|
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Halifa Hida, |
NA PETER FABIAN
GSENGO BLOG
MWANZA.
HALMASHAURI ya Jiji la Mwanza, litatumia kiasi cha zaidi ya Shilingi milioni 500 kuanza kuwalipa fidia wananchi 47 wa maeneo ya Kata ya Igoma jirani na makaburi ya waliokufa katika ajari ya Meli ya MV Bukoba ili kupisha eneo hilo kujengwa maaegesho ya magari makubwa na daladala.
Akizungumza na leo Ofisini kwake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Halifa Hida, alisema kwamba tayari Jiji hilo kuanzia Februari 9 mwaka huu limeanza kuwalipa fidia wananchi wa maeneo hayo waliofanyiwa uthamini kwa mujibu wa taratibu na sheria za ardhi na mipango miji.
“Halmashauri ya Jiji tumeanza kulipa fidia wananchi hao kutokana na kupatikana kwa fedha kiasi cha Sh. 500.84 milioni, hii inatokana na wananchi wa maeneo hayo kufanyiwa uthamini na kuzuiliwa kuyaendeleza maeneo yao kwa muda murefu jambo ambalo limekuwa likisababisha wananchi kuilaumu Halmashauri,” alisema.
Hida alisema kwamba wananchi wanaolipwa fidia ni wale waliokwenye orodha na waliofanyiwa uthamini Septemba 9 mwaka 2014, watalipwa kulingana na eneo la kila mmoja, Halmashauri ilipofanya zoezi hilo lakini ilishindwa kuwalipa kwa wakati wananchi hao kutokana na kukosa fedha baada ya kumaliza kufanya uthamini.
“Wananchi hawakutuelewa kabisa kila tulipokuwa tukiwaeleza wavute subira, pia tuliwaeleza Serikali haiwezi kukataa kulipa fidia halali kwa wananchi wake zaidi itachelewesha tu, hali hii ilionyesha kuwa kero na kusababisha wananchi kila mara kulalamikia halmashauri,”alisema.
Aidha Mkurugenzi Hida, alisema kwamba wananchi ambao wameanza kuchukua malipo ya fidia zao wanapaswa kuachia maeneo hayo ili kuwezesha kuanza mchakato wa mradi wa ujenzi wa kituo kikubwa cha maengesho ya magari makubwa ya mizigo na daladala ili kuwezesha magari makubwa ya mizigo kutoingia katikati ya mji.
“Jiji letu linakabiliwa na changamoto ya msongamano wa magari hali iliyopelekea kuangalia jinsi ya kupunguza ikiwa ni pamoja na kuanzisha maegesho ya magari makubwa (Teminor Track) ili kuzuia magari hayo ya mizigo kuingia katikati ya Jiji lakini pia tutajenga kituo cha daladala ili zisiegeshe barabarani kama ilivyo sasa,”alisema.
Hida alitoa wito kwa wananchi wa maeneo yote yaliyofanyiwa uthamini kufika na vielelezo ambavyo vitawawezesha kulipwa fidia kwa kila mwananchi aliyeguswa, pia rai yangu kwa wananchi ni kuhakikisha wanaondoka badala ya kuchukua fidia kisha kusubili kuondolewa kwa nguvu jambo ambalo si vyema likajitokeza.