Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 atakosa mechi ya kundi C dhidi ya Tanzania tarehe 23 mwezi Juni mjini Cairo baada ya kupewa kadi mbili za njano katika mechi ya kufuzu ya Senegal.
''Kutokuwepo kwake hakutatuathiri kwa njia yoyote'' , kocha Cisse aliambia vyombo vya habari vya Senegal kabla ya kuondoka katika kambi yao ya mazoezi katika eneo la Alicante Uhispania kuelekea Misri.
''Ni kweli kwamba uwepo wake ni muhimu sana kwetu lakini bila yeye tuko dhabiti.Shirikisho la soka CAF limeamua hivyobasi hatuna budi'', Cisse aliongezea.
Mane alipewa kadi ya njano katika mechi ambayo Senegal ilipata ushindi wa 1-0 dhidi ya Equitorial Guinea mnamo tarehe 17 Mwezi Novemba 2018 na pia alipokea kadi nyengine ya njano katika mechi ya ushindi wa 2-0 dhidi Madagascar mnamo tarehe 23 mwezi Machi 2019 ijapokuwa haijathibitishwa katika takwimu za mechi za Caf.
Caf imetakiwa kuthibitisha.
Mchuano huo nchini Misri, unaotarajiwa kuanza tarehe 21 mwezi Juni hadi 19 Julai , utakua wa Mane wa nne wa Afcon na itakuwa mara ya pili kukosa mechi ya ufunguzi ya Senegal.
Alikosa mechi ya ufunguzi ya Simba hao wa Teranga katika fainali za 2015 nchini Equitorial Guinea dhidi ya Ghana kwa kuwa alikuwa anauguza jeraha la kifundo cha mguu alilopata alipokuwa akiichezea klabu yake ya zamani Southampton.
Mane , ambaye alishinda taji la ligi ya mabingwa Ulaya akiichezea Liverpool mwezi huu, alijiunga na Simba wa Teranga katika mazoezi nchini Uhispania siku ya Alhamisi kabla ya yeye na wenzake kuelekea Misri siku ya Ijumaa.
Anatarajiwa kucheza mechi nyengine za Senegal mjini Cairo dhidi ya Algeria tarehe 27 mwezi Juni na Kenya siku nne baadaye.