ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, December 17, 2021

DC MOYO: HAJARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA MADARASA TARAFA YA IDODI,ISIMAN NA PAWAGA

 

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiwa anakagua miradi ya majengo ya madarasa kwa ajili ya wanafunzi wanaotarajiwa kuingia kidato cha kwanza mwakani mwezi wa kwanza mwanzoni huku akiwa haridhishwi na kasi ya ujenzi wa madarasa ya fedha za UVIKO 19
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiwa anakagua miradi ya majengo ya madarasa kwa ajili ya wanafunzi wanaotarajiwa kuingia kidato cha kwanza mwakani mwezi wa kwanza mwanzoni huku akiwa haridhishwi na kasi ya ujenzi wa madarasa ya fedha za UVIKO 19
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo akiwa anakagua miradi ya majengo ya madarasa kwa ajili ya wanafunzi wanaotarajiwa kuingia kidato cha kwanza mwakani mwezi wa kwanza mwanzoni huku akiwa haridhishwi na kasi ya ujenzi wa madarasa ya fedha za UVIKO 19

 
 Na Fredy Mgunda,Iringa

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo ameonesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vinavyojengwa kupitia msaada wa fedha za Uviko 19 akionya kuchukua hatua dhidi wasimamizi wa ujenzi.

 

Akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba hivyo katika Tarafa ya Idodi na Isimani alisema Serikali haiko tayari kushuhudia wanafunzi wakishindwa kuanza masomo kwa wakati kutokana na changamoto ya vyumba vya madarasa

 

Moyo aliwaagiza maafisa Tarafa pamoja na Watendaji wa kata ya vijiji yanapojengwa Madarasa hayo kuhakikisha vyumba vyote vinakamilika kwa wakati na kukabidhiwa kwa Serikali ifikapo Desemba 30 mwaka huu.

 

Mohamed Hassan Moyo Mkuu wa Wilaya ya Iringa amefika Tarafa ya Idodi na kujionea hali halisi ya maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vinavyojengwa kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano ddidi ya Uviko-19

 

Alisema kuwa serikali imetoa kila kitu kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya wanafunzi wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwenzi wa kwanza mwaka 2022 hivyo madarasa yote ya wilaya ya Iringa yanatakiwa kukamilika kabla ya mwaka 2022 ili yatumike kwa wakati kama ilivyo kusudiwa na serikali.

 

Moyo alisema kuwa Serikali haiko tayari kuona madarasa hayo yakichelewa kukamilika na kuwaagiza wasimamizi wa ujenzi kuhakikisha yanakamilika kabla ya desemba 30.

 

Aliwahimiza maafisa watendaji kuwasilisha kwa mkurugenzi changamoto zilizo zinazowekza kukwamisha kasi ya ujenzi wa vyumba hivyo ili Ofisi ya Halmashauri iweze kuzipatia ufumbuzi wa haraka ili madarasa hayo yaweze kutumika kwa wakati kama ilivyokusudiwa

 

Katika hatua nyingine mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo alisema kwa zaidi ya asilimia themanini (80%) ya majengo ya madarasa yanayaojengwa katika Tarafa ya Idodi na Isimani yanaendelea vizuri licha ya changamoto ndogo ndogo ambazo zimejitokeza kwenye baadhi ya shule kwa usimamizi usiolizisha wa baadhi ya watendaji wake.

 

Katika Ziara hiyo ametembelea Tarafa ya Idodi katika Shule ya Sekondari Mlowa, Idodi, Makifu na shule shikizi ya Kitisi akiwaeleza kutorishwa na kasi ya ujenzi wakati katika tarafa ya Isimani alitembelea shule ya sekondari Furahia,Nyerere,Izazi,Isiman,Ilambilole na Kiwele na shule mbili shikizi katika Tarafa hiyo ambapo kwa kiasi kikubwa yamekamilika vikibakia vitu vidogo tu vya kumalizia.

 

Katika ziara hiyo ya kukagua ujenzi wa madarasa hayo wananchi wamekuwa wakimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suhuru Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuleta maendeleo ya nchi na kuwapunguzia ugumu wa maisha wananchi wake.

CHANJO, LISHE NA AFYA MAZINGIRA NDIYO INAIBEBA SEHEMU KUBWA YA SEKTA YA AFYA NCHINI - DKT. GWAJIMA

Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Afya nchini uliomalizika jijini Dodoma.

Watawa kutoka mkoani Arusha, wakikabidhiwa cheti cha Ushindi wa Afya Mazingira jijini Dodoma, na Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa siku ya Mwisho ya Mkutano wa Maafisa Afya nchini uliomalizika mkoani Dodoma

Na Atley Kuni, WAMJW, DODOMA

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema, Chanjo, Lishe na Afya Mazingira ni maeneo muhimu ambayo yanabeba sehemu kubwa ya sekta ya Afya kwa ujumla wake na endapo wakifanikiwa kwenye maeneo hayo basi yatatokea mapinduzi makubwa katika Sekta ya Afya.

Dkt. Gwajima, amesema hayo leo Desemba 17, 2021 wakati akifunga Mkutano Mkuu wa  Mwaka wa Maafisa Afya Mazingira uliomalizika Jijini Dodoma kwa siku tatu ukihusisha Maafisa Afya na Wadau mbalimbali wa ajenda ya Afya Mazingira kutoka kwenye Mikoa yote 26 nchini, Halmashauri 184. 

Dkt. Gwajima amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan inatoa kipaumbele cha kutosha kwenye eneo hili kwani inatambua kuwa ni eneo muhimu katika kuboresha afya za watanzania. Na kwa kuzingatia umuhimu mwaka wa fedha 2019/2020 serikali imetoa kiasi Shs.25, 628, 654,250 kwa ajili ya utekelezaji wa  programu endelevu ya maji na usafi wa mazingira na mwaka  2021/2022 imetoa Sh.28,467,204,790 kwa ajili  hiyo ambapo zimetumika kujenga miundombinu ya maji, vyoo na vichomea taka katika vituo 660 vya kutolea huduma za afya nchini.

