ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, September 19, 2025

KATIBU MKUU UWT TAIFA KUCHELE AWAPA SOMO WANAWAKE WA KILOLO UMUHIMU WA KUPIGA KURA ZA KISHINDO

 


NA MWANDISHI WETU,KILOLO.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa Ndg. Suzan Peter Kunambi (MNEC), amewahimiza wanachama kujitokeza kwa wingi kupiga kura nyingi za  ndio hata kama kuna sehemu kuna mgombea amepita bila kupingwa.

Katibu Kunambi ameyabainisha hayo wakati wa   mkutano wa ndani katika Kata ya Nyalumbu, Wilaya ya Kilolo,ambapo amesema wanachama wanapaswa kutofanya makosa na badala yake kumpa kura nyingi za kishindo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

"Kitu kikubwa ambacho ninawaomba wanachama wa ccm wa kilolo hususan wanawake tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kupiga kura za ndio hata kama mgombea fulani amepitwa bila kupimgwa,"amebainisha Katibu huyo.

Amebainisha kwamba ni vema kuweka mikakati kabambe ambayo itaweza kukisaidia chama cha mapinduzi kiweze kupata ushindi wa kishindo katika Mafiga matatu ambayo ni nafasi ya Urais,Udiwani pamoja na Ubunge.

Aidha amesisitiza kuwepo kwa mshikamano wa pamoja kati ya  wanachama wa CCM pamoja na wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika octoba 29 mwaka huu.

MABAKI YA DAWA MAJUMBANI JANGA KWA UHAI NA MAZINGIRA.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere.

 KATIKA sehemu mbili zilizotangulia za ripoti hii maalum, tulieleza namna mabaki ya dawa na vifaa tiba majumbani yanavyoendelea kuwa chanzo hatarishi cha uchafuzi wa mazingira, kuongeza usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa na kuathiri moja kwa moja afya ya wananchi.

Pamoja na juhudi za kisheria na kisera zilizowekwa kudhibiti changamoto hiyo, utekelezaji wake bado ni wa kusuasua, huku wananchi wengi wakiwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu namna salama ya kushughulikia taka hizo. 

Sehemu hii ya mwisho inaleta majibu, mapendekezo na mustakabali wa taifa katika kupambana na bomu hili la kimyamya ambalo kila kaya inaweza kuwa linachangia maradhi, pasipo kujua. Endelea 

SERA IPO, LAKINI...

Sera ya Afya ya mwaka 2007, ambayo pia inahusisha usimamizi wa taka za huduma za afya, imeweka bayana dhamira ya kulinda afya ya jamii na mazingira kupitia udhibiti wa taka kuanzia zinapozalishwa hadi zinapoteketezwa. Sera hiyo inaelekeza kuwapo miundombinu salama, elimu kwa jamii na mfumo wa ufuatiliaji unaosimamiwa kikamilifu. 

Hata hivyo, hali halisi katika maeneo mengi, hasa vituo vya afya vya mtaani na majumbani, inapingana kabisa na misingi ya sera hiyo. Dk. Peter Maziku, Mhadhiri kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dar es Salaam, anasema changamoto kubwa ipo kwenye utekelezaji. 

“Vituo vingi vya afya vya mtaani havina vifaa maalumu vya kuteketeza taka hatarishi. Badala yake, taka hizo huunguzwa kwenye mashimo ya wazi, zikiambatana na taka nyingine. Hii ni hatari kubwa kwa afya ya jamii na mazingira,” anasema. Kwa mujibu wa Dk. Maziku, udhibiti wa taka hizi hauwezi kufanikiwa pasipo ufuatiliaji wa mara kwa mara na uwajibikaji kutoka kwa mamlaka husika. 

Anaongeza kuwa vitendo vya kuchoma taka ovyo vimekuwa vya kawaida hata katika baadhi ya vituo vya afya binafsi, kutokana na ukosefu wa rasilimali au uelewa wa kina. 

Dk. Stanley Mwita, mtafiti wa masuala ya afya, katika utafiti wake wa mwaka 2021, alibaini kuwa gharama kubwa na taratibu nyingi zinazohitajika ili kupata kibali cha kuteketeza taka za dawa ni miongoni mwa sababu zinazochangiautupaji holela wa  dawa na vifaa tiba. “

Wamiliki wa baadhi ya vituo binafsi hulazimika kutafuta njia mbadala, ambazo isivyo bahati si salama kwa mazingira kama vile kutupa kwenye mashimo au kwenye madampo kama taka za kawaida,” anasema Dk. Stanley. 

