ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, December 16, 2024

TAMASHA KUBWA SAME UTALII FESTIVAL SEASON 2 KUFANYIKA DESEMBA 20 -22 SAME KILIMANJARO

 

 


Na Oscar Assenga, 

TAMASHA Kubwa la Same Utalii Festival Season 2 linatarajiwa kufanyika Desemba 20 hadi 22 mwaka huu  katika wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro ambalo limeidhinishwa kufanyika kila mwaka lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu kuhamasisha utalii nchini.

Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni alisema kwamba maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri na  litatanguliwa na lingine Desemba 17 hadi 19 kutakuwa na matukio yatakayotanguliwa tamasha hilo.

Aliyataja matukio ambayo yatatangulia kabla ya kufanyika kwa Tamasha hilo ni Utalii wa Matibabu (Tourisim Clinic) ambapo wananchi watapata matibabu bure ya utalii na kutakuwepo na madaktari ambao watachunguzi wananchi wenye changamoto za magonjwa mbalimbali .

“Hii itafanyika kwa ajili ya wananchi wa Same na hata wale ambao watakuwa wamewahi mapema kwa ajili ya tamasha hili nao watanufaika na huduma hiyo wakati wakisubiri kuanza kwake”alisema

Mkuu huyo wa wilaya alisema kwamba katika kuelekea Tamasha hilo Desema 18 mwaka huu kutakuwa na treni itakuwa inatokea Dar kwenda wilaya ya Same kwa ajili ya utalii itakuwa imebeba watalii wa kitanzania na wengine kutoka nje ambapo itaanza safari zake Desemba 18 jioni na watafika Desemba  19 asubuhi.

“Lakini pia kutakuwa na mabehewa manne  kwa watalii wanaokuja ,behewa la nyama choma,vinjwaji na michezo aina mbalimbali kwa watoto ili watoto wasiboreke wawe na eneo lao la michezo na kutakuwa na mabehewa la mziki mpaka watakapofika same Desema 19 tayari kuanzia utalii 20 hadi 22”Alisema

Aidha alisema wameona utalii waubadilishe kidogo na wapo watakaokuja kwa njia ya magari ambapo Desema 20 kutakuwa na uzinduzi rasmi wa tamasha wataenda kutalii kwenye hifadhi ya Mkombazi na jioni watarudi kutakuwa na mkesha kwa ajili ya watalii mbalimbali  kupata burudani kutoka kwa wanamuziki mbalimbali watatumbuiza .

 

Mkuu huyo wa wilaya alisema katika kunogesha Tamasha hilo Desema 21  mwaka huu idadi ya watu wameongezeka kutoka 2000 kipindi kilichopita  na wanatarajiwa kuongezeka kufikia watu 20,000 kwa sababu wameongeza kipengen za marathon.

Alisema katika watu watakimbia kuanzia Kilomita 21,Kilomita 10  na Kilomita 5  na wengine watakwenda kutalii mlima Kidenge ambao ni mlima mzuri unaofanana na ukuta mmoja uliojengwa nchini china upo wilayani humo ambao ulifufuliwa hivi karibuni na wizara wameridhia uwe kivutio cha utalii.

Akizungumzia mlima huo alisema ni mzuri na unakona nzuri na Rais Dkt Samia Suluhu amewajengea barabara nzuri ili kuwezesha watalii kuweza kufika bila kuwepo kwa changamoto huku akitaja kivutio kingine kuwa ni upepo mkali na mlima shengena uliopo kwenye Hifadhi ya Msitu wa Chome una vivutio vingi  vya utalii kuna ndege ambao hawapatikana duniani ilisopokuwa huko shengena.

Alisema pia kuna chura ambaye hapatikana sehemu yoyote duniani na watu wataendelea na burudani ya mziki kutoka kwa wasani mbalimbali ambao watatumbuiza kwenye siku hiyo niwakaribishe watanzania wote kwa ujumla

“lakini pia kutakuwa na mabanda mbalimbali ya maonesho yataaandaliwa kwa ajili ya tamasha hilo litafanyikia same mjini na Marathon zitaanza hapo na kutakuwa na bidhaa mbalimbali zitakazonyeshwa na watalii”Alisema

“Lengo la Tamasha hili ni kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu tunavyofahamu aliweza kutangaza vivutio vya utalii nchini na kuweza kuingiza fedha za kigeni kupita Filamu ya The Rayal Tour sisi hapa Same tumebaini vipo vivutio vya utalii ambavyo havijatangazwa na hivyo kutumia nafasi hiyo kuzitangaza”Alisema

Hata hivyo alisema lengo pia ni wananchi wa wilaya ya Same wainuke kuichumi kupitia Same Utalii Festivali na hivyo kuinua kipato cha wajasiriamali,wamiliki wa hoteli,mama ntilie ,bodaboda na kuna bidhaa zinazotokana na utalii uliopo same nao wenyewe watapata fedha na hivyo kuinuka kiuchumi.


