ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, November 26, 2025

DKT. MWIGULU AWAONYA WAVUNJIFU WA SHERIA

 WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amevitaka vyombo vinavyosimamia usalama barabarani vitekeleze sheria hizo bila upendeleo kwani tabia ya kuogopana na kuoneana aibu imechangia baadhi ya watu kukwepa wajibu wakati wengine wakibebeshwa mzigo wa sheria.


“Yeyote atakayevunja sheria akamatwe na hatua zichukuliwe kwa usawa. Huyu mmoja anavunja sheria anakamatwa, analipa. Huyu mwingine anavunja mbele yake anaachwa. Kama una haraka, toka mapema zaidi si kufidia kwa kuvunja sheria.”

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Novemba 26, 2025) wakati akifungua Maadhimisho ya Kimataifa ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini katika ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa haitakuwa uungwana kuona baadhi ya watu wakilipa adhabu papo hapo wanapokosea ilhali wengine wakiachwa kupita bila kuchukuliwa hatua.

Amewaonya baadhi ya viongozi na madereva wa Serikali ambao wanaelewa sheria vizuri lakini bado wanazikiuka kwa makusudi. “Ni muhimu kuwasaidia watumiaji wa vyombo vya usafiri kama bodaboda na bajaji ambao kwa sehemu kubwa wanaweza kuwa hawazielewi sheria kikamilifu, badala ya kuwaadhibu kwa upendeleo.”

Dkt. Mwigulu amesisitiza umuhimu wa kuwapa Watanzania wote heshima na kuhakikisha sheria zilizowekwa zinatekelezwa kwa maslahi ya wote na kuongeza kuwa endapo zipo sheria ngumu kutekelezeka, basi zibadilishwe ili kila Mtanzania anufaike.


Ameviagiza vyombo vya usimamizi wa sheria vihakikishe kuwa watumiaji wote wa vyombo vya usafiri wanazingatia usimamizi wa sheria na kuchukua hatua kwa yoyote anayevunja sheria akamatwe na kuchukuliwa hatua bila kuonewa aibu.

“Inaudhi mtu amebeba mgonjwa anafuata sheria, halafu mwingine anapita tu anavunja sheria, hapati adhabu. Mlalahoi akivunja sheria anapata adhabu, tunawapa kazi watekeleza sheria kuwaomba radhi watu waliovunja sheria. Naelekeza kila mtu afuate sheria, uwe wa serikalini ama uwe binafsi, tumeweka sheria, zifuatwe kama zilivyo.”

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa maadhimisho hayo, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa alisema sekta ya uchukuzi ni mojawapo ya sekta wezeshi za uchumi duniani kota na kwamba watu wanahitaji njia za uchukuzi ili kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau wa usafirishaji nchini ili kuhakikisha masuala ya nishati safi yanapewa kipaumbele. Akitoa mfano, Waziri Mbarawa alisema: “Uendeshaji wa reli ya kisasa (SGR) unatumia nishati ya umeme, mabasi ya mwendokasi njia ya Mbagala yanatumia gesi asili na baadhi ya taxi na bajaji zinatumia gesi asili.”

Tuesday, November 25, 2025

WATAALAM WA KIMATAIFA WATOA MWELEKEO MPYA WA UCHUMI KATIKA KONGAMANO LA TIA MWANZA


TIA Yasistiza Utafiti na Ubunifu Katika Kuchochea Uchumi – Kongamano la Kimataifa la 4 la Usimamizi wa Biashara na Ukuaji wa Uchumi Lafana Mwanza

Mwanza, 25 Novemba 2025 – Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) leo imeongoza Kongamano la 4 la Kimataifa la Usimamizi wa Biashara na Ukuaji wa Uchumi, lililofanyika katika Ukumbi wa Nyerere, Gold Crest Hotel jijini Mwanza, likiwa na ujumbe mahsusi unaoangazia nafasi ya ubunifu, uvumbuzi na biashara katika kuchochea uchumi endelevu.


