ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, November 18, 2023

Benki ya CRDB yafungua tawi wilayani Magu mkoani Mwanza kusogeza huduma kwa wananchi

 

Magu. Tarehe 17 Novemba 2023: Siku chache baada ya kubeba tuzo za huduma bora na mtandao mpana wa mashine za kutolea fedha zinazotoa huduma, Benki ya CRDB imefungua tawi lake jipya wilayani Magu mkoani Mwanza.
 
Tawi hilo linaloifanya Benki ya CRDB kufikisha matawi 262 nchini kote, lilizinduliwa na Kaimu Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mheshimwa Hassan Masala ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Ilemela akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Amos Makalla.
 
Mheshimiwa Masala amesema jitihada za Benki ya CRDB kutanua wigo wake wa huduma zinaonekana na mchango wake utakuwa na tija kubwa kwenye jamii ya taifa zima kwani maendeleo ya kiuchumi yanategemea sana huduma za fedha.
“Tawi hili linaifanya Benki ya CRDB kufikisha jumla ya matawi 19 yanayotoa huduma mkoani mwetu hivyo nawasihi wananchi wenzangu wilayani Magu kulitumia vyema ili kujiinua kiuchumi. Hapa mtatunza fedha zenu kwa usalama zaidi, mtakopa kwa ajili ya biashara au malengo mengine binafsi hivyo kukamilisha mipango yenu kwa wakati. Nawashukuru Benki ya CRDB kwa kuja wilayani hapa, naamini wananchi watanufaika na fursa zenu bunifu zikiwamo za Programu ya Imbeju,” amesema Masala.
 
Akizungumza kwa niaba ya menejimenti, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya CRDB, Godfrey Rutasingwa amesema wateja watapata fursa ya kufungua akaunti zinazoendana na mahitaji yao halisi, mikopo binafsi, ya ujasirimali na biashara,  huduma za bima, kuunganishwa na mifumo ya kidijitali, pamoja na ushauri wa masuala ya fedha na uwekezaji.
 
Tangu ilipoanzishwa mwaka 1996, Rutasingwa amesema Benki ya CRDB imetanua mtandao wake wa huduma kutoka matawi 19 yaliyokuwepo mpaka 262, ukuaji unaoakisi dhima ya dhati ya benki hiyo kusogeza huduma karibu zaidi na Watanzania bila kujali wanaishi mjini au vijijini. 
“Tunakidhi mahitaji ya watumshi na wafanyakazi, wajasiriamali pamoja na wafanyabiashara. Kwa vijana na wanawake, tunayo Programu ya Imbeju inayotoa mtaji wezeshi. Programu hii ni mahsusi kwa makundi haya mawili hasa kwa wale ambao hawajakidhi vigezo vya benki. Ninawakaribisha wana Magu mje kupata huduma zetu,” amesema Rutasingwa.
 
Kwa wapenda michezo hasa mpira wa miguu, Rutasingwa amewaambia wana Magu na Watanzania wote kwa ujumla kuwa wateja waliopo na wale watakaofungua akaunti hivi sasa watapewa TemboCard itakayowapa fursa ya kushiriki kampeni ya 'Tisha na Tembocard Tukakiwashe AFCON' itakayowapeleka wateja 8 nchini Ivory Coast kushuhudia fainali za Michuano ya Mataifa Huru ya Afrika (AFCON).
 
“Safari znima italipiwa na Benki ya CRDB. Washindi watalipiwa kiingilio cha uwanjani na hoteli watakayolala itakuwa ni kwa gharama za Benki. Tunafahamu Watanzania wanapenda michezo hivyo huu ni wakati wao wa kuzitumia kadi zao ili washinde safari hiyo ya nchini Ivory Coast,” amesema Rutasingwa.
Wiki iliyopita, Benki ya CRDB ilishinda tuzo tatu kutoka Consumer Choice Awards Africa (CCAA) 2023 katika vipengele vya huduma kwa wateja, benki yeny emtandao mpana wa mashine za kutolea fedha (ATM) zinazofanya kazi pamoja na mkurugenzi mwenye usahawishi zaidi. 
 
Licha ya matawi yake yaliyoenea nchi nzima, Benki ya CRDB inao zaidi ya mawakala 25,000 wanaotoa huduma mtaani walipo wananchi nchi nzima, ATM 550 na matawi 21 yanayotembea. Vilevile, inazo mashine za ununuzi ya kadi (POS) zaidi ya 6,000 huku ikishirikiana na asasi ndogo washirika (microfinance) zaidi ya 500.
 