“Wananchi wamehamasika sana baada ya kufanyika lile tamasha la kwanza ambalo lilifanyika na hivyo kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa wana nchi na kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta ya utalii kuweka Same kwenye Mahoteli muhimu “Alisema

Akizungumza namna tamasha hilo lilivyoongeza idadi ya utalii alisema kabla wajaanza Same Utalii Festival takwimu zilionyesha katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi idadi ya watalii walikuwa kati ya 3,000 hadi 7,000 kwa mwaka.

Alisema baada ya tamasha kufanyika kwa mujibu wa takwimu za Hifadhi hiyo  watalii wameongezaka kutoka 3,000 hadi 7,000 hadi kufikia elfu 9,000 na wamebaini lazima kuwepo na hotel nyingi za kutosha hivyo kuwahamaisha wawekezaji kuwekeza kwenye wilaya hiyo ili huku akieleza hotel mbili zimejengwa kupitia uhamasishaji huo eneo la Shengena na jengine kwenye lango la hifadhi ya Mkomazi.

KAULI ZA POLISI, TRA KUHUSU KUPOTEA KWA MFANYABIASHARA ULOMI.

 


Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeanza kumtafuta mfanyabiashara Daisle Ulomi aliyetoweka katika mazingira yenye utata, Desemba 11, 2024 akiwa kazini kwake Sinza Kijiweni.

Wakati Polisi likitoa taarifa hiyo, mke wa Ulomi, Elizabeth Munisi  amesema tangu alipotoa taarifa Polisi kuhusu kupotelewa na mume wake Desemba 12, hadi sasa bado wako njiapanda, kwani hawajui aliko.

“Desemba 14 majira ya asubuhi nilipigiwa simu na RPC wa Temeke kuniambia bado hawajamuona na wanaendelea kumtafuta, lakini kwa leo bado hawajanipa mrejesho wowote, nasubiri,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa jana Jumapili Desemba 15, imesema Ulomi hakurudi nyumbani tangu alipoingia kazi kwake, ikidaiwa siku hiyo alionekana akitoka ofisini Sinza Kijiweni saa sita mchana kuelekea Mbagala, Bandari Kavu.

Katika taarifa hiyo, kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema wakati mfanyabiashara huyo anaondoka inadaiwa alikuwa anakwenda kukagua kontena la bidhaa zake baada ya kuitwa na watu waliodai walikuwa wanashughulikia kulitoa bandarini.

“Jeshi linaendelea na ufuatiliaji wa taarifa hiyo kwa kushirikiana na ndugu ili kujua na kubaini yupo wapi,” inaeleza taarifa.

Kamanda Muliro amesema Desemba 12, katika kituo cha Polisi Chang’ombe ilipokewa taarifa ya kutafutwa na familia yake mfanyabiashara huyo.

“Taarifa hiyo inadai Ulomi alikuwa anatumia usafiri wa pikipiki namba MC 415 DQC aliyokuwa akiendesha mwenyewe. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa kuhusiana na mtu huyo azitoe kwenye mamlaka yoyote ya Serikali iliyo karibu yake,” imeeleza taarifa ya Polisi.


Awali, kupitia mitandao ya kijamii kulisambaa taarifa ikieleza mfanyabiashara huyo alipotea wakati anaelekea Bandari Kavu alikoita na watu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kupitia mtandao wa X (zamani twitter) Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob aliandika akidai mfanyabiashara huyo alikwenda bandari kavu kukagua kontena lake baada ya kuitwa na watu wa TRA kwa ajili ya ukaguzi.

Desemba 14, 2024 TRA kupitia kitengo cha Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano, ilitoa taarifa kujitenga na tukio la kupotea Ulomi.

“TRA inautaarifu umma kuwa, mchakato wa uondoshaji wa mizigo bandarini hufanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu za kiforodha. Kwa mujibu wa kifungu cha 2(1) cha Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki, ni wakala wa forodha peke yake ndiye anayewajibika kusimamia taratibu zote za kiforodha za uondoshaji wa mizigo bandarini kwa niaba ya muagizaji wa mzigo na siyo muagizaji wa mzigo.

