HOTUBA YA MHESHIMIWA WAZIRI DR. DOROTHY GWAJIMA (MB),
KATIKA KONGAMANO LA WATAALAMU NA WATOA HUDUMA ZA USTAWI WA JAMII KATIKA UKUMBI
WA BENKI YA TANZANIA (BOT) TAREHE 24-27,
NOV 2021
·
Mhandisi Robert Gabriel: Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza,
·
Dkt Nandera E. Mhando, Kamishna
wa Idara ya Ustawi wa Jamii,
·
Dkt. Mariana Makuu, Mwenyekiti wa TASWO:
·
Wawakilishi wa Mashirika na Wadau
wa huduma za ustawi wa jamii: UNICEF, ABBOT
FUND, PACT, SOS VILLAGES
·
Viongozi wa TASWO,
·
Waadhiri wa vyuo vikuu vinavyozalisha
Wataalamu wa Ustawi wa Jamii,
·
Maafisa Ustawi wa Jamii
kutoka Mikoa ya Tanzania Bara,
·
Wadau na Watoa huduma za Ustawi
wa Jamii,
·
Ndugu Wanahabari,
·
Wageni waalikwa,
·
Mabibi na Mabwana,
Nawasalimu kwa jina la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania...
Awali ya yote napenda
kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyenzi Mungu mwingi wa rehema kwa
kutujalia uhai, uzima na nafasi ya kujumuika pamoja katika kongamano la mwaka la
Chama cha Wataalamu wa huduma za ustawi wa Jamii nchini. Pia, napenda kuwashukuru kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika
kongamano hili. Aidha, nawapongeza kwa maandalizi mazuri mliyoyafanya kwa lengo
la kufanikisha kongamano hili. Kipekee
niushukuru uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa kutoa ushirikiano na kuturuhusu
kufanya shughuli hii katika Mkoa huu.
Naomba
mtambue ya kwamba serikali kupitia Wizara yangu itaendelea kuimarisha mfumo wa utoaji
huduma za ustawi wa jamii na kuhakikisha kwamba haki za watu wenye mahitaji maalumu
walio pembezoni wanapata huduma zote za msingi kwa wakati.
Ndugu
Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,
Natambua kwamba Chama cha Wataalamu wa Ustawi
wa Jamii kimekuwa kikifanya kazi kwa karibu na serikali kwa kupitia Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) pamoja na wadau wengine wa maendeleo katika
kutatua changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma bora za ustawi
wajamii. Wizara yangu inatambua mchango mkubwa wa TASWO katika kusimamia na kutetea
haki za wanataaluma, watoa huduma pamoja na makundi nufaika ya huduma za ustawi
wa jamii hapa nchini.
Ndugu
Wanataaaluma ya Ustawi wa Jamii,
Kauli Mbiu ya mwaka huu 2021 ni “UBUNTU”. Hili ni neno la Kizullu lenye maana ya
“I AM because WE ARE”. Kauli mbiu hii ni nzuri kwani inasisitiza umuhimu wa
umoja, ushirikiano na kusaidiana kwa lengo la kumuimarisha kila mtu na hivyo kuongeza
ufanisi wa utoaji wa huduma za ustawi wa jamii. Zaidi, kauli mbiu hii inasaidia kukuza mahusiano baina yetu na kusaidia
kuwaweka watoa huduma na wanufaika na huduma karibu hivyo kutoa fursa ya kujenga
mshikamano kwa ajili ya kupanga namna ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoikabilI
jamii.
Kwa
kusema haya nipende kusisitiza umuhimu wa kukuza na kusimamia mahusiano kati yetu
kama watoa huduma na wanufaikaji wa huduma zinazotolewa.
Ndugu
Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,
Nipende kuwapongeza Maafisa Ustawi wa Jamii
katika ngazi zote za utoaji wa huduma kwa umahiri mkubwa wanaounyesha na kwa jitihada
mnazochukua kushughulikia changamoto na matatizo mbalimbali ya masuala ya: migogoro
ya ndoa na familia, huduma kwa wazee na watu wenye ulemavu, ukiukwaji wa haki
za watoto pamoja na ukatili wa kijinsia.
