ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, May 26, 2018

USIKU WA LEO NI LIVERPOOL AU REAL MADRID UEFA CHAMPIONS LEAGUE.

FAINALI ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2018 inafanyika leo Olimpiki NSK mjini Kiev, Ukraine ikizikutanisha Liverpool ya England na Real Madrid ya Hispania kuanzia Saa 21:45 usiku.

Hiyo itakuwa fainali ya 63 ya michuano hiyo inayoandaliwa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), na msimu wa 26 tangu ipewe jina jipya la Ligi ya Mabingwa Ulaya kutoka lile la zamani la Klabu Bingwa Ulaya.

Mshindi wa mchezo wa leo atakutana na mshindi wa fainali ya UEFA Europa 2018 katika Super Cup ya UEFA. Pia watafuzu kuanzia hatua ya Nusu Fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA mwaka 2018 FIFA kama wawakilishi wa UEFA Mabingwa watetezi, Real Madrid walitinga fainali ya 16 ya rekodi baada ya ushindi wa 4–3 jumla dhidi ya Bayern Munich ya Ujerumani wakiwatupa mashindanoni kwa mara ya pili mfululizo. 

Na hii ni fainali ya tatu mfululizo ya Real Madrid na fainali ya nne kwenye mashindano matano huku ikipewa nafasi ya kushinda taji la 13 la rekodi, baada ya awali kushinda katika miaka ya 1956, 1957, 1958, 1959, 1960, 1966, 1998, 2000, 2002, 2014, 2016 na 2017; na kufungwa katika fainali za 1962, 1964 na 1981. 

Liverpool wameingia fainali ya nane, na ya kwanza tangu mwaka 2007, ambayo walishinda kwa jumla ya mabao 7–6 dhidi ya Roma ya Italia. 

Wameshinda taji hilo mara tano katika miaka ya 1977, 1978, 1981, 1984 na 2005, na wamefungwa mara mbili kwenye fainali 1985 na 2007. 

Mwandishi mmoja aliyehudhuria mazoezi ya Real Madrid jana aligongwa usoni na mpira uliopigwa na Cristiano Ronaldo na kuchanika kidogo jirani ya jicho.

Real walikuwa wanafanya mazoezi Uwanja wa Olimpiki mjini Kiev kuelekea fainali leo na ndipo Ronaldo alipompiga na mpira mwandishi huyo. Lakini Ronaldo alimuomba msamaha kwa ishara ya mkono mwandisi huyo aliyepatiwa huduma ya kwanza uwanjani hapo.

Beki ghali aliyesajiliwa Liverpool kwa dau la Pauni Milioni 75 amesema kwamba Real Madrid hawajawahi kukutana na timu kama yao kabla.

Amesema; nani anajali? Alipoulizwa kama Wekundu hao walistahiloi kufika gainali ya Ligi ya Mabinghwa Ulaya.

Mashabiki wa Liverpool walishambuliwa na wababe mjini Kiev juzi, kabla ya Polisi kuthibitisha watu wawili walikamatwa.

Picha za kutisha zimeonyesha watu wakishambuliana kwa kwa magongo, meza na viti. Polisi wa Merseyside wamesema wana taarifa za tukio hilo na wana Maofisa wao mjini Kiev.

Gwiji wa England, David Beckham amemtaka mchezaji mwenzake wa zamani wa Real Madrid, Zinedine Zidane sasa kocha wa klanbu hiyo kushinda fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool: 'Tafadhali wafunge Liverpool'
Beckham ni mpenzi wa Manchester United ambao ni wapinzani wa Liverpool. 

Beckham aliondoka Old Trafford kuhamia Los Blancos kwa dau la Pauni Milioni 25 mwaka 2003.

MAKATIBU TAWALA WA MIKOA WAAGIZWA TAKWIMU ZA WAZEE IFIKAPO 30 JUNI 2018.


 Mhe. Seleman Jafo, akizungumza wakati wa Hafla ya kuwapatia Vitambulisho Wazee wa Jiji la Dodoma.


Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma akitoa salam za jiji muda mfupi kabla ya zoezi la ugawaji wa Vitambulisho kwa wazee halifanyika.

Mmoja ya Wazee akipokea kitambulisho mara baada yakuzinduliwa kwa zoezi lakuwapatia vitambulisho wazee Jiji la Dodoma.

Picha ya pamoja kati ya Mhe. Waziri Viongozi wa Halmashauri na wazee waliopatiwa vitambulisho.

