ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, May 21, 2025

AISHI MANULA ASAFIRI NA SIMBA SC ZANZIBAR MECHI NA BERKANE

 

KIPA Aishi Salum Manula amesafiri na kikosi cha Simba kwenda Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wa marudiano wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RSB Berkane ya Morocco Jumapili.


Katika mchezo huo utakaoanza Saa 10:00 jioni Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Simba inatakiwa kushinda 3-0 ili kutwaa taji hilo au ishinde 2-0 na bingwa apatikane kwa mikwaju ya penalti.


Aishi hakusafiri na timu katika mchezo wa kwanza Simba ikifungwa 2-0 Jumamosi iliyopita (Mei 17, 2025) Uwanja wa Manispaa ya Berkane mjini Berkane nchini Morocco.


Mabao ya RSB Berkane yalifungwa na kiungo Msenegal, Mamadou Lamine Camara dakika ya nane na mshambuliaji Oussama Lamlaoui la pili dakika ya 14.


Tayari CAF imesema bingwa wa Kombe la Shirikisho atapewa Kombe jipya kama ilivyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo yatazinduliwa kesho katika ofisi za wadhamini wakuu, TotalEnergies Jijini Johannesburg, Afrika Kusini – Hafla itakayoanza Saa 12:00 jioni na kuhudhuriwa na magwiji wa soka barani Afrika.

WANANCHI KITONGOJI CHA KWAKIBOSHA KATA YA MAPINGA BAGAMOYO WAIOMBA SERIKALI KUINGILIA KATI SAKATA LA KUBOMOLEWA NYUMA ZAO.

 HABARI NA VICTOR MASANGU, BAGAMOYO, PWANI

SAUTI NA ALBERT G.SENGO Wananchi zaidi ya 120 wa kitongoji cha Kwakibosha Kata ya Mapinga Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani wameiomba Serikali kuingilia kati sakata la kukithiri kwa wimbi la matapeli wa ardhi ambao wamekuwa wakiwanyanyasa na kuwaonea kwa kipindi cha muda mrefu ikiwemo kuwavunjia nyumba zao za makazi na kupelekea kukosa maeneo ya kuishi. Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mkutano maalmu wa hadhara wamesema kwamba kwa sasa wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kutokana na nyumba zao 12 kubomelewa na mmoja wa wanannchi anayejulikana kwa jina la Peter Junior na kuomba mamlaka zinazohusika achukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine. Kwa upande wake Mwenyekiti wa kitongoji cha Kibosha Shaban Rashid akizungumzia kuhusiana na hatma ya wananchi juu ya mtu huyo anayedaiwa kuwasumbua kwa muda mrefu amebainisha kusikitishwa kwake na vitendo vinavyofanywa na mtuhumiwa huyo ambaye amekuwa akiwanyanysa wananchi kwa kuwavunjia nyumba zao.

KUPITIA MRADI WA FEMA AILEADERS WABUNGE WABUNIFU NA MAKUNDI MENGINE WAPIGWA MSASA AKILI MNEMBA

 

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam


Kupitia Mradi wa FemAILeaders, Shirika la Women Political Leaders (WPL), GIZ Makao Makuu, GIZ Tanzania na Omuka imeandaa Mafunzo ya Akili Mnemba “Artificial Intelligence - AI” yaliyoanza Mei  19 hadi 20 mwaka 2025, Dar es Salaam yaliyolenga mambo mbalimbali ikiwemo ulinzi wa mtandao,ubunifu na matumizi ya AI.


Mafunzo haya yaliwaleta pamoja Wabunge, Wabunifu na Makundi mengine kwa lengo la kuangazia ubunifu na matumizi ya AI, ulinzi wa kimtandao, utatuzi wa changamoto za AI na uhitaji wa kisera.

Delegation ya Bunge iliongozwa na Mhe Salome Makamba na kujumisha Mhe Prof Joyce Ndalichako, Mhe Esther Matiko, Mhe Ng’wasi Kamani na Makatibu wa Kamati za Bunge, Adv Ganjatuni Kilemile na Pius Katabazi.

 

Tanzania imeendelea kuongoza barani Afrika kwa Kuimarisha Uelewa na Ushawishi wa Wabunge Wanawake ili wawe Vinara wa AI hivyo kuchangia kwa Tanzania kunufaika na fursa zinazotokana na Akili Mnemba - AI. Tanzania imechaguliwa kuwa Mfano wa Kuigwa barani Afrika katika eneo hili. 

 

Aidha, Mradi wa FemAILeaders umeweza kufanyika Tanzania kufuatia jitihada za Mhe Neema Lugangira (Mb) ambae pja ni Mwakilishi wa Afrika/Mjumbe Maalum wa Afrika wa Shirika la Women Political Leaders (WPL) hivyo ametumia nafasi hiyo kuileta fursa hii Tanzania.
 

BENKI YA CRDB KUIWEZESHA ZANZIBAR KUJENGA SHULE 23 ZA GHOROFA

 

Zanzibar. Tarehe 21 Mei 2025: Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zake za kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo baada ya kusaini mkataba wa mkopo nafuu wa takriban Euro milioni 80 (shilingi bilioni 240).

