ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, August 8, 2025

WANAHABARI KANDA YA ZIWA WAJENGEWA UWEZO KUHUSU URIPOTI WA UCHAGUZI MKUU 2025

 



Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, pamoja na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), imeendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari na watangazaji kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Mafunzo hayo yaliyofanyika leo, Agosti 7, 2025, katika ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu (BoT) jijini Mwanza, yamewakutanisha zaidi ya washiriki 120 kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Kigoma, Mara na Kagera.


Lengo kuu la mafunzo ni kuwawezesha wanahabari kuripoti masuala ya uchaguzi kwa weledi, usahihi na kwa kuzingatia maadili ya taaluma, huku wakishiriki kulinda amani na mshikamano wa taifa.

Miongoni mwa mada zilizowasilishwa ni:

- Uandishi wa habari za uchaguzi kwa usawa na maadili

- Matumizi salama ya mitandao ya kijamii na teknolojia ya Akili Bandia (AI)

- Usalama wa wanahabari wakati wa uchaguzi

- Ulinzi wa taarifa binafsi

- Namna ya kuripoti migogoro na majanga bila kuchochea hofu

Semina hiyo pia ilihusisha wawakilishi kutoka Jeshi la Polisi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (SJMC), Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, na wadau wengine wa sekta ya habari.

Washiriki wamehimizwa kuandika kwa ukweli na usawa kwa vyama vyote, na kusaidia kudumisha amani ya taifa. Hii ni sehemu ya mikakati ya serikali kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na ufanisi, huku vyombo vya habari vikicheza nafasi yao muhimu ya kuelimisha umma.

Mada ya kwanza imewasilishwa na Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ikieleza kwa kina namna wanahabari wanavyopaswa kuandika habari za uchaguzi kwa kuzingatia kanuni za kitaaluma, ukamilifu wa taarifa, usawa kwa vyama vya siasa, pamoja na kulinda amani na mshikamano wa kitaifa.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewasilisha mada kuhusu Kanuni za Utangazaji wa Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa za mwaka 2020, ikifafanua masharti ya utoaji wa muda wa matangazo yanayohusu shughuli za uchaguzi, usimamizi wa maudhui ya kampeni na wajibu wa watoa huduma za utangazaji kuhakikisha usawa, uadilifu na uwazi katika kuripoti shughuli za uchaguzi.
Jeshi la Polisi kupitia mwakilishi wake Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini DCP David Misime, limewasilisha mada kuhusu wajibu wa wanahabari na vyombo vya dola katika kulinda usalama kipindi cha uchaguzi. Washiriki walifahamishwa kuhusu umuhimu wa ushirikiano baina ya pande hizo mbili katika kuripoti matukio ya kiusalama kwa njia salama, yenye kuzingatia taratibu za kisheria na za kiusalama.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imewasilisha mada kuhusu maadili na sheria zinazowaongoza waandishi wa habari nchini, ikiangazia wajibu wa waandishi kuhakikisha taarifa zao hazivunji sheria, hazichochei chuki au vurugu na zinazingatia haki za watu wanaotajwa katika taarifa za habari.
Wataalamu wa maudhui ya utangazaji na habari kutoka Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC-UDSM), wamewasilisha mada kuhusu Mitandao ya Kijamii na Akili Bandia (AI) kuelekea Uchaguzi, iliyoeleza jinsi mitandao ya kijamii na teknolojia ya Akili Bandia (AI) inavyobadilisha mienendo ya uchaguzi, pamoja na changamoto za usambazaji wa taarifa potofu na athari zake kwa amani ya nchi. Waandishi walihimizwa kuwa makini na matumizi ya vyanzo vya kidijitali na kuhakikisha uthibitisho wa taarifa kabla ya kuchapisha.

TCRA imewasilisha pia mada kuhusu namna bora ya kuripoti migogoro na majanga wakati wa uchaguzi, kwa kuzingatia weledi, lugha inayotumika, na athari za taarifa hizo kwa umma. Washiriki walikumbushwa kuepuka kueneza hofu au taarifa zenye kuchochea hisia za uhasama.

Kwa upande wake Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ikiwasilishwa na Mkuu wa Mawasiliano Serikalini Innocent Mungy, imewasilisha mada kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa za watu binafsi katika kipindi cha uchaguzi, hasa wakati wa ukusanyaji, uchakataji na usambazaji wa taarifa zinazomhusu mtu mmoja mmoja. Waandishi walihimizwa kufuata misingi ya faragha na ulinzi wa taarifa katika kazi zao za kila siku.

