![]() |
| Taarifa ya Odisi ya Madini Mbogwe, Geita. |
OFISI ya Afisa Madini Mkazi Mbogwe imetoa ufafanuzi kuhusu tukio la ajali lililotokea katika Mgodi wa Dhahabu wa Msasa kwamba wakati tukio linatokea hapakuwa na shughuli zozote za uzalishaji katika eneo husika kwakuwa watendakazi wote walikuwa tayari wameondolewa kupisha ukarabati.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na ofisi hiyo ya madini Mbogwe, katika mgodi huo uliopo katika Kijiji cha Msasa, Runzewe, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita, Machi 29, 2026 majira ya saa 4:00 asubuhi, katika eneo la Area A kulitokea mpasuko wa ardhi ulioathiri maduara manne yenye namba KO 46A, 47A, 48A na 49A.
“Hadi sasa, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya timu ya uokozi, wakaguzi wa migodi na vyombo vya usalama, hakuna mtu aliyeripotiwa kupata majeraha wala kupoteza maisha kutokana na tukio hilo,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Imesema maduara hayo yalikuwa yamesimamishwa uzalishaji kufuatia maelekezo ya wakaguzi wa mgodi yaliyotolewa Machi 27, 2026 ili kufanyiwa ukarabati wa kiusalama. Na kwamba mpasuko huo ulisababisha maduara hayo kutitia ardhini, hali inayohusishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha kulegea kwa udongo na miamba.
“Baada ya kubainika dalili za hatari, wakaguzi wa mgodi walichukua hatua za haraka kuwaondoa mafundi waliokuwa chini ya ardhi pamoja na watu waliokuwa jirani na eneo hilo ambapo wote waliweza kutoka salama.
“Vikosi vya uokozi vilivyohusisha Ofisi ya Mgodi, Ofisi ya Madini, Kikosi cha Uokozi na Zimamoto, Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama vilifika mara moja katika eneo la tukio na kusimamisha shughuli zote za mgodi kwa muda, kuweka utepe wa tahadhari katika eneo lililoathirika na kudhibiti wananchi waliokuwa wakijaribu kusogea katika eneo la hatari,” Imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Imeongeza kuwa shughuli za ukaguzi katika mgodi huo hufanyika kila siku kupitia Ofisi ya Ukaguzi wa Mgodi inayoongozwa na Mkaguzi Mkuu wa Mgodi akisaidiwa na takribani wakaguzi 200 waliopo muda wote katika eneo la mgodi, chini ya usimamizi wa karibu wa Ofisi ya Ofisa Madini Mkazi Mbogwe, Mkaguzi Mkuu wa Migodi Tanzania pamoja na taasisi nyingine za serikali kwa mujibu wa sheria.
Tupe maoni yako

0 comments:
Post a Comment