ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, May 1, 2025

TRAORE ASHUKURU NCHI ZILIZOANDAMANA KUMUUNGA MKONO.


 .

Kiongozi wa utawala wa kijeshi nchini Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, ametoa shukurani zake za dhati kwa nchi zilizoandamana duniani kote jana Jumatano, akisema mshikamano huo umeimarisha imani yao kwamba mapigano wanayopigania ni kupatikana kwa ulimwengu mzuri na usawa zaidi na wenye haki.

"Napenda kutoa shukrani zangu kwa wazalendo wote wanaopenda amani, wapenda uhuru na wapendelea Afrika wote ambao waliandamana ulimwenguni kote Jumatano Aprili 30, 2025 kuunga mkono kujitolea kwetu na maono yetu ya Burkina Faso mpya na Afrika mpya, kujiweka huru kutoka kwa mikono ya ubeberu na ukoloni," Traore aliandika katika akaunti yake ya X.

Aliahidi kutobadilisha msimamo hata wakati anapopitia changamoto, badala yake "nitasimama kidete hadi watu wetu watakapokombolewa."

Maelfu ya raia barani kote Afrika kote waliandamana chini ya wito wa "Hands Off the AES!" kuonyesha mshikamano wao na Burkina Faso na kiongozi wake wa kijeshi, Kapteni Ibrahim Traoré.

Maandamano yalifanyika Burkina Faso, Ghana, na Liberia na kwengine yakiongozwa na mashirika ya mashinani.

Waandamanaji walilaani vikali uingiliaji wa mataifa ya kigeni na kusisitiza kuunga mkono nchi hiyo dhidi ya ubeberu.

Wimbi hili la mshikamano barani Afrika linafuatia ufichuzi wa hivi majuzi wa mamlaka ya kijeshi ya Burkina Faso kwamba ilizima "njama kubwa" ya kumpindua Traore Aprili 21.

Serikali ya Burkina Faso ilielezea njama hiyo kama juhudi ya "kuzua machafuko" na kubadilisha utawala chini ya uongozi wa Traoré.

"Chini ya Kapteni Traoré, Burkina Faso imekuwa ishara ya utu na ukakamavu wa Afrika," lilisema Vuguvugu la Kisoshalisti la Ghana ambalo liliandaa maandamano nchini Ghana.

"Tunasimama na watu wa Burkina Faso ambao wanapigania kurejesha utajiri wao na mustakabali wao kutoka kwenye makucha ya ukoloni mamboleo."

PADRI KITIMA AVAMIWA NA KUJERUHIWA POLISI YAMSHIKILIA MTU MMOJA.

 


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linachunguza tukio la kushambuliwa kwa Padri Charles Kitima, Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), ambaye alijeruhiwa kichwani usiku wa kuamkia Mei Mosi, 2025 katika eneo la maliwato ya kantini ya TEC, Kurasini.


Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, tukio hilo lilitokea majira ya saa nne na robo usiku.


Padri Kitima alikuwa ametoka kuhudhuria kikao cha viongozi wa dini kilichodumu kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa moja jioni. Baada ya kikao hicho, aliendelea kubaki katika kantini ya Baraza kwa ajili ya kupata kinywaji, ambapo baadaye alielekea maliwatoni na ndipo alipovamiwa na kushambuliwa na watu wawili waliotumia kitu butu.


Padri Kitima alipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya matibabu na hali yake inaelezwa kuwa inaendelea vizuri. Kabla ya kuhamishiwa Aga Khan, alipatiwa huduma ya kwanza katika kituo kidogo cha afya kilichopo ndani ya eneo la TEC.


Jeshi la Polisi linamshikilia mtu mmoja, Rauli Mahabi (maarufu kama Haraja), mkazi wa Kurasini, kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tukio hilo huku uchunguzi wa kina ukiendelea ili kuwabaini wote waliohusika na kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa mara moja.


Mashuhuda waliokuwepo katika eneo la tukio wameripoti kuwa Padri Kitima alionekana akizungumza na watu kadhaa kabla ya kuondoka kuelekea maliwatoni, na muda mfupi baadaye waliona watu wakikimbia eneo hilo, huku yeye akiomba msaada akiwa anatokwa damu.


