ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, February 1, 2025

YANGA SC YAREJEA KILELENI BAADA YA KUIKANDA KAGERA SUGAR 4-0

Wachezaji wa Yanga Mudathir Yahya Abbas (katikati) na Pacome Zouzoua (kulia) wakimpongeza Dube mara baada ya kutoa pasi iliyozaa goli la pili kwa timu hoyo iliyoibuka na ushindi wa bao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar.
 

CREDIT KWA Bin Zubeir.

MABINGWA watetezi, Yanga SC wamerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar jioni ya leo Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge Jijini Dar es Salaam.

Mudathir Yahya Abbas.
Mabao ya Yanga leo yamefungwa na nyota wazawa, mshambuliaji Clement Francis Mzize dakika ya 32, kiungo Mudathir Yahya Abbas dakika ya 60, kiungo Muivory Coast, Pacome Zouzoua Peodoh kwa penalti dakika ya 78 na mshambuliaji Mzambia, Kennedy Musonda dakika ya 86.

Yanga ingeweza kuondoka na ushindi wa mabao 5-0 leo kama kiungo Mburkinabe, Stephane Aziz Ki.

Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 42 katika mchezo wa 16 na kupanda juu ya msimamo, ikiizidi pointi mbili Simba ambayo pia ina mechi moja mkononi na kesho inacheza na Tabora United mjini Tabora.

Kwa upande wao Kagera Sugar baada ya kipigo cha leo 11 za mechi 16 nafasi ya 15 kwenye ligi ya timu 16 — mbele ya Ken Gold yenye pointi sita za mechi 16 pia.


WATAKAO JIANDIKISHA ZAIDI YA MARA MOJA KUKIONA CHA MTEMA KUNI -TUME HURU YA TAIFA YA UCHAGUZI

 HABARI NA VICTOR MASANGU/ PWANI

SAUTI NA ALBERT G.SENGO Tume huru ya Taifa ya uchaguzi imekemea vikali na kupiga marufuku kwa mtu yoyote kujiandikisha zaidi ya mara moja katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai na endapo wakibainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Kauli hiyo imetolewa na Makamu mwenyekiti wa Tume huru ya Taifa ya uchaguzi Mhe. Jaji Mbarouk Mbarouk ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa mkutano wa Tume na wadau mbali mbali wa uchaguzi wa Mkoa wa Pwani kuhusiana na suala zima la mwenendo mzima wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa mwaka 2025.

AJALI YA BASI NA RAV4 YAUWA WATATU KILIMANJARO

 Watu watatu wamefariki dunia papo hapo baada ya gari dogo aina ya Toyota Rav4 kugongana uso kwa uso na basi la abiria la Kampuni ya Ester Luxury, katika eneo la Mdawi, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, leo Jumamosi, Februari 1, 2025.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi, amekiri kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa imetokea asubuhi baada ya dereva wa Toyota Rav4 kupita magari mengine bila kuchukua tahadhari, hali iliyopelekea kugongana uso kwa uso na basi lililokuwa likitokea Moshi kwenda Dar es Salaam. Aidha Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe.Godfrey Mzava amesema kuwa hakuna majeruhi kwenye basi hilo, lakini watu watatu waliokuwa kwenye gari hilo dogo wamepoteza maisha. Miili ya marehemu hao, wanaume wawili na mwanamke mmoja imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi, huku mamlaka zikihimiza madereva kuwa waangalifu barabarani ili kuepusha ajali kama hii.

Thursday, January 30, 2025

VIDEO - DKT. BITEKO AONGOZA WAOMBOLEZAJI KUAGA MIILI YA WANAFUNZI WALIOFARIKI KWA RADI GEITA (9)

 Leo Januari 30, 2025 mkoani Geita, maelfu ya waombolezaji wamejitokeza kuaga miili ya wanafunzi saba wa Shule ya Sekondari Businda iliyopo wilayani Bukombe waliofariki kwa kupigwa na radi mnamo tarehe 27 januari, 2025.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameongoza shughuli za kuaga na kukabidhi ubani kwa wafiwa huku akiwataka kuwa wavumilivu hasa kipindi hiki cha majonzi.

DKT. BITEKO AONGOZA WAOMBOLEZAJI KUAGA MIILI YA WANAFUNZI WALIOFARIKI KWA RADI GEITA



📌 Rais Samia atuma salamu za pole, agharamia misiba na mazishi


📌 Mkuu wa Wilaya Bukombe aishukuru Idara ya Afya kwa juhudi za maokozi

📌 Viongozi wa dini wahimiza uvumilivu na uhimilivu kipindi cha majonzi

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Leo Januari 30, 2025 mkoani Geita, maelfu ya waombolezaji wamejitokeza kuaga miili ya wanafunzi saba wa Shule ya Sekondari Businda iliyopo wilayani Bukombe waliofariki kwa kupigwa na radi mnamo tarehe 27 januari, 2025.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameongoza shughuli za kuaga na kukabidhi ubani kwa wafiwa huku akiwataka kuwa wavumilivu hasa kipindi hiki cha majonzi.

