Karibu utazame wimbo huu ambao ni shukrani yetu kwa MUNGU kila jambo analolitenda katika maisha yetu ZAB. 69:30
Saturday, May 10, 2025
Friday, May 9, 2025
NSSF YAWATAKA WAAJIRI KUWASILISHA MICHANGO KWA WAKATI, YAENDELEA KUBORESHA HUDUMA KWA WANACHAMA
TANGA. Waajiri wa sekta binafsi wametakiwa kuzingatia wajibu wao wa kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati ili kuwawezesha wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kupata mafao yao kwa mujibu wa sheria.
Wito huo umetolewa tarehe 8 Mei 2025 jijini Tanga na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Bi. Mwamini Malemi, wakati akizindua rasmi Mkutano wa 54 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mfuko huo.
Bi. Malemi amesema michango ya waajiri ni uti wa mgongo wa uendeshaji wa Mfuko, hivyo kucheleweshwa kwake kunaathiri moja kwa moja ustawi wa wanachama na ufanisi wa utoaji huduma za mafao.
“Naomba nitumie nafasi hii kuwaasa waajiri wote kuhakikisha wanawasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati. Hili si jambo la hiari bali ni wajibu wa kisheria unaolenga kulinda haki za wafanyakazi”, amesisitiza Bi. Malemi.
Ameongeza kuwa, NSSF inaendelea kutoa huduma bora na endelevu kwa wanachama wake kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, uwajibikaji na matumizi ya teknolojia ili kuongeza uwazi na ufanisi katika shughuli za kila siku.
Akizungumza kuhusu mafanikio ya Mfuko, Bi. Malemi amesema NSSF imeendelea kuwa taasisi ya mfano katika sekta ya hifadhi ya jamii kwa kuimarisha mifumo ya TEHAMA, kuongeza kasi ya uandikishaji wanachama, kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na kufanya uwekezaji wenye tija.
Thursday, May 8, 2025
KAMATI YA SIASA YA CCM MKOA WA LINDI YAIPONGEZA KILWA KWA UTEKELEZAJI WA ILANI
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa, Mheshimiwa Kuruthum Issa Runje akikagua utekelezaji wa ilani ya CCM wilaya ya Kilwa mkoani Lindi
Viongozi wa chama chama mapinduzi mkoa wa Lindi wakiendeea na ukaguzi wa ilani ya CCM kwa kugua miradi mbalimbali katika wilaya ya Kilwa
Viongozi wa chama chama mapinduzi mkoa wa Lindi wakiendeea na ukaguzi wa ilani ya CCM kwa kugua miradi mbalimbali katika wilaya ya Kilwa
Na Fredy Mgunda, Kilwa Lindi
Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi ikiongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa, Mheshimiwa Kuruthum Issa Runje, imefanya ziara maalum Wilayani Kilwa kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025.
Katika ziara hiyo, kamati ilitembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye jumla ya thamani ya Shilingi 44,551,077,124.12. Miradi hiyo inahusisha nyanja mbalimbali muhimu kwa ustawi wa wananchi wa Kilwa, ikiwemo maji, elimu na afya.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni pamoja na Mradi wa Maji kwa Miji 28 ambao unagharimu Shilingi 44,007,870,224.12. Mradi huu mkubwa unatarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Kilwa.
Pia kamati ilikagua ujenzi wa nyumba ya mtumishi katika Shule ya Sekondari ya Mavuji (Shilingi 95,000,000), ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Msingi Naipuli (Shilingi 64,000,000), na ujenzi wa jengo la Vijana Rika katika Kituo cha Afya Tingi (Shilingi 22,006,900). Aidha, walitembelea mradi wa ujenzi wa mabweni mawili, madarasa manne na vyoo katika Shule ya Sekondari Mtanga wenye jumla ya thamani ya Shilingi 362,200,000.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mhe. Kuruthum Issa aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Baraza la Madiwani na watendaji wote kwa usimamizi thabiti na utekelezaji bora wa miradi hiyo. Alieleza kuwa utekelezaji huo unaonesha namna ambavyo Ilani ya CCM inatekelezwa kwa vitendo kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.
“Tunafurahishwa na kasi na uwajibikaji wa viongozi wetu wa Wilaya ya Kilwa katika kutekeleza Ilani ya Chama. Ushirikiano uliopo baina ya viongozi wa Serikali, CCM na wadau mbalimbali ni mfano wa kuigwa. Tuendelee kuchapa kazi kwa kushirikiana ili kuunga mkono jitihada za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Mhe. Kuruthum.
Ziara hiyo ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa chama hicho kuhakikisha kuwa ahadi zake kwa wananchi kupitia Ilani ya Uchaguzi zinatekelezwa kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo kwa wananchi.
BENKI YA CRDB YAWAHAKIKISHIA WAWEKEZAJI UKUAJI ENDELEVU WA UWEKEZAJI WAO.