Mafunzo haya yamelenga kuongeza uelewa wa pamoja baina ya wanahabari, watangazaji, vyombo vya dola na taasisi za uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, haki na ufanisi. Aidha, yamebainisha umuhimu wa teknolojia na matumizi yake sahihi katika kuripoti uchaguzi katika enzi ya kidijitali.


PICHA RAIS SAMIA KATIKA MAONESHO YA NANE NANE JIJINI DODOMA.

 

Hivi ndivyo Rais Samia Suluhu Hassan alivyo wasili katika viwanja vya Nane Nane - Nzuguni Dodoma, kwa ajili ya kushiriki kilele cha maadhimisho ya maonesho ya kilimo, mifugo na uvuvi kitaifa na kimataifa.
Maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kuonesha teknolojia, ubunifu na fursa mbalimbali katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, yakilenga kuongeza tija na ustawi wa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan leo tarehe 08, Agosti 2025   kwenye kilele cha Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea Jijini Dodoma  pamoja na mambo mengine pia ametembelea baadhi ya Mabanda na kujionea shughuli mbalimbali zinazoendelea viwanjani hapo.

Akizungumza Jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema kwa mara ya kwanza Maonesho ya Nanenane mwaka huu yamewakutanisha Watu kutoka Mataifa 26 Duniani na kuongeza kuwa maonesho hayo katika Nchi nzima yatakuwa na ubora uleule.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitembelea mabanda ya Maonesho ya Nanenane kujionea shughuli mbalimbali zinazoendelea katika viwanja vya Nanenane vilivyopo Nzuguni Jijini Dodoma tarehe 08 Agosti, 2025.

Matukio mbalimbali kwenye Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma tarehe 08 Agosti, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo baada ya kuzindua Maabara Kuu ya Kisasa ya Kilimo iliyopo Mtumba, Jijini Dodoma, tarehe 08 Agosti, 2025.






RADI YAUA WATOTO WAWILI, BIBI AKIJERUHIWA.


 Watoto wawili wa familia moja wamefariki dunia na bibi yao kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi katika Mtaa wa Bulola ‘A’, Kata ya Buswelu, wilayani Ilemela mkoani Mwanza.


Tukio hilo lilitokea jana Agosti 7, 2025 saa 7:30 mchana wakati mvua iliyoambatana na upepo na ngurumo kubwa ilipoanza kunyesha.

Hali hiyo ikitokea, Grace Kateti (52), ambaye ni mjasiriamali na mkazi wa Bulola, alikuwa akipika chakula cha mchana chini ya mti jirani na nyumba yao akiwa na wajukuu zake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amethibitisha vifo vya watoto hao Mwasi Michael (11), ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano na Charles Michael (6), mwanafunzi wa darasa la pili. Walikuwa wakisoma katika Shule ya Msingi Bulola.

Kamanda Mutafungwa amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure.

Amesema Grace, ambaye ni bibi wa watoto hao alijeruhiwa na anaendelea na matibabu katika Kituo cha Afya Buzuruga.

Thursday, August 7, 2025

WAZIRI GWAJIMA AZINDUA KAMPENI YA 'BADILIKA, TOKOMEZA UKATILI'

 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amezindua rasmi kampeni ya 'Badilika, Tokomeza Ukatili' itakayotekelezwa kwa miaka miwili 2025/27 mkoani Kigoma.

Akizindua kampeni hiyo iliyoandaliwa na shirika la maendeleo la nchini Ubelgini ENABEL katika uwanja wa Mwanga Centre mkoani Kigoma Jumatatu Julai 28, 2025, Waziri Dkt. Gwajima ametoa wito kwa jamii kubadili tabia, mitazamo na mienendo inayochochea ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Amesisitiza kuwa kila mwananchi anapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko huku akijiunga mwenyewe kama balozi wa mabadiliko na Kampeni ikilenga kuvuna mabalozi 150,000 katika mkoa huo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msukumo mkubwa katika kutokomeza ukatili kupitia sera madhubuti na mikakati ya kitaifa kama Sera ya Taifa ya Jinsia ya mwaka 2023 na Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II).

Aidha Waziri Dkt. Gwajima amelipongeza Shirika la ENABEL kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine ikiwemo shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI katika mapambano dhidi ya ukatili.