 Mhe. Diwani wa Kata ya Mkonze akishukuru kwaniaba ya wananchi wa Mkonze.




Makatibu Tawala wa Mikoa Waagizwa  Takwimu za Wazee ifikapo 30 Juni, 2018

Na. Atley Kuni-OR TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (Mb), amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa Tanzania Bara kuwasilisha taarifa za takwimu za wazee ifikapo      30, Juni 2018.

Waziri Jafo, alitoa kauli hiyo mapema leo alipokuwa akizindua  zoezi la kuwapatia  vitambulisho maalum wazee wapatao 1,118 wa Jiji la Dodoma kutoka kata za Mkonze, Mnadani, Uhuru, Madukani, Makole na Majengo. Vitambulisho hivyo, pamoja na mambo mengine vitawawezesha wazee hao kupata huduma za afya bure na kwa wakati.

“Ifikapo tarehe 15 Juni, 2018 kila kata iwe imetambua wazee na ifikapo tarehe 22 Juni, 2018 kila Halmashauri iwe imeunganisha taarifa za wazee kutoka katika kata zake zote” alisema Waziri. Aidha Waziri Jafo aliagiza kuwa, “ifikapo Juni, 26, 2018 kila Mkoa uwe umeunganisha taarifa zote na kuzituma kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI”.

Aliwaonyawale wote watakaoshindwa kutimiza agizo hilo kuchukuliwa hatua kulingana na miongozo, kwasababu watakuwa wameshindwa kutekeleza wajibu wao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Ndugu Godwin Kunambi akizungumza katika hafla hiyo alisema shabaha ni kuwafikia wazee wote kwenye Jiji hilo, na kubainisha kwamba, vitambulisho wanavyo vitoa kwa wazee hao vitatumika pia kuwapa kipaumbele wazee sehemu zote za kutolea huduma hususan ofisi za serikali.

“Mhe. Waziri tunataka vitambulisho hivi tunavyo wapatia wazee wetu leo viwasaidie pia kupata huduma kwa haraka na kwa wakati pindi wanapofika kwenye ofisi zingine za Serikali” alisema Kunambi.

Mbali na kutolea ufafanuzi wa matumizi ya vitambulisho hivyo, Mkurugenzi Kunambi alisema juu ya Jiji hilo lilivyo jipanga katika suala zima la makusanyo ya mapato ya ndani, ambayo ndio yamekuwa chachu ya kuboresha huduma za afya kwa makundi maalum hususan wazee.

“Mhe. Waziri, Jiji limepanga kukusanya Bil. 68 katika mwaka wa fedha ujao ikilinganishwa na mwaka huu wa fedha ambapo tulijiwekea lengo la kukusanya Bil. 20 nahadi kufikia mwezi Februari tulikuwa tumekusanya Bil. 14”. Kunambi ameongeza kuwa, katika mwaka ujao wa fedha wametenga kiasi cha Mil. 58 kwaajili yakuwezesha huduma za wazee kwenye Jiji hilo.

Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Deo Ndejembi, ametumia fursa hiyo kuwaonya baadhi ya watendaji wanao waambia wazee kwamba hakuna dawa.

“Kumekuwepo na malalamiko mengi siku za nyuma kutoka kwa wazee kuwa, baadhi ya watendaji wa afya wanawanyanyapaa wazee na kuwaambia hakuna dawa wafikapo vituoni, sasa Mhe Waziri, mimi niliseme kwa uwazi kabisa hatuta mvumilia mtu yeyote atakaye onekana ni kikwazo kwa wazee hawa kadi zimetoka wazee wahudumiwe, sio mnajiwekea vijiduka karibu na vituo halafu mnawaambia waende waka nunue” alionya Ndejembi

Awali akitoa taarifa ya uandaji wa vitambulisho Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Mohamed Nyembea, alisema utekelezaji wa zoezi hilo ulianza kwa hatua za awali kwa kuwatambua wazee katika Kata 41 za Jiji la Dodoma, ambapo jumla ya wazee 15,885 kutoka kata 33 miongoni mwa 41 wamekwisha tambuliwa  na miongoni mwao wanawake ni 9,132 na wanaume ni 6,753 ambapo ni sawa na asilimia 80.5 ya  kata zote 41 za Jiji la hilo.