Kwa wanaopenda kulipa kidititali, Benki ya CRDB inayo programu ya Simbanking pamoja na huduma kupitia mtandao wa internet “Internet banking.”

Wafanyakazi Benki ya CRDB waadhimisha Siku ya Wanaume Duniani

 

Katika kuadhimisha Siku ya Wanaume Duniani, Benki ya CRDB imefanya semina ya siku moja kwa wafanyakazi wake wanaume ili kuwajengea uwezo katika masuala ya kisaikolojia, kimwili na kijami.

Semina hiyo iliendeshwa na madaktari pamoja na wanasaikolojia, na kufanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam. 

Licha ya kuwajengea wafanyakazi uwezo wa kusimamia mambo yao binafsi, pia imelenga kuongeza morali na kuwatia moyo wa kujituma zaidi kila wanapowahudumia wateja ili kukidhi mahitaji na matarajio yao ya kifedha.

Siku ya Wanaume Duniani huadhimishwa kila ifikapo Novemba 19 ya kila mwaka ili kutoa nafasi kwa wanaume kujadili maendeleo yao binafsi pamoja na ya familia zao na kutafuta suluhu ya changamoto wanazokabiliana nazo.

Zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya kilele cha maadhimisho hayo, wafanyakazi wa Benki ya CRDB wamepitishwa kwenye mada kadhaa ikiwamo afya ya akili, afya ya uzazi, familia na malezi pamoja na saikolojia ya jamii.

Mjadala huo umelenga kuwajengea uwezo wa kurahisisha maisha yao ndani ya ndoa, maisha binafsi pamoja na jinsi wanavyochangamana na jamii bila kusahau maisha yao wakiwa kazini.
Mtaalamu wa Masuala ya Saikolojia nchini, Dkt. Ellie Waminian akizungumza katika semina ya siku moja kwa wafanyakazi wa Benki ya CRDB wanaume ili kuwajengea uwezo katika masuala ya kisaikolojia, kimwili na kijami, iliyofanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB ambaye ni Afisa Mkuu wa Fedha, Fredrick Nshekanabo akizungumza katika semina ya siku moja kwa wafanyakazi wa Benki ya CRDB wanaume ili kuwajengea uwezo katika masuala ya kisaikolojia, kimwili na kijami, ikiwa ni sehemu kuadhimisha Siku ya Wanaume Duniani, iliyofanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam. 
Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile akizungumza katika semina ya siku moja kwa wafanyakazi wa Benki ya CRDB wanaume ili kuwajengea uwezo katika masuala ya kisaikolojia, kimwili na kijami, ikiwa ni sehemu kuadhimisha Siku ya Wanaume Duniani, iliyofanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam. 
Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya CRDB, Timothy Fasha akizungumza katika semina ya siku moja kwa wafanyakazi wa Benki ya CRDB wanaume ili kuwajengea uwezo katika masuala ya kisaikolojia, kimwili na kijami, ikiwa ni sehemu kuadhimisha Siku ya Wanaume Duniani, iliyofanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam. 









RAIS SAMIA ATUNUKU SHAHADA YA SAYANSI YA KIJESHI

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan awatunuku Kamisheni kwa Maafisa wanafunzi Kundi la 04/20-shahada ya Sayansi ya Kijeshi na Kundi la 70/22 (Regular) kwa Cheo cha Luteni Usu katika sherehe zilizofanyika kwenye Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (Tanzania Millitary Academy - TMA) Monduli ,jijini Arusha tarehe 18 Novemba 2023.

MAFANIKIO HAYANA UMRI - UNAWEZA KUFANIKIWA BAADA YA KUSTAAFU

 NA ALBERT G.SENGO/MWANZA

Kuna mifano mingi ya watu waliostaafu kisha wakafanikiwa. Ungana na Mr. Ngonyani wa Assembe Insuarance anayetupitisha kwenye darasa la kufahamu pia yafyatayo:- - Jeh unazifahamu mbinu za kukabiliana na matumizi mabaya ya fedha yanayopelekea wastaafu wengi kufilisika? - Wastaafu wengi huwa na maono makubwa wakati pesheni zao zikielekea kuiva, laikini hujikuta fedha zimeisha na hawajafanya chochote cha maana, jeh unajua nini kinachotokea? _ Kuna ile hali kwa mstaafu kuhisi kutengwa, kutothaminiwa tena ukilinganisha na kipindi kabla ya kustaafu yaani mtu alipokuwa kazini, alikuwa akipigiwa simu kuitwa kwenye matukio mbalimbali, vikao mbalimbali vya familia bila yeye maamuzi hayafanyiki, lakini leo hayupo kazini hayo yote hayafanyiki tena. Neno gani kwa mtu aliye kwenye hali hiyo na kipi anapaswa kutambua. #samiasuluhuhassan #wazee #tanzania #wastaafu #mwanza #nmb