Dar es Salaam, Mei 6, 2025 – Kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya tokea kuanzishwa kwake, Benki ya CRDB imeandaa Kongamano la Wawekezaji jijini Dar es Salaam katika hoteli ya Johari Rotana, lililohudhuriwa na wawekezaji 200 wa taasisi na binafsi kuangazia utendaji wa benki hiyo, kupitia matokeo ya kifedha yaliyokaguliwa ya 2024, na kujadili matokeo ya utekelezaji wa mkakati wake wa biashara, ikiwamo matokeo ya fedha ya robo ya Kwanza ya 2025.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na Balozi wa Denmark nchini, Mheshimiwa Jasper Kammersgaard, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Hussein Laay, na kuongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Benki ya CRDB, Abdulmajid Mussa Nsekela, ambaye aliwasilisha mada juu ya utendaji wa benki hiyo, pamoja utekelezaji wa mikakati yake, na malengo ya baadaye.
Faida Kubwa Zaidi Katika Miaka 30
Katika hotuba yake, Nsekela aliwajulisha wawekezaji kuwa Kundi la Benki ya CRDB lilipata faida baada ya kodi kubwa zaidi katika historia yake ya Shilingi bilioni 551 mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 30.3 ikilinganishwa na mwaka uliopita 2023.

"Matokeo haya ya kihistoria ni ushahidi wa miaka 30 ya uongozi, ubunifu, na ubora wa huduma za kibenki," alisema Nsekela. "Yanaonyesha si tu nguvu ya hali yetu ya kifedha bali pia maisha tuliyogusa, biashara tulizowezesha, na uchumi tunaounga mkono katika kanda nzima."
Jumla ya mali iliongezeka kwa asilimia 24.5 kufikia Shilingi bilioni 16.7 trilioni, ikichochewa na ukuaji wa mikopo na ukusanyaji wa amana. Mikopo iliongezeka kwa asilimia 22.8 kufikia Shilingi 10.4 trilioni, ikisababishwa na usimamizi mzuri wa vihatarishi vya mikopo na mahitaji makubwa kutoka kwa sekta za biashara, wajasiriamali, na kilimo. Amana za wateja zilikua na kufikia Shilingi 10.9 trilioni, na asilimia 87 ikiwa ni amana za gharama nafuu (CASA). Kampuni tanzu za Benki ya CRDB zilichangia asilimia 6 katika faida baada ya kodi ya kundi:
· Benki ya CRDB Burundi ilipata faida baada ya kodi ya Shilingi bilioni 40.3, ikiwa na jumla ya mali Shilingi trilioni 1.5.
· CRDB Insurance, ikiwa ni mwaka wake wa kwanza, iliripoti faida ya Shilingi milioni 343, i kuongeza mapato ya kundi ya kando ya riba.
· Benki ya CRDB Congo, ingawa iko katika hatua za mwanzo, ilionyesha maendeleo mazuri, ikiwa na jumla ya mali za Shilingi bilioni ilipata hasara ya Shilingi bilioni 6.5 chini ya kiwango kilichotarajiwa. Matarajio ni kuona benki hii ikipata faida mapema zaidi ya makadirio ya awali.
· Kupitia Taasisi ya CRDB Foundation, Benki ya CRDB iliendelea na juhudi za ujumuishi wa kifedha, hususani wanawake na vijana zaidi ya milioni 1 kupitia mpango wa IMBEJU, ukiimarisha ahadi ya Benki katika kuchochea ujumuishi wa kifedha.
Uwekezaji katika Mifumo ya Kidijitali na Ukuaji wa Wateja