Akizungumza kumwakilisha mgeni Rasmi, Benjamin Magai ambaye ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali , amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika utafiti wa kisayansi, kama njia ya kutoa suluhisho la changamoto za kijamii na kiuchumi. Akibainisha kuwa utafiti ndio injini ya maendeleo, hasa katika maeneo kama ubunifu, teknolojia, tathmini, miundombinu na mikakati ya maendeleo yenye tija.


Dira ya Maendeleo ya 2050 Yawekwa 

Dhima: Uvumbuzi, Ubunifu na Biashara kwa Uchumi Endelevu

Kongamano la mwaka huu limebeba kaulimbiu “Uvumbuzi, Ubunifu na Biashara kwa Uchumi Endelevu.” Kaulimbiu hiyo imegawanywa katika mada 11, huku machapisho 41 ya tafiti yakitarajiwa kuwasilishwa.

Prof. Pallangyo alisema kuwa kabla ya mawasilisho ya tafiti, kutakuwa na watoa mada wakuu 8 (Keynote Speakers) kutoka ndani na nje ya Tanzania, ambao ni wabobezi katika nyanja zao. Miongoni mwao ni:

Watoa Mada Wakuu ni kama ifuatavyo:-

Ephias Ruhode (Uingereza) – Amefafanua namna mkakati wa biashara unavyopaswa kuongoza kabla ya teknolojia, hasa katika zama za Akili Bandia (AI) kupitia mada “In the Age of AI, Business Strategy Comes Before Technology.”
Gaoua Abdelouahab (Algeria) – Ameeleza namna mabadiliko ya kidigitali na ujasiriamali yanavyoweza kuwa injini ya mapinduzi ya kiuchumi, akichambua “The Algerian Experience.”
Prof. Oksana Kiseleva (Urusi) – Amesisitiza umuhimu wa Ecosystem za Ubunifu katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi duniani.
Dkt. Collin Kamalizeni (Afrika Kusini) – Amejadili nafasi ya uongozi shirikishi katika kuponya majeraha ya uchumi Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia mada “Reimagining Inclusive Leadership as a Catalyst for Economic Recovery in Sub-Saharan Africa.”

Prof. Tandy Lwoga (Tanzania)
– Amezindua mjadala juu ya jinsi ubunifu unavyoungana na ujasiriamali katika muktadha wa mifumo ya kidijitali kupitia mada “Innovation Meets Entrepreneurship: Rethinking Digital Collection Development for the Future-Ready User.” 

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Amos Pallangyo,  amekumbusha kuwa TIA ni mojawapo ya taasisi kongwe na muhimu nchini katika kutoa elimu ya uhasibu, ugavi na fani nyingine za biashara. Ikiwa na kampasi 8 nchini na zaidi ya wanafunzi 32,000, na taasisi hiyo imeendelea kuimarisha mfumo wa mafunzo unaozingatia umahiri (Competence Based Training – CBET), sambamba na kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam.

Akimkaribisha Profesa Goodluck Urassa kutoa salamu za Bodi, viongozi wote wametia mkazo umuhimu wa TIA kuendelea kuwa kichocheo cha sera na maarifa kwa taifa.

Baada ya mawasilisho ya tafiti, TIA imetangaza kuwa itachapisha kitabu maalum kitakachokusanya mapendekezo ya watafiti juu ya namna bora ya kutatua changamoto katika sekta za biashara na uchumi. Kitabu hicho kitasambazwa kwa wadau muhimu, ikiwemo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama mchango wa TIA katika kusaidia sera na maamuzi ya maendeleo.


Katika kuunga mkono juhudi za Serikali kukuza utalii, washiriki wa kongamano wamepangiwa kutembelea vivutio vya Jiji la Mwanza. Hii ni sehemu ya mkakati wa kutumia kongamano kama nyenzo ya kuhamasisha utalii wa ndani.