Ameongeza kuwa jitihada hizo zimesaidia kuwawezesha wanawake na wasichana kupitia miradi ya maendeleo kama vile mradi wa “Wezesha Binti” unaotekelezwa mkoani Kigoma na hivyo kuwa mfano bora wa namna vijana wa kike wanavyopatiwa elimu, ujuzi na fursa za ajira.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ubelgiji ENABEL, Koen Goekint ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano mkubwa na namna ilivyopokea kampeni hiyo huku akihaidi ushirikiano zaidi katika juhudi za kutokomeza ukatili wa kijinsia, kulinda usawa wa kijamii na kuwezesha wanawake kiuchumi na kijamii.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Michael Ngayanila amesema kupitia kampeni hiyo watahakikisha wanaifikia jamii ili kuhakikisha kila mmoja anakuwa anachukua hatua za kuzuia ukatili kabla haujatokea.

Akiongoza mdahalo wakati wa ufunguzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI, Yassin Ally amesema jitihada zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia na wadau wa maendeleo zimesaidia ukatili wa kijinsia kupungua mkoani Kigoma kutoka asilimia 61 mwaka 2016 hadi asilimia 34 mwaka 2025 huku mimba za utotoni zikipungua kutoka asilimia 32 hadi asilia 17.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akiwa na viongozi mbalimbali wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Badilika, Tokomeza Ukatili mkoani Kigoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza wakati wa uzinduzi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Michael Ngayanila akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, Simon Siro.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ubelgiji ENABEL, Koen Goekint akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Badilika, Tokomeza Ukatili inayotekelezwa mkoani Kigoma.
Meneja Mradi wa Wezesha Binti unaotekelezwa na shirika la ENABEL, Christine Rankote akitoa maelezo kuhusu mradi huo ambapo amesema lengo ni kuwafikia wanamabadiliko 150,000 hadi kufikia mwaka 2025 ambapo kila mmoja anatarajia kuwafikia wananchi watatu na hivyo jumla ya wanufaika wa mradi kuwa 450,000.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI, Yassin Ally (kulia) akiongoza mdahalo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Badilika, Tokomeza Ukatili mkoani Kigoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima (mwenye kofia) akiwasili uwanja wa Mwanga Centre mkoani Kigoma kuzindua kampeni ya Badilika, Tokomeza Ukatili.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI, Yassin Ally (mwenye kofia) akiwa na wananchi wakifurahia uzinduzi wa kampeni ya Badilika, Tokomeza Ukatili.
Wadau mbalimbali wakiwa na mabango yenye kuhamasisha jamii kutokomeza ukatili.
Wadau wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Tazama video hapa chini

HOSPITALI YA BUGANDO YATOA ELIMU YA UNYONYESHAJI KWA AKINAMAMA.

 

Hospitali ya Kanda Bugando ya jijini Mwanza imetoa elimu kwa akina mama kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji maziwa ya mama ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama Duniani inayoadhimishwa kuanzia tarehe 01- 07 Agosti 2025.

Akizungumza Jumatano Agosti 06, 2025 wakati wa utoaji elimu hiyo, Daktari Bingwa wa Watoto Hospitali ya Bugando- Dkt. Florentina Mashuda amesema maziwa ya mama yana virutubisho kamili hivyo mzazi anapaswa kumnyonyesha mtoto maziwa pekee kwa miezi sita bila kumpa lishe yoyote ikiwemo maji.

Amesema baada ya miezi sita, mama anaweza kumuandalia mtoto chakula laini huku akiendelea kumnyonyesha kwa hadi atakapofikisha umri wa miaka kuanzia miaka miwili hadi mitatu kwa ukuaji wa afya ya mtoto kimwili na kiakili.

"Maziwa ya mama yana virutubisho vyote pamoja na kinga ya mwili ambayo inasaidia kumkinga mtoto na magonjwa mbalimbali ikiwemo nimonia na kuharisha" alisema Dkt. Mashuda.

Pia Dkt. Mashuda ameongeza kuwa kumnyonyesha mtoto kuna faida kwa akina mama ikiwemo kuepuka hatari ya kupata magonjwa ya saratani ya matiti pamoja na kusaidia kurudisha kizazi kwenye hali yake ya kawaida baada ya kujifungua.

Mmoja wa wazazi waliopata elimu hiyo, Happyness Samwel amesema yatawasaidia kuwalea vyema watoto wao hasa kuzingatia unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya awali na kwamba watafikisha elimu hiyo katika jamii inayowazungumza.