Uwekezaji katika mifumo ya kidijitali umeendelea kuwa nguzo ya mikakati ya Benki ya CRDB, ambapo asilimia 98 ya miamala yote ya wateja mwaka 2024 ilifanyika kupitia njia mbadala. Kati ya hizi, asilimia 53 zilifanyika kupitia majukwaa ya kidijitali ikiwa ni pamoja na SimBanking, ambapo ilitoa mikopo ya kidijitali zaidi ya Shilingi bilioni 18, wakati asilimia 45 ya miamala ilifanyika kupitia CRDB Wakala. Ni asilimia 2 tu ya miamala ilifanyika kupitia matawi, ikionyesha mafanikio ya miakati ya Kundi la Benki ya CRDB.
Benki ilishuhudia ongezeko la wateja wapya milioni 1.5 kwa mwaka 2024, ikiwa ni pamoja na zaidi ya 340,000 kupitia CRDB Al Barakah, dirisha la benki ya Kiislamu. Tafiti zilizofanywa na wakaguzi huru zinaonyesha kuridhika wa wateja kwa asilimia 94, ikiwa ni ishara ya utoaji wa huduma bora na urahisi wa kidijitali.

Ubora wa Uendeshaji
Nsekela anabainisha kuwa Kundi la Benki ya CRDB lilishuhudia Uwiano wa Mikopo Chechefu wa asilimia 2.9, ikiwa ndani ya viwango vya udhibiti, faida ya mtaji ilikuwa asilimia 28. Uwiano wa gharama kwa mapato uliboreshwa hadi 45.9%, ikionyesha ufanisi wa kiutendaji. Uwezo wa mtaji ulikuwa asilimia 17.2, ukihakikisha ustahimilivu kwa upanuzi wa baadaye.
Matokeo ya Ushirikiano wa Kimkakati
Benki ya CRDB liliendelea kufungua fursa za kiuchumi kupitia ushirikiano wa kimkakati, ikikusanya zaidi ya Dola za Marekani Milioni 700 kusaidia sekta muhimu, ikiwa ni pamoja na Dola za Marekani Milioni 45 zilizoelekezwa kusaidia biashara za kikanda katika sekta muhimu kupitia kampuni tanzu za Burundi na DR Congo. Juhudi hizi zilichangia kuzalishwa kwa ajira zaidi ya 10,000.
"Matokeo ya haya ya ujumuishi wa kifedha na kiuchimu ni ishara ya mikakati thabiti ya ushirikano wa washirika wetu wa ndani na wa kimataifa," alisema Nsekela. "Iwe ni kupitia fedha za biashara, uwezeshaji wa vijana, au uwekezaji wa kijani, tumejikita katika kujenga ustawi kwa wote."

Akielezea kuhusu mafanikio ya Kundi, Nsekela alisema Bodi ya Wakiurugenzi ya benki hiyo imependekeza ongezeko la asilimia 30 katika gawio kwa kila hisa, kutoka Shilingi 50 hadi Shilingi 65 kwa hisa, ikiendelea kutengeneza thamani endelevu kwa wanahisa kutokana na uwekezaji wao.
Kongamano hilo pia lilijadili matokeo ya kifedha ya Robo ya Kwanza ya 2025, ambayo yalionyesha ukuaji endelevu, ambapo Benki ya CRDB na kampuni zake tanzu zilipata faida baada ya kodi ya Shilingi bilioni 173, ikiwa ni ongezeko la asilimia 36 ikilinganishwa na Robo ya Kwanza ya 2024. Mapato ya riba yaliongezeka hadi Shilingi bilioni 308, ikionyesha mweleko mzuri wa kiutendaji wa Kundi.
"Tuna furaha kutangaza mwanzo mzuri wa 2025," alisema Nsekela. "Tunaendelea na lengo letu la kuharakisha mabadiliko ya kidijitali, kupanua uwekezaji wetu wa kikanda, na kuimarisha uwezeshaji wetu kwa wajasiriamali hususan wetu vijana na wanawake, pamoja na kuboresha mikakati yetu katika kufadhili miradi ya kijani na ile inayozingatia mabadiliko ya tabia nchi."