Padri Charles Kitima mbali na kuwa Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), mbali na nafasi yake ndani ya Kanisa Katoliki, Padri Kitima anajulikana kwa misimamo yae ya kukosoa na kuwa mstari wa mbele katika masuala ya haki za binadamu, utawala wa sheria na uwajibikaji wa kijamii.

RAIS DKT. SAMIA AKISHIRIKI MAADHIMISHO YA MEI MOSI MKOANI SINGIDA

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Akishiriki Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani inayoadhimishwa Mkoani Singida kitaifa, leo tarehe 1 May, 2025.

Wednesday, April 30, 2025

NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU AHIMIZA WALIMU KUWALINDA WATOTO ANA WIMBI LA UKATILI

IMEANDIKWA NA. VICTOR MASANGU/PWANI SAUTI NA ALBERT G.SENGO Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Charles Mahera,amewataka walimu, wazazi, pamoja na walezi nchi nzima kuhakikisha kwamba wanaweka mipango madhubuti ambayo itaweza kuwalinda na kuwatunza watoto na wanafunzi kwa lengo ikiwa ni kuweza kupambana na wimbi la vitendo vya unyanyasaji na ukatili ili waweze kusoma katika mazingira ya usalama na amani. Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Aprili 29, 2025 wakati wa kufunga rasmi mafunzo ya matumizi bora na salama ya vifaa vya TEHAMA kwa walimu wa shule za msingi, yanayotekelezwa kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) ambayo yamefanyika katika ukumbi wa shirika la elimu Kibaha Mkoani Pwani na kushirikisha jumla ya walimu wapatao 1,800 kutoka mikoa minne ya Tanzania bara. Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Awali na Msingi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bi Suzanne Nusu, amebainisha kwamab kati ya Halmashauri 184 wamejitahidi zimefanikiwa kupata fursa ya kupelekewa vifaa hivyo vya tehama ambapo walimu nao wamenufaika na kupatiwa mafunzo. Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ya Tehama wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuweza kuona umuhimu wa kuwapa ujuzi wa kuwafundisha teknolojia na kuahidi kwenda kuyafanyia katika kwa weledi katika suala zima la utekelezaji wa majukumu yao katika kuboresha elimu. Mafunzo hayo ya Tehama yameshirikisha walimu wapatao 1800 yamewashirikisha washiriki mbali mbali kutoka Mikoa ya Geita, Tabora,Simiyu pamoja na Kagera ambapo lengo lake ni kuongeza viwango vya sifa za walimu kuanzia elimu ya awali hadi sekondari.

WALIOUA VIJANA BUNGENI KENYA WAFICHULIWA NA VIDEO NA PICHA ZA BBC

 Mnamo Juni 25, 2024, damu ilimwagika katika Bunge la Kenya.

Siku hiyo, maelfu ya waandamanaji walielekea bungeni ili kusitisha muswada wa fedha #FinanceBill2024 kupitishwa kuwa sheria.
Njiani walikutana na mabomu ya machozi, virungu, na hata milio ya risasi. Walipofika huko, na kulivamia bunge, baadhi ya milio ya risasi hiyo ikageuka kuwa hatari zaidi Takriban watu watatu waliuawa: mwanafunzi, muuza duka, na mwalimu. Tangu wakati huo, hakuna mtu aliyeshikiliwa kuwajibika kwa vifo vyao.

Tuesday, April 29, 2025

KUUNDWA KWA JAB NI HATUA YA KUIMARISHA NA KUBORESHA SEKTA YA HABARI - MAJALIWA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa,


Na Mwandishi Wetu/ARUSHA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imechukua hatua kadhaa katika kuimarisha na kuboresha sekta ya habari nchini ikiwa ni pamoja na kuunda Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.

Waziri Mkuu amesema hayo leo tarehe 29 Aprili, 2025 wakati akifunga Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari lililofanyika jijini Arusha kwa siku mbili.



“Kwenye sekta ya habari na utangazaji, falsafa ya “4Rs” za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, alizozibainisha baada ya kuingia madarakani mwezi Machi 2021, imetekelezwa kwa vitendo hususani kwenye eneo la “Reforms” (Mageuzi),” amesema Waziri Mkuu na kuongeza;


“Serikali ya Awamu ya Sita katika kutekeleza falsafa hii imechukuwa hatua mbalimbali kuimarisha sekta ya habari na utangazaji nchini kwa kuunda chombo kipya cha kushughulikia usajili wa taaluma ya waandishi wa habari yaani Bodi ya Ithibati”.