Ametoa pole kwa wazazi, walezi ndugu wa watoto pamoja na wanafunzi wa Businda kwa kuondokewa na wapendwa wao na wanajamii wa Businda Sekondari kwa jitihada na utoaji wa huduma wakati wa tukio hilo.


“ Imeandikwa kwamba shukuruni Mungu kwa kila jambo, Mungu ametukutanisha leo katika hali ya majonzi. Tukio hili litukumbushe kutenda mema wakati wote na tuamini kwamba Mungu ndiye mwenye uweza. Kipekee ningetamani kuwataja Madaktari wote kwa majina kutokana na msaada mkubwa walioutoa lakini itoshe kusema asante kwa kazi kubwa mliyoifanya” amesema Dkt. Biteko.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kupokea taarifa za msiba huo mzito amekuwa akifuatilia kwa karibu na kutoa maelekezo kwa ajili ya kuzifariji familia za wafiwa, wana Bukombe na Taifa kufuatia kuondokewa na vijana waliokuwa katika safari ya kutafuta elimu.
“Rais Samia amegharamia msiba pamoja na kutoa ubani kwa kila familia za wafiwa pamoja na kugharamia usafirishaji wa miili ya wanafunzi wawili kwenda Chato, Geita na Karatu mkoani Arusha kwa mazishi.

Viongozi mbalimbali wa dini wamewapa faraja wafiwa na kusema msiba haujawahi kuzoeleka lakini kwa mapenzi ya Mungu atakuwa mfariji wao.

Viongozi hao wamewataka wanadamu kujipanga wakati wote kwa kuwa hawajui ni wakati gani utafikwa na umauti kutokana na fumbo aliloliweka Mwenyezi Mungu.

Aidha, wamemwomba Mungu awape uvumilivu viongozi katika kipindi hiki cha majonzi. 

Wanafunzi hao saba waliokuwa wakisoma kidato cha tatu walikuwa na umri kati ya miaka 16 na 18, walikutwa na umauti kwa kupigwa na radi wakati wakiendelea na masomo darasani.

Waliofariki ni Erick Emmanuel Akonaay (17), Nikas Paul Tompoli (18) Gabriel Daud Makoye (17), Doto Marco Masasi (18), Asteria Reonard Mkina (16), Peter Nkinga Manyanda (17) na Erick Martine Bugalama (16)

Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bulangwa, Theodora James Mushi amesema  wanafunzi hao walipatwa na umauti wakiwa katika harakati za kusaka elimu. 

Wanafunzi wanne kati yao walifariki papo hapo na wengine watatu walifariki wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali na vituo mbalimbali vya Afya.

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhe. Paskazi Mragili ameishukuru Idara ya afya kwa utayari na uharaka wa utoaji huduma kwa wanafunzi wote 138 ambapo wanafunzi 89 waliathirika moja kwa moja na wengine waliruhusiwa kurudi nyumbani. Majeruhi wote wameruhusiwa na wale waliopata majeraha wanaendelea kutibiwa wakitokea nyumbani.

HALMASHAURI YA KIBAHA MJI YAMPA PONGEZI RAIS SAMIA KWA KUIPANDISHA KUWA MANISPAA.

 


NA  VICTOR MASANGU, KIBAHA

Baraza la madiwani katika  Halmashauri ya Kibaha mji  limetoa tamko na kuazimia  rasmi  kwa pamoja  kumpongeza Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuridhia maombi na kuweza kuipandisha adhi Halmashauri hiyo kuwa Manispaa pamoja kuteuliwa  na mkutano mkuu  maalumu  kuwa mgombea wa nafasi ya Urais pamoja na mgombea mwenza  Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibaha mji Mussa Ndomba  katika kikao cha baraza la madiwani la kawaida kwa kipindi cha robo ya pili ambapo amesema kwamba wameamua kwa kauli moja wanampongeza kwa dhati kupitishwa kwa kishindo na wajumbe wa mkutano huo.
 

Aidha Ndomba amebainisha kwamba baraza hilo limepongeza Rais kwa kutenga fedha nyingi  ambazo zimeweza kuleta chachu  kubwa katika suala zima na utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo katika sekta ya elimu, afya,  maji pamoja na miundombinu ya barabara ya maendeleo.