Dkt. Gwajima amewapongeza Maafisa Afya kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya tangu kuzinduliwa kwa zoezi la uchanjaji wa Chanjo ya UVIKO 19 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. Amesema, Maafisa Afya Mazingira wameendelea kutekeleza jukumu husika kikamilifu kwa kutoa elimu ya afya na kuwezesha jamii kubadilika kifikra juu ya upotoshaji uliokuwa ukiendelea juu ya chanjo.

“Pamoja na kupata chanjo, tunahitaji pia kuimarisha kinga ya miili yetu kwa kupata lishe bora inayotokana na kula mlo kamili ikiambatana na mazoezi ya mwili ambayo ni msingi wa afya njema. Ili wananchi waendelee kupata chakula bora na salama, Maafisa Afya Mazingira mna jukumu kubwa la kusimamia hili kwa kuhakikisha ubora na usalama wa chakula unazingatiwa hasa katika maeneo yote yanayouza bidhaa za chakula na vinywaji,” amesema Dkt. Gwajima.

Dkt. Gwajima amesema tafiti zinaonesha kwamba, sehemu kubwa ya matatizo ya kiafya yanayoshughulika nayo ni yale ambayo yanaweza kuzuilika kwa njia ya usafi wa mazingira huku wakitolea mfano kuwa, wastani wa wagonjwa sita (6) wa nje (OPD) kati ya kumi (10) wanaohudhuria katika vituo vya kutolea huduma za Afya wengi wao wanasumbuliwa na magonjwa ambayo yanaweza kudhibitiwa kwa njia ya usafi wa mwili na mazingira. Hivyo, kwa namna yeyote ile lazima eneo hili liimarishwe ili kuleta tija ndani ya sekta.

Mkutano huo ambao ulikuwa umebebwa na kaulimbiu ya Imarisha Huduma za Afya Mazingira na Usafi katika Mapambano ya UVIKO-19, Dkt. Gwajima amesema, inaakisi manufaa mtambuka kwa Afya Mazingira katika kukabiliana na kuenea kwa  ugonjwa wa UVIKO-19. Ameongeza kwa kusema, Afya Mazingira ni eneo pana linalojumuisha matumizi ya vyoo bora; usalama wa chakula; usalama wa maji ya kunywa; udhibiti wa taka ngumu; udhibiti wa majitaka; udhibiti wa uchafuzi wa hewa; udhibiti wa wadudu wadhurifu; makazi bora; usafi wa mwili; udhibiti wa magonjwa yanayoenezwa Kimataifa; utupaji wa mabaki ya binadamu; udhibiti wa kemikali na afya mahali pakazi.

Katika Hafla hiyo Mhe. Gwajima ameitaja Mikoa Vinara kwa Usafi wa Mazingia kwa Mwaka 2021 kuwa ni Manyara iliyopata asilimia 97.6, ukifuatiwa na Katavi ulipata asilimia 82.9 na Mkoa wa tatu ni Dodoma ulipata asilimia 80.5. Dkt. Gwajima amekabidhi vyeti na tuzo mbalimbali kwa washindi. Aidha, kwa niaba ya seriakli ameahidi kuhakikisha kunakuwa na vikao vya kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa utekelezaji kwa njia ya mtandao kila baada ya miezi mitatu na kwa cha kwanza ni tarehe 30 Januari, 2021.

Awali akitoa taarifa rais wa Chama cha Maafisa Afya Mazingira Tanzania Twaha Mubarak ameishukuru Serikali na Wadau wa Maendeleo ambapo kupitia Taasisi ya Benjamini Mkapa kwa mwaka 2020/21 imewezesha ajira ya 171 za wataalamu wa afya mazingira na kupunguza uhaba kwa asilimia mbili.


MTOTO ALIYEZIKWA AONEKANA, KABURI LAKE LAFUKULIWA.

 


Mtoto Leonard Morisha (11), mkazi wa Kijiji cha Ngemo, Mbogwe mkoani Geita, aliyefariki dunia na kuzikwa Juni 27, 2017, anadaiwa kufufuka baada ya Oktoba 2020 kuonekana wilayani Kahama na wazazi wake wamempata Desemba 12, 2021 akiwa amekatwa mishipa ya ulimi na hawezi kuongea.


Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Henry Mwaibambe, amethibitisha kutokea tukio hilo baada ya kuomba kibali cha mahakama na kufanikiwa kufukua mahali alipokuwa amezikwa mtoto huyo na kukuta nguo ambazo amezikiwa zikiwa hazijachakaa pamoja na suruali ya aliyekuwa baba yake ambaye pia alifariki 2019.

SHIRIKA LA CIAT, TALIRI WAKAMILISHA UTAFITI WA MALISHO YA MIFUGO

 

Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la Utafiti la CIAT, Dkt. An Notenbaert (katikati) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Dkt. Vincent Anney (kulia) kalenda ya Shirika hilo ya mwaka 2022 muda mfupi baada ya Dkt. Vincent kufunga kikao cha uwasilishaji wa  taarifa ya utekelezaji wa mradi wa utafiti wa malisho yaliyoboreshwa kilichofanyika leo (15.12.2021) kwenye kumbi wa kituo cha Mafunzo cha wakulima kilichopo Tukuyu jijini Mbeya. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Angelo Mwilawa.

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dkt. Vincent Anney (kulia) akieleza namna anavyovutiwa na shughuli za ufugaji muda mfupi baada ya kuwasili nje ya Ukumbi wa kituo cha Mafunzo cha wakulima kilichopo Tukuyu jijini Mbeya leo (15.12.2021). Wengine pichani kutoka kulia ni Mtafiti Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Dkt. Jonas Kizima, Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la Utafiti la CIAT, Dkt. An Notenbaert, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Prof. Erick Komba, Kaimu Meneja wa TALIRI-Uyole Dkt. Edwin Chang’a na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Wizara ya Mifugo na Uvuvi) Dkt. Angelo Mwilawa.