Ni hoja inayoungwa mkono na matukio mengi ya vitendo vya kiholela vya utupaji dawa maeneo ya makazi, ambako wananchi huzifukia dawa au kuzitupa katika mapipa ya taka, bila kujua athari zake kwa udongo, vyanzo vya maji na viumbe hai. 

UTARATIBU SAHIHI 

Benedict Brash, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Kati, anafafanua kuwa kuna utaratibu rasmi unaopaswa kufuatwa na vituo vya afya vya umma na binafsi katika uteketezaji dawa na vifaa tiba vilivyopitwa na muda. 

“Wamiliki wa vituo wanapaswa kuwasilisha ombi rasmi kwa TMDA likiwa na barua ya maombi, aina ya dawa, na thamani ya bidhaa hizo. Baada ya hapo, kibali hutolewa na uteketezaji hufanyika kwa njia salama kwa kutumia vifaa maalum,” anasema Brash. 

Kwa upande wa vifaa tiba kama sindano, Brash anasema huwa vinawekwa katika incinerator mashine maalum ya kuchoma taka kwa joto la juu ambalo huharibu kemikali na vimelea vyote hatarishi. Brash anasema TMDA pia inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya kuhifadhi au kutupa dawa ovyo. 

Lakini, changamoto kubwa inaonekana zaidi kwa wagonjwa wanaopatiwa huduma nyumbani. Hawana mwongozo maalum wa namna ya kushughulikia dawa zilizobaki, jambo linalosababisha wengi kuzihifadhi majumbani au kuzitupa kiholela, kwa dhana ya kuwa ni mali yao binafsi. 

ELIMU KWA JAMII 

Dk. Christina Kifunda, Mhadhiri wa masuala ya mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), anasisitiza kuwa elimu kwa jamii ndiyo silaha muhimu zaidi katika mapambano dhidi ya utupaji ovyo wa mabaki ya dawa. 

“Wananchi wengi hawajui kwamba  dawa zilizobaki zinaweza kuwa sumu kubwa. Tunahitaji kuwa na vituo rasmi vya ukusanyaji dawa hizo katika kila kata au mtaa,” anasema Dk. Kifunda. 

Anaongeza kuwa sekta ya afya inapaswa kutoa mwongozo wa moja kwa moja kwa wagonjwa kuhusu nini cha kufanya iwapo dawa walizopewa zitakuwa zimebaki. 

“Watoa huduma wa afya wawaeleze wagonjwa ‘dawa hizi ni kwa siku tano, ukibakiwa nazo, peleka sehemu maalum’. Mwongozo huo uwe wazi na utekelezwe,” anashauri Dk. Kifunda. 

JICHO LA CAG 

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022/23 ilifichua udhibiti hafifu katika vituo binafsi vya afya nchini. 

Mojawapo ya upungufu ulioonekana ni kutokuwa na maeneo maalum ya kuhifadhi dawa zilizopitwa na muda au vifaa tiba visivyotumika tena. 

CAG aliitaka serikali kuweka mfumo madhubuti wa kufuatilia uendeshaji vituo hivyo, hasa ikizingatiwa kuwa huduma za afya binafsi zimeongezeka kwa kasi, lakini uwezo wa kusimamia taka zao bado ni mdogo sana. 

Vilevile, kama mwanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania ina wajibu wa kuzingatia miongozo ya kimataifa kuhusu usimamizi wa taka za afya. 

WHO inapendekeza matumizi ya incinerators zilizoidhinishwa, ambazo zina uwezo wa kuchoma taka kwa joto la juu na kupunguza uchafuzi wa hewa unaotokana na gesi zenye sumu. 

Aidha, WHO inasisitiza kuwapo utaratibu wa kuzuia dawa zisizohitajika kuingia katika mzunguko wa matumizi, hasa katika mazingira ya dharura au vituo vya afya vyenye uhaba wa vifaa. 