Utoaji wa vitambulisho kwa wazee ni utekelezaji wa sera ya Taifa ya wazee ya mwaka 2003 ambapo inazungumzia mambo muhimu ya wazee ikiwepo kutenga dirisha maalum katika vituo vya kutolea huduma za afya.  

Friday, May 25, 2018

UPANUZI WA KITENGO CHA DHARULA HOSPITALI YA RUFAA YA BUGANDO WAPIGWA JEKI YA SHILINGI MILIONI 240 NA BENKI CRBD


GSENGOtV
Changamoto ya rasilimali fedha kwa baadhi ya vituo vya huduma za afya nchini imekuwa kikwazo katika uboreshaji wa huduma hizo kiasi cha kuifanya sekta hiyo kutofikia malengo yanayotarajiwa.
 Kwa kuliona hilo Benki ya CRDB nchini hii leo Tarehe 25 Mei 2018 imekabidhi hundi ya shilingi milioni 240, kwa ajili ya upanuzi wa idara ya wagonjwa mahututi ya hospitali ya rufaa ya Bugando (BMC) Jijini Mwanza, ili kukabiliana na tatizo la msongamano wa wagonjwa unaoikabili Hospitali hiyo. 
 Mkurugenzi mkuu wa Hospitali ya rufaa ya Bugando Dk. Abel Makubi, ameiomba serikali kutangaza ajira mpya za madaktari, ili kupunguza uhaba wa madaktari bingwa katika idara hiyo.
 Akizungumzia matumizi ya fedha hizo kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB nchini Dk. Charles Kimei, kaimu mkurugenzi wa benki hiyo Esther Kileo, amesema msaada huo umetolewa, ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
 Kutokana na umuhimu wa upanuzi wa Idara hiyo, Askofu mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Mwanza Jude Thadeus Ruwaich, ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya Hospitali hiyo, amesema msaada huo unahitajika, ili kutatua msongamano unaoikabili Hospitali hiyo.





 Kaimu mkurugenzi wa benki ya CRDB Esther Kileo akimpa mkono Askofu mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Mwanza Jude Thadeus Ruwaich mara wakati wa upigaji picha ya pamoja ya makabidhiano.
  CRDB katika picha ya pamoja na viongozi.
 Picha ya pamoja na wadau kitengo cha dharula.
 Baada ya makabidhiano hayo katika hatua nyingine, Benki hiyo imelikabidhi Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza Pikipiki tatu aina ya Boxer, zenye thamani ya shilingi milioni kumi ikiwa ni pamoja na gharama za usajili, ili kuboresha shughuli za ulinzi na usalama kwa mkoa wa Mwanza.
  Maelezo toka kwa mwenyeji kwa wageni.
 Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi akiwasilisha salamu za shukurani toka kwa IGP Simon Sirro kwa  Kaimu mkurugenzi Benki ya CRDB nchini baada ya kupokea pikipiki 3 kama sehemu ya kuliwezesha jeshi hili kuhudumia wananchi.
  Karibuni wageni.

 Picha ya pamoja.

MIZENGO PINDA NA MAKONGORO NYERERE WAULA UTEUZI WA JPM.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, amewateua Waziri Mkuu Mstaafu, Mzee Mizengo Kayanza Peter Pinda na Makongoro Nyerere kuwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC).










WAMILIKI WA VIWANDA VYA KUCHENJUA DHAHABU MKOANI MWANZA WAINGIWA HOFU YA KUFUNGA VIWANDA VYAO MARA BAADA YA KUINASA KAULI YA MKUU WA MKOA WA GEITA.


GSENGOtV
WAKATI Serikali ya Awamu ya tano ikikusudia kuanzisha soko la Kimataifa la madini jijini Mwanza ambapo tayari imeshatenga eneo kwaajili ya kuweka soko hilo ambalo licha ya kukuza sekta hiyo bali kudhibiti utoroshwaji wa madini nchini, upande wa pili, Mkuu wa mkoa wa Geita Robert Gabriel analalamikiwa na Umoja wa wamiliki wa viwanda vya uchenjuaji na wanunuzi wa dhahabu Mkoani Mwanza kwa kupiga marufuku wafanyabiashara wa madini kutoka mkoani kwake kusafirisha malighafi inayotumika kubebea dhahabu inayojulikana kama CARBON kwenda jijini Mwanza.

Thursday, May 24, 2018

WATANO KATI YA WALIOTOKA JELA KWA MSAMAHA WA RAIS WAUAWA NA WANANCHI.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon
CHANZO/MWANANCHI
Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amesema watu watano waliotoka gerezani kwa msamaha wa Rais John Magufuli wameuawa na wananchi baada ya kurejea katika matendo maovu.