Kaulimu mbiu ya ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama duniani mwaka huu 2025 ni, "thamini unyonyeshaji: weka mazingira wezeshi kwa mama na mtoto".
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Daktari Bingwa wa Watoto Hospitali ya Bugando- Dkt. Florentina Mashuda akitoa elimu ya unyonyeshaji kwa akina mama waliojifungua hospitalini hapo.
Muuguzi Hospitali ya Kanda Bugando, Elia Woiso akizungumza na akina mama waliojifungua wakati wa utoaji elimu ya unyonyeshaji kwa akina mama hao.
Daktari Bingwa wa Watoto Hospitali ya Bugando- Dkt. Florentina Mashuda akitoa elimu ya unyonyeshaji maziwa ya mama kwa akina mama waliojifungua hospitalini hapo.
Picha ya pamoja baada ya elimu ya unyonyeshaji maziwa ya mama.
Tazama Video hapa chini

Wednesday, August 6, 2025

ALIYEKUWA SPIKA WA ZAMANI BUNGE LA TANZANIA, JOB NDUGAI AFARIKI DUNIA.

 


Aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania na Mbunge wa Kongwa, Job Yustino Ndugai amefariki Dunia leo August 06,2025 akiwa anaendelea kupatiwa matibabu 
Hospitalini baada ya kuugua ghafla.

Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt Tulia Ackson amesema kifo cha Ndugai kimetokea hii leo jijini Dodoma. Sababu ya kifo chake haijaelezwa.

Mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.

"Kwa masikitiko makubwa, naomba kutoa taarifa ya kifo cha kiongozi wetu, mwanasiasa mkongwe na Spika Mstaafu wa Bunge Mheshimiwa Job Yustino Ndugai kilichotokea leo jijini Dodoma. Natoa pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Kongwa, Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu," alisema Tulia.

Spika mstaafu Ndugai kabla ya kifo chake aliibuka mshindi katika kura za maoni, kuwania ubunge katika jimbo la Kongwa mkoani Dodoma katikati mwa Tanzania, zilizopigwa hivi karibuni.

Ndugai alihudumu katika nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania kwa miaka 6, kuanzia mwishoni mwa 2015 hadi alipojiuzulu Januari, 2022.

Kabla ya hapo alihudumu kama Naibu Spika kati ya Novemba, 2010 Na Novemba, 2015.

Pamoja na kuwa mahiri kwa kuzifahamu vema kanuni za Bunge, aliwahi kukosolewa kwa kutoa kauli tata ikiwemo kusema alikuwa na uwezo wa kumzuia mbunge yeyote asizungumze kabisa bungeni.

Pia aliwahi kukosolewa kwa kusema aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli angelazimishwa kuendelea kugombea urais baada ya kumalizika vipindi viwili vinavyoruhusiwa kikatiba ”atake asitake”.


WABUNGE WA CCM 'WALIOANGUKA' KURA ZA WAJUMBE.


Katika kile kinachoonekana kama mabadiliko ya upepo wa kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wabunge kadhaa waliokuwa wakitetea nafasi zao wamejikuta wakitemwa na wajumbe wa chama hicho katika kura za maoni zilizofanyika Agosti 4, 2025, katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Ingawa matumaini yao ya kurejea kwenye kinyang'anyiro cha Uchaguzi Mkuu bado yapo mikononi mwa vikao vya juu vya CCM, uamuzi wa wajumbe unaonesha wazi kuwa baadhi ya majina makubwa huenda yakasalia kuwa historia.

Kada wa siku nyingi wa CCM na Waziri wa zamani, Hamis Kigwangala ameanguka katika jimbo la Nzega Vijijini baada ya kushika nafasi ya pili kwa kupata kura 1,715. Neto Kapalata ameongoza kwa kupata kura 2,570, nafasi ya tatu imekwenda kwa robert masegere aliyepata kura 1,635.s

Katika Jimbo la Vunjo, Dr. Charles Kimei ambaye amekuwa mbunge tangu 2020 ameangushwa na Enock Zadock Koola aliyeibuka mshindi kwa kura 1,999 dhidi ya Kimei aliyepata kura 861. Hii ni mara ya pili kwa Koola kushinda kura za maoni katika jimbo hilo, baada ya kufanya hivyo pia mwaka 2020, ingawa hakupitishwa.

