ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, October 25, 2025

WANANCHI MWANZA WAHIMIZA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025

 

Makundi mbalimbali ya wananchi jijini Mwanza yamejitokeza kwa wingi na kushiriki kongamano la kuhamasisha amani kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Kongamano hilo limeandaliwa na makundi hayo ambayo ni pamoja na machinga, bodaboda, wamiliki wa daladala, mama lishe na watu wenye ulemavu chini ya mlezi wao, Stanslaus Mabula ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana kwa awamu mbili kuanzia mwaka 2015/ 20225.

Katibu wa wamiliki wa daladala Mkoa wa Mwanza, Hussein Mosha akihimiza wananchi kulinda amani wakati wa Uchaguzi Mkuu 2025.
Akizungumza kwenye kongamano hilo lililofanyika Jumamosi Oktoba 25, 2025 katika uwanja wa Nyamagana, Katibu wa wamiliki wa daladala Mkoa wa Mwanza, Hussein Mosha amesema Mwanza wamejiandaa kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa amani na utulivu.

"Niwaombe kila mmoja tuendelee kudumisha amani ya nchi yetu, bila amani hata pikipiki zetu hatuwezi kuziendesha, amani yetu ndiyo maisha yetu" amesema Mwenyekiti wa waendesha bodaboda Mkoa wa Mwanza, Mohamed Idd akihimiza wananchi kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa amani.

Naye Katibu wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Zuena Mahamudu amewahimiza wananchi kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani wakati wa uchaguzi na badala yake wakashiriki zoezi la kupiga kura kwa wingi kwa mstakabali wa maisha yao.

Kwa upande wake mlezi wa makundi maalum ya wananchi walioandaa kongamano hilo, Stanslaus Mabula ambaye ni mbunge wa Nyamagana aliyemaliza muda wake amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kupiga kura kwa amani ili kuwachagua viongozi bora watakaowavusha kimaendeleo.

Katibu wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Zuena Mahamudu akizungumza kwenye kongamano hilo na kuhimiza wananchi kujitokeza kwa amani kupiga kura.
Mwenyekiti wa madereva wa daladala Mkoa wa Mwanza, Mjarifu Manyasi akihimiza wananchi kujitokeza kwa amani kushiriki uchaguzi Oktoba 29, 2025.
Mwenyekiti wa Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Said Tembo akihimiza amani kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Mkoa wa Mwanza, Mohamed Idd akihamasisha wananchi kushiriki kwa amani Uchaguzi Mkuu 2025.
Mlezi wa makundi maalum Nyamagana, Stanslaus Mabula akihimiza wananchi kushiriki kwa amani Uchaguzi Mkuu 2025.
Mlezi wa makundi maalum Nyamagana, Stanslaus Mabula akihimiza wananchi kushiriki kwa amani Uchaguzi Mkuu 2025.
Mlezi wa makundi maalum Nyamagana, Stanslaus Mabula akihimiza wananchi kushiriki kwa amani Uchaguzi Mkuu 2025.
Makundi mbalimbali ikiwemo bodaboda wakiwa kwenye kongamano la kuhamasisha amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Oktoba 29, 2025.
Makundi mbalimbali ikiwemo bodaboda wakiwa kwenye kongamano la kuhamasisha amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Oktoba 29, 2025.
Bodaboda wakitoka uwanja wa Nyamagana baada ya kongamano la kuhamasisha amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Oktoba 29, 2025.


Kongamano la Amani kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 limeambatana na kaulimbiu isemayo, "Amani Yetu, Maisha Yetu". 

VIONGOZI WA DINI KANDA YA KASKAZINI WATOA MAAZIMIO SABA WAKISISITIZA UCHAGUZI WA AMANI.

Na Mwandishi Wetu, Moshi

VIONGOZI wa dini kutoka ukanda wa kaskazini unaojumuisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga wameibua hoja saba muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na kutumia busara katika kipindi hiki nyeti kwa Taifa.

Viongozi hao walikutana kwenye Kongamano la Amani lililofanyika katika ukumbi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) – Uhuru Hosteli, Moshi. Washiriki walikuwa ni maaskofu, masheikh, mapadri, wachungaji pamoja na viongozi wa kamati za dini za vijana na wanawake.



