ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, April 16, 2025

SERIKALI YAZINDUA MRADI WA MAJI KIJIJI CHA TUNGAMAA PANGANI, WANANCHI ZAIDI YA 2500 KUNUFAIKA

 

 


Na Oscar Assenga,Pangani

ZAIDI ya Wananchi 2500 wa Kijiji cha Tungamaa wilayani Pangani mkoani Tanga watanufaika na mradi wa Maji baada ya Serikali kutekeleza mradi katika eneo hilo uliogharimu kiasi cha Milioni 500 kupitia Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA)

Akizungumza wakati akizindua mradi huo ambao umetekelezwa kwa muda mfupi kwa kutumia Force Akaunti, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt,Balozi Batilda Burian,Mkuu wa wilaya ya Pangani Gift Msuya alisema utakuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi.

Alisema matarajio yao kutokana na utekelezaji wa mradi huo na mengine mikubwa ya maji katika kata za nne za wilaya hiyo na maeneo mengine wana uhakika ifikapo Desemba mwaka huu upatikanaji wa maji utafikia asilimia 90.2.

Alisema hilo linatokana na miradi mikubwa inayotekelezwa, Mkwaja, Sange, Madanga na Bushiri na maeneo maengine wana uhakika kufikia kiwango hicho cha upatikanaji wa maji na kwa upande wa mijini wana miradi miwili ya inayotekelezwa wa hati fungani.

Ambapo alisema mradi huo wa hatifungani ni kuboresha miundombinu ya usambazaji wa maji mjini kwa kuiondosha ya zamani chakavu na kuweka mipya na mradi wa mji 28 ambao uliwekwa jiwe la msingi na Rais Dkt Samia Suluhu alipofanya ziara Tanga.

Alisema kwamba na mradi huo utafanyika kwenye kata kata ya Madanga,Ubangaa na Pangani Mashariki na Magharibu ambapo mpaka sasa upatikanaji wa maji Mijini ni asilimia 76 na mradi utakapokamilika Desemba watakiwa wamefikia upatikanaji wa maji asilimia 100 na kuvuka lengo la utekelezaji wa ilani asilimia 95 kwa upatikani wa maji mijini kwa wilaya ya Pangani.

“Ndugu zangu niwaambie kwamba hakuna mbadala wa maji ndio sababu hakuna maendeleo yanaweza kuja bila kuwepo kwa maji kwa sababu wananchi wakikosa maji hakutakuwa na utulivu wa kiasiasa wala uchumi hivyo uchumi unaonekana kwa sababu huduma za maji zinapatikana na niwapongeze Ruwasa kwa kazi nzuri na juhudi mnazozionyesha kuwapatia wananchi huduma safi ya maji salama na kutosheleza “Alisema

Awali akizungumza kuhusu mradi huo ,Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Omari Lugongo alisema kwamba mradi huo ulizinduliwa mwaka jana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi,Dkt Batilda Burian na mwaka huu ameuzindua mradi huo wa maji ambao miuondombinu yake inaruhusu kuteka maji sio kwenye vilula tu na inaruhusu kuunganisha maji majumbani.

“Kwenye mji huu ambao mradi umezinduliwa kuna kaya zaidi ya 600 na mpaka sasa kaya 20 zimeunganishwa maji kwenye nyumba zao kwa hiyo tunaendelea kuwahamasisha wananchi kuunganisha nyumba kwenye nyumba zao”Alisema

Aidha alisema kwa Mkoa wa Tanga tayari wilaya ya Pangani wamekwisha kutekeleza ilani ya CCM kwa asilimia 100 ambapo hali ya upatikanaji wa maji mpaka sasa ni asilimia 86 lakini kimkoa ni asilimia 75 .

Hata hivyo alisema kwa hiyo wilaya hiyo ilani imetekeleza kwa asilimia 100 na wilaya nyengine wanaendelea na wanatategemea ifikapo Desemba 2025 zaidi ya asilimia 90 wananchi wa Pangani watapata maji safi na salama kwa eneo la Vijijini na Mijini.