Akizungumza kwenye hafla ya kutiliana saini mkopo huo kati ya Benki ya CRDB na Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi amesema maendeleo ya taifa yanahitaji ushirikiano wa serikali na sekta binafsi na Benki ya CRDB imekuwa ikionyesha hilo kwa vitendo kwa kujitoa kwake kila inapohitajika kufanya hivyo.
“Mkopo wa Euro milioni 79.962 utatusaidia kujenga shule 23 za ghorofa mbili. Shule hizi zitajengwa Pemba na Unguja hivyo kusaidia kutatua uhaba wa vyumba vya madarasa kwa kiasi kikubwa. Lengo letu ni kuwaona vijana wetu wanasoma katika mazingira rafiki ya kukua kiumri na kielimu,” amesema Rais Dkt. Mwinyi.


Uboreshaji huu wa mazingira ya shule, Rais amesema ni muhimu ili kuwapata viongozi bora, madaktari, wahandisi, wahasibu, wanasheria na wasomi wengine mahiri hivyo ni lazima kuwekeza kwenye elimu.
“Kila mtu mwenye maono mazuri anatambua umuhimu wa elimu hivyo mkopo huu utakaoboresha miundombinu, umekuja kwa wakati sahihi sasa hivi. Nawapongeza Wizara ya Elimu kwa kulifanikisha hili kwani ilikuwa nikipita wananchi wanaomba shule ya ghorofa kila mahali mpaka kule Tumbatu. Sasa suala hilo limekamilika na fedha za ujenzi wake ndio hizi hapa,” amesema Rais Mwinyi.

Benki ya CRDB imetoa mkopo huo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikishirikiana na Benki ya Deutsche ya nchini Hispania kwa malengo ya kufanikisha ujenzi wa shule hizo zitakazokuwa na madarasa ya kisasa, vyoo bora, bustani za kuvutia, ofisi nadhifu za utawala, maabara na maktaba za kisasa pamoja na viwanja safi vya michezo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Adulmajid Nsekela amesema kwa muda mrefu wamekuwa wadau muhimu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Serikali zote yaani ile la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi mjini au vijijini.


“Kwa hatua tuliyofikia, kwa sasa pande zote yaani Benki ya CRDB, Benki ya Deutsche na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunakamilisha masharti ya awali ya mkopo kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi kusudiwa. Ni matumaini yetu kuwa masharti haya ya awali yatakamilishwa kabla ya mwishoni mwa mwezi ujao hivyo kuwezesha kuanza haraka iwezekanavyo utekelezaji wa mradi huu,” amesema Nsekela.
Nsekela ameongeza kuwa mkopo huo unajumuisha Euro milioni 69.312 sawa na asilimia 85 utakaotolewa kwa ushirikiano wao na Benki ya Deutsche huku kiasi kilichobaki cha Euro milioni 10.65 sawa na asilimia 15 kitatolewa na Benki ya CRDB peke yake suala lililopata baraka zote za SMZ kupitia Wizara ya Fedha na Mipango.

Nsekela pia amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa juhudi zake za kuimarisha uchumi wa Zanzibar ikiwamo uuzaji na uorodheshaji wa Hatifungani ya Sukuk iliyotolewa na SMZ mapema mwaka huu na kukusanya shilini bilioni 381 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa kufuata misingi ya dini ya Kiislamu.
Benki ya CRDB imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo visiwani Zanzibar ikishiriki kufanikisha miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 130. Kwa mkopo uliosainiwa, unaifanya Benki ya CRDB kufikisha jumla ya shilingi billion 375 ya uwezeshaji wa miradi inayosimamiwa na SMZ.





Monday, May 19, 2025

MADAKTARI BINGWA 47 WATIA NANGA MKOANI LINDI KUTOA HUDUMA ZA KIBINGWA

 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary akizunguza wakati  kuwapokea rasmi madaktari bingwa 47 chini ya mpango wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, awamu ya tatu, kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa katika hospitali zote za wilaya ndani ya mkoa huo.
Baadhi ya Madaktari bingwa ambao wamewasili mkoani Lindi kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi wote mkoani.

Na Fredy Mgunda, Lindi.

Serikali ya Mkoa wa Lindi imewapokea rasmi madaktari bingwa 47 chini ya mpango wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, awamu ya tatu, kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa katika hospitali zote za wilaya ndani ya mkoa huo.


Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary, alisema kuwa ujio wa madaktari hao ni sehemu ya jitihada za serikali kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, hasa wale walioko maeneo ya vijijini ambako awali walilazimika kusafiri mbali kupata huduma za kibingwa.


“Huduma hizi zitapatikana katika maeneo saba ndani ya mkoa kwa siku sita mfululizo kuanzia leo. Lengo ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora na kwa wakati,” alisema Bi. Omary.


Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kuboresha sekta ya afya kwa kujenga miundombinu ya kisasa, kununua vifaa tiba vya kisasa, pamoja na kuongeza wataalamu mbalimbali wa afya nchini.


Kwa upande wake, Mratibu wa timu hiyo ya madaktari, Michael Mbele, alieleza kuwa madaktari hao wamejipanga kikamilifu kutoa huduma zote muhimu za afya kwa wananchi wote, bila ubaguzi, katika hospitali za wilaya walizopangiwa.


“Tumewakilishwa na wataalamu wa kada zote za afya, kuanzia magonjwa ya ndani, watoto, wanawake, upasuaji na hata huduma za kisaikolojia. Huduma zote hizi sasa zitapatikana katika hospitali za wilaya,” alisema Mbele.


Wananchi wa Mkoa wa Lindi waliopata fursa ya kuhudumiwa walieleza furaha na shukrani kwa serikali, hususan kwa Mheshimiwa Rais, kwa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini, hatua ambayo wameitaja kama ya kipekee na ya kupongezwa.