Maazimio

Akisoma maazimio ya kongamano hilo, Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoa wa Kilimanjaro, Alhaj Awadh Lema, alisema wamekubaliana na mambo yafuatayo:

1. Kuhamasisha wapiga kura kuhakiki taarifa zao na kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

2. Kuendelea na makongamano ya amani** kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

3. Vyombo vya dola** kutumia hekima na busara katika utekelezaji wa majukumu yao, hasa siku ya uchaguzi.

4. Viongozi wa dini kuwaelimisha waumini** kuhusu haki na wajibu wao katika kulinda amani.

5. Kuepuka uchochezi** kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

6. Kupendekeza ushiriki mpana wa viongozi wa dini** katika vyombo vya maamuzi na utungaji wa sheria.

7. Kuhimiza kila mwananchi kutambua kuwa kulinda amani ni wajibu wake, hata anapodai haki.

Kauli za Viongozi wa Dini

Sheikh Shaban Mlewa,  Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, alisisitiza kuwa amani ni tunu adimu ambayo ikipotea ni vigumu kuirudisha, akitoa mfano wa nchi zilizojikuta kwenye machafuko baada ya uchaguzi.

“Ni muhimu Watanzania kuwa wazalendo, kupendana, kusameheana na kuwa waadilifu ili kuendeleza utulivu wa nchi yetu,” alisema.

Sheikh Shaban Juma, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, alieleza kuwa hakuna haki bila amani, akisisitiza kuwa msingi wa amani ni kumtambua Mungu, kutambua thamani ya nafsi yako na kulinda haki za wengine.

Wakili Mchungaji Daniel Swai, Msaidizi wa Askofu Mkuu wa KKKT – Dayosisi ya Kaskazini, alihimiza kila Mtanzania kutimiza haki yake ya kupiga kura na kulinda haki hiyo kwa njia ya amani.

"Ni kosa kubwa kuhamasisha watu kutotimiza wajibu wao wa kikatiba. Haki na amani ni mambo yanayokwenda pamoja," alieleza.

Padri Deogratias Matiika, Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Moshi, alisema haki ni msingi wa maendeleo ya taifa. Alisisitiza heshima kati ya wananchi na viongozi, na kukemea tabia ya kutoa matusi kwa viongozi kupitia mitandao ya kijamii.

Padri Francis Mahimbo,  kutoka Kanisa la Anglikana – Dayosisi ya Tanga, alihimiza kujengwa kwa jamii yenye kuvumiliana, akisema:

“Msingi wa amani ni haki. Taifa lisilolinda haki za watu wake haliwezi kuwa na utulivu wa kweli.”

 Wito kwa Watanzania

Katika kongamano hilo, viongozi wa kamati za dini za wanawake na vijana walitoa wito kwa Watanzania wote kushiriki uchaguzi kwa utulivu, kujiepusha na vurugu na kuwakataa wale wanaochochea uvunjifu wa sheria.





RC KUNENGE AKABIDHI VITENDEA KAZI IKIWEMO GARI SITA NA BOTI KWA JESHI LA ZIMAMOTO MKOA WA PWANI

 


Na Victor Masangu,Pwani 


MKUU  wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, amekabidhi rasmi magari sita kati ya 11, boti moja kubwa magari mawili ya wagonjwa mawili kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji la Mkoa huo yenye thamani ya Sh. bilioni 7.9.

Kunenge,amekabidhi vifaa hivyo  kwa Kamanda wa kik cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Pwani Jenifa Shirima katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Pwani iliyopo Manispaa ya Kibaha.


Hafla hiyo imehudhuriwa na watendaji wengine mbalimbali akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Pili Mnyema, Sekretarieti ya Mkoa wa Pwani pamoja na askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji la Mkoa huo.

Awali,akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa hivyo Kunenge ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha vitendea kazi vya vyombo vya ulinzi na usalama hususani Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.


Amesema upatikanaji wa magari na boti hizo utaimarisha uwezo wa Jeshi hilo katika kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuokoa maisha na mali za wananchi wakati wa majanga ya moto na maafa ya majini.

“Tunamshukuru  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika vifaa vya uokoaji na uboreshaji huu utasaidia kuongeza ufanisi katika kazi za zimamoto na kuimarisha usalama wa wananchi wetu", amesema Kunenge.