Tuesday, April 15, 2025

HALMASHAURI YA WILAYA YA BAGAMOYO YATEKELEZA AGIZO LA RAIS YAPANDA MITI 500 ENEO LA ZINGA KUBORESHA MAZINGIRA

NA VICTOR MASANGU/PWANI. IMESOMWA NA ALBERT G.SENGO Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani katika kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hasana la kutunza na kuhifadhi mazingira ambapo imefanikiwa kupanda miti zaidi ya mia 500 katika eneo la mnada wa mbuzi na ng'ombe uliopo katika Kata ya Zinga kwa mtoro lengo ikiwa ni kuweza kurudisha uoto wa halisi uliopotea pamoja na kupambana na wimbi la na ukataji wa miti ovyo ambao unasabisha hali ya ukame.

AZIZ KI WA MOTO, CHAMA AMEWAKA YANGA YAITANDIKA STAND UNITED 8-1 MWENGE

MABINGWA watetezi, Yanga SC wamefanikiwa kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), michuano inayodhaminiwa na Benki ya CRDB baada ya ushindi wa mabao 8-1 dhidi ya Stand United jioni ya leo Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

Nyota wa mchezo wa leo ni kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Burkina Faso aliyehusika kwenye mabao saba kwa kusaidia upatikanaji mabao matatu na yeye mwenyewe kufunga manne.

Alifunga mabao yake dakika za 10,48, 58 na 61 huku pia akiwasetia beki Nickson Kibabage kufunga dakika ya 20 na kiungo Mzambia, Clatous Chama mawili, dakika ya 32 na 40.

Bao la nane la Yanga liliparikana kwa ushirika wa wachezaji waliotokea benchi, mshambuliaji Mzambia - Kennedy Musonda akifunga kwa kumalizia krosi ya kiungo Farid Mussa, huku bao pekee la Stand United likifungwa na Msenda Senda dakika ya 48.

Yanga sasa itakutana na JKT Tanzania ambayo jana iliitoa Pamba Jiji FC ya Mwanza kwa kuichapa mabao 3-1 Uwanja wa Meja Jenerali Charles Isamuhyo, Mbweni Jijini Dar es Salaam.

Nusu Fainali itazikutanisha Simba SC  iliyoitoa Mbeya City kwa kuichapa mabao 3-1  juzi hapo hapo Uwanja wa KMC na Singida Black Stars iliyoitoa Kagera Sugar kwa kuifunga mabao 2-0 Uwanja wa CCM LITI mjini Singida jana.

CCM TANGA WAMSHUKURU MBUNGE UMMY MWALIMU KWA KUWEKEZA KWA VIJANA KUPITIA MICHEZO

 

Na Oscar Assenga,Tanga. 

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tanga, Shabani Hamisi, amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu, kwa kuandaa mashindano ya Oddo Ummy Cup kwa kushirikiana na chama cha mpira mkoa wa Tanga (TRFA) akisema kuwa ni hatua muhimu katika kukuza vipaji vya vijana jijini humo.

