata fursa ya kuzungumza na Mhe. Jumaa Aweso, Waziri wa Maji kwa njia ya simu kupitia Mhandisi Sanga na kupata nasaha zake.

Walipongeza utaratibu huo wa Katibu Mkuu Sanga wa kuwatembelea na kujadiliana kwa pamoja kuhusu utekelezaji wa majukumu yao na ufumbuzi wa pamoja wa changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili.

“Tunakushukuru sana Katibu Mkuu kwa utaratibu huu unaoendelea nao, tumepata nafasi ya kukueleza ana kwa ana masuala mbalimbali ya kiutendaji na tumefarijika kupata nasaha zako na za Mhe. Waziri ambazo zinaleta motisha kwenye utendaji wetu,” alisema Ligo Gambi, Fundi Sanifu Mamlaka ya Majisafi Mpanda (MUWASA).

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika vikao hivyo, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri ambaye aliambatana na Katibu Mkuu Sanga aliwaelekeza watumishi kuwa na maadili ya kazi, wajitume na wachape kazi kwa bidii ili kuleta matokeo chanya.

Katibu Mkuu Sanga amefanya ziara kwenye mikoa hiyo ili kujionea utekelezwaji wa miradi unaoendelea, kuzungumza na watumishi na kukagua uwezekano wa kujenga miradi mikubwa kwenye maeneo yenye vyanzo toshelevu vya maji.

Vikao hivyo vya Katibu Mkuu Wizara ya Maji na watumishi maarufu kama ‘zungumza na Katibu Mkuu,’ vinavyotoa fursa kwa watumishi kumueleza Katibu Mkuu na Menejimenti yake ya Wizara ya Maji jambo lolote linalowatatiza katika utendaji wa majukumu yao ili kupata ufumbuzi.


UBINGWA WA YANGA UMELETA MSHIKAMANO-WAZIRI MCHENGERWA

 



Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ameipongeza timu ya Yanga kwa kutwaa kombe la katika ligi Kuu ya NBC katika msimu huu.

Mhe. Mchengerwa  ameipongeza Klabu ya Yanga kwa kuchukua Ubingwa huo huku akipongeza mshikamano na furaha za mashabiki, ambazo wamezionyesha  wakati wa kukabidhiwa kombe hilo na mapokezi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

" Kwa aina ya shangwe za ubingwa zilizofanyika jana na leo ni sawa na zile za mataifa yaliyoendelea ya Ulaya. Hakika mpira wa miguu ni mchezo mkubwa na pendwa duniani ambao huwaunganisha watu pamoja na kuleta amani, mshikamano, furaha na umoja baina ya wananchi"

Ameongeza kuwa watanzania zaidi ya 90% ni wapenzi wa mchezo wa soka na amesisitiza kuwa serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha inaboresha miundombinu ya michezo na kuleta usawa katika michezo hasa mpira wa miguu ili  kila mtanzania aweze kupata furaha.
 
"Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa watanzania wanaendelea kupata furaha na faraja katika  michezo" amesisitiza Mhe . Mchengerwa

ADC YATOA NENO MCHAKATO WA KATIBA MPYA

 

KATIBU Mkuu wa Chama cha Aliance Demokratc Change (ADC) Doyo Hassan Doyo akizungumza na wananchi wa Kata ya Mabanda Jimbo la Handeni mjini
KATIBU Mkuu wa Chama cha Aliance Demokratc Change (ADC) Doyo Hassan Doyo kulia akigaiawa kadi kwa wanachama wapya waliojiunga na chama hicho mara baada ya kuzindua tawi hilo
KATIBU Mkuu wa Chama cha Aliance Demokratc Change (ADC) Doyo Hassan Doyo kulia akigaiawa kadi kwa wanachama wapya waliojiunga na chama hicho mara baada ya kuzindua tawi hilo
KATIBU Mkuu wa Chama cha Aliance Demokratc Change (ADC) Doyo Hassan Doyo kulia akigaiawa kadi kwa wanachama wapya waliojiunga na chama hicho mara baada ya kuzindua tawi hilo


 
KATIBU Mkuu wa Chama cha Aliance Demokratc Change (ADC) Doyo Hassan Doyo amesema suala la CCM kuzungumzia mchakato wa Katiba mpya kwamba imeridhia na wanasubiri Serikali ione namna gani linafufuliwa wamelipokea kwa mikono miwili.

Doyo aliyasema hayo leo mjini Handeni wakati akifungua Tawi Mtaa wa Mabanda Kata ya Mabanda Jimbo la Handeni Mjini  na kufanikiwa kupata wanachama zaidi ya 60 ambao walichukua kadi ya ADC  huku akiwashukuru wananchi kwa kukiunga mkono chama hicho .

Alisema hivi sasa wanasubiri Serikali iweze kuona namna gani jambo hilo linafufuliwa ili mchakato uanze huku akieleze wamelipokea kwa furaha japokuwa hawaamini kwamba CCM wana nia thabiti ya kujenga mifumo ya katiba ambayo watanzania wanaihitaji.

Alisema kutokana na wasiwasi huo wanaitaka Serikali ya CCM iweze kutoa tamko la haraka la kukubali huo mfumo na kwamba unaanza lini na mchakato wake utakuwaje kutokana na kwamba ni suala rahisi sana .

“Kwani sheria ya mabadiliko ya katiba imeshatungwa hivyo ni kuifufua tu na bunge bado linakaa na tunaamini kama Serikali ipo makini na suala ka katiba mpya na CCM imebariki hivyo itoa tamko haraka ni lini mchakato wa katiba mpya utaanza”Alisema Katibu Mkuu huyo.

Hata hivyo alisema suala la katiba mpya kwa watanzania ni muhimu sana na ndio maana wamekuwa wakilipigia kelele mara kwa mara ili kuhakikisha inapatikana.

Katika hatua nyengina Katibu huyo Mkuu aliwataka wananchi wa Kata hiyo kuhakikisha wanajitokea ,kwa wingi kuhesabiwa wakati wa zoezi la Sensa ya watu na Makazi linatalofanyika mwezi Agosti mwaka huu hapa nchini kutokana na kwamba ni tukio muhimu kwa nchi.