Katika Jimbo la Iringa Mjini, aliyekuwa mbunge Jesca Msambatavangu amejikuta nafasi ya nne kwa kura 408. Mshindi wa kura hizo ni Fadhil Ngajilo aliyepata kura 1,899, akifuatiwa na Wakili Moses (1,523) na Mchungaji Peter Msigwa (477).

Kyerwa, Mbunge Innocent Bilakwate ameangushwa na Khalid Nsekela aliyezoa kura 5,693 sawa na asilimia 71 huku Bilakwate akipata kura 1,567.

Katika Jimbom la Makambako, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Daniel Chongolo ameibuka mshindi wa kishindo kwa kura 6,151, na kumwacha mbali Deo Sanga (maarufu kama Jah People), aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 15, ambaye alipata kura 470 tu sawa na asilimia 7.1.

Tabora Mjini, Shabani Mrutu ameongoza kwa kura 6,612, akimshinda kwa mbali aliyekuwa mbunge Emmanuel Mwakasaka aliyepata kura 228 pekee. Mwakasaka alizidiwa hata na wapinzani wengine kama Hawa Mwaifunga (326) na Kisamba Tambwe (395).

Geita Mjini, Constantine Kanyasu ambaye amehudumu kwa miaka 10, amepata kura 2,097 na kushindwa na Chacha Wambura aliyepata kura 2,145. Upendo Peneza alipata kura 1,272 na wengine waliambulia makumi ya kura.

Kwa Jimbo jipya la Katoro, aliyekuwa Mbunge wa Busanda, Tumaini Magesa, alihamia huko lakini akashika nafasi ya tatu kwa kura 1,265 nyuma ya Kija Ntemi (2,134) na Ester James (2,075).

Katika jimbo la Namtumbo, aliyekuwa Mbunge Vita Kawawa ameshindwa mbele ya Dkt. Juma Zuberi Homera, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Homera alipata kura 11,836 asilimia 92 huku Kawawa akipata kura 852.

Mtwara Mjini, Joel Arthur Nanauka ameibuka mshindi kwa kura 2,045 dhidi ya Hassan Mtenga Mbunge anayemaliza muda wake aliyepata kura 1,607.s

Katika Jimbo la Lindi Mjini, Mbunge anayemaliza muda wake, Hamida Abdalla, ameangushwa na Mohamed Utali, aliyeibuka kidedea kwa kupata kura 1,474 kati ya kura 3,289 zilizopigwa. Hamida alipata kura 876 pekee, ishara ya wazi kuwa wajumbe wameamua kubadili mwelekeo wa uongozi katika eneo hilo.

Nyasa, hali haikuwa tofauti aliyekuwa Mbunge na Naibu Waziri wa zamani, Stella Manyanya, ameangushwa kwa kishindo na John Nchimbi, aliyepata kura 9,157 kati ya kura 10,695 zilizopigwa. Manyanya alipata kura 548 tu, matokeo ambayo ni pigo kubwa kwa mbunge huyo mkongwe aliyedumu kwa vipindi kadhaa ndani ya Bunge.

Katika Jimbo la Muleba Kaskazini, Adonis Bitegeko ameibuka mshindi kwenye kura za maoni za CCM kwa kumbwaga aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Mbunge wa muda mrefu, Dkt. Charles Mwijage. Ushindi huo umeweka historia mpya katika jimbo hilo, na kuongeza idadi ya vigogo waliotemwa kwenye mchakato wa ndani wa chama.

Haya ni baadhi ya majina ya wabunge walioshindwa kura za maoni. Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa kwenye vikao vya juu vya CCM, ambavyo vina mamlaka ya mwisho ya kuidhinisha majina ya wagombea.

Hata hivyo, uamuzi wa wajumbe umetuma ujumbe mzito kwamba mabadiliko yanahitajika, na sura mpya zinaungwa mkono. Kwa waliokuwa wabunge waliokataliwa na wanachama wao, matumaini pekee yaliyobaki ni uamuzi wa huruma kutoka juu kama utakuwepo.

Je, vikao vya juu vitarejesha majina yaliyokataliwa na msingi wa chama, au vitaacha sauti ya wajumbe iwe sauti ya wananchi? Macho na masikio sasa yako Dodoma.

KILOSA WAMSHUKURU RAIS SAMIA KUWAFIKISHIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

 

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu akimkabidhi Jiko banifu Mkazi wa Kilosa, Aneth Mseti Agosti 06, 2025 wakati wa uzinduzi wa mradi wa usambazaji wa majiko hayo kwa bei ya ruzuku ya shilingi 14,700 kwa jiko wilayani humo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage.