Aidha, Kunenge amelipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji la Mkoa wa Pwani kwa kazi nzuri ya kupambana na matukio ya moto na majanga mbalimbali ambapo amesema upatikanaji wa vifaa itawaongezea ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.


Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani, Jenifa Shirima, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulipa jeshi hilo kipaumbele katika upatikanaji wa rasilimali na vifaa muhimu.

Amesema magari na boti vilivyokabidhiwa vitasaidia kwa kiasi kikubwa katika majukumu ya uokoaji, ikiwemo usafirishaji wa wagonjwa, kudhibiti moto, na kutoa huduma za haraka katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani.


“Vifaa hivi vitasaidia kuongeza kasi ya majibu wakati wa dharura na kupunguza madhara yanayosababishwa na majanga ya moto na ajali hivyo tunamshukuru  Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa kuboresha huduma za zimamoto nchini,” amesema Kamanda Shirima.

Hatahivyo makabidhiano hayo ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuhakikisha taasisi za ulinzi na usalama zinakuwa na vifaa vya kisasa vinavyowezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Monday, October 20, 2025

MAGAZETINI: RUTO AFICHUA JINSI RAILA ALIHANGAIKA NA AFYA YAKE KATIKA SIKU ZAKE ZA MWISHO.

 


Jumatatu, Oktoba 20, magazeti ya kitaifa kutoka nchini Kenya yameripoti kwa kina kuhusu mazishi ya marehemu kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM), Raila Amollo Odinga, yaliyofanyika Bondo, kaunti ya Siaya. 

Magazeti hayo pia yaliripoti kuhusu mgawanyiko unaoibuka ndani ya chama cha ODM kuhusiana na azma ya Rais William Ruto ya kugombea tena urais mwaka 2027 

1. DAILY NATION 

Gazeti hilo liliripoti kuhusu ufa unaojitokeza ndani ya chama cha ODM kuhusu Uchaguzi wa 2027 kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Amollo Odinga. 

Wakati wa mazishi ya Raila Jumapili, Oktoba 19, maafisa wa juu wa chama cha ODM walitofautiana hadharani kuhusu msimamo wa chama juu ya kumuunga mkono Rais William Ruto katika azma yake ya kugombea tena mwaka 2027.

Kikundi kinachoongozwa na Gavana Gladys Wanga kilitangaza kuunga mkono serikali jumuishi. “Tumeendelea kumfuata Raila. Maagizo ya mwisho aliyotuachia ni tufanye kazi na wewe (Ruto) chini ya serikali jumuishi,” alisema Wanga. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, alisisitiza maneno ya mwisho ya Raila kuhusu uchaguzi wa 2027, akisema chama hakijafanya uamuzi wowote wa kumuunga mkono Ruto. 

“Hatujapitisha azimio lolote kama chama kusema tutaingiaje kwenye uchaguzi wa 2027. Kwa hivyo, popote ulipo, usikubali chama kijikite kwenye mambo ambayo hayajajadiliwa. Wacha mambo hayo yajadiliwe kwanza. Sisi ni ODM, nani aliyekuambia ODM haitakuwa na mgombea mwaka 2027? Kwanza fikiria kama ODM, tuna mpango ulio wazi ambao tumekubaliana; maamuzi mengine yatachukuliwa wakati ufaao,” Sifuna alieleza, akinukuu maneno ya mwisho ya Raila. 


2. THE STAR

 Gazeti hili liliangazia hotuba ya hisia za Rais William Ruto wakati wa kumuenzi marehemu Raila Odinga katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST), Bondo. 

Katika hotuba yake, Ruto alifichua jinsi waziri mkuu huyo wa zamani alivyopambana na matatizo ya kiafya siku chache kabla ya kufariki dunia nchini India. 

Rais alisema alianza kuwa na wasiwasi baada ya kugundua Raila alikuwa dhaifu alipokutana naye mara kadhaa. “Miezi moja na nusu iliyopita ilikuwa kipindi kigumu sana. Kila nilipokutana na Baba, sauti yake ilikuwa imekauka. 

Alikuwa akiniambia amechoka kwa sababu ya dawa alizokuwa akitumia, nami nikaanza kuwa na wasiwasi,” Ruto alikumbuka. 