"Kwa kauli moja baraza la madiwani tunatoa pongezi kubwa kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuipandisha adhi Halmashauri yetu ya mji Kibaha kuwa manispaa, pamoja kuteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya Urais ikiwa sambamaba na mgombe mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi kupitia chama cha mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa mwaka 2025.

Pia katika hatua nyingine baraza hilo la madiwani limemuomba Rais kuwapatia eneo la shirika la elimu Kibaha kwa ajili ya kuweza kuliendeleza ikiwa sambamba na  kupanga mji katika mambo mbali mballi ya huduma za kijamii sambamba na kurudisha huduma ya mabasi ya mwendo kasi kama ilivyokuwa hapo awali  kwani kwa sasa wananchi wanapata shida sana.  

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amaipongeza Halmashauri ya mji wa Kibaha kwa kuweza kupandishwa adhi kuwa Manispaa pamoja na kuweka juhudi katika suala zima la ukusanyaji wa mapato.

Aidha amesema kwamba Halmashauri ya Kibaha mji kwa sasa inabidi kubadilika na kuhakikisha kwamba wanaweka mikakati ya kupima viwanja ambavyo ni mashaba pori na kuweka mipango ya  kuweza kuwapatia hati ndani ya wiki moja.

MCC RAJAB: UWEKEZAJI WA RAIS SAMIA KATIKA SEKTA YA ELIMU TANGA UMEWAOKOA WATOTO KUFANYISHWA KAZI ZA NDANI

 

Na Oscar Assenga, TANGA

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Rajab Abdurhaman amesema uwekezaji uliofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu kwenye sekta ya elimu mkoani Tanga umesaidia kuwaokoa watoto kufanyishwa kazi za ndani.

Rajabu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga aliyasema hayo juzi wakati akizindua maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa chama hicho katika mkutano ulikuwa na lengo la kuunga mkono maamuzi ya mkutano mkuu maalumu wa CCM.

Maamuzi ya Mkutano Mkuu huo maalumu uliompitisha Dkt Samia Suluhu kuwa mgombea Urais, Dkt Emanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza pamoja na kumpitisha Stephen Wasira kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa uliofanyika kwenye eneo la Makorora Jijini Tanga.

Alisema hilo limetokana na uwekezaji wake kupitia elimu bure ambapo kwa mkoa wa Tanga kila mwezi kwa ada za watoto  Rais anatoa Bilioni 1.3 kwa mwezi ambayo ni bilioni 15.8 kwa miaka.

“Kwa maana ya kipindi cha miaka mitano amewalipua watoto wetu bilioni 78,Rais asingelipa fedha hizo kwa ajili ya ada za watoto wetu kwa shule za msingi na sekondari ilipaswa kila mwanafunzi kulipiwa na mzazi “Alisema


Aidha alisema kutokana na kulipiwa ada za watoto maana yake amewasaidia baadhi ya majukumu kwenye familia ambazo zisingeweza kulia ada hiyo ndio sababu zilizopelekea mkutano mkuu kumpitisha kuwa mgombea urais 2025.

“Lakini niwaambie hapa kwamba CCM kupitia ilani Serikali kwenye suala la elimu ya msingi na sekondari imefanya kazi kubwa sana kwa kufanya uwekezaji mkubwa hivyo kuongeza ufaulu kwa darasa la saba, kidato cha nne na cha sita “Alisema

“Hivyo mtu anapohitaji msichana wa kazi na mvulani wa kazi utasakia nenda korogwe na Lushoto kwa sababu ya watoto wengi kufeli kutokana na kutokuwa na uwekezaji mkubwa kwenye elimu hivyo kutokana na uwekezaji wa Rais umesaidia kukua kwa elimu kupandisha ufaulu”Alisema

Aliongeza kwamba leo hii katika matokeo ya darasa la saba wasiofaulu ni wachache sana na wanakwenda kwenye vyuo vya ufundi na ndio maana kuwapata wasichana wa kazi au vijana huwezi kuwapata kwa sababu watoto wote wapo shuleni.

 

Hata hivyo Mwenyekiti huyo alisema kwamba wanaunga mkono azimio la mkutano mkuu wa CCM Taifa ambalo lilimpitisha Dkt Samia Suluhu kuwa mgombea Urais katika uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Alisema pia wanaunga mkono maamuzi kumpitisha Dkt Emanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza na Dkt Mwinyi kuwa mgombea Urais wa Zanzibar na wana Tanga wanaupongeza mkutano mkuu kwa kumchagua Stephen Wasira kuwa makamu CCM Taifa.

“Wapo wanaojiuliza kwanini mkutano Mkuu Mkuu Maalumu CCM umeamua kwa kura zote za wajumbe kumpitisha Dkt Samia Suluhu nimewahi kusema mara kadhaa tunapohitaji maendeleo ya kweli kwenye nchi na Taifa lipige hatua mbele za kimaendeleo jambo la kwanza unalohitaji ni amani.