📌Wajitokeza kwa wingi kujipatia majiko banifu ya ruzuku

📌Wampongeza kwa kujali wananchi wake

📌Wasema ametatua adha iliyowasumbua kwa muda mrefu ya upatikanaji wa majiko banifu

 

Wananchi Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wameshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwafikishia mradi unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wa kusambaza majiko yaliyoboreshwa maarufu kama majiko banifu kwa bei ya ruzuku ya shilingi 14,700 kwa kila jiko.

Wametoa shukrani hizo Agosti 6, 2025 wakati wa uzinduzi wa mradi shilingi 9,400,799,626.7 wa kusambaza majiko banifu ambayo yatasambazwa kote nchini kwa bei ya ruzuku uliyofanyikia eneo la Stendi wilayani humo ambapo Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaka Hamdu akiwa mgeni rasmi.


“Rais Samia ni mkombozi wetu, sisi wajasiriamali ametusaidia sana, kwanza alituletea majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku na sasa tumepokea majiko haya banifu ambayo nayo yanakwenda kuwa msaada mkubwa kwa shughuli zetu za kila siku,” alisema Daines Samwel ambaye ni mjasiriamali eneo la Stendi ya Kilosa.

Naye Aisha Swai, mkazi wa Uhindini wilayani humo alisema majiko haya yanakwenda kupunguza gharama za maisha kwani hapo awali alikuwa akitumia zaidi ya shilingi 20,000 kununua mkaa kwaajili ya shughuli zake siku za mama lishe na kwamba kutokana na sifa ya majiko hayo ya kutumia mkaa mchache itamsaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa shughuli zake.


Akizindua mradi, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu alisema Wilaya ya Kilosa ni mnufaika mkubwa wa miradi inayosimamiwa na REA na aliipongeza kwa kuendelea kutekeleza na kusimamia maono na maelekezo ya Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo ya usambazaji wa umeme na usambazaji wa nishati safi ya kupikia.

“Kwa hapa Kilosa, tunashukuru sana, vijiji vyote vimefikishiwa umeme na kazi inaendelea ya kufikisha umeme kwenye vitongoji; leo hii tupo hapa kuzindua mradi mkubwa wa zaidi ya shilingi bilioni tisa wa majiko banifu yanayotolewa kwa bei ya ruzuku,” alisema Hamdu.



Alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia mradi huo ambao alisema ni suluhu ya uharibifu wa misitu inayoizunguka wilaya hiyo lakini pia ni mkombozi wa afya za wananchi hao ambao wamekuwa kwa kiwango kikubwa wakikata miti kwa ajili ya kuni za kupikia.

“Ndani ya wilaya ya Kilosa unaweza kusema kwa 100% wananchi wamekuwa wakitumia nishati isiyosalama, nishati ambayo siyo sahihi; tuliona njia nyepesi ni kutumia kuni lakini kumbe mambo yamebadilika misitu yetu inapaswa kubaki salama na afya zetu pia kutoathirika tena na moshi wa kuni,” alisisitiza Hamdu.


Akizungumzia mradi kwa ujumla wake, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage alisema kuwa REA imejipanga kikamilifu kuhakikisha lengo lililomo katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia linafikiwa.

“Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan imetambua changamoto wanayopata wananchi wake na ndio sababu imeweka ruzuku kubwa ili kuwafikia wananchi wengi Zaidi. Miti inakatwa kwa wingi, akina mama na watoto wanapata madhara kiafya na ili kuondokana na madhara haya tumejuka na majiko banifu nchi nzima na kwa kuanzia kwa hapa Morogoro kila wilaya itafikishiwa majiko 1,195,” alifafanua Mha. Advera.


Alibainisha kuwa kampuni saba zimeshinda zabuni za kusambaza majiko banifu katika mikoa mbalimbali kote nchini na kwamba kila mwananchi mwenye kuhitaji jiko banifu kupitia mradi huo anapaswa kuwa na kitambulisho cha Taifa ili kuiwezesha Serikali kutunza kumbukumbu na kupata takwimu halisi ya utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia.

Mhadisi Advera alibainisha kuwa mradi huo wa majiko banifu unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali na Jumla ya majiko 200,000 yatasambazwa nchi nzima.

Alisema REA itaendelea kutekeleza miradi ya Nishati Safi ya kupikia nchi nzima na kwa kutumia vyanzo na teknojia mbalimbali ili kuhakikisha watanzania wengi wananufaika.