Picha inanoyoonesha mradi wa wananchi wazalendo utakavyokua.
Kibasila Estate Public limited company (KEPLC) ni kampuni inayomilikiwa na Wananchi wa kawaida wanaoishi kwenye nyumba 106 walizouziwa na Serikali kwa Mikataba Maalum ya mtu mmoja mmoja kupitia wakala wa majengo Tanzania (TBA), chini ya Wizara ya Miundombinu tokea mwaka 2004. Nyumba hizo zipo katika eneo maarufu liitwalo SHULE YA UHURU, katika makutano ya barabara ya Msimbazi/Lindi, Kata ya Gerezani, wilaya ya Ilala jijini Dar-Es-salaam.
Vikao vinavyoendelea kujadili maswala mbalimbali ya mradi huo.
Mara tu baada yakuuziwa na kupata mikataba yao, wananchi hawa waliamua kujiunga pamoja kwa mtindo wa kuhamasishana na kunadi wazo la kuunda Ushirika yaani Kibasila Housing Cooperative Society, waiombe serikali iwamilikishe eneo lao kwa pamoja, ili wapate urahisi wa kukopesheka na hatimaye kuzijenga upya nyumba zao, waweze kuishi katika nyumba bora zenye thamani wanayostahili na kukidhi viwango vya
mipango miji.
MALENGO YA MRADI
Wananchi wa Gerezani/Kibasila wamepania kuliendeleza eneo lao kibiashara kwa kujenga Vitega uchumi na kuvikodisha ili kupata gawio litakalo wawezesha kuinua hali zao kimaisha, kiuchumi na kijamii na sehemu ya fedha za faida zitumike kulipia gharama za Mradi utakaojengwa.
Kupandisha thamani ya ardhi yao kwa kujenga majengo ya kisasa na yenye kuvutia na hatimaye kubadilisha sura ya eneo la Gerezani na kuwa kitovu cha biashara na kuwa kivutio cha watalii.
Kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuinua maisha ya wananchi wake na kwa kupitia mradi huu maisha yao yataboreshwa.
Kutoa fursa kwa watanzania wengine kuajiriwa, kupata mahali bora pa kuishi na Serikali yao kunufaika kwa kodi kwa kupitia biashara mbalimbali zitakazofanyika katika eneo lao. Na kwa kuwepo na makazi ya kupangisha ya bei ya kati na ya juu.
Kumfanya Mkazi kumiliki na kuendesha uchumi wa nchi yake kivitendo na kuwa mfano wa watanzania wengine.