“Kwa mujibu wa kumbukumbu zetu, mfanyabiashara, Daisle Simon Ulomi aliichagua kampuni ya wakala wa forodha ya Twende Freight Forwarders Limited kupitia barua yake kwa TRA ya   Desemba 5, 2024 kuwajibika kuondosha mizigo yake bandarini kulingana na taratibu za forodha,” imeeleza taarifa hiyo.

TRA imesema imekuwa ikifanya kazi na wakala wake ambaye bado hajakamilisha taratibu za kiforodha kuondosha mzigo husika na kwamba, TRA haijawahi kumuita wala kufanya naye kazi mfanyabiashara huyo katika ofisi zake kwa jambo lolote.


“Suala la kutoonekana kwa mfanyabiashara huyo ni jambo la kipolisi ambalo TRA haihusiki nalo,” imesema taarifa hiyo.

MAFUNZO YA UFUATILIAJI NA TATHMNI KWA WIZARA, IDARA ZINAZOJITEGEMEA, WAKALA WA SEREKALI NA MASHIRIKA YA UMMA YAFANYIKA JIJINI TANGA

 



Mwandishi Wetu.


Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kupitia kitengo chake maalumu cha ushauri wa kitaalam na kwa kushirikiana na washirika wa chuo kimeendelea kutekeleza makubaliano na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu ya kuimarisha mifumo ya Ufuatiliaji na Tathmini nchini. 


Kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ofisi ya Msajili wa Hazina, Chuo kimeweza kutoa mafunzo ya awamu ya kwanza (Level 1) kwa siku 3 na kuwashirikisha watumishi wa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali na Mashirika ya umma kuanzia tarehe 02 hadi 04 na 11 hadi 13 Disemba, 2024 katika ukumbi wa New Kiboko Hall Jijini Tanga.


Akiahirisha mafunzo hayo Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw.Charlton Charles Meena amewataka washiriki wote wa mafunzo kwenda kuwa walimu kwa watumishi wengine, pia amesisitiza kwa mshiriki yeyote alieshiriki mafunzo kwa awamu ya kwanza ni vema wakashiriki awamu zote tatu ili kuwa na uwelewa mzuri wa uratibu wa shughuli za Ufuatiliaji na Tathimini za kazi za serikali.

 
Mafunzo yameshirikisha watumishi wa umma zaidi ya 200, na yamewawezesha washiriki kujifunza kutofautisha na kutumia ipasavyo aina tofauti za Ufuatiliaji na Tathmini, kuamua jinsi ya kufuatilia na kutathmini miradi, mipango ya kimaendeleo au sera, ikiwa ni pamoja na kuweka bayana matokeo muhimu katika ngazi ya programu kwa kutumia mfumo wa kimantiki (Logical Framework) au miundo ya nadharia ya mabadiliko (Theory of Change).


Aidha mafunzo hayo yamelenga kuwasaidia kuunda viashiria sahihi (SMART), kwaajili Ufuatiliaji na Tathmini, kutumia zana mbalimbali za Ufuatiliaji na Tathmini kwaajili ya ukusanyaji na uchanganuzi wa takwimu, kubuni na kusimamia Tathmini kwa kutumia kanuni za Kiafrika za Tathmini na vigezo vya OECD-DAC na kuandaa ripoti bora za Ufuatiliaji na Tathmini kwaajili ya matumizi ya Serikali, Idara, Wizara, Mashirika na Wakala za Serikali. 

Aliongezea kuwa kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo, Chuo Kikuu Huria kitaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na Msajili wa Hazina kuandaa awamu nyingine ya mafunzo ya awamu ya kwanza ili kuweza kuzifikia baadhi ya Wizara, Idara zinazojitegemea, mashirika na wakala za serekali ambazo zilishindwa kuleta watumishi kwenye awamu hii ya kwanza ya mafunzo.
 
Pia alisisitiza kuwa ni vyema kukawa na uelewa kuwa baada ya awamu ya kwanza, kutakua na awamu ya pili na ya tatu ambazo kwa Pamoja, zitawezesha  watumishi kubobea katika eneo la Ufuatiliaji na Tathmini wa shughuli za Serikali na hivyo kuboresha utendaji kazi wa serikali na utoaji huduma kwa wananchi.