Waziri Mkuu Majaliwa amesema Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari iliyozinduliwa mwaka huu ina jukumu la kusimamia viwango vya kitaaluma kwa wanahabari ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa matakwa ya kisheria chini ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229. 


Amesema hatua nyingine zilizochukuliwa na Serikali ni kuhakikisha inawezesha shirika la Habari la utangazaji kuwepo kisheria pamoja na kuimarisha Idara ya Habari Maelezo kwa kununua vitendea kazi vikiwemo Magari na vifaa vya kurushia matangazo mbashara.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu inayosema “Uhabarishaji kwenye Dunia Mpya: Mchango wa Akili Mnemba katika uhuru wa vyombo vya habari” inalenga kujadili athari za teknolojia ya akili mnemba katika uendeshaji wa vyombo vya Habari na uhuru wake. 


Amesema Serikali katika kuhakikisha Akili Mnemba (AI) inatumika kwa njia inayowezesha badala ya kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari, imeanzisha mchakato wa kuandaa sera maalum ya AI na waandishi wanaowajibu wa kuchangia ili kupata sera nzuri.


“Sera hii itatoa mwongozo wa matumizi ya AI katika vyombo vya habari, ili kuhakikisha kwamba teknolojia mpya zinaendana na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari, uwazi, na uadilifu wa uandishi wa Habari, hivyo mtumie muda wenu hapa kujadili na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha sera hiyo,” amesema Waziri Mkuu.





WAZIRI MKUU AWASILI ARUSHA AFUNGUA MKUTANO WA 73 WA ACI AFRICA .

 

Na. Vero Ignatus/Arusha.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa amewasili Mkoani Arusha na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Christian Makonda pamoja na viongozi wengine wa Serikali na Chama leo tarehe 28 Aprili, 2025.

Waziri Mkuu anatarajia kufungua Mkutano wa 73 wa Baraza la Kimataifa la viwanja vya ndege kwa kanda ya Afrika (ACI Afrika) unaofanyika kwenye Hotel ya Mount Meru.

Awali akitoa salamu kwa mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda Arusha amemshukuru Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mnyaa Mbarawa

kwa kuridhia uwanja huo mzuri wa kisasa katika mkoa wa Arusha ambapo unaweza ukawa namba moja basi ama namba mbili katika nchi ya Tanzania .

Vile vile ameshukuru Prof. Godius Walter Kahyarara Katibu Mkuu wa Wizara kwa kuridhiwa uwanja huo kutumika kwa ndege ndogo zinazounganisha Afrika ya Mashariki kwa wageni wanaotaka kutua katika uwanja huo

"Nafahamu hatua zinaendelea vizuri na siyo muda mrefu Mamlaka watatangaza ya kwamba Arusha unaweza kutumia sasa uwanja wa ndege kama point of interest na kuwaruhusu wageni wenye private jet kuja Arusha bila kuhangaika kwenda Kilimanjaro. Alisema Makonda.


SERIKALI ITAFANYIA KAZI HARAKA MAAZIMIO YA KONGAMANO LA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI- MSIGWA.

 

Wadau na Waandishi wa Habari wakifuatilia uwasilishaji wa mada na majadiliano katika siku ya kwanza ya Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari lililofanyika JANA tarehe 28 Aprili, 2025 jijini Arusha.



Na Mwandishi Wetu.

Serikali imesema itahakikisha inafanyia kazi mapendekezo yote yatakayotolewa kwenye maazimio ya pamoja ya Waandishi wa Habari baada ya kuhitimisha Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari kwa mwaka 2025.

Hakikisho hilo la Serikali linatolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson wakati akitoa neno la kufunga Siku ya Kwanza ya Kongamano hilo linalofanyika jijini Arusha kwa uratibu wa Jamii Africa, UNESCO na Wizara yenyewe.

"Nimesikia maazimio ya awali mliyoyatoa hapa, ni muhimu sana na mimi nitaomba mkishakamilisha ile nakala ya mwisho mtupatie ili na sisi serikalini yale ambayo tunatakiwa tuchukue hatua tuyafanyie kazi, basi tutafanyia kazi mara moja", amesema Msigwa.
Amewapongeza wadau wote walioshiriki Kongamano hilo na kwa majadiliano waliyoyafanya ikiwemo suala la matumizi ya Akili Mnemba kwa kuwa ni jambo muhimu kwenye kazi za uandishi wa habari kwa sasa.