Mfugaji kutoka kitongoji cha Itebe Wilayani Rungwe, Ezekia Kimanga (kulia) akitoa  zawadi kwa niaba ya wafugaji wote wa Wilaya ya Rungwe kwa Afisa Utafiti wa Shirika la kimataifa la utafiti la CIAT aliyekuwa akifanya kazi kwa upande wa Nyanda za juu kusini, Beatus Nzogela ikiwa ni ishara ya kutambua mchango uliotolewa na Shirika hilo kwa wafugaji wa kanda hiyo kwa kipindi cha miaka 4 ya utekelezaji wa mradi wa utafiti wa uzalishaji malisho ya mifugo  yaliyoboreshwa ambao leo (15.12.2021) ndio umefikia tamati.




Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la utafiti la CIAT leo (15.12.2021) wamewasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa utafiti wa malisho yaliyoboreshwa uliotekelezwa kwa miaka 4 katika kanda ya nyanda za juu kusini.

Mgeni rasmi katika kikao cha kuwasilisha taarifa hiyo  kilichofanyika kwenye Ukumbi wa kituo cha Mafunzo cha wakulima kilichopo Tukuyu jijini Mbeya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Dkt. Vincent Anney amezipongeza pande zote kwa hatua hiyo ambapo ametoa rai kwa watekelezaji wa matokeo ya utafiti huo kuhakikisha elimu na ujuzi uliopo kwenye taarifa hiyo unaenea kwa wafugaji wote nchini.

 “Ili tuwe na ufugaji wenye tija ni lazima utafiti unaombatana na majaribio ufanyike kama ambavyo mradi huu umefanya kwa kushirikiana na Serikali hivyo nashauri iundwe kamati maalum ya kufuatilia uendelezaji wa yote yaliyofanyika wakati wa mradi ili tutumie fursa tuliyoipata kusonga mbele badala ya kusubiri mradi mwingine” Amesema Dkt. Anney.

Dkt. Anney amebainisha kuwa mradi huo umewahamasisha wafugaji kuzalisha malisho ambayo yameleta tija na kuongeza  uzalishaji wa  mazao yanayotokana na mifugo  hivyo ametoa rai kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweka mipango madhubuti ya kutafuta masoko ya mazao hayo.

“ Uzalishaji mkubwa wa malisho yaliyoboreshwa unaofanywa na wafugaji wetu hivi sasa kupitia mradi huu umesababisha uzalishaji wa maziwa mengi hivyo wafugaji wameanza  kukosa soko la maziwa hayo na kwa sababu hawatumii nguvu kubwa kwenye kuyazalisha tofauti na ilivyokuwa awali wanaweza kuona hiyo hali ni ya kawaida kwa hiyo  ni lazima tuwasaidie ili maziwa hayo yawaletee tija ya kutosha” Amesisitiza Dkt. Anney.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Prof. Erick Komba mbali na kuonesha furaha ya kuhitimisha mradi huo kwa mafanikio  ameweka wazi  kuwa Taasisi yake ipo tayari kushirikiana na wadau wote wenye lengo la kuendeleza sekta ya mifugo nchini kama ilivyofanya na Shirika hilo.

“Mbali na utafiti wa malisho, Taasisi yetu pia inafanya utafiti katika vyakula vya mifugo na ulishaje wake, Uzalishaji, uzazi, afya ya mifugo na haki za wanyama ambapo ili kutekeleza shughuli zake Taasisi yetu inapata fedha kutoka Serikalini, vyanzo vyetu vya ndani na kupitia wadau wa maendeleo kama CIAT na wengineo” Ameongeza Prof. Komba.

Prof. Komba amesema kuwa hivi sasa Taasisi yake inaendelea na tafiti mbalimbali ikiwa ni pamoja na utafiti mpya unaolenga kutengeneza teknolojia na mtandao wa ushauri katika ubora wa maziwa ambao unafanyika katika kanda ya Mashariki ya Taasisi hiyo iliyopo mkoani Tanga, utafiti wa vyakula vya mifugo vinavyojumuisha michanganyiko ya bei rahisi  inayompa mnyama afya bora,

“Lakini pia tuna  majaribio mengi sana huko vituoni yanayohusu  uzalishaji  mifugo, matunzo ya mifugo, unenepeshaji, uchambuzi na kutathmini mifugo na mawe lishe katika eneo la ulaji na ukuaji wa mbuzi zoezi linaloendelea kwenye kituo chetu cha Kongwa” Amesema Prof. Komba.

Naye Mwakilishi wa Shirika la CIAT, Dkt. An Notenbaert ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano waliouonesha wakati wote wa kutekeleza mradi huo ambao pia ulilenga kufanya utafiti wa malisho bora kwa mifugo na kuandaa taarifa ya utafiti itakayotumiwa na watekelezaji wa Sera katika kuinua sekta ya mifugo nchini.

“Pia nitoe shukrani zangu kwa Shirika la IFARD kwa kukubali kutoa fedha za kutekeleza mradi huu hivyo iwaombe wafugaji na wazalishaji wa malisho ya mifugo nchini pamoja na mradi huu kufikia kikomo, waendelee kusambaza mbegu za malisho haya yaliyoboreshwa katika maeneo mengine yaliyosalia hapa nchini ili kila mfugaji anufaike na malisho haya” Amesema Dkt. Notenbaert.

Kwa upande wa mmoja wa wafugaji walionufaika kutokana na mradi huo kutoka mkoani Njombe, Juliana Mlagala amesema kuwa malisho hayo yaliyoboreshwa yamewaongezea ari ya kuendelea kufuga baada ya kuonesha matokeo chanya kwenye mifugo yao.