Ndugu
Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,
Ninatambua kuwa, Wataalamu wa Ustawi wa
Jamii wanafanya kazi kubwa sana katika Idara ya Afya kupitia vituo vya afya, hospitali
za wilaya , hospitali za mikoa pamoja na hospitali za rufaa. Maafisa hawa
hutumika kutoa huduma za msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha kabla na
baada ya matibabu, maelekezo ya namna ya kujikinga na maambukizi zaidi ya
magonjwa, kushiriki kampeni za elimu kwa umma, ufuatiliaji na tafiti za kijamii
kwa lengo la kutoa huduma bora za afya kwa wahitaji, utambuzi na usimamizi wa
huduma za msamaha kwa wagonjwa na wazee. Pamoja na hayo, maafisa hawa wanahamasisha
jamii, kufanya utambuzi na kuwaunganisha wanajamii na Wazee katika Bima ya
Mfuko wa Afya Jamii (CHF).
Ndugu
Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,
Pamoja na kazi nzuri mnazozifanya kwa
makundi yote maalumu hapa nchini, ninatambua kuwa, bado kuna changamoto mbalimbali
ndani ya jamii zetu ikiwemo ongezeko la watoto wa mitaani ambalo limekuwa likiongezeka
siku hadi siku. Hadi sasa kuna jumla ya watoto wanaoishi na kufanyakazi mitaani ni 5,390 (1,538 wasichana na 3,852 wavulana)
walitambuliwa katika Mikoa ya Mwanza, Arusha, Iringa, Mbeya and Dodoma. Kati ya
watoto hao, jumla ya Watoto 135 (43 Ke and 92 Me) waliweza kuunganishwa
na familia zao, watoto 821 (302 Ke and 519 Me) waliweza kupewa vifaa
saidizi na kupelekwa shuleni, na watoto 75 (17 Ke and 58 Me) walipewa
mafunzo ya uanagenzi.
Ndugu
Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,
Ongezeko la watoto wa mitaani
limechangiwa na mambo mbalimbali yanayojitokeza katika jamii kama vile:
kutengana kwa wazazi, wazazi kujikita zaidi katika utafutaji maisha na
uzalishaji mali, umasikini wa kaya, vifo vya wazazi na walezi, msukumo wa
makundi rika kutokana na mmomonyoko wa maadili katika jamii na wakati mwingine
hulka ya mtoto mwenyewe.
Ndugu
Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,
Wizara yangu inaendelea kutekeleza
jukumu la ulinzi na usalama wa Watoto walio katika mazingira hatarishi kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali. Kipekee nipende kuushukuru Mfuko wa ABBOT kwa
kuweza kuunga mkono jitihada za serikali, ambapo kwa pamoja tumeweza
kufanikisha ujenzi wa Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo yaliyoko katika jiji la Dodoma.
Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo, yalizinduliwa rasmi tarehe 16 Juni, 2021 na
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dr. Philip Isdory
Mapango.
Ndugu
Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,
Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo, yana
uwezo wa kuhudumia watoto 250, hivi
sasa kuna jumla ya Watoto 55, kati
yao wakiume ni 34 na wakike ni 21.
Makao hayo yana nyumba za kuishi watumishi, kituo cha huduma za ufundi na
uanagenzi pamoja na kituo cha kulelea watoto wadogo mchana.
Huduma za
msingi zinazotolewa katika makao hayo kwa ajili ya Watoto ni pamoja na huduma
za afya, elimu, chakula, malazi na mavazi. Pamoja na hayo watoto hao hupatiwa
huduma ya mafunzo ya uanagenzi, ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia ikiwa
ni pamoja na kuwaandaa kuwaunganisha na jamii na familia zao.
Ndugu Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,
Wizara
yangu inaendelea kutoa huduma kwa watoto walio katika mkinzano na sheria katika
shule ya Maadilisho Irambo. Kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia 2017-2021,
shule hiyo imeweza kuwahudumia watoto 154 (148 Me na 06 Ke). Katika mwaka huu
wa fedha 2020/2021 kuna jumla ya Watoto 36 (33 Me na 3 Ke) wanaoendelea
kupatiwa huduma ya marekebisho ya tabia, unasihi, uanagenzi na kuunganishwa na
jamii baada ya kumaliza kutumikia adhabu zao. Aidha, Serikali inaendelea kusimamia mahabusu
za Watoto tano (5) zinazotoa huduma ambazo ziko katika Mkoa wa Arusha,
Kilimanjaro, Tanga, Mbeya na Dar es Salaam na tupo katika hatua za mwisho za
marekebisho ya Mahabusu ya Watoto Mtwara. Kwa muda wa miaka mitano iliyopita
kuanzia 2017-2021 kuna jumla ya Watoto 315 (277 Me na 38 Ke) wameweza kupatiwa
huduma katika Mahabusu hizo za Watoto nchini.