RAIS SAMIA AUWA NDEGE WATATU KWA JIWE MOJA AJA NA MELI INAYOBEBA TRENI

 ALBERT GSENGO/MWANZA

Serikali imesema uwekezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa meli na miundombinu yake unaofanywa na serikali ya awamu ya sita katika ziwa viktoria,Tanganyika na Nyasa umefikia takribani shilingi trilioni moja,uwekezaji ambao haujawahi kutokea tangu taifa lipate uhuru.










Thursday, November 16, 2023

NEC YAKUTANA NA VYAMA VYA SIASA KUHUSU UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

 

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele akizungumza na wawakilishi kutoka Vyama vya Siasa kuhusu majaribio ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yanayotarajiwa kufanyika katika Kata za Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora na Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.
Vyama vya siasa vimehimizwa kushiriki kwenye majaribio ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yanayotarajiwa kufanyika katika Kata za Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora na Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele ametoa wito huo leo tarehe 16 Novemba, 2023 wakati akifungua mkutano wa Tume na vyama vya siasa jijini Dar es Salaam.
 
“Vyama vya siasa kwenye zoezi hili vitashiriki kwa kuweka wakala mmoja katika kila kituo cha kuandikisha wapiga kura, lengo ni kushuhudia na kujiridhisha juu ya taratibu zitakazotumika wakati wa majaribio ya uboreshaji wa Daftari,” amesema Jaji Mwambegele.
 
Amenongeza kuwa majaribio ya uboreshaji yanafanyika kwa lengo la kupima uwezo wa vifaa na mifumo itakayotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kufanyika nchi nzima kwa tarehe zitakazopangwa na kutangazwa na Tume.
 
Majaribio ya uboreshaji yatahusisha kuandikisha raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi na atakayetimiza umri wa miaka 18 kabla au ifikapo tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
 
Kundi lingine litakalohusika kwenye zoezi hili ni; wapiga kura wanaoboresha taarifa zao ambao wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo lingine, waliopoteza au kadi zilizoharibika, wanaorekebisha taarifa zao na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari.
 
Majaribio ya uboreshaji yatafanyika katika vituo 16 vya kuandikisha wapiga kura. Kati ya hivyo, vituo 10 ni vya Kata ya Ng’ambo na vituo sita (6) ni kutoka Kata ya Ikoma. Vituo vya uandikishaji vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
 
“Tume inatoa wito kwa wakazi wa Kata ya Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na Kata ya Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, kujitokeza kwa wingi kushiriki katika majaribio ya uboreshaji wa Daftari na kutoa ushirikiano kwa Tume wakati wote wa utekelezaji wa jukumu hili muhimu kwa mustakabali wa Taifa,” amesema Jaji Mwambegele.
Sehemu ya viongozi wa vyama vya siasa vikishiriki katika mkutano huo wa Tume na Vyama vya siasa.

Sehemu ya viongozi wa vyama vya siasa vikishiriki katika mkutano huo wa Tume na Vyama vya siasa.
Viongozi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) nao wakiwa katika mkutano hao.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uboreshaji wa majaribio wa Daftari La Kudumu la Wapiga Kura. 
BVR Kits zenye vifaa mbalimbali vinavyowasiliana ili kuchukua na kutunza taarifa za wapiga kura BVR Kits za sasa ambazo zinatumia programu ya android tofauti na BVR Kits za awali ambazo zilikuwa zinatumia programu ya Microsoft Windows.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele akifafanua jambo wakati wa majadiliano. 
Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa wakichangia mada wakati wqa mkutano huo wa Tume na Vyama vya siasa katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam leo Novemba 16,2023. 
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima akifafanua jambo wakati wa mjadala na wawakilishi wa vyama vya siasa. 

DC KIBAHA AFANYA UZINDUZI WA KANZIDATA KWA WAFANYABIASHARA WADOGO PWANI

 
NA VICTOR MASANGU,KIBAHA

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon amezindua rasmi mfumo kwa wafanyabiashara ndogo ndogo(Wamachinga) ambao uwapa fursa ya kuweza kujisajili kwa njia ya simu zao lengo ikiwa ni kutambulika kwa urahisi pamoja na kufahamu aina ya bidhaa wanazoziuza.