OSHA YAKABIDHI VIFAA CHUO CHA UFUNDI MIRONGO JIJINI MWANZA

 

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi, akiwasilisha hotuba yake wakati wa Bonanza la OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR BONANZA 2025) lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyakabungo Jijini Mwanza akiwa ni Mgeni Rasmi wa Bonanza hilo. Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda wakimkabidhi Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Mirongo vifaa mbalimbali vya msaada vilivyotolewa na OSHA kukiwezesha chuo hicho. Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kompyuta, makoti ya usalama na vifaa vya michezo. 

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda wakimkabidhi Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Mirongo vifaa mbalimbali vya msaada vilivyotolewa na OSHA kukiwezesha chuo hicho. Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kompyuta, makoti ya usalama na vifaa vya michezo.
Mwenyekiti wa timu ya OSHA Iliyoshiriki SHIMIWI mwaka 2025 Ndugu Charles Mhilu akimkabidhi kikombe  Mtendaji Mkuu wa OSHA Bi Khadija Mwenda, mara timu hiyo ya OSHA kuibuka timu Bora yenye nidhamu miongoni mwa timu 50 shindani kwenye mashindano yailyoshirikisha zaidi ya timu 50 toka taasisi,wakala za Serikali na Timu toka RAS mashindano yaliyofanyika hivi karibuni jijini Mwanza.

Na  Fredy Mgunda,Mwanza.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mheshimiwa Amina Makilagi, amewataka waajiri na wafanyakazi kote nchini kuitekeleza kikamilifu Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Na. 5 ya mwaka 2003 ili kupunguza au kuondoa kabisa ajali na magonjwa yanayotokana na mazingira duni ya kazi.


Mheshimiwa Makilagi alitoa wito huo jana wakati wa Bonanza la OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR Bonanza 2025) lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyakabungo, Wilaya ya Nyamagana, Jijini Mwanza. Bonanza hilo lilihusisha shughuli mbalimbali za kijamii na michezo kwa lengo la kuimarisha mshikamano kati ya OSHA na jamii inayohudumiwa, pamoja na kutoa msaada kwa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Mirongo, wakiwemo wenye ulemavu.


Katika tukio hilo, OSHA ilikabidhi vifaa mbalimbali kwa Chuo cha Ufundi Mirongo, vikiwemo kompyuta, vifaa kinga vya usalama kazini, pamoja na vifaa vya michezo kama mipira na jezi za michezo.


Akizungumza kama Mgeni Rasmi, Mheshimiwa Makilagi aliipongeza OSHA kwa juhudi zake za kuhakikisha mazingira salama na yenye afya sehemu za kazi na kuonesha moyo wa huruma kwa makundi maalum katika jamii.


“Nitoe rai kwa waajiri na wafanyakazi nchini kuisoma na kuitekeleza Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Sheria hii ikitekelezwa ipasavyo, maeneo ya kazi yatakuwa salama, bila ajali wala magonjwa, hivyo kuongeza tija kazini,” alisema Mkuu wa Wilaya Makilagi.


Aidha, aliihakikishia OSHA ushirikiano wa Halmashauri na Ofisi yake katika kusimamia usajili na ukaguzi wa maeneo ya kazi, sambamba na kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya maboresho ya mazingira ya kazi.


Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, alisema Bonanza hilo ni sehemu ya mpango wa taasisi hiyo wa kurudisha kwa jamii (Corporate Social Responsibility) na kwamba msaada uliotolewa kwa Chuo cha Mirongo umetokana na tathmini iliyofanywa na wataalam wa OSHA baada ya kutembelea chuo hicho.


“Tunaamini kuwa kwa kusaidia vyuo vya ufundi kama Mirongo, tunachangia kwa kiasi kikubwa maandalizi ya wataalamu wa baadaye katika fani muhimu za kiufundi na kazi,” alisema Bi. Mwenda.


Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mirongo, Bi. Herieth Richard, pamoja na mwanafunzi wa fani ya ushonaji, Bi. Aneth Augustino, waliishukuru OSHA kwa msaada huo ambao wamesema umeongeza ari ya kujifunza na kushiriki katika shughuli za kijamii.


Bonanza hilo lilihusisha michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha, na michezo ya jadi kama kukimbia kwenye magunia, kukimbia na ndimu kwenye kijiko, rede na kukamata kuku. Washiriki walitoka OSHA na vyuo vya Ufundi vya Mirongo, Nyakato na Kisesa.