Ndugu
Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,
Kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Wizara
iliweza kupokea jumla ya maombi 149 ya
malezi ya kambo na kuasili. Miongoni mwa maombi hayo, maombi 50 yalipatiwa vibali vya kuendelea na
mchakato wa malezi ya kambo, ambapo watoto 38
(20 Ke na 18 Me) walipatiwa ya malezi ridhaa ya malezi ya kambo na Watoto 17 (12 Ke na 5 Me) waliasiliwa.
Aidha,
Wizara imeweza kusajili jumla ya vituo
301 vya kulelea Watoto Wadodo mchana vilivyosajiliwa na Vituo 33 vya kulelea Watoto Wachanga
viliweza kupata usajili.
Idadi hiyo inapelekea kuwa na jumla ya Vituo vya kulelea watoto wadogo mchana 1,844 kwa nchi nzima. Katika vituo
vya kulelea Watoto Wadodo mchana vilivyosajiliwa kuna jumla ya Watoto 163,394 (85,175 Me na 78,219 Ke).
Vilevile, tunaendelea na usajili wa
Makao ya Watoto yanayotoa huduma kwa Watoto walio katika mazingira hatarishi, hadi
sasa kuna jumla ya Makao 239 nchi nzima.
Ndugu Wanataaaluma ya Ustawi
wa Jamii,
Wizara imekamilisha kufanya mapitio
ya Sera ya Wazee ya mwaka 2003 na kuandaa andiko la Sera hiyo, Mpango wa
Utekelezaji wake na Waraka wa wasilisho la Sera katika Baraza la Mawaziri
ambalo tayari limeshawasilishwa. Serikali imeendelea kufanya utambuzi wa kaya
masikini na kutoa bima za afya na matibabu bila malipo kwa wazee na jamii kwa
ujumla. Jitihada hizo zimefanyika tangu mwaka 2015 ambapo hadi kufikia Juni,
2021 jumla Wazee wasiojiweza 2,203,414 (1,198,338 Ke na 1,005,076 Me) walitambuliwa. Jumla ya Wazee 1,256,544 wameweza kupatiwa kadi za bima ya Afya na
matibabu bila malipo.
Hadi
kufikia sasa kuna jumla ya madirisha ya huduma kwa Wazee 2,335 katika
hospitali na vituo vya afya kwa ajili ya kuharakisha na kutoa huduma za afya
stahiki kwa Wazee nchi nzima.
Ndugu Wanataaaluma ya
Ustawi wa Jamii,
Tumeendelea na utoaji huduma ya makazi kwa wazee
wasiojiweza hapa nchini kwa kushirikiana na wadau. Hivi sasa tuna jumla ya
makazi ya Wazee 15, ambayo yana
jumla ya Wazee 291, kati yao Wanaume ni 180 na Wanawake ni 111.
Huduma katika makazi hayo hutolewa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa
huduma kwa wazee.
Aidha, wizara imeendelea kuratibu na kusimamia huduma
katika makazi binafsi ya Wazee hapa nchini, ambapo hivi sasa kuna jumla ya
makazi binafsi ya Wazee 14 yanayotoa
huduma kwa Wazee 451, kati yao Wazee 216 ni wanaume na 235 ni wanawake.
Ndugu
Wanataaaluma ya Ustawi wa Jamii,
Hata hivyo, tunaendelea kuenzi
makubaliano mbalimbali ya kitaifa ikiwa ni pamoja na siku ya Wazee dunia ambayo
huadhimishwa kila ifikapo tarehe 01 Oktoba ya kila mwaka. Kwa mwaka 2020/2021
kwa kushirikiana na Mkoa wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Wizara iliweza kushiriki
katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Wilaya ya Kondoa, ambapo jumla ya Wazee
226 kutoka katika Halmashauri 8 za Mkoa wa Dodoma na wengine kutoka
Dar es Salaam waliweza kushiriki kilele cha siku hiyo. Katika siku hiyo, jumla
ya Wazee 111 walipatiwa huduma bila malipo ya uchunguzi wa Afya na tiba.
Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi
ya Rais TAMISEMI, imeweza kushiriki katika utatuzi wa migogoro ya ndoa na
familia. Jumla ya migogoro 4,932 iliweza
kushigulikiwa. Nitumie fursa hii kuahidi kuendeleza ushirikiano
na wataalamu wa ustawi wa jamii kwa ujumla wao katika kuhakikisha huduma za
ustawi wa jamii zinaboreshwa na zinawafikia walengwa kwa wakati. Niwapongeze wadau
wote ambao wameendelea kushirikiana na serikali za kijamii nyakati zote. Mnekuwa
bega kwa benga na serikali katika kutoa misaada ya kibinadamu na huduma ya kisaikolojia
kwa wananchi hasa kipindi hiki ambacho nchi inapitia janga la UVIKO-19.
Ndugu
Wanataaaluma na watoa huduma za ustawi wa Jamii,
Wizara inatumbua
kuwa, sekta ya ustawi wa jamii ni mtambuka kwa maana ya huduma zake zinatakiwa kila
sehemu kama vile idara ya afya kwa kiwango kikubwa sana, mashuleni, wizara mbalimbali,
halmashauri zote kwa kiwango kikubwa kuanzia Mkoa, Wilaya, Kata na Vijiji, Idara
na Taasisi mbalimbali, nk. Hii imepelekea kuwe na uhitaji mkubwa sana wa wataalam
kwa kiwango ambacho serikali haiwezi kumudu kuajili mara moja. Hivyo, naagiza,
wakati Serikali inaendelea kujipanga kuona namna ambayo itaongeza kuwaajiri wataalamu
hawa, basi idara mbalimbali zitumie mwongozo wa Wizara wa kuajiri wataalamu wakujitolea
ili kupunguza uhaba huo. Nitoe wito kwa wadau wote kutumia mwongozo wa kitaifa wa
watu wanaojitolea kusaidia kuajiri wataalam wa ustawi wa jamii katika ngazi mbalimbali
ili kukidhi utoaji wa huduma.
Ndugu
Wanataaaluma ya Ustawi wa Jamii,
Ninatambua uwepo wa changamoto
mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma bora na zenye viwango kwa wanajamii
katika ngazi ya msingi, ambapo miongoni mwa changamoto hizo ni:
§ Ufinyu
wa bajeti katika Sehemu / Kitengo cha Ustawi wa Jamii chenye dhamana ya
kuzifikia jamii na utekelezaji wa afua mbalimbali zinazolenga kutoa suluhu ya
matatizo ndani ya jamii,
§ Muundo
wa Idara ya Ustawi wa Jamii na namna unavyochangia kukwamisha utoaji wa huduma
bora na taarifa za utendaji. Hivi sasa eneo la huduma kwa Watu wenye Ulemavu lipo
katika Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati Sehemu ya Huduma za Familia, Watoto, Watoto
walio katika Mkinzano na Sheria pamoja na Wazee wapo chini ya Wizara ya Afya,
maendeleo ya Jamii, Jinsia, na Wazee,
§ Muungano
dhaifu wa kimawasiliano na kitendaji kati ya Idara ya Ustawi wa Jamii na Sehemu
ya Ustawi wa Jamii katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI unasababisha kukwama kwa
uratibu madhubuti wa utoaji huduma na kupelekea ukosefu wa taarifa na takwimu
sahihi za kitendaji kutokana na utekelezaji wa afua za huduma za ustawi wa
jamii. Tatizo hili lilipata kuwepo upande wa Idara za Afya za pande zote mbili
ila kwa sasa limepungua sana,
§ Uhaba
wa Maafisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri za Wilaya.
Ndugu
Wanataaaluma ya Ustawi wa Jamii
Serikali imechukua hatua mbalimbali kwa
lengo la kuboresha utoaji huduma za ustawi wa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa
miongozo ya huduma na kuratibu mafunzo kwa maafisa Ustawi wa Jamii waliopo
katika Halmshauri mbalimbali hapa nchini. Zoezi hilo ni endelevu na
linatekelezwa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa huduma za Ustawi wa
Jamii hapa nchini.
Ndugu
Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,
Nimesikia risala iliyowasilishwa na Mwenyekiti
wa TASWO Taifa kuhusiana na changamoto mbalimbali zinazokwamisha huduma za
ustawi wa jamii kutolewa kwa ubora unaotakiwa. Serikali imeendelea kuzifanyia kazi
baadhi ya changamoto hizo.