Bodi na Wawekezaji Wafurahia Ukuaji Endelevu
Akizungumza katika kongamano hilo Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Ally Laay, amewaahidi wawekezaji kuwa Bodi ya Wakurugenzi itaendelea kuweka sera na miongozo itakayochchea ukuaji endelevu na muda mrefu. "Tunaposherehekea miaka 30 ya safari ya Benki ya CRDB, matokeo haya yanathibitisha uwazi wa kimkakati na ustahimilivu wetu. Tuna msingi imara unaowezesha ukuaji wa baadaye, hivyo niwaombe wawekezaji kuendelea kuwekeza na kuiamini benki yao," alisema Dkt. Laay.
Dkt. Laay pia alitumia fursa hiyo kuwaalika wanahisa wa Benki ya CRDB katika Mkutano Mkuu wa 30, utakaofanyika tarehe 17 Mei 2025, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Mkutano Mkuu huo utatanguliwa na Semina ya Wanahisa, ambapo Mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isidor Mpango. "Hii ni fursa adhimu kwetu kusherehekea kwa pamoja mafanikio tuliyoyapata katika safari yetu ya miaka 30. Ni matumaini yangu kuwa tutajitokeza kwa wingi," alimaliza Dkt. Laay.







Monday, May 5, 2025
DR. JEMBE AFAFANUA KWANINI WEMA HAWANA MAISHA - ASHIRIKI MAZISHI YA MWANAMKE KINARA MWANZA
"Mama Katua ameishi kama kitabu, Hadithi nzuri ambayo imeishia kwenye masikitiko majonzi na huzuni kubwa. Mwanza nzima imemiminika hapa ikionyesha kuguswa na hili" anasema Mkurugenzi wa Jembe Media LTD, Dr. Sebastian Ndege ambaye pia ni CEO wa makampuni ya Ndege Insurance na Jembe Development.
KWENYE MAHOJIANO:- Dr Jembe - "Ngoja Niwape siri, Kuna watu kwenye Maisha ni wema mno na hawana mbadala naye Mungu akiona mnawapenda saaana ndiyo huwa anaondoka nao, mpaka wakati mwingine najionya nisiwe mwema sana" Mwandishi PK - "Ili usife" Dr Jembe - "Eeeeeeh" ..........Kisha wote wakacheka.........!!! Dr Jembe - "Kwasababu wengi wanaofanya wema sana Mungu anaondoka nao, sijui huwa ni nini hicho?" " Kwahiyo ndiyo maana wakati mwingine huwa naamua kuwa mkaksi..... ili niendelee kuwepo" " Lakini yote kwayote mapenzi ya Mungu lazima tuyakubali na nikisema hivi siyo tusitendeane wema la hasha..... watu wema wana faida,tuishi nao na kuwashikilia kwani ukiwapoteza we ndio mwenye hasara... Jifunze kutunza watu hao" MTANGAZAJI :- PASCHAL KADUSHI MAANDISHI :- ALBERT G. SENGOSunday, May 4, 2025
DARAJA LA J P MAGUFULI (KIGONGO BUSISI) LIKO TAYARI KWA MATUMIZI
NA ALBERT G.SENGO/MWANZA
MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Daraja la Kigogo-Busisi maarufu kama Daraja la JPM lipo tayari kwaajili ya matumizi na kuwa muda wowote kuanzia sasa watu wataruhusiwa kupita wakati likisubiri kuzinduliwa. Msigwa amebainisha hayo mnamo tarehe 3 Mei 2035 akiwa katikati ya daraja hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari alioambatana nao kwaajili ya ukaguzi wa miradi mbari mbali ya maendeleo inayotekelezwa katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Alisema daraja hilo linalounganisha Wilaya mbili za Sengerema na Misungwi linaunganisha pia mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Alisema kuanza kutumika kwa daraja hilo kutafungua fursa za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni katika mataifa pamoja na mikoa yote inayounganishwa na daraja hilo