Chuo cha Ufundi Mirongo kinamilikiwa na Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), na hutoa mafunzo ya umeme, useremala, ushonaji na uchomeleaji kwa vijana wakiwemo wenye mahitaji maalum.

KOKA AOMBA RIDHAA YA KUCHAGULIWA NA WANANCHI KATA YA VISIGA ILI KUWALETEA CHACHU YA MAENDELEO

 


NA VICTOR MASANGU,KIBAHA  

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kibaha mjini kupitia tiketi ya Chama cha mapinduzi Silvestry Koka amesema kwamba  endapo akipata ridhaa ya kuchaguliwa ataboresha sekta ya elimu na afya kwa wakazi wa kata ya Visiga.


Koka ameyasema hayo wakati wa  mkutano wa  kampeni katika kata ya Visiga uliohudhuliwa na viongozi mbali mbali wa chama pamoja na wananchi.

Koka amesema kwamba endapo akichaguliwa kupata nafasi hiyo atahakikisha anaboresha elimu kwa kutoa madawati elfu 1000 kwa shule za msingi ili lengo ikiwa ni kuongeza kiwango cha ufaulu.

Amebainisha kwamba pia atashirikiana bega kwa bega na serikali katika kujenga shule moja mpya ya msingi ikiwa sambamba na shule moija mpya ya sekondari katika kata ya Visiga.

Kadhalika Koka amebainisha kuwa katika kuwawekea mazingira  mazuri wanafunzi atahakikisha anaboresha miundombinu ya matundu ya vyoo katika baadhi ya shule.

Akizungumzia kuhusiana na  miundombinu ya nishati ya umeme amebainisha atalivalia njuga suala la nishati ya umeme katika baadhi ya mitaa ikiwemo eneo la Zegereni,Saheni na maeneo mengine ya pembezoni.

Kwa upande wake Mgombea Udiwani kata ya Visiga Mohamed Mpaki amesema kwamba atahakikisha anatekeleza  ilani ya chama kwa vitendo katika miradi mbali mbali ya maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka lengo kubwa ni kuweza kushinda kwa kishindo katika nafasi ya Urais,Ubunge na Udiwani.

Thursday, September 18, 2025

ORODHA YA WACHEZAJI WA SIMBA SC WALIOPO BOTSWANA

 

SIMBA SC baada ya kupoteza Ngao ya Jamii, Septemba 16 2025 mbele ya Yanga SC msafara ulikwea pipa na umefika salama Botswana kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali dhidi ya Gaborone United.

Hii hapa orodha ya wachezaji wa Simba SC waliopo Botswana watakuwa na kazi Jumamosi ya Septemba 20 2025:-

Makipa

Moussa Camara, Yakoub Suleiman na Alexender Erasto.

Mabeki

Shomari Kapombe, Anthony Mligo. Rushine De Reuck, Wilson Nangu, Naby Camara.

Viungo

Yusuph Kagoma, Allasane Kante, Kibu Dennis, Ellie Mpanzu. Ladack Chasambi, Mzamiru Yassin, Neo Maema. Joshua Mutale, Jean Ahoua, Daud Semfuko Morice Abraham.

Washambuliaji

Steven Mukwala, Seleman Mwalimu, Jonathan Sowah.

SUBIRA MGALU KUWAKOMBOA WANANCHI BAGAMOYO FURSA ZA AJIRA NA BARABARA ZA LAMI

 


NA VICTOR MASANGU, BAGAMOYO 


Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bagamoyo kupitia tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM) Subira Mgalu ameahidi kuboresha huduma ya afya,maji na miundombinu ya barabara endapo akipewa ridhaa ya kuwaongoza wananchi.
Mgalu amebainisha kwamba katika kata zote 11 atahakikisha anaweka mikakati madhubuti ya kuboresha miundombinu ya barabara katika kiwango cha lami.

Pia Mgalu amebainisha kuwa endapo akichaguliwa ataleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo katika nyanja mbali mbali ikiwemo sekta ya afya,elimu,maji,kuboresha ujenzi wa mifereji ya kisasa pamoja na huduma za kijamii.

