Tukio hilo lilitokea jana ijumaa majira ya asubuhi jirani na msikiti wa Shia katika eneo la makutano ya barabara ya Morogoro na mtaa wa Indira Ghandi.
Imefahamika kuwa jengo hilo linamilikiwa na mfanyabiashara mmoja wa jijini Dar es salaam Bw. ladha khimji kwa ubia na shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Aidha, harakati zaidi za uokoaji zilikuwa zikiendelea kufanywa na vikosi vya uokoaji.
Rais Jakaya kikwete alifika katika eneo latukio hilo majira ya saa 7:00 mchana hiyo jana akifuatana na mkewe Bi. Salma kikwete na kabla yake viongozi kadhaa wa serikali na makamanda wa polisi katika Kanda Maalum ya Dar es salaam walikuwa wameshafika kusaidia shughuli za uokoaji, miongoni mwao akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam aid Meck Sadick.
Baadhi ya mashuhuda walieleza kuwa mabaki ya jengo hilo yalionyesha kuwa mchanga ulikuwa mwingi mno kulinganisha na saruji, hali inayodhaniwa kuwa ni moja ya sababu za kuporomoka kwa jengo hilo lililogharimu mamilioni ya pesa.
Hivi karibuni Waziri wa Ujenzi aliiagiza Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji wa Majenzi (AQRB) kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia sheria kwa kutanguliza uzalendo na kuepuka kufanya kazi kwa misingi ya rushwa.
Akifungua kikao cha siku mbili cha bodi hiyo majuzi katika ukumbi wa Chuo cha Benki kuu ya Tanzania Tawi la Mwanza, Dr. Magufuli aliwaeleza wataalamu na wajumbe wa kikao hicho kwamba wanayo dhamana kubwa ya kutekeleza majukumu ya taaluma yao kwa kuzingatia maadili, sheria, wajibu na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Dr. Magufuli alisema kwamba kuporomoka kwa baadhi ya magorofa katika sehemu mbalimbali hapa nchini ni ushahidi tosha kuwa ujenzi wa majengo unakiuka utaratibu na alisisitiza wataalamu hao kuwa makini katika utendaji wa kazi zao.
Aidha magufuli ameitaka AQRB kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria wataalamu watakaohusika na usimamizi na ukadiriaji mbovu na majengo yatakayoporomoka muda mfupi baada ya kujengwa au kuwa chini ya kiwango.
Kwa upande mwingine waziri huyo amewataka wataalamu hao kupanua wigo wa majukumu yao nakuanza kukagua miradi ya barabara katika halmashauri za majiji, manispaa na wilaya na kutoa taarifa serikalini kwa lengo la kuhakikisha kuwa miradi hiyo ina thamani ya fedha kama ilivyokusudiwa.