Bw. Msigwa amesema Serikali itaendelea kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari nchini na kwamba hilo linajidhihirisha kwani kumekuwa na mazingira rafiki kwa Waandishi wa Habari pale wanapotekeleza majukumu yao.

"Sisi Waandishi wa Habari kwenye Awamu hii ya sita tumekuwa tukifanya kazi katika mazingira rafiki sana, kwa sababu ya maelekezo ambayo Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) anayasimamia," amesisitiza Msigwa na kuongeza;




"Aliyoyasema tangu siku ya kwanza alipoingia madarakani ndiyo anayoyatekeleza na sisi lazima tutekeleze maelekezo yake kuhakikisha kuna uhuru wa vyombo vya habari, kuhakikisha waandishi wa Habari hawabughudhiwi lakini kuendelea kujenga mazingira bora kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao."

Kongamano hilo la Maadhimisho ya Siku ya Siku ya Uhuru wa Habari linatarajiwa kufungwa LEO tarehe 29 Aprili, 2025 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.

"TUSIONGELEE AMANI KAMA HATUTAKI KUONGELEA HAKI" PADRI KITIMA

 Ni kupitia Channeli ya inayomilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania {TEC} ikiwa ni moja ya chombo cha Uinjilishaji kwa njia ya Sauti na Video, fuatilia yale yaliyojiri.


Monday, April 28, 2025

JK ASHIRIKI KUTOA MAFUNZO CHUO KIKUU CHA HAVARD HUKO BOSTON KWA MAWAZIRI WA NCHI ZINAZOENDELEA


Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete yuko mjini Boston, Marekani, ambako anashiriki katika kutoa mafunzo kwa Mawaziri wa Fedha na Mawaziri wa Mipango kutoka nchi mbalimbali zinazoendelea. 


Mafunzo hayo yanafanyika chini ya Mpango wa Uongozi wa Ngazi ya Mawaziri wa Harvard, maarufu kama Harvard Ministerial Leadership Program, unaoendeshwa na Chuo Kikuu cha Harvard.

Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Kikwete ni mmoja wa Viongozi Wakuu wa Kitaifa Wastaafu walioalikwa kushiriki kama wakufunzi, wakitumia uzoefu wao wa uongozi kuhamasisha na kuwajengea uwezo viongozi wa kizazi kipya.

Mbali na Viongozi Wakuu wa Kitaifa Wastaafu, mafunzo haya pia yanashirikisha Wakuu wa Taasisi za Kimataifa, wawakilishi wa mashirika binafsi, pamoja na mabingwa wa masuala ya sera, uchumi na maendeleo kutoka maeneo mbalimbali duniani.



MBUNGE KOKA AFANYA KUFURU YA MAENDELEO UTEKELEZAJI WA ILANI YA CHAMA KWA VITENDO

 


NA VICTOR MASANGU,KIBAHA 

Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Mhe.Sylvestry Koka amesema kwamba katika kipindi cha miaka mitano kwa mwaka 2020/2025 ameweza kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo ambayo yametokana na juhudi zake binafsi pamoja na fedha ambazo zimetolewa na  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan

Koka ameyabainisha  hayo wakati wa mkutano mkuu maalumu wa Jimbo la Kibaha mjini wa utekelezaji wa ilani ya chama kwa kipindi cha miaka mitano kwa mwaka wa 2020 hadi 2025 katika nyanja mbali mbali.

Koka amesema kwamba  kitendo cha kuwa na Rais msikivu kimekuwa chachu ya maendeleo katika Jimbo la Kibaha mjini ambapo kero katika sekta mbalimbali zimetatuliwa na hivyo kuwafanya wabunge kumsaidia kwa urahisi utekelezaji wa ilani ya Chama.

"Raisi wetu ni mama msikivu anapoelezwa shida za wananchi hachelewi tutoa maelekezo ya utatuzi wa haraka kwa maendeleo yaliyopatikana kwenye Jimbo letu tuna kila sababu ya kumpa kura za heshima muda utakapofika," amesema.

