ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, March 30, 2026

NEMC KUPEWA NGUVU ZAIDI KUDHIBITI MAZINGIRA-MASAUN

 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Yusuf Masauni, amesema serikali inatarajia kufanya maboresho ya sheria ili kuipa mamlaka zaidi Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kushughulikia moja kwa moja wanaokiuka sheria za mazingira, bila kujali kama ni taasisi za umma au binafsi.

Akizungumza Machi 30, 2026 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa taka ili kulinda mazingira na afya za wananchi.

Aidha, Masauni amewataka wananchi kutumia kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Taka Sifuri kama fursa ya kujifunza namna ya kubadilisha taka kuwa rasilimali yenye tija, hatua itakayosaidia kuongeza kipato na kukuza uchumi wa taifa.

Ameongeza kuwa NEMC inahitaji kupatiwa vitendea kazi vya kisasa, ikiwemo helikopta na droni, ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake na kudhibiti uchafuzi wa mazingira.

Sambamba na hilo, ametoa onyo kali kwa wote wanaochafua mazingira, wakiwemo wazalishaji wa mifuko ya plastiki, wanaotupa taka hovyo, wanaomwaga maji machafu baharini na wanaosababisha kelele mitaani, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa bila upendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema mkoa wa Dar es Salaam umeanza mpango wa kufundisha somo la uhifadhi wa mazingira kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, ambapo tayari shule 10 zimechaguliwa kuanza utekelezaji wake.

RAIS DKT.SAMIA APOKEA RIPOTI YA CAG, TAKUKURU NA PPRA LEO IKULU JIJINI DAR ES SALAAM.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali mara baada ya kupokea Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye hafla ya kupokea Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Charles Kichere akisoma Muhtasri wa Ripoti yake kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 kutoka kwa Bw. Charles Kichere, Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Bw. Crispin Chalamila akisoma Muhtasari wa Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Bw. Crispin Chalamila, Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 30 Machi, 2026.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) Bw. Dennis Simba akisoma Muhtasari wa Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Bw. Dennis Simba, Ikulu jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Machi, 2026.

MAFURIKO SIMANJIRO 169,638 WAOMBA MSAADA WA DHARURA

news

TAKRIBANI wananchi 169,638 wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wamekumbwa na mafuriko makubwa yaliyosababisha uharibifu wa makazi, mali na mashamba, hali inayozidi kuongeza ugumu wa maisha kwa wakazi wa eneo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala, amesema licha ya idadi hiyo ya wananchi walioathirika lakini pia mafuriko hayo yameharibu zaidi ya ekari 97,429 za mashamba kwa kujaa maji.

Imeelezwa kuwa mafuriko hayo yameathiri kwa kiasi kikubwa kata za Shambalai, Nduruma, Mirerani na Naisinyai, ambako maji yameingia ndani ya nyumba na kusomba mali mbalimbali pamoja na kuharibu vyanzo vya chakula, huku ukihitajika msaada wa dharura.

“Athari hizo zimeacha wananchi wengi bila makazi, chakula na mahitaji muhimu, na wengine wamelazimika kuishi kwa ndugu na jamaa wakati wakisubiri msaada zaidi,” amesema.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, mkazi wa Mererani, Henson Loy, amesema tatizo la mafuriko limekuwepo kwa muda mrefu lakini mwaka huu limeongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi.

“Moja ya sababu kuu ya hali hiyo ni miundombinu mibovu ya mifereji ya maji pamoja na barabara kuwa chini, hali inayosababisha maji kushindwa kupita na hivyo kuelekezwa moja kwa moja kwenye makazi ya wananchi,” amesema.

Mkazi wa Utupendana, Jonathan Mkali, amesema mafuriko hayo hujitokeza mara kwa mara kila msimu wa mvua na hudumu kwa muda mrefu, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi ikiwemo kukatika kwa mawasiliano na shughuli za kiuchumi.

Katika juhudi za kusaidia waathirika, kampuni ya Permanent Minerals imetoa msaada wa vifaa mbalimbali ikiwemo chakula vifaa vya shule vya watoto,vyandarua,venye thamani ya takriban Sh. milioni 22, ikiwa ni sehemu ya mchango wa wadau katika kukabiliana na athari za mafuriko hayo.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ameendelea kutoa wito kwa taasisi mbalimbali, mashirika na wananchi kujitokeza kusaidia zaidi, akisisitiza kuwa mahitaji bado ni makubwa kutokana na ukubwa wa janga hilo.

Aidha, wananchi wameiomba serikali kuchukua hatua za kudumu kwa kuboresha miundombinu ya mifereji ya maji, kupanua mitaro na kuinua barabara ili kuzuia kujirudia kwa mafuriko hayo katika siku zijazo.

"HAPAKUWA NA MTU WAKATI AJALI IKITOKEA MGODINI" - RIPOTI YASEMA

 

Taarifa ya Odisi ya Madini Mbogwe, Geita.


OFISI ya Afisa Madini Mkazi Mbogwe imetoa ufafanuzi kuhusu tukio la ajali lililotokea katika Mgodi wa Dhahabu wa Msasa kwamba wakati tukio linatokea hapakuwa na shughuli zozote za uzalishaji katika eneo husika kwakuwa watendakazi wote walikuwa tayari wameondolewa kupisha ukarabati.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na ofisi hiyo ya madini Mbogwe, katika mgodi huo uliopo katika Kijiji cha Msasa, Runzewe, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita, Machi 29, 2026 majira ya saa 4:00 asubuhi, katika eneo la Area A kulitokea mpasuko wa ardhi ulioathiri maduara manne yenye namba KO 46A, 47A, 48A na 49A.

“Hadi sasa, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya timu ya uokozi, wakaguzi wa migodi na vyombo vya usalama, hakuna mtu aliyeripotiwa kupata majeraha wala kupoteza maisha kutokana na tukio hilo,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

 Imesema maduara hayo yalikuwa yamesimamishwa uzalishaji kufuatia maelekezo ya wakaguzi wa mgodi yaliyotolewa Machi 27, 2026 ili kufanyiwa ukarabati wa kiusalama. Na kwamba mpasuko huo ulisababisha maduara hayo kutitia ardhini, hali inayohusishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha kulegea kwa udongo na miamba.

“Baada ya kubainika dalili za hatari, wakaguzi wa mgodi walichukua hatua za haraka kuwaondoa mafundi waliokuwa chini ya ardhi pamoja na watu waliokuwa jirani na eneo hilo ambapo wote waliweza kutoka salama.

“Vikosi vya uokozi vilivyohusisha Ofisi ya Mgodi, Ofisi ya Madini, Kikosi cha Uokozi na Zimamoto, Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama vilifika mara moja katika eneo la tukio na kusimamisha shughuli zote za mgodi kwa muda, kuweka utepe wa tahadhari katika eneo lililoathirika na kudhibiti wananchi waliokuwa wakijaribu kusogea katika eneo la hatari,” Imesema sehemu ya taarifa hiyo.

 Imeongeza kuwa shughuli za ukaguzi katika mgodi huo hufanyika kila siku kupitia Ofisi ya Ukaguzi wa Mgodi inayoongozwa na Mkaguzi Mkuu wa Mgodi akisaidiwa na takribani wakaguzi 200 waliopo muda wote katika eneo la mgodi, chini ya usimamizi wa karibu wa Ofisi ya Ofisa Madini Mkazi Mbogwe, Mkaguzi Mkuu wa Migodi Tanzania pamoja na taasisi nyingine za serikali kwa mujibu wa sheria.