“Tangu tuanze kutumia malisho haya yaliyoboreshwa tumekuwa na uhakika wa chakula bora cha  mifugo yetu na tumeokoa muda mwingi sana ambao zamani tulikuwa tunaupoteza kwenda kutafuta malisho ya mifugo yetu  hivyo ninaomba Serikali iendelee kutuletea miradi ya aina hii ili tuendelee kunufaika kutokana na shughuli hizi za ufugaji” Amesema Mlagala.

Mradi wa Utafiti wa kilimo cha  malisho yaliyoboreshwa bila kuathiri mazingira umetekelezwa na Shirika  la kimataifa la Utafiti la CIAT kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Idara ya Mafunzo, Utafiti na Ugani kupitia taasisi yake ya TALIRI ambapo umetekelezwa kwa miaka 4 katika Halmashauri 3 ambazo ni Mufindi, Njombe na Rungwe.

MAAFISA AFYA ONDOENI UNYONGE, SIMAMIENI SHERIA – DKT. MAGEMBE


 Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya, Dkt. Grace Magembe, akifungua Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Afya jijini Dodoma

 Baadhi ya Maafisa Afya wakiwa wanamsikiliza Dkt. Grace Magembe, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, wakati wa hafla ya Ufungzi wa Mkutano wa Maafisa hao wa Mwaka.


 Anyitike Mwakitalima, Mkuu wa kitengo cha Chakula, Maji na Usafi wa Mazingira... Wizara ya Afya, akiongea wakati wa mkutano huo wa Mwaka
 Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Afya Mazingira na Usafi, Wizara ya Afya Dkt. Khalid Mansa, akitoa tathmini ya utekelezaji wa miaka minne kwenye masuala ya Afya Mazngira



Na Atley Kuni, WAMJW-DODOMA

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya, Dkt. Grace Magembe, amewataka Maafisa Afya mazingira, kote nchini kuondoa woga katika utekelezaji wa majukumu yao na badala yake, wasimamie sheria wanapotekeleza wajibu wao.

Magembe amesema, Suala la Utunzaji wa Mazingira ndio msingi wa Afya Bora kwa wananchi na ndio inasaidia jamii kuondokana na magonjwa mbalimbali ikiwepo kipindupindu ambacho chanzo chake kikuu ni ulaji wa kinyesi.

Dkt. Magembe ametoa kauli hiyo mapema leo Desemba 15, 2021 wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Afya Mazingira unaondelea jijini Dodoma ambao umeratibiwa na Wizara ya Afya kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Wadau wa Maendeleo.

“Hamtakiwi kuwa wanyonge mnapotekeleza wajibu wenu, mimi nikiwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, niliwahi kumng’ang’ania mtu aliyetupa uchafu kupitia dirisha la gari na alipo kaidi nilisimama kwenye msingi wa sheria hadi akapokea adhabu inayo mstahiki, hivyo lazima mjue dhamana mliyopewa ni kubwa ni vema mkaitendea haki”. Amesema Dkt. Magembe.

Awali akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Masuala ya mazingira nchini, Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Afya Mazingira na Usafi, Wizara ya Afya Dkt. Khalid Massa, amesema, kwa sasa hali ya watu kuwa na vyoo bora nchini imeongezeka kutoka asilimia 42 ya mwaka 2017 na kufikia asilimia asilimia 70 kwa mwaka 2021.

Dkt. Massa amesema mafanikio hayo yametokana na mikakati waliojiwekea hivyo kupunguza kaya zisizo kuwa na vyoo kutoka asilimia 9.6 hadi kufikia asilimia 1.3 kwa mwaka 2021.

Vilevile amesema vyombo vya kunawia mikono kwenye kaya vimeongezeka kutoka asilimia 5.6 ya mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 41.7 kwa mwaka 2021, lakini pia wameendelea kuchukua hatua za kulinda mipaka kwa kuwaajiri na kuwapeleka vijana wapatao 70 kwa ajili ya masuala ya Afya Mazingira mipakani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Maafisa Afya na Mazingira nchini Twaha Mubarak ameiomba Serikali, kuangalia utaratibu wa uteuzi wa Maafisa Afya hao, kwani kwa kipindi cha sasa hawaridhishwi na uteuzi wao kunafanywa na Mganga Mkuu wa Wilaya au wa Mkoa suala ambalo Dkt. Grace Magembe, aliyekuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo   ameahidi kulifanyia kazi.

Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Afya Mazingira wenye Kaulimbiu isemayo Uimarishaji wa huduma za Afya Mazingira na usafi katika mapambano ya Uviko -19 unafanyika jijini Dodoma, ukiwa na lengo la kujitathmini juu ya utendaji kazi wao na kuweka mikakati kwa ajili ya Mwaka ujao.  


MBARAWA 'AVURUGWA' MRADI WA BIL 11/-

 


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amemtaka mhandisi wa Jengo la abiria katika Uwanja wa ndege wa Mwanza kufika mara moja kurekebisha dosari katika mradi huo wa Sh bilioni 11 ambao ujenzi wake haujakidhi viwango vya kimataifa.


Vilevile ameita Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), kushirikiana na wataalamu kushauri namna gani ifanyike ili ujenzi ukidhi viwango vinavyotakiwa.


Prof. Mbarawa amesema hayo jijini Mwanza wakati alipofika kukagua ujenzi wajengo hilo unaoendelea ambao mpaka sasa umefikia asilimia 85.


Amesema hajaridhishwa na mradi huo ambapo amesisitiza kuwa mradi huo umekosa vigezo vya kimataifa vinavyosimamiwa na Shirika la Kimataifa la Anga (ICAO).