Akizungumza kama mgeni rasmi kwenye fainali ya mashindano hayo, Hamisi alisema kuwa michezo ni ajira kwa vijana kama zilivyo ajira nyingine, na ni njia mojawapo ya kuimarisha mahusiano na kuwaepusha na vitendo viovu.
"Kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge, nipo hapa kama mgeni rasmi kuhakikisha kuwa mashindano haya yanakuwa chachu kwa vijana katika kujikwamua kiuchumi. Michezo ni ajira, na pia ni njia bora ya kujenga nidhamu na mahusiano bora katika jamii," alisema.
Aidha Alisema kuwa Ummy Mwalimu amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha vijana wa Tanga wanashiriki katika michezo mbalimbali na kutumia fursa zinazojitokeza. Alisisitiza kuwa mbunge huyo yuko tayari kushirikiana na vijana katika nyanja tofauti ili kuwawezesha kufikia ndoto zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tanga (TRFA), Martin Kibua, aliwataka wachezaji na makocha kuzingatia sheria za mchezo, huku akipiga marufuku wachezaji kuhama hama katika timu bila kufuata utaratibu rasmi.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Hassan Nyelo, alieleza kuwa ligi ya mwaka huu imekuwa ya kihistoria kutokana na udhamini mkubwa uliotolewa na Mbunge huyo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa ligi ya wilaya kupata udhamini wa asilimia 100, ikijumuisha michezo 98 na zawadi zote.
"Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa katika sekta ya michezo. Ameahidi kuendeleza juhudi hizi kwa michezo mingine zaidi baada ya mpira wa miguu," aliongeza.
Nyelo alihitimisha kwa kuwaomba vijana na wakazi wa Tanga kuendelea kumuunga mkono Mhe. Oddo Mwalimu kwa juhudi zake za kukuza maendeleo ya vijana kupitia michezo.




HALMASHAURI YA BAGAMOYO YAUNGA JUHUDI ZA RAIS SAMIA KATIKA KUBORESHA MAZINGIRA YAPANDA MITI 500 ZINGA

 


VICTOR MASANGU, BAGAMOYO

Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani  katika kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hasana  la  kutunza na kuhifadhi  mazingira ambapo imefanikiwa kupanda miti   zaidi ya mia 500  katika eneo la mnada wa mbuzi na ng'ombe uliopo katika Kata ya Zinga kwa mtoro lengo ikiwa ni kuweza kurudisha uoto wa halisi uliopotea  pamoja na  kupambana na wimbi la  na ukataji wa miti ovyo ambao unasabisha hali ya ukame.

Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo Stellah Msofe wakati wa maadhimisho ya siku ya upandaji wa miti ngazi ya Wilaya ambayo yamefanyika katika eneo la Zinga kwa mtoro ambapo amewataka wakuu wa idara, watendaji,zikiwemo taasisi binafsi kuweka mikakati ya kuhimiza suala la upandaji wa miti ili kutimiza agizo la serikali la kupanda miti milioni 1.5 kwa kila mwaka.

Alisema kwamba serikali imeamua kwenda kupanda miti katika eneo hilo la mnada wa Zinga kutokana na kubaini kwamba mazingira yake yameathirika kwa kiasi  kutokana na kuwepo kwa shughuli mbali mbali za kibinadamu ikiwemo suala la uchimbaji wa mchanga hivyo wakaona kun aumuhimu mkubwa sana katika kuhakikisha anapanda miti mingi ambayo itasaidia kurejesha hali yake ya kawaida.


Naye Mkuu wa kitengo cha maliasili na mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoto Dkt. Obed Mwinuka amebainisha kwamba lengo lao  kubwa ni kutekeleza kampeni ya  kitaifa katika kuboresha mazingira ambapo wamefanikiwa kupanda miti ipatayo 500 katika eneo hilo la mnada wa mbuzi na ng'ombe lililopo kata ya Zinga.
 
Pia alisema kwamba lengo kubwa la Halmashauri ni kuhakikisha kwamba wanapanda miti mingi ambayo itaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na changamoto ya ukame ambao umekuwepo katika baadhi ya maeneo na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha utunzaji wa mazingira .

Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo amebainisha kwamba hadi sasa wameshafanikiwa kupanda miti zaidi ya laki saba na kwamba lengo na mikakati waliyojiwekea ni kufikia lengo la  serikali la kupanda miti  milioni 1.5 ambayo itakuwa ni mkombozi mkubwa katika kurudisha hali nzuri ya uoto wa hasiri.

Mmoja wa wawekezaji katika mnada huo wa Zinga kwa mtoro  Hassan  Kashingo  akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake ameahidi kushirikiana bega kw abegaa naa serikali ikiwa pamoja na kuitunza miti hiyo 500 ambayo imepandwa katika eneo hilo la mnada.