Mkuu huyo amezindua mfumo huo wakati wa mkutano maalumu ambao uliandaliwa kwa lengo la kuweza kujadili mambo mbali mbali ikiwemo suala muhimu la wafanyabiashara hao wahame kutoka mfumo wa zamani na kujisajili kwa njia ya kisasa zaidi ili watambulike.

"Kitu kikubwa wafanyabiashara ndogo ndogo natambua mpo wengi lakini suala la kuhakikisha sisi kama serikali tunawatambua ni vema mkajisajili kwa kutumia simu zenu na lengo lake kubwa ni kutambulika mnafanya nini katika shughuli zenu hii itatusaidia kupata na takwimu halisi,"alisema Saimon.
Kadhalika Mkuu huyo aliongeza kwamba ni lazima kujiwekea mipango madhubuti ambayo itaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa wafanyabiashara kuendesha shughuli zao katika mazingira mazuri na  ambayo yametengwa rasmi kwa shughuli zao.

Pia aliongeza serikali ya Wilaya itaendelea kushirikiana bega kwa bega na wafanyabiashara wote wadogo wadogo na kuwawezesha kiuchumi ili wawze kufikia malengo ambayo yamejiwekea ikiwemo kuweza kutambulika na serikali kupata takwimu za idadi yao.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la umoja wa machinga Mkoa wa Pwani (SHIUMA) Filemon Malinga alibainisha kwamba lengo lao ni kuwahimiza wafanyabiashara wote kujisajili kwa njia ya kisasa zaidi.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa endapo wafanyabiashara hao wakiingizwa katika mfumo mpya na kusajiliwa kwa njia ya simu zao itasaidia kupata idadi ya takwimu halisi ikiwemo na aina ya biashara ambazo wanazifanya katika maeneo yao mbali mbali.

"Tumejitahidi kupata wataalamu wa Tehama kutoka taasisi ya TIVA ambapo imeweza kupata fursa ya kuelimisha jinsi ya umuhimu wa wafanyabiashara hao kujisajili kwa mfumo wa kanzi data ambayo hii tutaondoka na ile hali ya kujisajili katika makaratasi,"aliongeza Mwenyekiyi.

Aidha Mwinyekiti huyo hapo awali waliwasajili wanachama wao kwa kutumia makaratasi lakini kutokana na teknolojia ilivyokuwa watajisajili kwa kutumia simu zao za kiganjani ili kuondokana na usumbufu wa hapo awali katika suala zima la ukusanyaji wa taarifa.

Kwa upende wake Mwenyekiti wa soko la Mnalani(Loliondo) Mohamed  Mnembwe amesema kwamba utaratibu huo wa wafanyabiashara kuweza kuingia katika mfumo wa kujisajili utasasaidia kujua idadi halisi pamoja na bidhaa wanazouza.

"Leo tumekutana katika huu mkutano ambao umewajumuisha wafanyabiashara ndogo ndogo wa Mkoa wa Pwani na haya maelekezo tuliyopewa na mtaakanu wa Tehama yataweza kutusaidia sisi kama wafanyabiashara "alisema Mnembwe.

Mnembwe alisema kwamba ana imani endapo wafanyabiashara wote wakielimishwa umuhimu wa kujisajili kwq simu kutaweza kuleta mabadiliko ya kimaendeleo kutoka na kufanya kazi kwa mfumo wa kidigitali na itasaidia kutambulika.

TIZAMA UPENDO WA ASKARI HUYU

 NA ALBERT G. SENGO

Askari Polisi wa kikosi cha usalama barabarani Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Koplo William akiwavalisha viatu watoto wawili ambao walikuwa na changamoto ya kutokuwa na viatu vya shule kwani wanaishi katika mazingira magumu huko Msolwa, Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Mkoa wa Pwani, tarehe 15, Novemba, 2023. Hivi karibuni askari huyo aligundua changamoto hiyo kwa watoto wakati akiwa kwenye kivuko cha watembea kwa miguu na kuamua kuwanunulia viatu ili kuwakinga na magonjwa hususani katika kipindi hiki cha mvua.

Wednesday, November 15, 2023

MWANZA: Wavuvi waanza kunufaika na mradi wa nishati ya jua

 

Teknolojia mpya ya ukaushaji dagaa kwa kutumia mitambo ya nishati ya umeme wa jua imetajwa kuwa mwarobaini wa kukabiliana na changamoto ya upotevu wa dagaa na hivyo kuongeza tija kwa wavuvi na wachuuzi mkoani Mwanza.

Teknolojia hiyo imebuniwa na kampuni ya Millenium Engineers ya jijini Mwanza inayotekeleza mradi wa ukaushaji na uchakataji dagaa kwa kutumia nishati ya jua katika mwalo wa Kayenze Ndogo wilayani Ilemela na kisiwa cha Kasalazi wilayani Sengerema.

Pia mradi huo unelenga kuzalisha na kusambaza taa za sola zenye mwanga wa kutosha kwa shughuli za uvuvi na hivyo wavuvi kuondokana na taa za karabai na betrii za asidi ambazo si rafiki kwa mazingira na viumbe hai.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Millenium Engineers, Mhandisi Diana Mbogo amesema; “tumeleta mitambo ya kwanza Afrika Mashariki kwa ajili ya kukaushia dagaa kwa kutumia nishati jadidifu. Hii itasaidia kupunguza upotevu wa dagaa zinazooza hususani nyakati za mvua kutokana na ukaushaji wa kutumia chanja”.

Akikagua utekelezaji wa mradi huo katika mwalo wa Kayenze Ndogo wilayani Ilemeka, Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu REA, Mhandisi Advera Mwijage amesema Serikali imechangia asilimia 30 (milioni 560) ya utekelezaji wa wa mradi huo ili kuhimiza matumizi ya nishati safi na salama katika kuinua uchumi wa wananchi na taifa.

“REA tunampongeza mwekezaji wa mradi huu na tunawakaribisha wawekezaji wengine maana uvuvi uko maeneo mbalimbali ikiwemo Mara na Kagera. Mitambo hii ina uwezo wa kukausha dagaa wengi kwa muda mfupi na hivyo kuleta tija kwa wananchi” amesema Mhandisi Mwijage.

Baadhi ya wachuuzi katika mwalo wa Kayenze Ndogo akiwemo Agness Selestine na Latifa Buchoji wamesema ukaushaji dagaa kwa kutumia nishati ya jua umewaondolea adha hasa wakati wa mvua na sasa dagaa zinakauka kwa ubora zaidi.

Kwa upande wake Frank Faustine ambaye ni mvuvi wa dagaa katika mwalo huo kwa zaidi ya miaka 15 amewahimiza wavuvi wenzake kuachana na uvuvi wa kutumia taa za karabai na kugeukia matumizi ya taa za sola kwani zina mwanga wa kutosha unaochochea mavuno zaidi ya dalai.

Mradi wa taa na ukaushaji dagaa kwa kutumia nishaji jua unatekelezwa na kampuni ya Millenium Engineers ya jijini Mwanza kwa thamani ya shilingi bilioni 1.2 ukifadhili wa wakala wa nishati vijijini REA, taasisi ya EEP Africa na STICHTING DOEN.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Millenium Engineers, Mhandisi Diana Mbogo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mradi wa ukaushaji dagaa kwa kutumia nishaji ya umeme jua katika mwalo wa Kayenze Ndogo wilayani Ilemela.
Wanahabari wakifanya mahojiano na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Millenium Engineers, Mhandisi Diana Mbogo.
Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu REA, Mhandisi Advera Mwijage akizungumzia umuhimu wa mradi huo katika kuinua uchumi wa wananchi na taifa.
Wanahabari wakifanya mahijiano na Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu REA, Mhandisi Advera Mwijage (kulia).
Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu REA, Mhandisi Advera Mwijage akijionea taa za sola zinazokubalika kwa matumizi ya uvuvi zikiwa zinachajiwa.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Millenium Engineers, Mhandisi Diana Mbogo akishuhudia taa za sola zikiwa zinachajiwa kwa ajili ya matumizi ya uvuvi.
Mkurugenzi wa Fedha kampauni ya Millenium Engineers, Victoria Japhet akijionea taa za sola zikichajiwa kwa ajili ya matumizi ya uvuvi.
Mmoja wa wavuvi katika mwalo wa Kayenze Ndogo, Frank Faustine akieleza umuhimu wa taa za sola katika shughuli za uvuvi.
Wavuvi katika mwalo wa Kayenze Ndogo wilayani Ilemela wakiwa kwenye maandalizi ya kuelekea kwenye shughuli za uvuvi katika Ziwa Victoria.
Mchuuzi wa dagaaa, Agnes Selestine akikausha dagaa kwenye mitambo ya ukaushaji dagaa inayotumia nishaji ya jua.
Mchuuzi wa dagaa katika mwalo wa Kayenze Ndogo, Latifa Buchoji akianika dagaa kwenye ndani ya mtambo wa ukaushaji kwa kutumia nishaji ya jua.
Mwonekano wa mitambo ya kukaushia dagaa kwa kutumia nishati ya jua katika mwalo wa Kayenze Ndogo wilayani Ilemela.
PIA SOMA>>> HABARI ZAIDI HAPA