“Mwenye dhamana ya viwanja vya ndege sio Mkoa wala Halmashauri bali ni TAA, nashangaa kusikia hakuna mhandisi anayesimamia jengo hili kutoka kwao hivyo basi naagiza watoke Dar es Salaam waje kusimamia hili jengo ili tupate thamani ya fedha na viwango vinavyostahili, hatutaki kufanya makosa alafu badae tuje tulaumiane”, amesema Prof. Mbarawa.


Ameongeza kuwa majengo yanayostahili kujengwa katika viwanja vya ndege vya kimataifa ni tofauti na majengo mengine kwani yana viwango vyake vinavyostahili ambapo hapa havikufatwa.


“Tunatakiwa kujenga jengo liatakalodumu miaka 20 hadi 30 hatuwezi kujenga hivi hivi tu hapa tulipofikia wataalam waje waangalie nini kiboreshwe ili jengo likidhi mahitaji”, amesisitiza Prof. Mbarawa.


Aidha, Prof. Mbarawa ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha viwanjavingi vya ndege hapa nchini na hiki Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kinatarajiwa kuwa cha Kimataifa hivyo lazima fedha zinazotolewa thamani yake ionekane na kupitishwa kwa viwango vya Shirika la Kimataifa la Anga (ICAO).


“Sisi kama Serikali tutahakikisha fedha zinaletwa ila mwisho wa siku tunahitaji kuona thamani ya fedha na kila anayehusika asimame kwenye eneo lake”, amesema Prof. Mbarawa.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, ameeleza kuwa Mkoa imekwishaunda timu ya watalaam na tayari wameshaleta specification, michoro sahihi na kazi zinanedelea za kuboresha jengo hilo ili likidhi viwango vinavyostahili.

RAIS SAMIA AIHAKIKISHIA DUNIA KUSIMAMIA HAKI YA USAWA WA KIUCHUMI KWA WANAWAKE.

 


Na WAMJW, Dodoma 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameihakikishia Dunia kusimamia eneo la Haki ya Usawa wa kiuchumi kwa wanawake Tanzania ikiwa ni eneo la pili kati ya maeneo Sita ya kizazi chenye usawa. 


Mhe. Rais Samia ameyasema hayo wakati akizindua Kamati ya Kitaifa itakayoshauri nchi kuhusu utekelezaji wa ahadi za nchi kwenye Jukwaa la kizazi chenye usawa leo tarehe 16 Desemba, 2021 jijini Dodoma. 


Rais Samia amesema sehemu kubwa ya Dunia haijatoa nafasi ya kutumia asilimia 50 ya nguvu kazi ya Wanawake katika kuimarisha Maendeleo ya uchumi. 


Ameongeza kuwa wanawake bado ni waathirika wakubwa katika mabadiliko na athari za kiuchumi na kisiasa yanayoendelea katika maeneo mbalimbali na tafiti zinaonesha nguvu kazi hiyo ikitumika vizuri itachangia Dola za Kimarekani trilioni 28. 


Amesema, ni muda sasa wa kuzifanyia kazi kikamilifu sera, sheria na mipango inayowekwa na Serikali ya kuinua Hali ya uchumi ya kuleta ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla ili kuweza kufikia malengo hivyo ni lazima kuwe na usimamizi, uratibu utathmini na ufuatiliaji wa sera na utekelezaji wa mipango. 


"Baada ya miaka 20 tangu kutolewa kwa azimio la Beijing la kumkomboa mwanamke bado Serikali nyingi zimeshindwa kutekeleza sera ya kumuinua mwanamke kutokana vikwazo mbalimbali ikiwemo Afya, elimu, Mila kandamizi, mitaji, masoko, teknolojia na unyanyasaji wa aina mbalimbali" amesema Rais Samia. 


Aidha, amebainisha kuwa Serikali imeridhia na inatekeleza mikataba na maazimio ya kikanda na Kimataifa ikiwemo mkataba wa kutokomeza aina zote za ubaguzi Kwa wanawake wa mwaka 1978, azimio la Bejing la mwaka 1995 na mkataba wa Kimataifa wa haki za mtoto wa 1979. 


Awali, akitoa taarifa ya Kamati hiyo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alisema kuzinduliwa kwa Kamati hii kutasaidia kuimarisha na kuharakisha kasi ya shughuli zilizopangwa katika kutekeleza ahadi zilizotolewa kufikia kizazi chenye usawa.


Dkt. Gwajima amesema umuhimu wa eneo hili la Haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake ni mkubwa katika kuendeleza jitihada za Serikali  amabyo imedhamiria kwa dhati kuleta usawa wa kijinsia ambao ni msingi muhimu katika kuchochea Maendeleo ya Ustawi wa Jamii. 


"Jukwaa limeainisha maeneo sita ya utekelezaji ambayo yanakabili changamoto za Wanawake, ukatili wa kijinsia, haki na usawa wa kiuchumi, haki za uzazi, mabadiliko ya tabianchi, Teknolojia na ubunifu na uongozi" amesema Mhe. Gwajima 


Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt . John Jingu, alisema uzinduzi huu ni kuashiria cha nchi kutekeleza kwa vitendo ahadi alizozitoa Mhe. Rais kupitia Makamu wa Rais Dkt. Phillip Mpango katika Jukwaa la usawa wa kijinsia lililofanyika mwezi Juni mwaka huu Jijini Paris. 

MKURUGENZI SHIRIKA LA KIVULINI APONGEZA MAONO YA RAIS SAMIA.

 

Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Kitaifa itakayoshughulikia Utekelezaji wa Ahadi za Nchi kwenye Jukwaa la Kizazi chenye Usawa.

Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto KIVULINI la jijini Mwanza, ndugu Yassin Ally amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa ya kufikiria kuanzisha Wizara mpya itakayoshughulikia masuala ya jinsia, maendeleo ya jamii na wanawake tofauti na ilivyo sasa ambapo masuala hayo yanashughulikiwa na Wizara moja ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mkurugenzi huyo ametoa pongezi hizo Disemba 16, 2021 baada ya Rais Samia kuhitimisha hotuba yake aliyoitoa kwenye hafla ya uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Kitaifa itakayoshughulikia Utekelezaji wa Ahadi za Nchi kwenye Jukwaa la Kizazi chenye Usawa iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally.

Ndugu Ally amesema uamuzi wa Rais Samia una manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kuipunguzia mzito Wizara ya Afya na kuiongezea ufanisi kwenye utekelezaji wa majukumu yake huku pia ukiongeza ufanisi kwenye Wizara mpya itakayoshughulikia jinsia, maendeleo ya jamii na wanawake katika kusimamia Mipango, Sera na Bajeti.

Aidha ameongeza kuwa hatua hiyo pia itaimarisha Wizara hiyo mpya kuzisimamia vyema Halmashauri nchini ili kutenga bajeji kwa ajili ya utekelezaji wa mpango kazi wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya wadau wa maendeleo ya jamii, jinsia, wazee, wanawake na watoto.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Awali Rais Samia amesema uamuzi wake wa kuitenga Wizara ya Afya na Wizara itakayoshughulikia masuala ya jinsia, maendeleo na wanawake unalenga kuimarisha utekelezaji wa Sera na mipango ya Nchi huku pia ukiiondolea mzigo mzito Wizara ya Afya katika kupambana na majanga mbalimbali na kuboresha huduma za afya.

Amesema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa pamoja zinafanya kazi kubwa na nzuri na jitihada bado zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha kuwa yale yote yaliyoahidiwa yanatekelezwa vyema.
Wananchi na Viongozi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Kitaifa itakayoshughulikia Utekelezaji wa Ahadi za Nchi kwenye Jukwaa la Kizazi chenye Usawa. 

Hata hivyo Rais Samia amesema licha ya kazi nzuri pamoja na jitihada zinazofanywa na Wizara hizo bado malengo yaliyokusudiwa hayajafikiwa vyema hivyo maamuzi yake ni kuitenga Wizara ya Afya na Wizara nyingine itakayoshughulikia masuala ya Jinsia, Maendeleo na Wanawake katika Serikali ya Muungano wa Tanzania na kwamba atamshawishi pia Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi ili naye afanye mabadiliko kama hayo.

Thursday, December 16, 2021

#BREAKING: MALORI YAGONGANA USO KWA USO WAWILI WAFARIKI...

 

Watu wawili wamefariki katika ajali ya malori iliyotokea eneo la mkambarani barabara ya Morogoro - Dar es Salam nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro .

AWESO AMFUTA KAZI MKURUGENZI MAMLAKA YA MAJI MPANDA.

 


WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amemuondoa  katika Nafasi ya Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mpanda-Katavi Mikaya Gyimbi kwa kushindwa kutekeleza Majukumu yake kikamilifu na kwa weledi.


Aweso ametoa uamuzi huo baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa Tenki la maji na nyumba ya mlinzi iliopo halmashauri ya manispaa ya Mpanda mkoani Katavi na kubaini uzembe katika usimamizi wa mradi na thamani ya fedha iliyotumika.


Pia, Waziri Aweso ameagiza Mhandisi aliesaini mradi huu pamoja na mkandarasi aliyeutekeleza kufika mara moja kesho ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mpanda mkoani Katavi kwa hatua zaidi.

AFYA NA RAIS SAMIA.

 


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Njinsia Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima amempongeza Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa kwa Utashi wake wa kukusudia kuigawanya Wizara ya Afya amesema kuwa kutokana maagizo ya mkutano wa June 8 2021 jijini Dodoma Wizara zinazoshughulikia maswala ya Jinsia upande wa Tanzabnia Bara na Zanzibar ilianza kulifanyia kazi agizo kwa kuhakikisha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatimiza ahadi yake ya kuwa  kinara katika eneo la haki na usawa wa kiuchumi nchini ambapo wanawake na wanaume watakuwa na fursa na haki sawa katika kunufaika na uwezeshaji kiuchumi. 

Pamoja na kuzindua Kamati hii leo,  Wizara  pia imeweza kuratibu uandaliwaji wa Mpangokazi Jumuishi na Shirikishi  wa Taifa.





MMOJA AFARIKI KWA KUPIGWA NA RADI, 48 WAKOSA MAKAZI TANDAHIMBA.

 


Mtu mmoja amefariki baada ya kupigwa na radi huku wengine  48 wakikosa makazi katika kijiji cha Huruma kata ya Kwanyama wilayani Tandahimba baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kunyesha na kuezua paa za nyumba zao.


Akizungumza baada ya kufika katika kijiji hicho mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Patrick Sawala amesema  mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali imeleta madhara makubwa katika kijiji hicho.


Ameeleza kuwa Serikali imejipanga kuimarisha ulinzi wa wanachi hao na mali zao katika kipindi hiki ambacho wameanza kurekebisha makazi yao.


"Hili eneo limekuwa lilikumbwa na athari za mvua na upepo mara kwa mara mnatakiwa kuimarisha nyumba zenu. Tunatoa pole kwa wafiwa na kaya zote 48 zilizokutwa na madhara haya tutaimarisha ulinzi ili kihakikisha kuwa mnakuwa salama nyie na familia zenu," amesema Sawala.

Diwani wa kata hiyo Hamza Barakali amesema  amepokea taarifa hizo kwa masikitiko  kutokana na mvua hiyo kuleta maafa kwa mwananchi wake.


"Mvua ilinyesha kubwa na iliambatana na upepo mkali na kusababisha mtu mmoja kufikwa na umauti, naungana na  wananchi wa kata yangu nitasimamia mazishi na kuungana na wananchi wote ambao eneo lao limeathirika."