Kiongozi wa nchi alifichua kuwa Raila alikuwa ametembelea Dubai na Marekani kutafuta matibabu. “Alikuwa ameenda Dubai na Marekani, na madaktari walimwambia mambo fulani kuhusu afya yake. Aliporudi, madaktari wake walimpa dawa zaidi,” alisema rais. Ruto alisimulia kuwa alitembelea nyumbani kwa Raila Karen, ambapo pamoja na familia yake, akiwemo Mama Ida Odinga, walikubaliana kumsafirisha Raila hadi India kwa matibabu kwa gharama ya serikali. 

“Kwanza alifikiria kwenda Ujerumani na China kabla ya kuamua India, ambako ana marafiki. Tulirahisisha kila kitu alichotaka waziri mkuu wa zamani,” alifafanua Ruto. 

Licha ya jitihada zake kuhakikisha Raila anapata matibabu bora, Ruto alisema alihuzunika sana alipokea ujumbe kutoka kwa Oburu Oginga kuhusu hali mbaya ya afya ya Raila.

 “Nilipokuwa njiani kuelekea ofisini (Oktoba 15), nilipokea ujumbe kutoka kwa Oburu (Odinga) akisema Raila hakuwa sawa. Nilishangaa kwa sababu alisema alikuwa anahisi vizuri. Nilipiga simu kadhaa, na dakika chache baadaye Oburu alinipigia tena na kuniambia, ‘Inaonekana Baba ametuwacha.’ Ilikuwa dakika chache baada ya saa moja asubuhi,” Ruto alisimulia. 

3. THE STANDARDS

Gazeti hili liliripoti kwa upana hotuba ya Mwakilishi wa Kenya katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Winnie Odinga. Wakati wa kumuenzi baba yake, Winnie alidokeza kwamba anaweza kujiingiza kwenye siasa za humu nchini ili kuziba pengo aliloacha waziri mkuu huyo wa zamani. Katika hotuba yake, Winnie alimshukuru rais kwa kumpa baba yake heshima za kitaifa na mazishi ya kifahari yenye heshima za kijeshi. 

DC KAGANDA: WATAKAOHUJUMU UCHAGUZI WATAKUMBANA NA MKONO WA SHERIA

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda.
Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, 

 

Kaganda ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 20, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vyovyote vitakavyolenga kuvuruga amani wakati wa uchaguzi.


“Tutawachukulia hatua za kisheria wote watakaothubutu kuhujumu zoezi la kupiga kura,” amesema Kaganda.

Aidha, amehimiza wananchi wote kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo akibainisha kuwa kupiga kura ni haki ya kikatiba na njia muhimu ya kuchangia maendeleo ya taifa.


“Ukiamua kukaa nyumbani na usifike kupiga kura, usije kujuta baadaye. Nafasi unayo, ila ukishindwa kuitumia, utakuwa umepoteza haki yako ya msingi,” amesisitiza.


Mkuu huyo wa wilaya amewahakikishia wananchi wote wa mjini na vijijini kuwa ulinzi na usalama umeimarishwa, hivyo waende wakapige kura kwa amani na utulivu, wakitumia haki yao ya kuwachagua Rais, wabunge na madiwani wanaowataka.

JAMHURI KUJIBU PINGAMIZI LA LISSU KWENYE KESI YA UHAINI LEO.

  Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.


Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, inaendelea kuunguruma leo Jumatatu, Oktoba 20, 2025, katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambapo upande wa Jamhuri unatarajiwa kuanza kujibu hoja za pingamizi zilizotolewa na Lissu.

Pingamizi hizo zinahusu upokelewaji wa video inayomuonesha Lissu akitamka maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini, ambayo upande wa mashtaka unataka iwe sehemu ya vielelezo vya ushahidi.

Lissu anakabiliwa na shtaka la kutoa maneno ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Katika hatua hii ya usikilizwaji wa ushahidi wa Jamhuri, mahakama inatarajiwa kujibu hoja nne za pingamizi zilizowasilishwa na Lissu mnamo Oktoba 17, 2025, kuhusu kupinga vielelezo vilivyotolewa na shahidi wa tatu wa Jamhuri, akidai visipokelewe kama ushahidi halali mahakamani.