Sirro aliyewataka wanaoachiwa huru kwa msamaha wa rais kutorejea katika matendo hayo, ametoa kauli hiyo   leo Alhamisi Mei 24, 2018 mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa vituo vya polisi vya kisasa vya Mburahati, Kiluvya-Gogoni na Mbweni vilivyozinduliwa leo.

“Nia ya Rais Magufuli kuwapa msamaha ilikuwa njema lakini kuna baadhi ya watu wameitumia vibaya fursa hiyo na hadi sasa watu watano wamekwishauawa na wananchi,” amesema.

“Ukitoka gerezani kwa msamaha, maana yake umerekebisha mwenendo wako na wananchi wanatarajia uwe hivyo, lakini kama ukifanya vinginevyo Serikali isilaumiwe.”

Akizungumzia utendaji wa jeshi hilo, Sirro amesema tangu ashike madaraka hayo polisi wamewapeleka askari 1,267 kwenye mafunzo ya medani za kivita na wako imara.

Pia tumepeleka askari wa upelelezi zaidi ya 1,000 kwenye mafunzo ya ujuzi na ustadi wa kupeleleza kesi mbalimbali. Baada ya kuwapa mafunzo haya, tunataka kesi za kawaida upelelezi wake uwe umekamilika ndani ya miezi sita” amesema na kubainisha kuwa kesi kubwa upelelezi wake uwe umekamilika ndani ya miezi 12.

Pia, amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia Sh10 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari, kutoa kibali cha ajira kwa askari wapya 1,500 na kuwaruhusu wawapandishe vyeo askari wenye kustahili kuanzia cheo cha koplo hadi naibu kamishna wa polisi (DCP).




THOMAS ULIMWENGU AREJEA AFRIKA.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania Thomas Ulimwengu, amerejea barani Afrika na sasa atajiunga na klabu ya Al Hilal ya nchini Sudani.

Ulimwengu aliyewahi kucheza TP Mazembe kwa mafanikio makubwa akifanikiwa kutwaa mataji mbalimbali likiwemo la Klabu bingwa Afrika, anarejea Afrika baada ya kuachana na klabu ya AFC Eskilstuna iliyokuwa ikishiriki Ligi kuu nchini Sweden kabla ya kushuka daraja msimu uliopita.

Mshambuliaji huyo, anatazamiwa kutua katika klabu hiyo ya Al hilal na taarifa za awali zinaeleza kuwa atasaini mkataba wa miaka miwili kukitumikia kikosi hicho.
Hapo awali aliwahi kucheza na mtanzania mwenzake Mbwana Samatta katika klabu ya TP Mazembe na kwa sasa pacha wake huyo anahudumu katika kikosi cha KRC Genk ya nchini Ubelgiji.

ZIARA YA KATIBU MKUU, MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KATIKA JIJI LA MWANZA:




THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF –Chama Cha Wananchi)
THE DIRECTORATE OF INFORMATION, PUBLICITY AND PUBLIC RELATION
P.O. BOX 3637 Zanzibar, Tanzania
TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI
ZIARA YA KATIBU MKUU, MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KATIKA JIJI LA MWANZA:
Leo Tarehe 23/5/2018 saa 10 Jioni Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad atawasili Jijini Mwanza na kupokelewa na Wanachama na Viongozi wa CUF wa ngazi mbalimbali za Chama. Katibu Mkuu ataongozana katika msafara huo na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma Mhe. Mbarala Maharagande, atakuwa Mwanza kwa ziara ya siku Tatu baada ya kupata mualiko kutoka kwa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UNION OF TANZANIA PRES CLUB-UTPC) yenye makao yake Makuu Mkoani Mwanza. UTPC- kwa sasa ina klabu wanachama (Press Clubs) 28 toka Tanzania Bara na Visiwani.
UTPC kwa kushirikiana na vyombo vya Habari inaendesha kipindi cha TUJADILIANE kinachowakutanisha waandishi wa Habari kutoka katika redio zote zilizopo Mkoani Mwanza, TV pamoja na magazeti na imekuwa ikiwaalika wageni kutoka Serikalini, Asasi za kiraia, na watu mashuhuri wakiwemo wanasiasa kutoka hapa nchini. Pamoja na shughuli zingine kesho Tarehe 24/5/2018 kuanzia saa 5 kamili asubuhi katika ukumbi wa hotel ya JB BELMOUNT Jijini Mwanza atashiriki katika kipindi maalumu cha TUJADILIANE. Katika kipindi hicho Maalim Seif atapata fursa kuelezea masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na jamii kwa ujumla na pia atapata fursa ya kuelezea DIRA YA CUF, MWELEKEO WA CUF, MAFANIKIO YA CUF, CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI CUF NA NAMNA YA UTATUZI WAKE.
Katibu Mkuu, Maalim Seif atakutanishwa na waandishi wa habari wa Jijini Mwanza na mahojiano ya kipindi hicho yatarushwa MUBASHARA “LIVE” kupitia mitandao ya kijamii hususani Facebook, na pia yatasikika kupitia Radio SAUT, RFA, Kiss FM, Afya Radio, Metro FM, Radio Sengerema, HSC, Living water, Ukombozi FC, Iqra FM, Kwa Neema Radio za Jijini Mwanza na Safari FM ya Mkoani Mtwara. Pia kupitia Facebook Account ya Julius Mtatiro na links zingine mbalimbali. Na baadae katika vipindi vya Television. Pamoja na kuwa uso kwa uso na jopo la waandishi wa habari Jijini Mwanza, mahojiano hayo yatakayoongozwa na Ndugu Dotto Emmanuel Bulendu.
Tunapenda kuchukua fursa hii kuwajulisha rasmi Programu hiyo kwa ufuatiliaji na kama kuna masuala ambayo unahitaji Maalim Seif aulizwe usisite kututumia na au kumtumia mratibu wa kipindi hicho Dotto Bulendu kupitia akaunti yake ya Facebook.
HAKI SAWA KWA WOTE
………………………
SALIM BIMANI
MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA
MAWASILIANO: 0777 414 112/ 0752 325 227
Imetolewa leo Tarehe 23/5/2018

MKONO WA MAMA JANET MAGUFULI BADO UNAHITAJIKA KITUO CHA KULEA WAZEE BUKUMBI MWANZA


GSENGOtV
Bado wazee wanaoishi katika kituo cha ustawi wa Jamii cha Bukumbi kijiji cha Kigongo kata ya Idetemya wilayani Misungwi mkoani Mwanza wanaishi kwenye mazingira magumu.

 Wakiwa ndani ya makazi yao, mnamo tarehe 7 April 2018 Katika kuadhimisha Kumbukumbu ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Abeid Amani Karume, wazee hao wanatembelewa na wadau wa Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya 'METDO Tanzania' iliyoambatana na waandishi wa habari kutoka Jembe Fm pamoja na waimbaji wa Muziki wa Injili toka mkoa wa Mwanza wenye kundi lao linalioitwa 'The Chosen Generation' ambapo wazee hao wanapaza sauti zao juu ya masaibu na changamoto wanazokumbana nazo, wakiomba salamu hizo zifike kwa First lady wa Tanzania 'Mama Janet Magufuli' pamoja na wananchi wenye mapenzi mema.
.   

UTEUZI ALIOUFANYA JPM SAA CHACHE ZILIZOPITA.

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa  mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi  ya chai Tanzania (TBT) na Mkurugenzi  wa Taasisi ya Utafiti wa kilimo Tanzania (TARI).

Katika taarifa ilitolewa na Ofisi ya Kurugenzi Mawasiliano Ikulu leo Mei 23, 2018 imeeleza kuwa Mhandisi Steven Daudi Mlote, ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya chai Tanzania (TBT) na kuongeza kuwa Mhandisi Mlote anachukua nafasi iliyoachwa wazi na mtangulizi wake Mh. Anne Makinda ambae amemaliza muda wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo imeongeza kwamba uteuzi wa Mhandisi Mlote ulianza Mei 21, 2018.

Sambamba na hayo Rais Dkt John Magufuli amemteua Dkt. Geofrey Mkamilo kuwa Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa kilimo Tanzania (TARI),  uteuzi wake umeanza Mei 22, 2018 na anachukua nafasi ya Dkt. Fidelis Angelo Myaka ambaye amestaafu.

TUZO YA MCHEZAJI BORA LIGI KUU KUTOLEWA JUNI 23.


Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) Tanzania Bara inatarajiwakufanyika Juni 23 mwaka huu ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Kufanyika kwa tuzo hizo ni utaratibu ambao Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limejiwekea kila mwaka baada ya kumalizika ligi kutoa tuzo kwa waliofanya vizuri kwa kushirikiana na Wadhamini wakuu wa VPL Kampuni ya Simu za mkononi ya Vodacom Plc na msimu huu tutakuwa na washirika wengine Azam Tv, Benki ya KCB na Premier Bet

Licha ya Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka wa ligi, pia kunatolewa tuzo mbalimbali, ambapo kwa mwaka huu tuzo moja imeondolewa na nyingine imeongezwa ikiwa ni katika kuboresha.

Tuzo iliyoondolewa ni ya Mchezaji Bora wa Kigeni na imefanyika hivyo ili kuwapa fursa wachezaji wote kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa VPL badala yakuwatenganisha.

Pia msimu huu imongezwa Tuzo ya Mwamuzi Bora Msaidizi ambayo haikuwepo msimu uliopita, hiyo ni kutokana kuthamini nafasi ya waamuzi wasaidizi.

Kwa mazingira hayo tuzo zitakazotolewa Juni 23, ambapo wadhamini wakuu ni Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom ni hizi zifuatazo:

Bingwa
Mshindi wa Pili
Mshindi wa Tatu
Mshindi wa Nne
 Mfungaji Bora
Timu yenye nidhamu
U20 Player (Tuzo ya Ismail Khalfan)
Mchezaji Bora Chipukizi
Mwamuzi Bora Msaidizi
Mwamuzi Bora
Kipa Bora
Kocha Bora
Goli Bora
VPL Best Eleven
Mchezaji wa heshima

Zawadi kwa kila kategori pamoja na majina ya wanaowania tuzo ukiacha bingwa, mshindi wa pili, wa tatu, wa nne na mfungaji bora ambao hujulikana kulingana na ligi inavyoendelea zitatangazwa siku za usoni.

Wednesday, May 23, 2018

AIRTEL NA VETA WASHIRIKIANA KUANDAA KONGAMANO LA ELIMU KUPITIA MTANDAO.

Godfrey Magila kutoka taasisi ya DTBi akitoa mada wakati kongamano la elimu kupitia mtandao yenye lengo la kuhamasisha kusoma kwa kujitengemea kwa miongoni mwa vijana hapa nchini kupitia teknologia ya VSOMO. Kongamano hilo liliandaliwa na Airtel Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Tanzania VETA na DTBi
 Mkurugenzi wa Mawasiliano Airtel Tanzania Beatrice Singano akitoa mada wakati kongamano la elimu kupitia mtandao yenye lengo la kuhamasisha kusoma kwa kujitengemea kwa miongoni mwa vijana hapa nchini kupitia teknologia ya VSOMO. Kongamano hilo liliandaliwa na Airtel Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Tanzania VETA na DTBi

 Mratibu wa VSOMO kutoka Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Tanzania VETA Charles Mapuli  akitoa mada wakati kongamano la elimu kupitia mtandao yenye lengo la kuhamasisha kusoma kwa kujitengemea kwa miongoni mwa vijana hapa nchini kupitia teknologia ya VSOMO. Kongamano hilo liliandaliwa na Airtel Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Tanzania VETA na DTBi

Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Tanzania VETA wameshiriki kongamano la elimu kupitia mtandao yenye lengo la kuhamasisha ubunifu kwa vijana na kuonesha jinsi kijana anavyoweza kusoma kwa kujitengemea kwa kutumia ubunifu wa  aplikesheni ya VSOMO inayotoa  elimu kwa mtandao.
Kwa miaka miwili sasa, VETA kupitia applikesheni ya VSOMO imekuwa ikitoa elimu kupitia mtandao kwa wanafunzi ambao wanataka kupata elimu ya ufundi stadi kwa udhamini wa Airtel Tanzania.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo wakati wa kongamani hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Airtel Tanzania Beatrice Singano alisema kampuni ya Airtel iliamua kuwa mmoja wa wadau wa teknolojia hii ya kutoa elimu ya VSOMO ikiwa ni moja wa mkakati wake wa kurudisha sehemu ya faida yake katika kusaidia Jamii. Kwa kuweza kutambua umuhimu wa Jamii inayotuzunguka, tuna miradi ya kusaidia vijana kujikwamua yenye lengo ya kuwapa vijana ujuzi ili wajiajiri au wapate ajira kwenye sekta mbali mbali ili kuunga mkono juhudi za serikali za kujenga uchumi wa viwanda.
Airtel Tanzania inayo furaha kuona kuwa matumizi ya smartphone yakiwa ni darasa au ikiwa ni moja ya njia ya kutumika kupata elimu ya ufundi. Hii haiukuwa rahisi kufanya peke yetu ndio sababu tuliamua kushirikiana na VETA kama taasisi ya serikali yenye mamlaka ya kutumia elimu ya ufundi hapa nchini huku DTBi wakiwa ndio waliombuni applikesheni ya VSOMO, alisema Singano.
Airtel na washirika wake VETA na DTBi kwa sasa wana utaratibu mpya wa malipo kwa awamu ili kuwezesha wanafunzi wanaotaka kupata elimu ya ufundi stadi kufanya bila kupata changamoto za kulipa karo, aliongeza Singano.
Mkuu wa chuo cha VETA Kipawa Injinia Sospeter Dickson Mkasanga alisema kuwa teknolojia imekuwa sana katika dunia ya leo na Tanzania kama nchi pia imefaidika sana. Kwa kutumia teknolojia, kila kitu sasa kinawezekana. Ni kwa kutumia teknolojia tumeweza kutoa elimu ya ufundi stadi kwa zaidi ya vijana 100 wakiwa hawapo darasani. Hii ni kitu ya kujivunia kwa sababu vijana hao wameweza kujiajiri na wengine wameajiri kwenye sekta mbali mbali kwa tunawakabidhi vyeti baada ya kumaliza elimu yao, alisema Mkasanga.
VSOMO imeweza kuwa mkombozi wa elimu ya ufundi stadi kwa kutumia teknolojia. Kwa kutumia simu za  smartphone, wanafunzi wanapata ufundi stadi wa kozi yeyote wayohitaji. Naomba nitoe wito kwa vijana wote nchini ambao wangependa kupata elimu ya ufundi stadi wajiunge na wapakue applikesheni ya VSOMO kwani ni rahisi na pia malipo ya kozi ni nafuu, aliongeza Mkasanga.
Kwa upande wake, Godfrey Magila kutoka DTBi alisema kuwa ili kufanya teknolojia iwe na tija kwa Jamii, ni muhimu kwa Jamii kupata elimu ya umuhimu na matumizi ya teknolojia ili kufaidika nayo na pia kufanya baadhi ya mambo yawe rahisi katika maisha yao.

Jamii zetu zinapata changamoto kufikia malengo yao. Kwa sasa, teknolojia imekuwa kwenye vidole vyetu na ndio sababu watu wengi wanatumia smartphone ambazo zina uwezo wa kuweka memori kubwa. Kama Jamii yetu ingeweza kutambua na kuelewa elimu iliyopo kwenye smartphone hizo ingekuwa ni jambo la maana, alisema Magila.

Tangu kuzinduliwa kwa VSOMO Juni 2016, inaonyesha kuwa zaidi ya vijana 30,000 washapakua applikesheni ya VSOMO huku zaidi ya 10,000 wakijisajili na zaidi ya 100 wakiwa tayari washamaliza kusoma kupitia applikesheni hiyo na kukabidhiwa vyeti vyao.

Kozi ambazo ulitolewa ni Huduma ya chakula na mbinu za kuhudumia wateja, Matengenezo ya kompyuta, umeme wa viwandani, ufundi Bomba wa Majumbani , Umeme wa magari, Ufundi umeme wa manyumbani, Ufundi pikipiki, Ufundi wa simu za mkononi, Ufundi Alluminium,  Utaalamu wa maswala ya urembo pamoja ma Ufundi wa kuchomea vyuma

BENKI YA CRDB NA JESHI LA MAGEREZA KUENDELEA KUBORESHA UHUSIANO WA KIBISHARA

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (kushoto) akizungumza na baadhi ya maafisa waandamizi wa Jeshi la Magereza nchini, juu ya kuangalia njia bora za kudumisha uhusiano baina ya Benki ya CRDB na Jeshi la Magereza nchini, katika Makao Makuu wa Magereza, jijini Dar es salaam, Mei 23, 2018. Kulia ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dokta Charles Kimei leo amekutana na Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini Dokta Juma Malewa ili kuangalia njia bora zaidi za kudumisha na kuboresha uhusiano baina ya pande zote mbili. Akizungumza katika mkutano huo ambao pia ulijumuisha maafisa waandamizi kutoka Benki ya CRDB na Jeshi la Magereza, Dokta Kimei alilishukuru Jeshi hilo kwa kuwa mdau mkubwa wa Benki kupitia mikopo, akaunti za mishahara za askari na SACCOSS ya Magereza ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitoa huduma kwa askari Magereza.

