Dar es Salaam. Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema aliyeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa ameupa umoja huo ushindi wa viti 116 vya wabunge katika Bunge la kumi na moja litakaloanza Novemba 17, Mjini Dodoma.
Idadi hiyo ya wabunge ndiyo kubwa kuwahi kufikiwa na upinzani tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na tangu kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza wa ushindani wa vyama mwaka 1995.
Idadi ya wabunge wa Ukawa imeongezeka baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) jana kukamilisha kazi ya kuwateua wabunge wa viti maalumu ambao orodha yake itawasilishwa kwenye vyama husika.
Katika uchaguzi wa mwaka huu uliohusisha majimbo 258 kati ya 262, CCM imeshinda ubunge katika majimbo 188, CUF 35, Chadema 34, NCCR–Mageuzi kiti kimoja. NLD haikupata kiti wakati ACT – Wazalendo ilipata kiti kimoja.
Idadi wa wabunge wa Ukawa inatokana na jumla ya wabunge wa vyama vinavyounda umoja huo ambavyo ni Chadema, CUF na NCCR.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema CCM imepata viti maalumu 64, Chadema 36 na CUF 10.
“Vyama vingine havijapata wabunge wa viti maalumu kwa sababu havikufikisha asilimia tano ya kura za wabunge kwenye majimbo, kwa mujibu wa Katiba,” alisema Jaji Lubuva.
Kwa hesabu hiyo, Chadema imefikisha wabunge 70 kutoka 48 wa mwaka 2010, CUF ina wabunge 45 kutoka 36 wa mwaka 2010 wakati NCCR-Mageuzi imeshuka kutoka wabunge wanne wa 2010 hadi mmoja na kufanya idadi ya wabunge wa Ukawa kuwa jumla 116. CCM imefikisha wabunge 252.
Lubuva alisema jumla ya wabunge wa viti maalumu waliopatikana kwenye vyama vyote ni 110 kati ya 113 wanaotakiwa na watatu wanaosalia watapatikana baada ya kufanyika uchaguzi ambao uliahirishwa kwenye majimbo manane kutokana na sababu za vifo vya wagombea sita na kasoro mbalimbali katika majimbo mawili.
Majimbo ambayo wagombea walifariki dunia ni Masasi, Ludewa, Lushoto, Ulanga Mashariki, Arusha Mjini na Handeni Mjini wakati majimbo yenye kasoro ni Lulindi na Kijitoupele.
Jaji Lubuva alisema CCM imepata idadi hiyo ya wabunge wa viti maalumu baada ya kupata jumla kura 8,333,955 za wabunge, Chadema kura 4,627,923 za wabunge na CUF kura 1,257,955.
Kwa matokeo hayo, vyama 19 kati ya 22 vimeambulia patupu baada ya kupata kura zisizozidi asilimia tano ya kura zote halali za wabunge.
Jaji Lubuva alisema: “Tumetoa matokeo ya wabunge wa viti maalumu baada ya kupewa mamlaka kikatiba ya kutangaza wabunge wa viti maalumu vya wabunge wanawake visivyopungua asilimia 30 ya wabunge wote.”
Alisema kwa mujibu wa uamuzi wa Serikali wa mwaka 2010, idadi ya wabunge wanawake wa viti maalumu iliongezwa na kufikia asilimia 40, ambayo pia imetumika katika uteuzi wa mwaka huu.
“Haya yote ni kwa mujibu wa Ibara ya 66 Kifungu cha (1) na (b) na Ibara ya 78 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa kwa pamoja na Kifungu 86A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343,” alisema Jaji Lubuva.
Akizungumzia matokeo hayo, Kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe alisema chama chake kimefikisha asilimia 4 tu ya kura za wabunge, hivyo hakikutimiza vigezo vya kupata wabunge wa viti maalumu.
“Napenda kupongeza vyama vyote vilivyotimiza takwa la kisheria na hivyo kupata viti vya ubunge. Kwa namna yoyote, ile demokrasia ya Bunge imeimarika kwa idadi ya wabunge wa upinzani kuongezeka,” alisema na kuongeza:
“Sisi ACT – Wazalendo tumepata tunachostahili na kazi iliyo mbele yetu sasa ni kujenga chama kama taasisi imara na kufanya siasa za masuala. Tutatumia kiti kimoja tulichopata na madiwani 50 tuliopata nchi nzima na Manispaa ya Kigoma tutakayoongoza kuhakikisha tunaonyesha tofauti yetu na vyama vingine.”
Mkuu wa Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alielezwa kushangazwa kwake na NEC kukwepa jukumu la kufanya uteuzi na kutaja majina ya wabunge wateule wa viti maalumu na badala yake kuvisukumia vyama vya siasa kufanya hivyo. Alisema hadi jana jioni, bado majina ya wabunge wa viti hivyo yalikuwa hayajawasilishwa kwenye chama chao.
“Kwa nini NEC wamekwepa jukumu la kufanya uteuzi na kutaja majina ya wabunge wateule wa viti maalumu kisha wanatupia mpira kwa vyama,?” alihoji Makene.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya alisema ongezeko la wabunge wa Ukawa bungeni litasaidia kuwapo kwa mijadala mizito, kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. “Ongezeko la wabunge wa Ukawa litaongeza meno na kuwa na mijadala mizito, kwa sababu wabunge wengi wanao uwezo wa kujenga hoja, kufanya utafiti na wanajua kwa nini wamepewa nafasi hiyo,” alisema. CHANZO MWANANCHI.