Kadhalika ameahidi kusimamia suala la mradi mkubwa wa  ujenzi wa bandari ambayo itaweza kusimamia kwa kiasi kikubwa kutoa fursa za ajira kwa wananchi wa Bamogamoyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi(CCM) Martha Mlata ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo amewataka wanachama na wananchi wa Bagamoyo kumpa ushirikiano wa kutosha Subira kwa kumpatia kura nyingi za kishindo kwa lengo la  kuwaletea maendeleo.




Aidha Mwenyekiti huyo amesema anatambua uwezo mkubwa alionao Subira hivyo ataweza kusikiliza kero na kutatua changamoto za wananchi.

"Wana Bagamoyo mmepata mgombea ubunge mwenye uwezo mkubwa sana katika masuala mbali ya kimaendeleo na ninamtambua siku nyingi hivyo nina imani ataleta mabadiliko makubwa kwa wananchi ,"amebainisha Mwenyrkiti.

Naye Mgombea ubunge wa viti maalumu Mkoa wa Pwani kupitia (UWT) Hawa Mchafu ameomba wanachama wa CCM pamoja na wananchi kumpa kura nyingi za kishindo Rais Dkt.Samia,Subira pamoja na madiwani.

Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Aboubakar Mlawa amesema kwamba wamejipanga kikamilifu na wamejiandaa vya kutosha kwa ajili ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika octoba 29 mwaka huu.

Uzinduzi rasmi wa kampeni  katika Jimbo la Bagamoyo umehudhuliwa na viongozi mbali mbali wa chama ambapo umekwenda sambamba na kuwanadi wagombea wa udiwani,Ubunge pamoja na nafasi ya Rais.

MWENGE WA UHURU WAWEKA JIWE LA MSINGI WODI YA MAMA NA MTOTO MWAMI NTALE

 

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi, ameweka jiwe la msingi katika wodi ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya cha Mwami N’tale, kilichopo kata ya Heru, Halmashauri ya Mji Kasulu.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi, ameweka jiwe la msingi katika wodi ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya cha Mwami N’tale, kilichopo kata ya Heru, Halmashauri ya Mji Kasulu.

Na Fredy Mgunda,Kasulu/Kigoma.

 Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi, ameweka jiwe la msingi katika wodi ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya cha Mwami N’tale, kilichopo kata ya Heru, Halmashauri ya Mji Kasulu.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Ussi amesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao kwa amani, utulivu, na kuchagua viongozi wanaowataka. Amesema kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu inahimiza amani kama msingi wa maendeleo ya taifa.

“Maendeleo tunayoyaona leo ni matokeo ya utulivu na amani inayotamalaki nchini. Hivyo ni wajibu wetu kuilinda na kuithamini hali hii,” alisema Ussi.

Mradi wa ujenzi wa kituo hicho umegharimu kiasi cha Tsh milioni 300, na tayari umekamilika kwa asilimia 100. Utaanza kutoa huduma za afya kwa kina mama na watoto katika eneo la Heru na maeneo jirani.

Kituo hiki kinatarajiwa kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya mama na mtoto kwa kutoa huduma bora, za karibu, na za uhakika kwa wananchi.

Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwa chombo muhimu katika kuhamasisha maendeleo, uwajibikaji, na uzalendo miongoni mwa Watanzania.

KATIBU MKUU UWT AUNGURUMA KWA WANAWAKE IRINGA AWAFUNDA JUU UMOJA KIPINDI CHA UCHAGUZI MKUU

 


NA MWANDISHI WETU,IRINGA


Katibu Mkuu wa umoja wa wanawake (UWT)  Taifa Ndg. Suzan Peter Kunambi (MNEC) amewahimiza wanawake kuweka misingi imara ya kuwa na umoja na mshikamano hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu  ambao unatarajiwa kufanyika Octoba 29 mwaka huu.

Katibu huyo ameyasema hayo wakati wa mikutano mbali mbali kwa ajili ya kuweza kuwanadi na kuwaombea kura wagombea wa CCM katika nafasi ya Urais,Ubunge pamoja na udiwani.

"Kitu kikubwa nawaomba wanawake wenzangu wa iringa mjini pamoja na iringa vijijini kuhakikisha mnashikamana kwa pamoja ili tuweze kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaks huu,"amebainisha Katibu huyo.