Monday, November 24, 2025

UBUNIFU WA KIPEKEE KISIWA CHA SAANANE WAIBUKA A TUZO

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Kamishna Msadizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George, akipokea Tuzo ya Ubunifu wa Mazao ya Utalii, jijini Dar es Salaam.

Ubunifu wake wa kipekee umevuka mipaka ya kawaida na sasa umetambuliwa kitaifa!

 
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane jijini Mwanza, Dkt. Tutindaga George, ametwaa Tuzo Maalum ya Ubunifu wa Mazao ya Utalii kama sehemu ya Top 100 Executives List Awards 2025.

Katika hafla ya heshima iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Novemba 20, 2025, Dkt. Tutindaga alitangazwa rasmi kuwa  
"Chief Innovation / Head of Product Design and Innovation of the Year."

Mazao ya Utalii Yaliyompa Tuzo
Kupitia kazi yake katika Hifadhi ya Saanane, Dkt. Tutindaga amebuni na kuboresha bidhaa kadhaa za kipekee za utalii, zikiwemo:  
• Boat Safari katika Ziwa Victoria
• Rock Hiking
• Maeneo ya mapumziko ya kisasa (picnic sites) 
• Michezo ya majini
• Kutazama machweo ya jua
• Uboreshaji wa malazi ya kitalii
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Tutindaga George, akionesha Tuzo yake ya Ubunifu wa Mazao ya Utalii.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Dkt. Tutindaga aliwashukuru wote waliomuunga mkono na kutoa mwito kwa Watanzania kutembelea vivutio vyetu vya asili:

“Nashukuru sana kupata nafasi hii. Kama Mhifadhi, naendelea kuwakaribisha kutembelea Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane.”

 Aliongeza kwa kumshukuru Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Musa Kuji, kwa kuendeleza mazingira wezeshi kwa wanawake katika uongozi na ubunifu:

“Tuzo hii si yangu peke yangu, ni heshima kwa TANAPA nzima, ushahidi kuwa ubunifu unazaa matokeo.”

Hifadhi zetu ni hazina ya Taifa
Kila unapozitembelea, unachangia uhifadhi, uchumi na maendeleo ya jamii.  

 


SIMBA SC YACHAPWA 1-0 NA PETRO DE LUANDA LIGI YA MABINGWA DAR

 

TIMU ya Simba SC imeanza vibaya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa bao 1-0 na Petro de Luanda ya Angola katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi D jioni ya Jumapili ya tarehe 23 Nov 2025 Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.


Bao pekee lililoizamisha Simba SC limefungwa na kiungo Mreno, Bernardo Oliveira Dias dakika ya 78 alipofumua shuti la umbali wa Nita 20 ambalo lilimbabatiza beki raia wa Afrika Kusini, Rushine De Reuck na kubadili njia likimpoteza mwelekeo kipa namba moja Tanzania, Yakoub Suleiman Ali.


Mechi nyingine ya Kundi D jana Espérance ililazimishwa sare ya bila mabao na Stade Malien ya Mali Uwanja wa Hammadi Agrebi, Tunisde Jijini Tunis nchini Tunisia.


Mechi zijazo Simba SC itasafiri kuwafuata Stade Malien Novemba 29 Uwanja wa Machi 26 Jijini Bamako nchini Mali, wakati Petro de Luanda wanarejea nyumbani kuwakaribisha Espérance de Tunis November 29. Uwanja wa Novemba 11 Jijini Luanda.

MUDATHIR APANDA JUKWAANI KUMFUATA RAIS ENG. HERSI BAADA YA GOLI LA DUBE

 

 
WENYEJI, Yanga SC wameanza vyema hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco jioni ya Jumamosi ya Tarehe 22 Novemba 2025 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. 

Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee katika mchezo huo wa kwanza wa Kund B, mshambuliaji wa Kimataifa wa Zimbabwe, Prince Mpumelelo Dube dakika ya 58 akimalizia pasi ndefu ya kiungo mzawa, Mudathir Yahya Abbas.

Hii inakuwa mara ya kwanza kihistoria Yanga kushinda mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiposhiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1998.