Monday, April 14, 2025

KIJANA ALIYEANGUKIWA NA KIFUSI NA KUHARIBIKA MFUMO WA MKOJO ANAOMBA MSAADA WA MATIBABU

 NA ALBERT GSENGO/MWANZA

"Ndugu zangu naomba msaada wa fedha za matibabu au kupata bima ya matibabu ili nipate kuondokana na maumivu haya ninayoyapata sasa, natanani siku moja niishi na familia kama wanaume wengine, kwani sijawahi kuonja raha ya kuwa mwanaume yaani baba" "Niko tayari hata kutibiwa kwa bondi (mkopo) ili nikishapatiwa matibabu na kupona nipatiwe kazi au kibarua ambacho kitafidia fedha za matibabu yangu" Hizi ni baadhi tu ya kauli zilizojaa simanzi za kijana asiyejuwa kesho yake itakuwa vipi, Daudi Jegi Lusanja mwenye umri wa miaka 21 mwenye tatizo la njia ya haja ndogo akikojoa kwa msaada wa mpira uliounganishwa moja kwa moja kutoka kwenye kibofu chake cha mkojo mara baada ya kupata ajali ya kuangukiwa na kifusi cha mawe kwenye mgodi wa wachimbaji wadogo (kabla ya mwekezaji) uliopo kijiji cha Dutwa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu nchini Tanzania. Akitembea taratibu kwa kujikongoja na kuzungumza kwa shida bila uchangamfu Daudi Lusanya anasema ajali hiyo ilimpata mwaka 2021 na sasa yapata miaka mitatu akiwa anakojoa kwa shida. Ameomba wasamaria wema, makampuni, vikundi na watu wa kada zozote kumsaidia kuondokana na changamoto kubwa aliyonayo inayomsababisha kushindwa kufanya kazi zoyote kumwezesha kupata kipato na kuendesha maisha. Kwa msaada na kumtumia fedha za matibabu wasiliana naye kupitia simu namba +255 680 408 335 Jina litakalojitokeza ni Willy Mwapili.

AWAMU YA PILI UBORESHAJI, UWEKAJI WAZI WA DAFTARI LA WAPIGA KURA KUANZA MEI.

 Na. Mwandishi Wetu 

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili utafanyika sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura kuanzia tarehe 01 Mei, 2025 na kukamilika tarehe 04 Julai, 2025.

Akizungumza jijini Dodoma leo tarehe 14 Aprili, 2025 Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani, Mhe. Jacobs Mwambegele amesema zoezi la uboreshaji wa Daftari litafanyika kwa mizunguko mitatu ambapo mzunguko wa kwanza utajumuisha mikoa 15, mzunguko wa pili mikao 16 na mzunguko wa tatu utajumuisha vituo vya magereza na vyuo vya mafunzo. 

Ameitaja mikoa itakayohusika kwenye mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kuwa ni pamoja na Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe ambapo zoezi hilo litafanyika tarehe 01 hadi 07 Mei, 2025.

Mikoa ya mzunguko wa pili ni pamoja na Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba ambapo zoezi hilo litafanyika tarehe 16 hadi 22 Mei, 2025.

“Mzunguko wa tatu wa zoezi la uboreshaji wa Daftari utahusisha vituo 130 vilivyopo kwenye magereza ya Tanzania Bara na vituo 10 vilivyopo katika Vyuo vya Mafunzo Tanzania Zanzibar kwa wakati mmoja na utafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 28 Juni, 2025 hadi tarehe 04 Julai, 2025,” amesema Jaji Mwambegele.

Ameongeza kuwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa awamu ya pili, utafanyika ngazi ya kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya jimbo kwa Tanzania Zanzibar, ambapo jumla ya vituo 7,869 vitahusika, vituo 7,659 vipo Tanzania Bara na vituo 210 vipo Tanzania Zanzibar.