Aidha Katibu huyo kupitia mikutano hiyo ameweza kupata fursa ya kuwapokea wanachama wapya 7 kutoka  Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Baadhi ya wanachama hao ambao wamejiunga na CCM  wameahidi kuungana na wanachama wa CCM katika kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu wa UWT  Suzan Peter Kunambi amemnadi wagombea wa CCM nafasi ya Udiwani kata ya Migori  Ndg. Fatma Moge, huku akiwaomba wananchi  kumchagua kwa kura nyingi za kishindo  Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Pia katibu huyo amewaomba wana ccm kumpa ridhaa ya kuwaongoza na kumpa kura nyingi   Ndg.William Lukuvi ambaye ni Mgombea wa Ubunge Jimbo la Isimani  Wilaya ya Iringa Vijijini.


SIMBA SC WAKWEA PIPA KUELEKEA BOTSWANA KUWAVAA GABORONE UTD JUMAMOSI LIGI YA MABINGWA

 

KIKOSI cha Simba SC kimeondoka JANA mchana kutoka Jijini Dar es Salaam kwenda Botswana kwa ajili ya mchezo wa kwanza Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Gaborone United Jumamosi kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa wa Botswana Jijini Gaborone.


Timu hizo zitarudiana Jumapili ya Septemba 28 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na mshindi wa jumla atakutana na mshindi wa jumla kati ya Simba Bhora ya Zimbabwe na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini.

FOLZ 'AZIMA' SHEREHE ZA WACHEZA YANGA DHIDI YA SIMBA.

 


KOCHA wa Yanga, Romain Folz, amewataka wachezaji wa timu hiyo kusahau ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Simba na kugeukia mechi yao ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete de Benguela ya Angola.

Mara baada ya mchezo wa juzi wa Ngao ya Jamii kumalizika huku wachezaji wa timu hiyo wakiwa na furaha, Folz aliitisha kikao cha dharura na kuwataka wachezaji hao kusahahu ushindi huo na kuelekeza mawazo na nguvu zao kwenye mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezaji mmoja wa timu hiyo ameliambia gazeti hili kuwa furaha yao ya kuifunga Simba ilikatishwa ghafla na Kocha Folz, alipowakumbusha kuwa wana mechi ngumu dhidi ya Wiliete na waache kushangilia mechi hiyo ya Ngao ya Jamii.

"Baada ya kuifunga Simba tulirudi vyumbani tukiwa na furaha kubwa, wenyewe tunashangilia, kocha Folz, alipoingia alikuta tunashangilia sana, akatuamuru tukae chini haraka, akatuambia ile ilikuwa mechi ya 'bonanza', tujiandae na mechi kamili ni dhidi ya Wiliete wikiendi hii, basi ikabidi tukae kimya wote," alisema mchezaji huyo.


Alisema kocha huyo amewataka kuweka mkazo kenye mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa na kusahau ushindi wa Ngao ya Jamii.

Kikosi cha Yanga tayari kimetua nchini Angola tayari kwa mchezo huo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Yanga itacheza mchezo huo kesho kwenye uwanja wa 11 de Novembro, jijini Luanda saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na baadaye kurudiana jijini Dar es Salaam Septemba 27.

Wakati Simba na Yanga zikiwa zimeondoka nchini, Azam ilikuwa ya kwanza, Ijumaa iliyopita kwenda Juba, nchini Sudan Kusini kwa ajili ya mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya El Merrikh Bentiu, unaotarajiwa kuchezwa, Jumamosi, Uwanja wa Juba, nchini humo, saa 11:00 jioni kwa sasa za Tanzania.

SAMIA: UKIPIGA KURA KATULIE NYUMBANI KUDUMISHA AMANI.

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan.

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan amesema atahakikisha amani na utulivu vinatawala katika msimu wote wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Katika kauli yake hiyo, amewasihi wananchi kufuata utaratibu uliowekwa wa kupiga kura na kurudi nyumbani, kwa kuwa uchaguzi ni tendo la kidemokrasia na sio vita.

Dk Samia ametoa kauli hiyo Jumatano Septemba 17, 2025 alipozungumza na wananchi wa Makunduchi visiwani Zanzibar, wakati wa mkutano wake wa kampeni za urais, alioufanyia katika Uwanja wa Kajengwa.

“Uchaguzi ni tendo la kidemokrasia, ni watu kwenda kwa utaratibu uliowekwa, kuweka kura zetu rudi nyumbani katulie ili nchi ibaki salama,” amesema.

