|
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Joseph Msukuma. |
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita kimemtaka
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Geita Bi. Irine Mwakalinga kujipima na kuona kama
anatosha kuwatumikia wananchi wa mji huo badala ya kutumia maamuzi ya ubabe na
kuwaburuza katika utekelezaji wa majukumu yake. MSIKILIZE KWA KUBOFYA PLAY.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM mkoani
humo Joseph Msukuma alipozungumza na waandishi wa habari juzi jijini Mwanza, alieleza
kuwa, Mkurugenzi Irene Mwakalinga amekuwa mwanzilishi wa kuibua migogoro kwa maamuzi
yake ya kibabe bila kuwahusisha wananchi na badala yake amekuwa akitoa maamuzi kwa
kisingizio cha utekelezaji wa sheria za Mipango Miji.
Msukuma alieleza kuwa kufatia uamuzi huo kupingwa na
wananchi na kuufikisha kwa viongozi wa CCM Mkoa wa Geita na kuchukua hatua ya
kuingilia kati kutaka kufahamu ukweli juu ya jambo hilo kulizua mjadala mkali
na kupelekea kuibuka mgogoro kwa muda wa siku 25 baina ya viongozi wa Chama
hicho na Mkurugenzi huyo pamoja na Mwenyekiti Halmashauri hiyo.
“Hivi karibuni wananchi ambao ni wafanyabiashara wa
mji wa Geita waliamuliwa kuondolea katika soko lililopo katikati mjini humo
kutokana na eneo hilo kudaiwa kupewa mwekezaji bila kuwahusisha wananchi jambo
lililozua mgogoro baina ya wananchi na mzabuni aliyefika kuanza ujenzi wa choo
kwenye eneo hilo, hali iliyopelekea wananchi kulalamika kwa viongozi wa CCM
Mkoa huo,”alieleza.
|
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Joseph Msukuma akizugumza na waandishi wa habari jijini Mwanza. |
Msukuma alieleza kwamba Mkurugenzi huyo amekuwa na
tabia ya kutoa maagizo hayo na kuamuru kuwaondoa wananchi waliokuwa wanafanya
shughuli za biashara katika baadhi ya masoko lilikwemo la katikati ya mji huo
hali iliyopelekea uongozi wa CCM Mkoa kumuomba Mkuu wa Mgoa wa Geita Said
Magalula kuitisha kikao cha pamoja kushirikisha wadau wote.
“Mkuu wa Mkoa Magalula alikubaliana na ombi la Chama
na jana aliitisha kikao hicho ambacho kiliwashirikisha viongozi wa Halmashauri,
CCM Mkoa na Wilaya, wananchi ambao ni wafanyabiashara wa soko hilo ili kujaribu kubaini
ukweli iwapo taratibu zilifuatwa na wananchi kuhusishwa juu ya ujenzi huo ikiwa
pia kupewa eneo mbadala la kufanyia shughuli zao,” alisema.
Kwa mujibu wa Msukuma wakati wa kikao hicho maelezo
kutoka pande mbili kati ya Halmashauri na wananchi zilisikilizwa kwa umakini na
Mkuu wa Mkoa na wajumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa huo, ambapo
wananchi walikubali kuupokea mradi huo lakini unatekelezwa eneo gani ndipo
kuliibua hoja ya malalamiko kutoka kwa wananchi.
Alieleza kuwa baada ya kelele za malalamiko ya
wananchi huku majibu yaliyotolewa na Mkurugenzi huyo yakionekana
kutojitosheleza hali iliyobainika kukiukwa kwa utaratibu mzima ikiwa ni pamoja
na utolewaji wa zabuni hiyo jambo ambalo, Mkuu wa mkoa alifikia uamuzi wa kutoa
amri ya kusitishwa haraka kwa ujenzi wa mradi huo unataraji kugharimu Sh.
Milioni 90.
“Tulikubaliana kwa pamoja kuwa choo hicho sasa
kijengwe eneo la awali lilipo jengo la zamani linalo milikiwa na halmashauri,
tumeafikiana na wadau wote kwenye kikao hicho, tunataraji maamuzi na
maagizo ya serikali ya mkoa yatafuatwa na kuwa mwisho wa mgogoro huo, kwa hili
nampongeza sana Magalula na Kamati yake pamoja na wananchi kuwa
waelewa,”alisema.
"Hebu pima hili Mkurugenzi mama Mwakalinga alianzisha tozo ambazo hazikuzingatia sheria, tozo ambazo hazikusainiwa na Waziri Mkuu, tozo zilizokuwa za aina yake kwa kuamrisha Misikiti, Makanisa, Shule kulipa tozo na kweli zilitekeleza na ushahidi tunao tulimpa hadi Waziri Mkuu, kama wadau hao wakirudi nyuma na kudai fedha zao hasara kwa nani? sasa ajitathimini kwa hayo kama anatosha basi aendelee na utekelezaji lakini kama hatoshi basi ajiweke kando kupisha wengine"
Aidha Msukuma amedai kuwa mnamo Mwaka 2012 Mkurugenzi huyo alitengeneza mitaro ile hali akijua kuwa barabara husika litakwenda kufanyiwa matengenezo makubwa hivyo itavunjwa, mitaro hiyo iliyogharimu zaidi ya milioni 115 ilipo kamilika tu baada ya mwezi mmoja ilivunjwa na serikali ikaingia hasara.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa mara kadhaa kupitia vikao mbalimbali wamekuwa wakimshauri Mkurugenzi huyo kuwa masuala yote ya maamuzi yanayohusu wananchi lazima akutane na wananchi wachangie maoni yao na wampe ushauri badala ya kukaa tu mezani bila utafiti na kutoa tamko.
"Ninadiriki kumwita mzigo kwa sababu moja, Mweshimiwa Waziri wa TAMISEMI alipokuja wananchi walimuonyesha eneo la Stendi, stendi ile ili chakachuliwa na waziri alitoa siku sitini iwe imerekebishwa lasivyo atakuja kumrekebisha yeye, alichokifanya nikurundika udongo ambao uko mpaka leo, sasa kama yeye hawezi tunaendeleaje sisi wanasiasa kuvumilia kuona Mawaziri wetu wakiitwa mizigo wakati mizigo tunayo huku" alisema Msukuma na kuongeza kwa kusema.
"Sasa sisi wawakilishi wa chama wasaidizi wa Mawaziri, wasaidizi wa Rais tunasema wale wote watakaojitathimini na kujiona kuwa mizigo kwa halmashauri zetu wajitathimini na kutafuta sehemu nyigine za kwenda"
Juhudi za kumpata Bi. Irene (Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita) kwaajili ya kutoa uamuzi na msimamo wake bado zinaendelea, kwani licha ya kupigiwa simu mara kadhaa simu yake iliita bila kupokelewa.