“Tunatarajia kuwa katika awamu ya pili ya uboreshaji, wapiga kura wapya 1,396,609 wataandikishwa, wapiga kura 1,092,383 wataboresha taarifa zao na wapiga kura 148,624 watafutwa kwenye Daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye Daftari,” amesema Jaji Mwambegele. 

Amesema zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 16(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 kinachoipa Tume jukumu la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili mara baada ya uchaguzi mkuu na kabla ya uteuzi wa wagombea kwa uchaguzi mkuu unaofuata.

Amesema zoezi hilo litahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika na kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na taarifa nyingine; 

Mambo mengine ni kuhamisha taarifa za wapiga kura waliohama kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa  taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo.

Wakati huohuo, Jaji Mwambegele amesema kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 11(1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume pia ina jukumu la kuandaa Daftari la Awali la Wapiga Kura na kuliweka wazi kwa umma. 

Amesema lengo la uwekaji wazi wa Daftari hilo ni kutoa fursa kwa wananchi kukagua, kufanya marekebisho ya taarifa za wapiga kura na uwekaji wa pingamizi dhidi ya wapiga kura waliomo kwenye daftari ambao hawana sifa.

“Daftari la Awali la Wapiga Kura litabandikwa katika vituo vyote vilivyotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza. Zoezi hili la uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura litafanyika pamoja na uboreshaji wa Daftari wa awamu ya pili,” amesema. 

Tume iliboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza kuanzia tarehe 20 Julai, 2024 na kukamilisha tarehe 25 Machi, 2025.



MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA MAWAKILI KUJADILI CHANGAMOTO ZA KISHERIA

 Na Janeth Raphael MichuziTv - Dodoma 

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali,Hamza Johari,amewataka wanachama wa chama cha Mawakili,kutumia fursa ya mkutano Mkuu kujadili changamoto mbalimbali za kisheria ikiwemo kuzifanyia kazi.

Johari amesema hayo leo jijini Dodoma,wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa chama cha mawakili wa serikali,wenye lengo wa kujadili mustakabali wa chama hiko lakini pia kujitathmini utendaji kazi wao.

"Nawapongeza kwa kuandaa Mkutano huu naomba tumieni nafasi hii kujadili changamoto zilizopo ili kuzifanyia KAZI,"amesema Johari.

Mbali na hayo amemshkuru Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Samwe Maneno pamoja na menejimenti nzima ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,ikiwemo chama cha mawakili wa serikali,kutokana na kazi nzuri ya maandalizi ya Mkutano mkuu wa mwaka waliyofanya.

"Naupongeza uongozi wa wa chama cha Mawakili,mmeandaa vizuri mkutano huu,nimefarijika kwa sababu toka nichaguliwe ni mara yangu ya kwanza nakutana na mawakili wote nchini,"amesema Johari.

Kutokana na pongezi hizo,anasema anaamini mkutano wa 2026 utakuwa zaidi ya huu wa 2025,naimani utakuwa na sura tofauti,huku akisisitiza chama hiko kijikite kujadili mambo mbalimbali yanayohusu Chama chao na Maendelea ya sekta ya Sheria kwa ujumla.

Naye Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amwel Maneno  amesema kuna kila sababu ya kuimarisha Chama hicho cha Mawakili wa Serikali Ili kiweze kutimiza kusudi la kuanzishwa kwake na kwa kuzingatia kwamba kilianzishwa Ili kuwaleta pamoja Mawakili wa Serikali.

Amesema kada hiyo inapokuwa pamoja  wanafanya majukumu yao wakiwa na imani kubwa na  umoja  Ili kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria 

Hata hivyo Naibu Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali amesema wao kama mawakili watahakikisha wanatekekeza majukumu yao na kuimarisha Chama hicho Ili  kiwe Chama imara kuliko Chama chochote cha kitaaluma hapa Nchini.