Amewataka wananchi visiwani humo, kuhakikisha katika uchaguzi wanadumisha amani na utulivu, kwani tukio hilo sio tendo la vita.

Dk Samia amesema baada ya kuapishwa kuwa Rais, alikutana na wazee wa Pemba, pamoja na mambo mengine walimwelekeza kuhakikisha anadumisha amani na utulivu, jambo ambalo ameapa kuhakikisha linatimia.

“Si muda wote kushika silaha kunaleta suluhisho, muda wote kushika silaha yoyote, iwe ya moto au ya kimila hakuleti suluhisho la maana. Niwaombe sana wote wanaotusikiliza, amani na utulivu wa nchi yetu ni jambo la muhimu zaidi kuliko mengine yote hasa wakati huu wa uchaguzi,” amesema.

Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania, vimejipanga vema kulinda nchi.

“Sasa hutaki kishindo kapige kura rudi nyumbani tulia, tumejipanga vema. Kwa hiyo nisisitize suala la amani na utulivu,” amesema Dk Samia.

Kauli hiyo ya Dk Samia, imesisitizwa pia na Mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk Hussein Ali Mwinyi aliyesema amani, umoja, mshikamano na maridhiano nchini Tanzania kwa kuwa ndicho kipaumbele cha chama hicho.

MASHAHIDI 100 KUWASILISHA USHAHIDI KESI YA KUPOROMOKA JENGO KARIAKOO

Mashahidi 100 kuwasilisha ushahidi kesi ya kuporomoka jengo Kariakoo

Zaidi ya mashahidi 100 wanatarajiwa kuwasilisha ushahidi katika kesi ya mauaji bila kukusudia inayowakabili wafanyabiashara sita, kufuatia kuporomoka kwa jengo la ghorofa mnamo Novemba 16, 2024, katika Mtaa wa Mchikichi na Kongo, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Kesi hiyo iliwasilishwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kusomwa maelezo ya mashahidi na vielelezo kwa washitakiwa. Hata hivyo, hatua hiyo haikufanyika kutokana na upande wa mashtaka kutokamilisha maandalizi.

Wakili wa Serikali, Clemence Kato, aliieleza mahakama kuwa kesi hiyo inatarajiwa kuwa na mashahidi zaidi ya 100, lakini hadi sasa ni nusu pekee ya mashahidi ambao maelezo yao yamekwishachapwa.

“Waheshimiwa, tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kusoma maelezo ya mashahidi na vielelezo kwa washitakiwa, kwa kuwa bado hatujakamilisha maandalizi,” alisema Wakili Kato mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Mhini alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 9, 2025.

Washitakiwa:-

Wafanyabiashara wanaokabiliwa na kesi hiyo ni:

  • Lendela Mdete, mkazi wa Mbezi
  • Zenabu Islam maarufu kama Zaibanu, mkazi wa Kariakoo
  • Ashour Ashour, mkazi wa Ilala
  • Soster Nziku na Stephen Nziku, wakazi wa Mbezi Beach
  • Aloyce Sangawe, mkazi wa Sinza Wanadaiwa kusababisha vifo kwa uzembe baada ya jengo walilohusishwa nalo kuporomoka na kuua wakazi na wafanyakazi waliokuwemo.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, jalada hilo bado halijakamilika na linasubiri kuwasilishwa katika Mahakama Kuu, kutokana na uzito wa kosa linalowakabili washitakiwa.

MGOMBEA UDIWANI KATA YA KIBAMBA ATEMA CHECHE AAHIDI NEEMA YA MAJI NA BARABARA KWA WANANCHI

 


NA VICTOR MASANGU,KIBAMBA 


Mgombea mteule wa nafasi ya  udiwani kata ya Kibamba kupitia tiketi ya Chama cha mapinduzi (CCM) Otaigo Mwita ameahidi kuboresha  sekta ya afya,elimu na huduma ya maji endapo akipata ridhaa ya kuchaguliwa katika uchaguzi mkuuu wa mwaka 2025.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa ufunguzi rasmi  wa kampeni za uchaguzi ngazi ya Kata ya Kibamba ambapo amesema kwamba lengo lake kubwa ni kuleta chacha ya maendeleo katika nyanja mbali mbali.

Pia Otaigo amebainisha kwamba endapo akichaguliwa ataweka mipango madhubuti ya kutatua kero kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Kibamba.

