Kocha wa timu ya Strasbourg, Liam Rosenior ndiye kocha mpya wa klabu ya Ligi Kuu Uningereza, Chelsea.
Mwingereza huyo mwenye umri wa miaka 41 anatarajiwa kuchukua nafasi ya Enzo Maresca, ambaye aliondoka siku ya Mwaka Mpya.
Mapema Jumanne, katika mkutano wake wa mwisho na waandishi wa habari kama meneja wa Strasbourg, Rosenior alithibitisha kwamba "amekubali kwa maneno" kuwa kocha wa Chelsea.
"Siwezi kukataa fursa hii ya kujiunga na klabu kubwa, kikosi kikubwa ambacho ni mabingwa wa Kombe la Dunia la Klabu," Rosenior alisema.
"Sijasaini bado. Lakini tumeshakubaliana kwa kila kitu na huenda nikasaini saa chache zijazo," Rosenior alisema.
"Kukabidhiwa jukumu hili kunamaanisha jambo kubwa kwangu na nataka kuwashukuru wote waliohusika kwa fursa hii. Nitafanya kila kitu ili kuleta mafanikio ambayo klabu hii inastahili."
Rosenior amesema kocha msaidizi wa kikosi cha kwanza cha Strasbourg Kalifa Cisse, kocha mwingine msaidizi Justin Walker na mkuu wa uchambuzi Ben Warner watajiunga naye Chelsea.
Ronseior aliteuliwa na Strasbourg Julai 2024 na kuiongoza klabu hiyo ya Ufaransa hadi nafasi ya saba katika Ligue 1 msimu uliopita.




