KATIKA sehemu mbili zilizotangulia za ripoti hii maalum, tulieleza namna mabaki ya dawa na vifaa tiba majumbani yanavyoendelea kuwa chanzo hatarishi cha uchafuzi wa mazingira, kuongeza usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa na kuathiri moja kwa moja afya ya wananchi.
Pamoja na juhudi za kisheria na kisera zilizowekwa kudhibiti changamoto hiyo, utekelezaji wake bado ni wa kusuasua, huku wananchi wengi wakiwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu namna salama ya kushughulikia taka hizo.
Sehemu hii ya mwisho inaleta majibu, mapendekezo na mustakabali wa taifa katika kupambana na bomu hili la kimyamya ambalo kila kaya inaweza kuwa linachangia maradhi, pasipo kujua. Endelea
SERA IPO, LAKINI...
Sera ya Afya ya mwaka 2007, ambayo pia inahusisha usimamizi wa taka za huduma za afya, imeweka bayana dhamira ya kulinda afya ya jamii na mazingira kupitia udhibiti wa taka kuanzia zinapozalishwa hadi zinapoteketezwa. Sera hiyo inaelekeza kuwapo miundombinu salama, elimu kwa jamii na mfumo wa ufuatiliaji unaosimamiwa kikamilifu.
Hata hivyo, hali halisi katika maeneo mengi, hasa vituo vya afya vya mtaani na majumbani, inapingana kabisa na misingi ya sera hiyo. Dk. Peter Maziku, Mhadhiri kutoka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dar es Salaam, anasema changamoto kubwa ipo kwenye utekelezaji.
“Vituo vingi vya afya vya mtaani havina vifaa maalumu vya kuteketeza taka hatarishi. Badala yake, taka hizo huunguzwa kwenye mashimo ya wazi, zikiambatana na taka nyingine. Hii ni hatari kubwa kwa afya ya jamii na mazingira,” anasema. Kwa mujibu wa Dk. Maziku, udhibiti wa taka hizi hauwezi kufanikiwa pasipo ufuatiliaji wa mara kwa mara na uwajibikaji kutoka kwa mamlaka husika.
Anaongeza kuwa vitendo vya kuchoma taka ovyo vimekuwa vya kawaida hata katika baadhi ya vituo vya afya binafsi, kutokana na ukosefu wa rasilimali au uelewa wa kina.
Dk. Stanley Mwita, mtafiti wa masuala ya afya, katika utafiti wake wa mwaka 2021, alibaini kuwa gharama kubwa na taratibu nyingi zinazohitajika ili kupata kibali cha kuteketeza taka za dawa ni miongoni mwa sababu zinazochangiautupaji holela wa dawa na vifaa tiba. “
Wamiliki wa baadhi ya vituo binafsi hulazimika kutafuta njia mbadala, ambazo isivyo bahati si salama kwa mazingira kama vile kutupa kwenye mashimo au kwenye madampo kama taka za kawaida,” anasema Dk. Stanley.
Ni hoja inayoungwa mkono na matukio mengi ya vitendo vya kiholela vya utupaji dawa maeneo ya makazi, ambako wananchi huzifukia dawa au kuzitupa katika mapipa ya taka, bila kujua athari zake kwa udongo, vyanzo vya maji na viumbe hai.
UTARATIBU SAHIHI
Benedict Brash, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Kati, anafafanua kuwa kuna utaratibu rasmi unaopaswa kufuatwa na vituo vya afya vya umma na binafsi katika uteketezaji dawa na vifaa tiba vilivyopitwa na muda.
“Wamiliki wa vituo wanapaswa kuwasilisha ombi rasmi kwa TMDA likiwa na barua ya maombi, aina ya dawa, na thamani ya bidhaa hizo. Baada ya hapo, kibali hutolewa na uteketezaji hufanyika kwa njia salama kwa kutumia vifaa maalum,” anasema Brash.
Kwa upande wa vifaa tiba kama sindano, Brash anasema huwa vinawekwa katika incinerator mashine maalum ya kuchoma taka kwa joto la juu ambalo huharibu kemikali na vimelea vyote hatarishi. Brash anasema TMDA pia inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya kuhifadhi au kutupa dawa ovyo.
Lakini, changamoto kubwa inaonekana zaidi kwa wagonjwa wanaopatiwa huduma nyumbani. Hawana mwongozo maalum wa namna ya kushughulikia dawa zilizobaki, jambo linalosababisha wengi kuzihifadhi majumbani au kuzitupa kiholela, kwa dhana ya kuwa ni mali yao binafsi.
ELIMU KWA JAMII
Dk. Christina Kifunda, Mhadhiri wa masuala ya mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), anasisitiza kuwa elimu kwa jamii ndiyo silaha muhimu zaidi katika mapambano dhidi ya utupaji ovyo wa mabaki ya dawa.
“Wananchi wengi hawajui kwamba dawa zilizobaki zinaweza kuwa sumu kubwa. Tunahitaji kuwa na vituo rasmi vya ukusanyaji dawa hizo katika kila kata au mtaa,” anasema Dk. Kifunda.
Anaongeza kuwa sekta ya afya inapaswa kutoa mwongozo wa moja kwa moja kwa wagonjwa kuhusu nini cha kufanya iwapo dawa walizopewa zitakuwa zimebaki.
“Watoa huduma wa afya wawaeleze wagonjwa ‘dawa hizi ni kwa siku tano, ukibakiwa nazo, peleka sehemu maalum’. Mwongozo huo uwe wazi na utekelezwe,” anashauri Dk. Kifunda.
JICHO LA CAG
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022/23 ilifichua udhibiti hafifu katika vituo binafsi vya afya nchini.
Mojawapo ya upungufu ulioonekana ni kutokuwa na maeneo maalum ya kuhifadhi dawa zilizopitwa na muda au vifaa tiba visivyotumika tena.
CAG aliitaka serikali kuweka mfumo madhubuti wa kufuatilia uendeshaji vituo hivyo, hasa ikizingatiwa kuwa huduma za afya binafsi zimeongezeka kwa kasi, lakini uwezo wa kusimamia taka zao bado ni mdogo sana.
Vilevile, kama mwanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania ina wajibu wa kuzingatia miongozo ya kimataifa kuhusu usimamizi wa taka za afya.
WHO inapendekeza matumizi ya incinerators zilizoidhinishwa, ambazo zina uwezo wa kuchoma taka kwa joto la juu na kupunguza uchafuzi wa hewa unaotokana na gesi zenye sumu.
Aidha, WHO inasisitiza kuwapo utaratibu wa kuzuia dawa zisizohitajika kuingia katika mzunguko wa matumizi, hasa katika mazingira ya dharura au vituo vya afya vyenye uhaba wa vifaa.
Tupe maoni yako

0 comments:
Post a Comment