Naye Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Kibaha mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka amesema chama hicho kinasimamia utekelezaji wa ilani ambapo miradi mbalimbali umetekelezwa  kwa fedha kutoka Serikali kuu na mapato ya ndani.

Awali Katibu wa CCM Kibaha mjini Isack Kaleiya alisema wanaendelea kusimamia taratibu na kanuni za chama na kwa kila anayeenda kinyume na kanuni na taratibu za chama hatua zinachukuluwa kupitia kamati ya maadili.

Wajumbe zaidi ya 8000  wa CCM kutoka kata 14 wa ameshiiriki mikutano ya Jimbo iliyofanyika kwa siku tano kwa ajili ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani iliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Mhe.Silvestry Koka:


MNGEZA B BINGWA WA ERASTO CUP MUHEZA,HALMASHAURI KUWAUNGA MKONO MADIWANI WATAKAOANZISHA LIGI KWENYE MAENEO YAO

Na Oscar Assenga,MUHEZA.

HALMASHAURI ya wilaya ya Muheza Mkoani Tanga imesema kwamba itaendelea kuwaunga mkono madiwani ambao watakaoanzisha Ligi mbalimbali katika maeneo yao kwa lengo la kuhamasisha michezo na kufungua fursa za ajira kupitia sekta hiyo.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muheza Issa Msumari wakati Fainali ya Ligi ya Erasto Cup ambayo imeanzishwa na Diwani wa Kata ya Tongwe Erasto Mhina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri kwa lengo la kuhamasisha vijana kushiriki kwenye michezo.
Msumari ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wilayani Muheza alimpongeza Diwani huyo kwa kuonyesha udhubutu na kupambana kuhakikisha anawapelekea burudani vijana wa Kata hiyo.
Katika mchezo huo wa fainali timu ya Mngeza B iliibuka na ushindi wa penati 5-4 dhidi ya Kwevumo FC katika mchezo ambao ulikuwa na upinzani mkubwa baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika dakika 90 mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Pongwe kata ya Tongwe wilayani Muheza.
“Kwa wastani ligi hii imeongeza uchangamfu mkubwa na vijiji 6 na vitongoji 27 kuna badhi ya vijana walikuwa hawatambuani na ligi hiyo hivyo uwepo wake umekuwa chachu ya kuwaleta vijana pamoja na kufahamiana na inakuwa rahisi kuhamasisha mambo ya kijamii”Alisema
Aidha alisema ushiriki wa watu unakuwa ni mkubwa sana ambapo wilaya hiyo wanaunga mkono michezo kwa sababu inatengeneza ajira na kuondoa tatizo la vijana kukaa mtaani bila kazi ya kufanya hivyo wanaipa kipaumbele kama ya vijana watacheza na kutokea kwenye ligi mbalimbali watatengeneza vijana wengi ambao wataitangaza wilaya hiyo kupitia soka.
“Tutaendelea kuunga mkono michezo kwa sababu kupitia huko vijan a wanaweze kutengeneza pesa kama ilivyo kwa vijana wengine waliotokea wilaya ya Muheza Mzize na Semtawa na nieleze kwamba diwani ambayo ataanzisha michezo tutamuunga mkono kutokana na kwamba kupitia michezo inaweza kuwasaidia kuweza kujikwamua kiuchumi wao na jamii “Alisema






MBIO ZA KILOMITA 5 ZA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI ZAFANA, JIJINI ARUSHA (World Press Freedom Day, 5K Fun Run)

 

Mbio za kilomita 5 za maadhimisho ya siku ya vyombo habari Duniani zafanyika leo jijini Arusha, katika viwanja vya Ghymkana/ Mgambo.

Mbio hizo zilianzia kwenye uwanja wa Ghymkana /Mgambo na kumalizikia hapo hapo Ghymkhana; ambapo zilihudhuriwa na wanahabari mbalimbali , wadau wa habari na wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa.


Maadhimisho ya Vyombo vya habari duniani yanafanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 27 hadi 30 Aprili 2025, ambapo siku ya kwanza yameanza na mbio za kilomita 5 na kesho kutafanyika mikutano mbalimbali katika hoteli ya Gran Melia.


Maadhimisho hayo yanaratibiwa na JamiiAfrica au zamani Jamii Forums, Serikali , shirika la Kimataifa la Elimu , Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na wadau wengine wa Habari nchini na Kimataifa.