"Kwaweli inasikitisha nimepita kwenye nyumba zilizofikwa na madhara kweli nimetokwa na machozi sio jambo rahisi vyakula, malazi makazi yote yanahitajika  ili wananchi hawa waweze kirudi katika hali zao za kawaida," amesema Barakali

MARUFUKU KUWASHUSHA VYEO WAKUU WA SHULE - MHE. UMMY

 



SERIKALI imepiga marufuku tabia ya wakurugenzi wa halmashauri chini kuwashusha vyeo walimu wakuu wa shule  pindi shule zao zinapopata matokeo mabaya.


Marufuku hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, wakati akifungua mkutano wa wakuu wa  shule za sekondari nchini katika ukumbi wa  Mlimani City, Dar es Salaam.


Mkutano huo wa siku tatu umeratibiwa na Global Education Link (GEL) kwa kushirikiana na  Umoja wa Walimu Wakuu Shule za Sekondari (TAHOSSA).


 Mhe. Ummy alisema inashangaza kuona walimu wakuu wakishushwa vyeo holela na wakurugenzi kila shule inapofanya vibaya wakati mwalimu huyo hajawezeshwa.


“Walimu mmekuwa msaada mkubwa sana kwa maendeleo ya elimu lakini hii tabia ya kuwaonea kwa kuwashusha vyeo imeshamiri na siikubali. Sasa kuanzia sasa sitaki kusikia  tabia hii nitawalinda walimu wangu dhidi ya unyanyasaji wa mtu yeyote,” alisema Mhe. Ummy.


Mtoto anapofeli sio tatizo la Mwalimu tu kila mmoja wetu anajukumu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata matokeo bora mwalimu, mlezi/mzazi, jamii wote tunahusika sasa kwanini ahukumiwe Mkuu wa shule tu alihoji Mhe. Ummy.


Na Mkurugenzi unapomvua madaraka Mkuu wa shule je yeye ametekeleza majukumu yake amemuwezesha Mkuu wa shule hiyo ipasavyo; Naomba kwa pamoja tushirikiane katika kuboresha matokeo ya wanafunzi na sio kuadhibiwa mtu mmoja tu.

Tuesday, December 14, 2021

WIZARA YA AFYA NCHINI TANZANIA YAANZISHA MFUMO WA KUPOKEA MAONI KUBORESHA HUDUMA

 


Na.WAMJW....DODOMA 14/12/2021

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima ameanzisha utekelezaji wa mfumo wa kukusanya maoni toka kwa watendaji wa taasisi anazosimamia kuanzia makao makuu ya wizara idara zote mbili ya afya na maendeleo ya jamii. Mfumo huu una lengo la kuwa na utaratibu wa ndani wa watendaji kutoa maoni dhidi ya mifumo ya uendeshaji wa taasisi zao ili kuboresha kwa uendelevu mpango mkakati wa kuimarisha mifumo ya uendeshaji wa Taasisi anazosimamia kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa watumishi wa sekta hiyo.


Amebainisha hayo leo Tarehe 14 Desemba 2021 Jijini Dodoma katika ofisi za Wizara ya Afya jengo la Bima ya Afya na baadaye Mji wa Serikali Mtumba wakati akiendesha zoezi hilo la kikao maalumu cha Mtumishi Sema na Waziri wa Afya kwa Maoni na Maboresho Mahala pa Kazi. Akirejea hotuba yake aliporiti kama Waziri kwenye sekta hiyo Disemba, 2020 amesema ni kipindi cha mwaka mmoja sasa umepita hivyo ni sahihi kabisa kufanya tathmini rasmi na kusimika mfumo wa tathmini endelevu kwa ajili ya kuinua zaidi viwango vya ufanisi wa sekta.


Dkt. Gwajima amesema kuwa zikiwa zimebaki siku chache kukamilisha mwaka 2021 ameona vema kufanya tathmini hii ili kujipanga vema zaidi kwa kutumia uzoefu wa mwaka mmoja wa utekelezaji kwa lengo la kwenda kasi zaidi na kufikia matarajio ya wananchi kama ambavyo Mheshimiwa Rais anatarajia. Amesema, taasisi imara inajengwa kwa kujipima na kujitathmini kisha kuja na mpango wa pamoja ulioshirikishi katika wajibikaji wa pamoja uliojengwa kwenye mifumo imara zaidi iliyoshirikisha maoni na mtazamo wa pamoja. 


Dkt. Gwajima amesema Taasisi ya Afya inatakiwa kuwa kimbilio kwa wananchi wanaofika kupata huduma kwa kufanya kazi kwa bidii kujituma na kujitolea ili kuepuka changamoto mbalimbali ambazo hutokea kwa kukosa mifumo imara ya uendeshaji …." Ndugu watumishi hatua ya kwanza ya safari ya kwenda kwenye mfumo imara wa uwajibikaji wa pamoja inaanza na fikra ya pamoja kwamba ninalotamani mimi au sisi litokee liwe la wote. Amesema tusitake wateja tu ndiyo wafanye tathmini dhidi yetu bali hata sisi tufanyiane tathmini sisi kwa sisi kwa hoja na kwa nia njema ya kuboresha mifumo ya kiutendaji." Amesema Dkt Gwajima


Amesema kuwa tusioneane aibu katika utoaji wa maoni kwa kuwa hakuna aliye mkamilifu hata kama ni kiongozi wa ngazi ya juu anatakiwa kupata mrejesho na ushauri ili kuendelea kuboresha mifumo kwani sifa moja ya uongozi bora ni pamoja na ukweli, uwazi na ushirikishaji. hivyo watumishi wanatakiwa kuwa huru katika utoaji wa maoni kwani yatalindwa na kuthaminiwa na kufanyia kazi na mrejesho kutolewa na huu ndiyo utakuwa utaratibu wa maisha yetu mahala pa kazi (institutional culture). Watumishi wote kwa umoja wao waitikia wito huo ambapo, wametoa maoni yao kwa uhuru na kumkabidhi waziri wa afya.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amemshukuru Mhe. Waziri kwa utaratibu huo ambao amesema ni nadra katika taasisi kwa viongozi kupimana…"Ni jambo la kihistoria kuwa na utaratibu huu kwani utasaidia kuwajenga watumishi wote kuwa na mtazamo mmoja kuanzia ngazi ya uongozi, mara nyingi viongozi huwa hawafahamu hali halisi ya changamoto za watumishi wa chini yao" amesema Dkt. Jingu.