“Niliwahi kuwaambia Tanga neno amani tunapenda kulidharau kwa sababu tumezoea kulitamka kila wakati unajua hata chakula unapokuwa unakula kila siku unafika wakati unakinai  ... watanzania neno hilo linahubiriwa misitiki na kanisani kila wakati inawezekana lakini tujifunze yaliyotokea na yanayotokea kwenye mataifa ya wenzetu barani Afrika na maeneo mengine duniani hvyo tuitunze amani yetu”Alisema

Wednesday, January 29, 2025

UWT KIBAHA MJI,KOKA MWENDO MDUNDO KUMPAMBANIA RAIS SAMIA KATIKA UCHAGUZI 2025


 NA VICTOR MASANGU,


Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka ameungana kwa pamoja na umoja wa wanawake wa (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini katika kumuunga mkono Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kupitishwa na mkutano mkuu wa chama kuweza kugombea  tena nafasi ya Rais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu  2025.



Koka ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha baraza la UWT Wilaya ya Kibaha mjini ambapo amesema kuwa Rais Samia ameweza kufanya mambo makubwa katika kutekeleza Ilani ya chama kwa vitendo ikiwemo kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo na kuwataka wanawake hao kuachana na migogoro na makundi ambayo hayana faida ndani ya chama.

Aidha Koka alisema kwamba anatambua wanawake ni jeshi kubwa hivyo wanapaswa kuhakikisha wanajipanga  kwa kuwa na umoja na mshikamano wa pamoja katika kumpa sapoti ya kutosha ili aweze kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa nafasi ya Urais na kwamba wanatakiwa kuwa mstari wa mbele na kuachana na wote wowote katika kumpambania Rais Samia.

"Kwa upande wangu mimi kama Mbunge wenu namshukuru sana kwa dhati Rais wetu kwani ameweza kufanya mambo mengi hivyo wanawake wa UWT  wa Jimbo la Kibaha mjini pamoja na maeneo mengine mnapaswa kutokufanya makosa na mnapaswa kuunga mkono juhudi za Rais na kuhakikisha anashinda kwa kishindo  kwa asilimia kubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Kadhalika Koka alimpongeza kwa dhati Rais Dkt, Samia kwa kuweza kuridhia maombi ya Halmashauri ya  Kibaha  mji na kuipa adhi ya kuwa Manispaa hivyo kutokana na kazi nzuri za utekelezaji wa majukumu yake ipasavyo ya anapaswa kupewa sapoti na ushirikiano wa hali na mali ili aweze kuendelea kuwatumikia wananchi na kutatua changamoto zao wanazozikabili.

Naye Mwenyekiti wa umoja wa  wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja ametumia kikao hicho kuwakumbusha wajumbe kwamba hawezi kuvumilia hata kidogo baadhi ya vikundi vya watu wachache   ambao wenye tabia ya kukihujumu chama na kwamba endapo wakibainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

Alibainisha kwamba kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wanawake  kukichafua chama kwa kuvunja sheria na taratibu kwa kuendesha mipango kinyemela ambayo ni nje kabisa na miongozi ya chama na kwamba kwa sasa wamejipanga na kujizatiti ili kuweza kuwaandikia barua kwa lengo la kuwaonya.

Naye Katibu wa UWT Kibaha mjini Cecilia Ndaro akisoma taarifa ya utekelezaji kwa mgeni rasmi amesema kwamba  hali ya kisiasa katika Halmashauri ya Kibaha mjini ni shwari na kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu  amabo unatarajiwa kufanyika mwaka huu wa 2025 na kuongeza kwamba wataendelea kuongeza idadi ya wanachama.

Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mama Selina Koka ambaye pia ni mlezi wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini aliwaomba wanawake hao kuendelea kumpa ushirikiano wa kutosha katika suala zima la kukijenga chama ikiwemo kuachana kabisa na kuwa na tofauti na makandokando na badala yake wawe kitu kimoja katika kuimarisha umoja wao.


Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka amewataka wanachama wote kuweka misingi ya kuzingatia taratibu za chama na kuachana kabisa na tabia ya kuwa na propaganda na badala yake wajipange kwa ajili ya uchagzui mkuu wa mwaka 2025.

Kwa upande wake Katibu wa chama cha mapinduzi (CCM) Isack Kaleiya amebainisha kwamba kuna baadhi ya wanachama bado ni  tatizo hivyo watahakikisha wale wote ambao wamekuwa wakienda kinyume na taratibu za chama watawajibishwa ipasavyo kwani chama  hakitomuonea huruma  hata kidogo mtu ambaye atakwenda kinyume.