Ndugu
Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,
Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi
ya Rais – TAMISEMI na ufadhili kutoka Shirika la PACT TANZANIA, UNICEF na JSI
tumefanikiwa kutoa Mwongozo wa Mipango na Bajeti ya Huduma za Ustawi wa Jamii
katika ngazi ya Halmashauri (Comprehensive
Council Social Welfare Operational Guideline - CCSWOPG) unaolenga,
§ kuweka
uwiano sawa maeneo ya vipaumbele vya huduma za ustawi wa jamii kwa nchi nzima,
§ kuweka
uwiano wa afua za utatuzi wa changamoto katika jamii,
§ kuwa
na uhakika wa huduma kwa wakati kwa makundi yote yaliyo katika mazingira
hatarishi,
§ kuweka
uwanda mpana wa wadau kuunda afua jumuishi za utatuzi wa changamoto katika
jamii,
§ kuboresha
na kuimarisha ushirikiano baina ya wadau na watoa huduma za ustawi wa jamii,
§ Kuweka
uchambuzi sanifu wa mahitaji ya huduma za kijamii, kubaini rasilimali zilizopo
na aina ya huduma inayopaswa kutolewa.
Ndugu
Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,
Ninajua mna kiu na hamu kubwa ya kuona
sheria ya Taaluma ya Ustawi wa Jamii inakamilika na kuanza kutumika ili iweze
kuweka udhibiti kwa wanataaluma na watoa huduma za ustawi wa jamii. Sheria hiyo
itaweka bayana viwango vya ubora wa huduma vinayotakiwa katika jamii. Aidha, itakuwa msingi mzuri wa uanzishaji wa
baraza la usimamizi na udhibiti wa wanataaluma na watoa huduma za ustawi wa
jamii nchini.
Wizara
yangu inatambua umuhimu sheria hiyo, hivyo napenda kuwahakikishia kuwa tupo
katika hatua za mwisho za ukamilishaji wake, na mara itakapokamilika
nitaiwasilisha katika mamlaka husika ili iweze kupata ridhaa ya kuanza kutumika
ndani ya nchi yetu.
Ndugu
Wanataaluma ya Ustawi wa Jamii,
Ni kweli kuna uhaba wa Maafisa Ustawi wa
Jamii, hata hivyo, Wizara imeendelea
kuomba vibali vya ajira kwa ajili ya kupunguza tatizo lililopo na kufika huduma
stahiki kwa wanajamii. Hivyo, kadiri tutakavyopatiwa watumishi wapya, wizara
yangu itawapangia kazi katika maeneo na vituo vyenye uhitaji zaidi kwa lengo la
kuboresha huduma.
Suala
la Muungano dhaifu wa kimawasiliano na kitendaji kati ya Idara ya Ustawi wa
Jamii na Sehemu ya Ustawi wa Jamii katika OR-TAMISEMI limeshatafutiwa ufumbuzi
ambapo kuanzia mwezi Septemba, 2021 kumekuwa na vikao vya kiutendaji baina ya
pande hizi mbili vinavyolenga kushirikishana mipango na mikakati madhubuti ya
utaoji huduma jumuishi katika jamii. Vikao hivi vitakuwa vinafanyika kwenye
kila robo ya mwaka wa fedha kuanzia mwaka huu wa fedha 2021/2022.
Changoto ya muundo wa Idara kati ya Wizara
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na Ofisi ya Waziri Mkuu nimelipokea
na niahidi kuliwasilisha katika mamlaka husika.
Ndugu Wanataaaluma ya
Ustawi wa Jamii,
Ninawasihi muendelee kuelimisha
jamii kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kuvaa barakoa,
kutumia vitakasa mikono, kunawa mikono kwa maji tiririka na kutokukusanyika sehemu
moja bila sababu ya msingi. Aidha, nitoe rai kwa jamii waendelee kupata chanjo
ya UVIKO-19 inayotolewa katika vituo vya Afya na hospitali maalumu nchi nzima. Aidha,
ninawaomba muanze kutoa elimu kwa umma ili wananchi waweze kujiandaa kushiriki
Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022 kwa nchi nzima.
Mwisho.
Ninawapongeza
sana Maafisa Ustawi wa nchi nzima kwa kutekeleza maazimio mbalimbali ya
Kimataifa, Kikanda pamoja na Miongozo, Sera na Sheria za nchi zinazotolenga
kutoa huduma bora na ulinzi kwa makundi yote maalumu mnayoyahudumia.
Baada
ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa, kongamano la Wataalamu na watoa huduma za ustawi wa jamii limefunguliwa
rasmi.
NAWASHUKURU KWA KUNISIKILIZA
NA NAWATAKIA KONGAMANO JEMA