Naye Mganga Mkuu wa Serikali Dkt Sichalwe amemshukuru  Waziri wa Afya Dkt. Gwajima kwa ubunifu aliouanzisha, huku akiwataka Watumishi waliojitokeza kuitumia fursa hiyo kama sehemu ya maboresho ili kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

CCM YASHINDA UDIWANI MBARALI.

 

Picha na maktaba.

MSIMAMIZI wa Uchaguzi Jimbo la Mbarali, mkoani Mbeya, Missana Kwangura amemtangaza Furaha Chalamila kuwa diwani mteule wa Kata ya Ipwani baada ya kupita bila kupingwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Akitangaza matokeo hayo, Kwangura alisema Chalamila amepita bila kupingwa baada ya wagombea wenzake waliochukua fomu kujitoa kwenye uchaguzi huo.


Alisema waliochukua fomu za kugombea walikuwa wanne kutoka vyama vya CCM, CCK, UDP na ACT-Wazalendo na kwamba vyama viwili vilirejesha fomu ambavyo ni CCM na ACT-Wazalendo. Alisema Novemba 16, mwaka huu, mgombea wa ACT-Wazalendo alijitoa na alikwenda kuapa mahakamani.


“Sheria ya Uchaguzi kifungu cha 45 kidogo cha 2 kinasema kwamba, endapo mgombea atabaki mmoja katika kata, Msimamizi wa Uchaguzi atakubaliana na hali hiyo na atatoa taarifa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na kumjulisha mgombea kwa barua kuwa amechaguliwa, ila atatakiwa kutangazwa siku ambayo uchaguzi mdogo unafanyika kwa mujibu wa ratiba,” alisema.


Baada ya kukabidhiwa hati ya ushindi, Chalamila aliahidi kuwawakilisha vyema wananchi wa Kata ya Ipwani kwenye Baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya hiyo.


“Nakishukuru chama changu cha CCM kwa kuniamini, hawakukosea kunichagua, nitafanyakazi na nyinyi bega kwa bega kupitia sera na Ilani ya CCM kutatua changamoto zilizopo zikiwamo za barabara, maji, afya, umeme na ninawaahidi sitawaangusha,” alisema Chalamila. Katibu wa CCM Wilaya ya Mbarali, Clemence Mponzi alieleza kufarijika chama hicho kupata diwani mwingine katika halmashauri hiyo.


Alimtaka diwani huyo mteule avunje makundi na ashirikiane na wenzake waliokuwa kwenye kinyang’anyiro. Chalamila amechukua nafasi hiyo kutokana na aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Mahamud Banichuma Mlwale kufariki dunia Agosti 28, mwaka huu.

Koffi Olomidé afutiwa kosa la ubakaji lakini ahukumiwa kwa kuwazuilia wacheza densi.

 


Mahakama ya rufaa nchini Ufaransa imemuondolea mwanamuziki Koffi Olomidé kosa la unyanayasaji wa kingono, lakini ikamtia hatiani kwa kuwashikilia wanawake bila hiari yao.


Mahakama ilibatilisha uamuzi wa 2019 uliompata na hatia ya ubakaji wa mmoja wa wachezaji densi alipokuwa na umri wa miaka 15.


Lakini alipatikana na hatia ya kuwanyima wanawake uhuru wao katika jumba la kifahari huko Paris kati ya 2002 na 2006.


Atatumikia kifungo cha miezi 18 kilichoahirishwa kwa muda na kuwalipa fidia.


Mwendesha mashtaka ya umma alikuwa amependekeza ahukumiwe kifungo cha chini ya miaka minane.


Watuhumiwa wake "bila shaka hawakuridhishwa na hukumu ya unyanyasaji wa kingono kwa sababi kwa hili lilikuwa kitu cha muhimu zaidi ", alisema wakili David Desgranges ambaye alikuwa akiwawakilisha wanawake hao.


Mmoja wao alikuwa amedai kuwa aliwashambuliwa "katika mahoteli, wakati mwingine ndani ya gari... na katika studio za kurekodi muziki".


Mahakama mjini Versailles haikumpata na hatia ya unyanyasaji wa kingono, huku jaji akifutilia mbali shtaka la ubakaji kutokana na "kubadilika na wakati mwingine kukinzana" kwa ushahidi kutoka kwa waliomtuhumu.


Hata hivyo mahakama iligundua kuwa kitendo chake dhidi ya wanawake hao "kiliwanyima uhuru kwa kuwekwa chini ya uangalizi wa mara kwa mara " na washirika wake wawili ambao waliwazuilia kwenye chumba wakiwa wamefungwa nyuso zao.


Mbali na adhabu hiyo iliyosimamishwa aliamriwa kulipa faini ya euro 10,000-32,000 ($11,000-36,000) kwa kila mcheza densi.


Olomidé, ambaye jina lake halisi ni Antoine Agbepa Mumba, ni mmoja wa wanamuziki maarufu zaidi barani Afrika.


Msani huyo mwenye umri wa miaka 65 ni nyota mkubwa wa muziki wa rumba na soukous ambayo ni maarufu sana Afrika. Mojawapo ya vibao vilivyopendwa zaidi katika kazi yake ya muda mrefu ni Loi ya 1997.


Mwimbaji huyo amekabiliwa kisheria mara kadhaa hapo awali: