ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, March 1, 2014

LIGI SOKA DARAJA LA KWANZA TZ BARA TOTO YAINYUKA 2-0 POLISI MARA

Ma-Kapteni wa timu za Toto (kulia) na Polisi Mara (kushoto) wakisalimiana mbele ya waamuzi kabla ya mchezo wao wa Ligi Soka Daraja la Kwanza Tanzania Bara, uliochezwa uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, dakika 90 zikimalizika Toto 2, Polisi Mara 0.
Kikosi cha Polisi Mara kilichoshuka leo dimbani CCM Kirumba kukabiliana na Toto Africans.
Mchezo wa Ligi soka daraja la Kwanza Tanzania bara katika kundi C baina ya Toto Africans na Polisi Mara umemalizika dimbani CCM Kirumba jioni ya leo kwa Toto Africans ya jijini humo kuibuka na ushindi mnono nyumbani kwa kuwabugiza Maafande wa Mara, bao mbili sifuri (2-0) Zaidi sikiliza taarifa ifuatayo toka Mwanza:- (BOFYA PLAY)

TATHIMINI YA MCHEZO WA YANGA DHIDI YA AL AHLY.

Na, Shaffih Dauda

Mpira umekwisha Yanga wanaondoka na ushindi

90' Yanga wanaongoza bado

82' Canavaro anaipatia Yanga bao la kwanza - Yanga 1 - 0 Al Ahly

70' Zikiwa zimebaki dk 20 mchezo kumalizika milango bado migumu - Yanga 0 - 0 Al Ahly

60' Yanga 0 - 0 Al Ahly

 49' Yanga wameshapata kona tisa na zote tasa

Kipindi cha pili cha mchezo kimeanza, Young Africans 0 - 0 Al Ahly
Mpira ni mapumziko, Young Africans 0 - 0 Al Ahly - Yanga wametengeneza nafasi tatu za wazi wameshindwa kuzitumia.43' Yanga 0 Al Ahly 0.

40' Milango ya timu zote bado migumu

37’ Yanga 0 Al Ahly 0.

Dakika ya 30, Young Africans 0 - 0 Al Ahly

26' Hamis Kiiza anakosa bao la wazi hapa

24' Yanga 0 - 0 Al Ahly

18' Emmanuel Okwi anapiga shuti kali kipa anaucheza na kupata majeraha

14' Yanga 0 - 0 Al Ahly

11’ Yanga wanapata kona ya pili inaokolewa na wachezaji wa Ahly. (0-0)

10’ Penaltyyyyyy hapana Refa anakataa kwa madai mshambuliaji wa Al Ahly alijidondosha. (0-0)

09’ Msuva anacheza fyongo pale. (0-0)

07’ Yanga wametawala kati, Msuva na Niyonzima wanaonana vizuri. (0-0)

5' Yanga wanapata kona na inaokolewa na Al Ahly

3' Al Ahly wanalishambulia lango la Yanga lakini Dida anaokoa hatari

1' Young Africans 0 - 0 Al Ahly 

Mpira ndio umeanza hapa Uwanja wa Taifa kati ya wenyeji Young Africans Vs Al AhlyKIKOSI CHA NACIONAL AL AHLY 

Ekramy, Moawad, Nagiub, Wael Gomaa, Fathy, Rabea, Ashaur, Mousa Edan, Gedo, na Amri Gamal

KIKOSI CHA YANGA 
1. Deogratias Munish "Dida" - 30
2. Mbuyu Twite - 6
3. Oscar Joshua - 4
4. Nadir Haroub "Cannavaro" - 23 (C)
5. Kelvin Yondani "Cotton" - 6
6. Frank Domayo "Chumvi" - 18
7. Saimon Msuva - 27
8. Haruna Niyonzima - 8
9. Emmanuel Okwi - 25
10. Mrisho Ngasa - 17
11. Hamisi Kizza - 20

Subs:
1. Juma Kaseja - 1
2. Juma Abdul - 12
3. David Luhende - 3
4. Athuman idd "Chuji" - 24
5. Hassan Dilunga - 26
6. Said Bahanuzi - 11
7. Didier Kavumbagu - 7

YANGA USO KWA USO NA AL-AHLY LEO.

Yanga ya Tanzania.
Al-Ahly ya Misri.
Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Mabingwa barani Afrika, Young Africans, maarufu kama "Yanga" leo hii wanakabiliana na mabingwa watetezi wa kombe hilo, Al-Ahly ya Misri katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kuingia katika hatua ya raundi ya kwanza ya michuano hii, Yanga waliitupa nje timu ya Comorro, Komorozine kwa kuichabanga jumla ya magoli 12-2. Katika mchezo wa kwanza na Komorozine, uliofanyika jijini Dar es Saalm,Yanga iliitwisha mzigo wa magoli 7-0 na kuiadhibu tena nyumbani kwao Comorro mabao 5-2, hivyo kujikuta katika raudni ya kwanza ikipangiwa kukutana na al-Ahly.
Yanga imekuwa na msukumo mkubwa wa kupata ushindi baada ya mwenendo wake wa kufanya vizuri katika michezo ya kimataifa na ligi kuu ya nyumbani. Katika mapambano yaliyopita kati ya Yanga na Al-Ahly, daima timu hiyo ya Misri imekuwa ikiibuka mbabe kwa kuifunga na kuitoa Yanga katika mashindano kama hayo kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, mthalani mwaka 2009, katika hatua kama hii Yanga ilichapwa na al-ahly mabao 4-0 na kutolewa nje.
Hata hivyo, safari hii, Yanga imeonekana kupania kusonga mbele katika michuano hiyo ya Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF, kwani imefanya maandalizi makubwa ikiwemo kupiga kambi ya wiki mbili nchini Uturuki, barani Ulaya na kuendelea kufanya vizuri katika ligi kuu ya nyumbani.
Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi Hans Pluijn anajivunia kikosi chake na kutamba kwamba safari hii, al-Ahly hawatatoka salama katika Uwanja wa Taifa, akijigamba kwamba atawafunga kwani anazifahamu vizuri mbinu za timu hiyo.

Mechi nyingine zitakazochezwa leo za mabingwa wa kombe la Afrika ni Gor Mahia ya Kenya watakuwa wenyeji wa EST ya Tunisia, Kampala City Council ya Uganda itasafiri kwenda Zambia kumenyana na Nkana Red Devil.
BBC: SWAHILI.

TOTAL YAZINDUA MPANGO WA KUMALIZA TATIZO LA UPATIKANAJI WA UMEME.


Mgeni rasmi, Waziri wa Nishati na Madini, Mh. Prof. Sospeter Muhongo akihutubia wageni waalikwa (hawapo pichani) waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa bidhaa za AWANGO uliofanyika ndani ya hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam, usiku wa jana. Waziri Muhongo aliwapongeza TOTAL kwa juhudi wanazozifanya kusaidia jamii ya Watanzania kupata chanzo cha nishati kitakachowaletea maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Pembeni ni baadhi ya bidhaa hizo zinazotumia nishati ya jua
Waziri wa nishati na madini Prof. Sospeter Muhongo (kulia), mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa bidhaa zinazotumia nishati ya jua kuzalisha umeme zinazojulikana kama AWANGO, wa kwanza kushoto ni Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mh. Marcel Escure pamoja na Mkurugenzi mkuu wa TOTAL nchini Tanzania Bw. Stephane Gay wakishuhudia tukio mojawapo katika hafla hiyo.
Kikundi cha burudani kikionyesha umahiri wa kutoa burudani kwa wageni waalikwa (hawapo pichani) kuashiria uzinduzi rasmi wa AWANGO. AWANGO ni bidhaa zilizo chini ya Mradi wa ‘Total Access to Solar’ ulioanzishwa na kampuni ya TOTAL mwaka 2010 kusaidia kutatua tatizo la upungufu wa nishati kwa nchi zinazoendelea ukiwalenga watu wa kipato cha chini hasa wa vijijini na pembezoni mwa miji.
Meneja wa Maswala ya Kisheria na Ushirika wa kampuni ya TOTAL Tanzania Bi. Marsha Msuya akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya uzinduzi wa bidhaa za AWANGO zilizo chini ya mradi wa TOTAL unaojulikana kama ‘Total Access to Solar’ (TATS) wenye lengo la kutatua tatizo la ukosefu wa umeme nchini Tanzania kwa jamii ya watu wa kipato cha chini. Bi. Marsha alisema kuwa bidhaa hizo zitafika katika mikoa yote nchi nzima.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TOTAL YAZINDUA AWANGO KUMALIZA TATIZO LA UPATIKANAJI WA UMEME KWA WATU WA KIPATO CHA CHINI TANZANIA
Dar es salaam, 27 Februari, 2014.
Tatizo la ukosefu wa nishati ya umeme kwa jamii ya watu wa kipato cha chini Tanzania linatarajiwa kufikia kikomo, baada ya TOTAL, moja ya kampuni inayoongoza katika biashara ya nishati duniani, kupitia mradi wa ‘Total Access to Solar (TATS)’ kutambulisha aina mpya ya bidhaa za taa pamoja na vifaa vya kuchajia simu vinavyotumia nishati ya jua vyenye kudumu na vinavyopatikana gharama nafuu nchini Tanzania.   
 
Total Access to Solar (TATS) ni mradi ulioanzishwa na TOTAL mwaka 2010, ukiwa na shabaha ya kuhakikisha upatikanaji wa suluhisho la vifaa vya nishati mbadala katika soko la dunia kwa matumizi ya kijamii na kiuchumi ikilenga jamii ya kipato cha chini.  Mradi wa TATS unaendana na mlengo wa kibiashara wa TOTAL ambao ni “Kuwajibika katika upatikanaji wa nishati kwa watu wengi zaidi kadri inavyowezekana, na kupambana na mahitaji ya dunia”

Miradi ya TATS yote inalenga katika kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika shughuli za kijamii na kiuchumi kwa kutumia nishati itokanayo na vyanzo vya uhakika vikiwemo Jua, Gesi, Mafuta na mabaki ya plastiki. Kwa kugundua mahitaji makubwa ya nishati mbadala kwa Watanzania, TOTAL Tanzania kupitia TATS imezindua rasmi bidhaa mpya zilizo chini ya mradi wa AWANGO, zikiwa ni maalum kwa ajili ya jamii ya Kitanzania.

AWANGO ni mradi unaoleta bidhaa zinazotumia nishati ya jua kuweza kuzalisha umeme. Lengo kuu ni kuwezesha matumizi ya nishati ya jua kama suluhu itakayowezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika na nafuu kwa jamii ya watu wa kipato cha chini wanaoishi vijijini na pembezoni mwa miji.

Kabla ya kuzinduliwa Tanzania, mradi wa AWANGO ulishaanza kufanya kazi katika nchi nne duniani huku ukifanyiwa majaribio kwa zaidi ya mwaka mmoja. Baada ya mafanikio katika nchi za Cameroon, Indonesia, Kenya na Jamhuri ya Kongo, zaidi ya taa 125,000 na vifaa vya Jua viliuzwa, baadae mradi huu ulikua na kufikia nchi nyingine nane.

Akihutubia wakati wa uzinduzi wa AWANGO, mgeni rasmi Mhe. Prof. Sospeter Muhongo, ambae ni Waziri wa Nishati na Madini aliwapongeza TOTAL kwa kusaidia kutatua kero ya upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini, “kwa niaba ya Serikali, nawapongeza TOTAL kwa kwenda mbali zaidi na kuona uhitaji wa wananchi wetu juu ya mabadiliko na kupiga hatua ya kutatua tatizo upatikanaji wa nishati”.

“TOTAL Wameweza kugundua njia bora ya kuisaidia jamii kwa kuleta vifaa ambavyo vitawasaidia kwenye shughuli za kijamii na kiuchumi. Kama wizara husika tunatambua mchango wa TOTAL kwenye hili na tunawahimiza kuendelea na juhudi zao za kutoa nishati ya gharama nafuu itayopatikana kwa urahisi kwa umma wa Watanzania.” Alisema Prof. Muhongo. 

Kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya umeme yanayoongezeka kila siku, bidhaa za AWANGO zimetengenezwa kukabiliana na ongezeko hili. Ufanisi, unafuu na kudumu kwa muda mrefu ndio sababu kubwa zinazofanya ya vifaa vya AWANGO kuwa tofauti na vifaa vingine vilivyozoeleka kutumika na jamii ya kipato cha chini.

Akizungumza juu ya upatikanaji wa bidhaa hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa TOTAL Tanzania Bw. Stephane Gay alisema kwamba bidhaa hizi zitapatikana katika vituo vyote vya mafuta vya TOTAL vilivyopo takribani mikoa yote ya Tanzania, lakini pia kampuni hiyo itashirikiana na wadau wa maendeleo zikiwema asasi za kijamii katika usambazaji, ikiwa ni Dhamira ya kupeleka bidhaa za AWANGO nchi nzima.

Ikiwa kama bidhaa ya kibiashara inayosaidia jamii, AWANGO imejidhatiti katika kutoa huduma bora na ufanisi mkubwa kama ilivyo TOTAL. Mradi huu unatazamiwa kuwa na matokeo matatu katika njia tofauti za Kiuchumi, kijamii na kulinda mazingira. Shabaha kubwa ni kumpa Mwananchi wa kipato cha chini nguvu ya kujikwamia kimaendeleo kijamii na kiuchumi.

KUHUSU TOTAL
TOTAL Tanzania Ltd ni kampuni inayojishughulisha na usambazaji wa bidhaa za nishati ya petroli na mafuta ghafi. Kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 1969 ikiwa na makao makuu yake Dar Es Salaam, Tanzania

KILA IJUMAA SKYLIGHT BAND YAZIDI KUKONGA NYOYO MASHABIKI ZAKE

DSC_0229
Joniko Flower akiongoza safu ya Skylight Band kutoa burudani kwa mashabiki wa Bendi hiyo Ijumaa iliyopita kwenye kiwanja chao cha Nyumbani Thai Village Masaki jijini Dar.... Ni kila Ijumaa zote za wiki wanakuwa hapo kwa ajili ya kuwapa burudani mashabiki wake!!!
DSC_0244
Meneja wa Band Aneth Kushaba AK47 na Winfrida Richard wakiwajibika jukwaani kuwapa utamu mashabiki wa Skylight Band.
DSC_0253
Hashim Donode na Winfrida Richard wakitawala jukwaa huku wakisindikizwa na Digna Mbepera pamoja na Mary Lucos.
DSC_0173
Madiva wa Skylight Band wakisaka Dough....... Kutoka kushoto ni Winfrida Richard, Mary Lucos na Digna Mbepera.
DSC_0284
Babu Athumani akiwapa raha mashabiki wa Skylight Band.
DSC_0163
Joniko Flower, Sony Masamba na Sam Mapenzi wakisebeneka taratibu bila jasho..!!!
DSC_0322
Mheshimiwa Bundala akiwa na kijana wake Emmanuel Francis (wenye vest) wakisebeneka na midundo ya Skylight Band.
DSC_0366
Hapo ni Yachuma chuma mwanzo mwisho...!!
DSC_0334
Skylight Band ndio habari ya mujini usiku wa leo ndani ya kiota cha Thai Village Masaki jijini Dar.
DSC_0337
Pananogaje......Picha inaongea...!!
DSC_0347
Wadau wakishow love na Ukodak.
DSC_0361
Wadau wa Skylight Band wakipata Ukodak.
DSC_0385
Mchezaji mkongwe wa Kabumbu John Mwansasu akishow love na Lubea wa Skylight Band pamoja na mdau ndani ya kiota cha Thai Village Ijumaa iliyopita.
DSC_0353
Mdau Dagma (mwenye miwani), Pacha wa Customer Care, Lubea pamoja na Mdau wakipata Ukodak.

Thursday, February 27, 2014

ALILAZIMIKA KUKEKETWA ILI ASOMESHWE.

ESTER CHARLES (16) ambaye anasoma kidato cha tatu katika shule ya Sekondari Rebu iliyoko wilayani Tarime mkoani Mara, alishindwa kujizuia na kudondosha machozi katika ukumbi wa kantini ya jeshi la polisi wilayani Tarime baada ya kueleza masaibu aliyokumbana nayo kwa kufanyiwa ukeketaji na wazazi wake.

Anapofanyiwa ukeketaji huaminika kuwa mwanamke kamili aliyeondolewa mkosi na ambaye anastahili kuolewa. Wakati anafanyiwa ukatili huo, Esta alikuwa anasoma darasa la saba katika shule ya msingi Rebu, ambapo mara baada ya kukeketwa, anasema alipata maumivu makali ikiwa ni pamoja na kutokwa na damu nyingi.

Anasema alikubali kufanyiwa ukeketaji na wazazi wake baada ya kufaulu mtihani wa darasa la saba na alikuwa na hamu ya kuendelea na masomo, lakini akapewa masharti na wazazi wake kuwa ili aendelee na masomo lazima akeketwe.

“Sikuwa na jinsi, nilijua ningeenda kukumbana na maumivu makali na kwasababu nilikuwa napenda  shule ilinibidi kukeketwa” anaeleza.
Kutoka maktaba ni moja ya nyenzo za ukeketaji.
UKEKETAJI UNAFANYIKAJE?
Anasema aliamshwa saa 11:30 alfajiri akiongozana na mama yake na wanawake wengine watatu alikwenda kuungana na wasichana wenzake waliokuwa kwenye orodha ya kufanyiwa ukeketaji na kupelekwa mtoni kuogeshwa!

Tuliogeshwa na kupewa maneno ya ujasiri ili tusilie wakati wa kukeketwa “ anasema na kuongeza kuwa Ngariba alilipwa kiasi cha Sh. 10,000/= kwa kila msichana aliyekeketwa (kwa wakati huo). Esta anasema kuna eneo maalum lililotengwa kwaajili ya shughuli hiyo na msichana hushikwa mikono yake kwa nyuma na mama aliyekeketwa.

“Baada ya kufika eneo lile, tulitangaziwa na ngariba kuwa kila mmoja awe na wembe wake, ambao ndiyo alitumia kukeketa” anasema.

Anachokumbuka siku hiyo ni kujikuta tayari amekwisha keketwa huku akitokwa na damu nyingi na maumivu makali. Anasema baada ya kukeketwa, wasichana wote waliwekwa katika uangalizi wa akina mama wasaidizi wakiwemo baadhi ya ngariba, huku wakiwapatia dawa za kienyeji wale wanaovuja damu iliisiedelee kuvuja.

“Nilishindwa kula, nilikunywa uji tu, siku ya pili nilipata maumivu makali baada ya kuamshwa asubuhi kwenda kuogeshwa” anaeleza.
Wakisikiliza kwa makini ni washiriki wa Kongamano hilo lililokuwa mahususi kwa ajili ya kuibua changamoto zilizopo katika jamii kuhusu suala la ukeketaji
Anasema msichana anapotoka jandoni inambidi ashiriki tendo la ndoa na mwanaume ambaye amefanyiwa tohara kama ishara ya kukubali kuwa binti aliyekeketwa kuwa mwanamke kamili na anayestahili kuolewa. Msichana aliyekeketwa huitwa ‘Omonke’.

Anaiomba serikali, asasi za kiraia na waandishi wa habari kutoa elimu ya madhara ya ukeketaji kwa watoto wa kike, na kwa ngariba wapewe elimu ya kutosha dhidi ya madhara ya ukeketaji.

“Wengi huku Tarime wanafanya hivyo, wakijivunia kukeketwa kutekeleza mila lakini pia ngariba bado hawajapata elimu ya madhara ya ukeketaji, naiomba serikalia na wadau wengine watoe elimu zaidi juu ya madhara ya ukeketaji” anasema na kuongeza kuwa jamii yao huamini kuwa wakimkeketa motto wa kike huleta Baraka katika familia.
NI MADHARA GANI ALIYOKUMBANA NAYO?
Anasema baada ya kukeketwa aliumia sana na aliathirika kisaikolojia ikiwemo kuzomewa nna wasichana wa rika yake ambao hawakuwa tayari kukeketwa.

“Siku niliyokeketwa, nilipata shida sana, nilikuwa na hofu hata wenzangu walikuwa wakinicheka, hata nilipopona nilichukua muda kurudi shule, niliathirika sana” anasema madhara mengine aliyo yapata ni pamoja na kuchanika sehemu zake za siri, kutokana na kukeketwa akiwa na wasiwasi kama atajifungua salama siku za baadaye.

“Mimi nahisi hata wakati wa kujifungua, nitapata matatizo, naomba wazazi wetu wabadilike waanze kwenda na wakati na watambue kuwa wanapotufanyia ukeketaji wanatufanyia ukatili wa kijinsia na kilema cha maisha” anasema.

Anasema kuwa kuna uwezekano wa wasichana wanaokeketwa kupata virusi vya ukimwi kutokana na kukeketwa ba ngariba mmoja, ambaye hukeketa zaidi ya wasichana 50 kwa siku.

Ester anaahidi kuhakikisha wadogo zake Neema na Happy kuwa hawato keketwa kwani yeye kashakuwa mkubwa anayejitambua ana kujua kujieleza.

NDOTO ZA BAADAYE ZA ESTA.
“Nitasomea uandishi wa habari, nitafanya kazi kwa bidii na natamani niwe kama Waziri wa Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Watoto, Sophia Simba. Nampenda jinsi anavyo wahudumia wanawake” anasema.

Ameiomba serikali kupitia jeshi la polisi kuwakamata mangariba wote wanao husika kufanikisha ukeketaji na kuwafikisha mahakamani, ili sheria ichukuemkondo wake .

Anaitaka jamii ya Wakurya kuendeleza watoto wa kike kitaaluma zaidi badala ya kuwaoza wakiwa katika umri mdogo, na hivyo kushindwa kuhilili kutunza familia.
Kamanda Emmanuel Mkoma.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime – Rorya, Emmanuel Mkoma anasema kuwa jeshi la polisi kwa kushirikiana na wadau wengine wilayani Tarime, limeanza kutoa mafunzo ya tohara mbadala itakayo iwezesha jamii kutambua athari za ukeketaji kwa watoto wa kike.
Askari polisi, wanafunzi wa shule za sekondali na tiba ni sehemu ya kusanyiko la washiriki wa Kongamano lililokuwa mahususi kwa ajili ya kuibua changamoto zilizopo katika jamii kuhusu suala la ukeketaji.
Hisia za mmoja kati ya wanafunzi wa kiume na uelewa wa suala la ukatili wa kijinsia na ukeketaji wilayani Tarime mkoani Mara.
Wakisikiliza kwa makini ni wadau wa KIVULINI, Jeshi la Polisi na Wanahabari.
Lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu kwa jamii, ambapo watoto wa kike watapewa elimu ya malezi ya Afya zao itakayo wasaidia wasikeketwe, msisitizo wake ni kuelimisha jamii ione madhara ya ukeketaji na kadri siku zitakavyo kwenda jeshi la polisi linaimani kuwa jamii itaachana na ukeketaji.

TFF YASITISHA MKATABA NA KOCHA KIM POULSEN

Kim Poulsen.
Hatimaye Shirikisho la Kabumbu nchini Tanzania TFF limetangaza kuvunja mkataba wake na Kocha mkuu wa Timu ya taifa ya soka ya Tanzania Taifa Stars Kim Poulsen kwa kile kilichoelezwa maafikiano ya pamoja baina ya kocha huyo,TFF, na Serikali.
Jamal Malinzi ambaye ni Rais wa Shirikisho la soka Tanzania amesema kuwa huo ni utaratibu wa kawaida hasa baada ya wadau mbali mbali kuona kuwa huu ni wakati wa kufanya mabadiliko ya lazima katika benchi la ufundi la Taifa Stars ambayo inajiandaa kwa mechi za kufuzu kwa Fainali za kombe la mataifa Afrika hapo mwakani zitakazofanyika nchini Morocco.
Kuhusu gharama za kuvunja mkataba na Kocha huyo Bwana Malinzi amesema serikali haitagharamia uvunjaji huo wa mkataba na kocha huyo na badala yake wapo wadau waliojitokeza kugharamia kutokana na kuona umuhimu wa kufanya mabadiliko katika kipindi hiki kwa faida ya soka la Tanzania.
Kwa Upande wake Kocha Kim Poulsen amesema na rekodi yake inaonyesha kuimarika kwa soka la Tanzania katika kipindi cha takriban miaka miwili aliyokuwa akikinoa kikosi cha Taifa Stars lakini kusitishwa mkataba ni jambo la kawaida kwa kocha yeyote baada ya kipindi fulani kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine na ndiyo sehemu ya maisha.
“Kama kocha unapoona ndiyo umefanya kazi yako,unapaswa kuangalia mbele zaidi baada ya kufanya kazi yako si lazima uendelee kuwa hapo, mnakaa na kujadiliana na kuachana kwa amani kisha unapaswa kusonga mbele,ninaondoka nikiwa najivunia kipindi nilichofundisha soka hapa,na ninawatakia kila la kheri Tanzania na Taifa Stars kwa ujumla.”alisema Poulsen.
Kuhusu Kocha mpya wa Taifa Stars Jamal Malinzi ambaye ni Rais wa TFF amesema hadi sasa wapo makocha watatu raia wa Uholanzi ni wawili na Mjerumani mmoja wanaosailiwa kwa ajili ya kumrithi Kim Poulsen,lakini moja ya vigezo Malinzi amesema kuwa ni lazima kocha huyo awe amewahi kuipeleka kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika moja ya nchi zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara.
Katika hatua nyingine kocha Salum Madadi ameteuliwa kukaimu nafasi iliyoachwa wazi na Kim Poulsen ambapo kocha huyo akisaidiwa na Hafidh Badru kutoka Zanzibar watasimamia Taifa Stars kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Namibia iliyoko kwenye kalenda ya FIFA baadaye mwezi ujao.
CHANZO: BBC SWAHILI

SAFARI NYAMA CHOMA - ARUSHA NA MOSHI

Jaji kiongozi, Laurent Salvi akitoa maelezo ya mfano wa namna ya
kukagua nyama iliyoiva kwa washiriki wa warsha ya nyama choma,
iliyoandaliwa na waandaaji wa mashindano ya Safri Lager Nyama choma
Festival.(picha na mpiga picha wetu).
Jaji kiongozi akimkabidhi cheti cha ushiriki, mwakilishi wa Baa ya
Makanyaga, Freeman Rogarth, baada ya kumalizika kwa warsha hiyo.(picha na mpiga picha wetu).
Jaji kiongozi akimkabidhi mwakilishi wa Baa ya East Afrika, Beda
Paschal cheti cha ushiriki katika hafla ya kufunga mafunzo ya namna ya
kuchoma nyama.(picha na mpiga picha wetu).
Na Mwandishi Wetu. 
Moshi na Arusha.
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Safari Lager jana imetoa mafunzo kwa wachomanyama kutoka Baa mbalimbali za Mkoa wa Moshi na Arusha ikiwa ni maandalizi ya mashindano ya Safari Nyama Choma kwa mwaka 2014 yatakayo fanyika katika viwanja vya General Tyremachi 15 na viwanja vya CCM mkoa kwa Mkoa wa Kilimanjaro machi 16 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja masoko wa TBL, Leia Hermenegild alisema lengo la kutoa mafunzo ni kutoa elimu kwa wachoma nyama ukizingati auchomaji nyama ni moja sehemu ya kujiingizia kipato katika Bar.

Leiya alisema kutokana na hali hiyo wakaona ni vema wakaendesha Semina kwa wachoma nyama ili waweze kukidhi vigezo vya mahitaji ya Wateja ili waweze kufurahia Nyama choma kama ilivyo kwa vyakula vingine ili kuendana na kauli Mbiu ya Bia ya Safari Lager isemayo“ Safari Lager bila nyama choma haijakamilika.”

Aliongeza kuwa baada ya mafunzo hayo yaliyo tolewa kwa wachoma nyama wa Baa ambao walitunukiwa vyeti vya ushiriki  pia kutakuwa na mashindano ya kuchoma nyama ambapo washindi 10 watapatikana kutokana na watakaofuzu vigezo namasharti waliyopewa katika semina hiyo.

Alisema Fainali za Mashindano zitafanyika Machi15 kwa mkoa wa Arusha na machi 16 kwa mkoa wa kilimanjaro, Mwaka huu ambapo washindi watapewa zawadi kuanzia mshindi wa kwanza atakaye jinyakulia Shilingi Milioni moja na Kikombe, mshindi wa pili Lakinane, Mshindi wa tatu Laki 6, 

Mshindi wa nne laki nne na Mshindi wa Tano shilingi laki mbili huku mshindi wa Sita hadi wa Kumi watajinyakulia kifuta jasho cha shilingi 50,000/= kwa kila mkoa.

Alisema namna ya kuwapata washindi ni kutokana na wateja kupiga kura katika utaratibu utakaobandikwa katika Baa shiriki ambapo mteja atapiga kura kupitia simu ya mkononi ili kuichagua baa inayo choma nyama vizuri.

Kwaupande wake Mkufunzi wa Mafunzo hayo, Laurence Salvia mbaye pia ni Jaji Mkuu wa mashindano hayo amesema huwezi kuandaa mashindano bila ya kutoa Elimu, hivyo TBL wamefikiria jambo la msingi sana lenye manufaa kwa waandaaji yaani wachoma nyama mpaka kwa watumiani yaani mlaji.

Bwana Lawrence binfsi aliishukuru TBL kupitia bia ya Safari Lager kufikiria jambo zuri la kufadhili elimu kwa wachoma nyama jambo ambalo sifaida kwa wachomanyama tubali hata watumiaji sasa watakula nyama inayostahili.

ALICHOSEMA SHIBUDA HII LEO KATIKA BUNGE LA KATIBA: APINGA KURA YA WAZI.

SHIBUDA APINGA KURA ZA WAZI BUNGE LA KATIBA.
"Hapa hatukuja kwa maslahi ya kusema ya kwamba tukisigana tuondoke hapana. Hapa tumekuja kutoka na katiba"

"Nashauri tuachane na dhana ya uenzetu na si mwenzetu kwani zitazaa fitna ambazo zitazaa kusigana na kupotoka mwenendo wetu"

"Kukosekana na busara inayotanguliwa na hekima hii huwa inaibua maslahi ya kusigana na huibua fikra za kuzaa mikongamano ambayo haina maana"

"Tuhakikishe tunakuza upatanifu umoja na mshikamano kupitia kanuni zetu zinazotuongoza la sivyo nasikitika kwamba kura ya uwazi haijengi uaminifu wa kumpa mtu shurti ya maadili ya utiifu, kwa hiyo napendekeza mfumo wa kura za usiri ili kulinda amani na utulivu".

Wednesday, February 26, 2014

MBUNGE AIRO AMTAKA DC WA RORYA KUACHA KASHFA PIA AWAACHE WATAALAMU WAFANYE KAZI YAO.

Na PETER FABIAN
MBUNGE wa Jimbo la Rorya Bw. Lamerck Airo amemvaa Mkuu wa Wilaya ya Rorya akimtaka kuacha kuwasha kuwashutumu wanasiasa kuwa ndo wanakwamisha ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ya Rorya na kuwakingia kifua wataalamu wanaofanya ubadhilifu wa fedha za umma.

Mbunge Airo alisema kuwa kitendo cha Mweka Hazina kufanya ubadhilifu wa milioni 111.7 na kuhamishwa huku baadhi ya Madiwani 16 wakibariki aondoke kwa kuhamishwa bila kuchukuliwa hatua jambo ambalo limeshangaza wengi wakiwemo Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo.

Airo pia ameitaka serikali kupitia Wizara ya TAMISEMI kuchua hatua za haraka kumrejesha Wilayani humo aliyekuwa Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Bw. Renatus  Mtasiwa baada ya kufanya ubadhilifu wa zaidi ya shilingi milioni 111.7 za Halmashauri hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Mwanza , Mbunge huyo alisema kwamba kutokana na kitendo cha kuhamishwa kwa aliyekuwa Mweka Hazina Mtasiwa kufanya ubadhilifu wa fedha za Ruzuku ya shule (Capitation) kiasi cha shilingi milioni 21, fedha za likizo za walimu kiasi cha shilingi milioni 90 kuzichota na kuzitumia tofauti na ilivyokusudiwa ni wizi ambao anatakiwa kuchukuliwa hatua kali za kimaadili na kisheria.

Bw. Airo alisikitishwa na taarifa za Mweka Hazina huyo, ambapo alidai kuwa siku mbili kabla ya Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Rorya ambacho kiliketi hivi karibuni nayeye kushindwa kuhudhulia kutokana na kuwa kwenye majukumu mengine ya Kamati ya Bunge ambapo inadaiwa kuwapatia baadhi ya madiwani pombe na kuwalewesha kwa siku mbili ili kutomjadili na kuruhusu ahamishwe kama ilivyoelezwa kwenye kikao hicho.

“Nimesikitishwa sana na hili suala kwani Mweka Hazina alikuwa anakaimu Nafasi ya Mkurugenzi akitoka na muda mfupi akifanya ubadhilifu kwa kiwango cha fedha shilingi milioni 111.7 lakini alichokifanya akaenda kuomba uhamisho Wizarani na sasa kahamishiwa Hamashauri moja Mkoani Morogoro hivi hili kweli ni halali” alihoji kwa mshangao .

Aliongeza kuwa pamoja na kuwepo ubadhilifu huo baadhi ya Madiwani sita (6), Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rorya Bw. Charles Ochele na Mkurugenzi halmashauri hiyo kwenye kikao hicho walitaka baraza liazimie kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kumtaka arejeshe fedha za Likizo na Walimu alizotafuna lakini baadhi ya madiwani 16 kati ya 23 walidaiwa kuhongwa na kunyweshwa pombe kuwapinga.

Aidha Mbunge Airo alisisitiza kuwa suala hilo bado atalivalia njuga hadi kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa TAMISEMI Bi Hawa Ghasia ili kumshughulikia Mweka hazina huyo ikiwa ni pamoja na kumrejesha ili kurudisha fedha alizotafuna kama alivyo ahidi akijibu maswali ya baadhi ya wabunge waliotaka wezi kwenye halmashauri wasihamishwe na hata wakihamishwa warudi kujibu tuhuma zao za wizi.

Akizungumzia suala la Mkuu wa Wilaya Rorya kuwatuhumu moja kwa moja wanasiasa kuwa ndiyo wanakwamisha ukusanyaji wa makusanyo ya mapato ya Halmashauri ya Wilaya hiyo na kushuka kwa kiwango kikubwa, alisema kwamba hatua hiyo iliyojitokeza kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Mara (RCC) hivi karibuni ilikuwa na lengo la kupotosha ukweli kwa wajumbe wa kikao hicho.

Mbunge Airo alisema taarifa iliyozungumzwa na DC wa Rorya haikuwa na ukweli na inaonyesha anavyokurupuka kujibu hoja ambazo alipaswa kumachia Mkurugenzi kuzijibu ambaye ni Mtaalamu na mwenye kuwa na takwimu au hata Mwenyekiti na si yeye ambaye amekuwa mtu wa kudanganywa na kisha  kuzungumza vyombo vya habari bila utafiti wa kina.

“Nilimsikia akidai kuwa baadhi ya wanasiasa ndo wamechangia kushuka kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri kupitia vyanzo vyake na alikwenda mbali kuwatuhumu wanasiasa bila hata kumshirikisha Mkurugenzi na Mwenyekiti Bw. Ochele kwani wao ndio walipaswa kujibu au ndiyo walikuwa na majibu sahihi ya kile kilichopelekea kushuka kwa ukusanyaji huo kwa mwaka wa 2013/2014 ya bajeti iliyopita.

Alifafanua kuwa kutokana na kauli hiyo, ameamua kuweka wazi kilichotokea kwenye Jimbo lake na Halmashauri hiyo kwa kueleza kuwa kwanza amesikitishwa na kauli aliyoitoa DC huyo ya kuwatuhumu baadhi ya wanasiasa lakini katika makisio ya bajeti ya mwaka 2013/2014 walipanga kukusanya shilingi milioni 615 za ada ya malipo ya kuuza viwanja, lakini hazikukusanywa na badala yake ilikusanywa shingi milioni 21,293,000/= tu.

“Hapa malengo hayakufikiwa sasa viwanja havikuuzwa kutokana na Serikali kushindwa kupeleka kwa wakati fedha ya kulipia fidia kama Halmashauri ilivyoomba  huku makusanyo ya ada baada ya kuuzwa viwanja ikiwa ya maombi ya viwanja hivyo ilikuwa ikusanywe kiasi cha shilingi milioni 12 na badala yake wamepata milioni 92.8”alisema

Aliongeza kuwa, makusanyo ya kodi za viwanja baada ya kuviuza walitegemea kukusanya milioni 16 zakini walikusanya shilingi milioni 5, 279,000/= tu sawa na asilimia 33 huku makusanyo ya ambayo ambayo hayakufikiwa ikiwa ni zaidi ya shilingi mia sita kutokana na kukosekana malipo ya fedha za fidia baada ya kucheleweshwa na serikali na kupelekea kushuka kwa makusanyo na mapato ya halmashauri hiyo.

Aidha ushuru wa maegesho ya Pikipiki kuna Kampuni ilipewa zabuni ya kuwa wakala wa kukusanya ambapo kwa mwezi inawasilisha shilingi 60,000/= jambo ambalo linashanghaza sana na ukizingatia kuna  kizuizi cha magari na pikipiki ambapo magari makubwa ya mizigo hulipia shilingi 30,000/=  na kufanya chanzo hicho nacho kushindwa kukusanya vyema mapato ya halmashauri hiyo.

“Hapa wanasiasa wanahusika vipi kuona mapato yanakusanywa na kampuni iliyopewa zabuni na kukusanya ushuru chini ya malengo yaliyokusudiwa halafu waheshimiwa madiwani wanapohoji wanaanza kusakamwa na mkuu wa wilaya kwamba ndo wanasababisha hili halikubaliki na tunasema mkuu wa wilaya hana weledi wa kuwashambulia wanasiasa na ache kufanya hivyo” alisisitiza.

Ametoa wito kwa wananchi kumuunga mkono katika kutetea haki za wana Rorya katika Halmashauri yao , Lakini pia amemtaka Mkuu wa Wilaya hiyo kuacha kuwasakama wanasiasa na kwamba wakati anateuliwa kwenda Wilaya ya Rorya alikuta tayari wao wamechaguliwa kuwatumikia wananchi na ikizingatiwa wao ni wana rorya hivyo aache tabia ya kukurupuka kuwasema hovyo na ache mara moja.

USAID YAENDESHA ELIMU YA LISHE WILAYANI KONGWA MKOANI DODOMA

Katibu tawala wilaya Kongwa,Bw Joseph Kisyeli,akimywesha mtoto uji ulioongezwa virutubishi,katika kampeni za uhamasishaji wa chakula cha mtoto chenye virutubishi,katika kata ya ngomai. Zinazoendeshwa na  USAID Tuboreshe Chakula ambazo zilifanyika mjini humo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kongwa ,Bw Joseph Mwita Kisyeli,akihutubia wananchi juu ya umuhimu na faida za chakula kilichoongezwa virutubishi,kwa mtoto miezi 6 - miaka 5,katika kampeni ya lishe ilizofanyika kata Ngomai wilaya ya Kongwa chini ya udhamini wa na USAID Tuboreshe Chakula
Mkazi wa Kongwa  akimsikiliza kwa makini,Mtaalamu wa lishe toka USAID Tuboreshe chakula, Bi Mariam akielimisha faida na umuhimu wa virutubishi kwa mtoto umri wa miezi 6-miaka5.
Mtaalamu wa Lishe Bi Julita kutoka USAID Tuboreshe Chakula Project akimuelekeza mgeni rasmi katibu tawala wilaya Kongwa, Bw Joseph Kisyela umuhimu na jinsi ya kutumia Virutubishi ambavyo ni muhimu kwa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi miaka 5. Sherehe hizo zilifanyika Wilaya Kongwa,kata ngomai mkoani Dodoma.
Baadhi ya kina mama wenyeji wa kijiji cha ngomai,wakishiriki zoezi la kunywesha watoto kampeni za lishe bora zinazoendeshwa na mradi wa USAID Tuboreshe chakula.
Kikundi maarufu cha ngoma wilaya kongwa kata ya ngomai,kikitumbuiza wakati wa sherehe za uzinduzi wa kampeni ya uhamasishaji wa virutubishi  zinazoendeshwa na USAID Tuboreshe Chakula katika kata ya Ngomai wilayani Kongwa.
Katibu tawala wa wilaya ya Kongwa na viongozi wenzake wakipata elimu zaidi kwa kusikikiza wataalamu wa lishe kutoka mradi wa USAID Tuboreshe Chakula katika kampeni za lishe zinazoendelea wilayani humo.
Timu ya wataalamu wa lishe kutoka mradi wa USAID Tuboreshe Chakula wanaoendesha kampeni ya lishe wilaya mbalimbali za hapa nchini.

AIRTEL YADHAMINI TUZO YA MWANAMAKUKA 2014

Airtel yadhamini Tuzo ya Mwanamakuka 2014

Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel  leo imetangaza kudhamini tuzo za Mwanamakuka zenye lengo la kusaidia wanawake kutoka katika maeneo mbalimbali kujiinua kiuchumi

Tuzo za Mwanamakuka zinaandaliwa na The Unity of Women friends kila mwaka zikiwatambua wanawake jasiri waliopambana kubadili maisha yao kutoka katika hali ngumu, duni na umaskini

Akiongea kuhusu udhamini wa Tuzo hizo Afisa Uhusiano wa Airtel Bi Jane Matinde alisema” Airtel inaamini kwamba ujasiriamali ni muhimu katika kufikia maendeleo ya kiuchumi na kuondoa umaskini. Kwa kudhamini tuzo hizi za mwanamakuka tunajikita katika kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi na kuwa sehemu ya shughuli za maendeleo ya wanawake nchini”.

Kwa miaka mitatu mfululizo Airtel tumekuwa moja ya wadhamini wa tuzo hizi za mwanamakuka ambazo zimebadili maisha ya wanawake na kuwawezesha kuwa wafanyabiashara wenye mafanikio. Tutaendelea kuonyesha dhamira yetu katika mipango ambayo itasaidia wanawake walio katika mazingira magumu kujikwamua kiuchumi na kukuza maendeleo ya taifa."

Jane aliongeza kwa kusema , kuna msemo unaosema ukimwezesha mwanamke umewezesha jamii nzima. Airtel tumejipanga kuwawezesha wanawake kiuchumi kwani tunaamini kwa kufanya hivyo tutakuwa tumewezesha jamii kwa ujumla

Kwa upande wake mwenyekiti na Mratibu wa Mradi wa The Unity of Women friends Maryam Shamo alisema” Tunashukuru Airtel kwa kushirikiana nasi katika kufanikisha tuzo hizi ambazo ushirika huu umekua wa mafanikio makubwa. Lengo la tuzo hizi ni kuwahamasisha na kuwavutia wanawake  kufikia ndoto zao. Lakini hasa tuna hakikisha kuwa zoezi hili na matokeo yake yanaleta mafanikio ya kudumu na kubadili maisha yao”

 Tuzo za mwanamakuka za mwaka huu zitafanyika sambamba na kusherehekea siku ya wanawake Dunia, Mwanamakuka family bonanza itafanyika tarehe 15 machi 2014 , siku ya Jumamosi katika viwanja vya Escape 1 Dar es Saalam kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 2 Usiku.