KAMPUNI ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) imekamilisha ujenzi wa nyumba mbili (nyumba pacha) za polisi katika mtaa wa Mgusu kata ya Mgusu wilayani Geita mkoani hapa.
Ujenzi wa nyumba hizo uliofanywa na GGML umehusisha ufadhili wa kiasi cha sh milioni 77 kwa zilizotumika kukamilisha maboma yaliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi lengo likiwa ni kuboresha makazi ya askari polisi.

Kaimu Mkurugenzi wa GGML, Duan Campbell akiongea katika uzinduzi huo.
Akiongea wakati wa hafla ya kukabidhi nyumba hizo kwa jeshi la Polisi mkoani Geita, Kaimu Mkurugenzi wa GGML, Duan Campbell amesema kuwa mbali na uchimbaji dhahabu, mgodi huo pia unashiriki katika maendeleo mbalimbali ya kijamii.
Bw.Duan alisema kukamilika kwa mradi huo huo ni muhimu kwani siyo tu unajenga mahusiano ya mgodi na jamii, lakini pia kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yanayozunguka mgodi na wananchi kwa ujumla.
Alisema sera ya GGML inaamini kuwa Jamii imara inategemea taasisi imara za ndani, na moja ya taasisi zinazoshikilia uimara na ustawi wa jamii kila siku ni jeshi la polisi.
"Askari polisi wanaposaidiwa kwa kupata makazi bora, utulivu na heshima, uwezo wao wa kuitumikia jamii unaimarika zaidi, hali hii huongeza utayari wa kazi na kuimarisha usalama wa raia na mali zao.
"Kampuni ya GGML tunaamini kwamba Geita salama na yenye ulinzi wa uhakika inachangia moja kwa moja uendelevu wa shughuli zetu", alisema na kuongeza;
"Usalama hauishii ndani ya mgodi pekee, bali usalama upo pia majumbani, barabarani, shuleni, na mitaani ambako watu wanaishi na kufanya kazi", alisisitiza Duan.
Naye Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Mgusu, Nazoro Marcel alisema mradi ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2019/20 kupitia nguvu za wananchi na wadau wa maendeleo kwa kuchangia ujenzi wa msingi na boma kwa thamani ya sh milioni 19.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo alisema ushirikiano kati ya wananchi, wadau wa maendeleo na viongozi wa Serikali imeleta matokeo chanya kupunguza matukio ya uharifu Geita.
Kamanda Jongo alikiri kuwa mchango GGML kwenye sekta ya ulinzi na usalama inawafanya kuwa wadau wakubwa wa amani ambapo wamesaidia kuboresha utendaji wa polisi mkoani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Bw. Martine Shigela.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela aliipongeza GGML kwa msaada huo huku akiwaomba kutenga bajeti ya ujenzi wa kituo bora cha polisi cha kata ya Mgusui li kukidhi mahitaji ya eneo hilo.