"Lengo langu kubwa la kuwania nafasi hii ni kwa ajili ya kuweza kushirikiana na serikali katika kuwaletea wananchi wa Kibamba maendeleo mbali mbali ikiwemo suala la maji.afya,miundombinu ya barabara,pamoja na huduma za kijamii,"amebainisha Otaigo.

Kwa upande wake mgombea Ubunge  mteule wa Jimbo la Kibamba kupitia tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM) Angella Kairuki pindi atakapochaguliwa atahakikisha anaboresha miundombinu ya barabara za mitaa ili ziweze kupitika kwa urahisi.

Kairuki ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kampeni hizo amesema lengo lake kubwa ni kutatua  kero na changamoto mbali mbali za wananchi katika nyanja mbali mbali.

"Wananchi wa Kibamba naomba sana mnichague na kunipa kura nyingi ili niweze kuwatumikia katika nyanja mbali mbali ikiwemo suala la maji,miundombinu ya barabara pamoja na kuboresha huduma ya afya pamoja na mahitaji mengjne ya msingi,"amesema Mgombea Kairuki.

Uzinduzi wa kampeni za chama chama cha mapinduzi (CCM) ngazi ya kata ulihudhuliwa na viongozi mbali mbali wa chama,serikali pamoja na wananchi ambao walifika kwa ajili ya kusikiliza sera za wagombea mgombea udiwani pamona na Ubunge.

Re: MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA AENDELEA KUWAPIGA MSASA WANASIASA


Na Mwandishi Wetu - Kilindi.

Vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu nchini mwaka 2025,katika Jimbo la Kilindi vimetakiwa kufanya kampeni za kistaarabu ili kuendeleza utulivu na amani iliopo nchini.

Wito huo umetolewa na Afisa mwandamizi kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa Bi. Edna Assey katika kikao cha mafunzo na vyama vya siasa vyenye wagombea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, katika jimbo la Kilindi kilichofanyika tarehe 17/09/2025 katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya wilaya ya Kilindi.
“Wakati wa kufanya kampeni zenu acheni sera ziongee” alisema Afisa mwandamizi Bi Assey na kuvitaka vyama vya siasa kunadi sera zao ili zieleweke kwa wananchi na kuacha kutumia maneno na vitendo ambavyo vinaweza kuhatarisha kuvunjika kwa amani na utulivu.
Aliongeza kusema kuwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ina majukumu mbalimbali ikiwemo kusimamia utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa sura ya 258 na kuvitaja vitendo vinavyokatazwa na sheria ya vyama vya siasa kuwa ni pamoja na Kunadi sera zinazopingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Katiba ya Zanzibar na Sheria nyingine za nchi, Kuunda kikundi cha ulinzi na usalama cha aina yeyote au kuwa na taasisi inayolenga kufanya majukumu ya jeshi la polisi au vikosi vingine vya ulinzi na usalama wa nchi.
Kuratibu, kuendesha au kufadhili mafunzo yeyote ya kutumia nguvu au silaha kwa wananchama wake au kwa mtu yeyote Kuhamasisha udini,ukabila na ukanda ,kuhamasisha kuvunjika kwa Muungano wa Tanzania au kuwa na lengo la kufanya siasa upande mmoja wa Muungano Vitendo vingine vinavyokatazwa na sheria ya vyama vya siasa ni kuruhusu au kuhamasisha matumizi ya nguvu kama njia ya kufikia malengo ya kisiasa.
Kuruhusu viongozi au wananchama wake kutumia maneno ya matusi,dhihaka,kashfa na uchochezi yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani Kupeperusha bendera ya chama,kufanya siasa au kufungua tawi katika maeneo ya kazi,shule,vyuo,ibada
,majengo ya serikali au umma Kutoa matamshi,kuandaa machapisho,kuharibu au kufanya kitendo chochote chenye dhamira ya kudhalilisha au kudhihaki bendera ya chama kingine na kufanya mikutano au maandamano bila kufuata utaratibu wa kisheria.
Kwa upande wao viongozi wa vyama vya siasa Wilayani Kilindi waliipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwa maandalizi mazuri ya uchaguzi na kuomba kuendeleza ushirikiano mzuri kati ya serikali na vyama vya siasa.