“Nichukue fursa hii kulishukuru Jeshi la Magereza kwa biashara ambayo limekuwa likitupatia, niipongeze SACCOSS ya Magereza kwa uamuzi wa kuwa Wakala wa FahariHuduma, hii si tu itawaongezea kipato kupitia kamisheni za uwakala, pia itasogeza huduma za kibenki karibu na Maaskari Magereza”, alisema Dokta Kimei.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa akizungumza katika kikao na uongozi wa Benki ya CRDB, uliomtembelea ofinisi kwake, Makao Makuu ya Magereza jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei. 


Akielezea juu ya fursa mbalimbali zinazotolewa na Benki ya CRDB kwa wafanyakazi Dokta Kimei alisema hivi karibuni Benki imeshusha riba inayo toza katika mikopo binafsi toka 20% mpaka 17%, muda wa marejesho umeongezwa toka miezi 72 hadi miezi 84, wakati kiwango cha kukopa kimeongezwa kutoka shilingi milioni 50 mpaka kufikia Shilingi Milioni 100 hivyo kuwapa wateja wigo mpana zaidi wa kukopa ili kufikia malengo.
Dokta Kimei pia alitumia fursa hiyo kuwahamasisha askari wa Jeshi la Magereza kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo huku akibainisha ya kuwa Benki ya CRDB imeanzisha utaratibu maalum wa kununua madeni na mikopo ya askari kutoka katika Taasisi zingine za Kifedha. Hivyo kutoa fursa kwa askari wenye mikopo Benki nyingine, kukopa toka Benki yao pendwa ya CRDB. Mpaka kufikia mwisho wa mwezi Aprili 2018 tayari Benki ya CRDB ilikuwa imeshakopesha zaidi ya maofisa 5,415 wa Jeshi la Magereza ambapo jumla ya shilingi 29.4 bilioni zilikuwa zimekopeshwa kwao.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (kushoto) akimkabidhi zawadi maalum, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa, wakati alipomtembelea ofisini kwake, Makao Makuu wa Magereza, jijini Dar es salaam, Mei 23, 2018. Mkutano huo ulikuwa na lengo kudumisha uhusiano wa kibiashara baina ya Benki ya CRDB na Jeshi la Magereza nchini. 


Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini Dokta Juma Malewa alimshukuru Dokta Kimei kwa kutembelea Jeshi hilo na kuipongeza Benki ya CRDB kwa maboresho hayo katika huduma zake, huku akiisifu zaidi huduma ya Salary Advance ambayo alisema kwa kiasi kikubwa imesaidia kuboresha maisha ya askari. Dokta Malewa alisema katika maboresho hayo yanayoendelea Jeshi la Magereza lingependa kutumia mfumo wa kibenki katika kukusanya mapato yake katika miradi na huduma mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

“Nikuombe Dokta Kimei na uongozi mzima wa Benki ya CRDB kuona uwezekano wa kuweka huduma za kibenki kama ATM na Matawi kwenye maeneo ya Magereza yenye uhitaji mkubwa wa huduma hiyo”, aliongezea Dokta Malewa. Dokta Malewa pia aliiomba Benki ya CRDB kushiriki katika miradi mbalimbali ya Maendeleo inayotekelezwa na Jeshi hilo ikiwamo ujenzi wa hospitali ya Jeshi la Magereza Ukonga, miradi ya Kilimo cha kisasa na chenye tija, mradi wa kokoto Msalato pamoja na uwekezaji katika miradi ya viwanda vidogo vidogo.
Baadhi ya Maafisa waandamizi wa Jeshi la Magereza nchini, wakiongozwa na Naibu Kamishna wa Jeshi hilo, Kamishna Festo Sanga (wa kwanza kulia) wakati wa kikao maalum na uongozi wa Benki ya CRDB, uliotembelea Makao Makuu ya Magereza, jijini Dar es salaam leo.
“Ningependa kuona pia Benki ya CRDB kuwa mteja wa bidhaa na huduma zinazotolewa na Jeshi la Magereza mfano Benki kutumia samani za ofisi na Magereza kupewa Kandarasi za ujenzi wa miradi ya Benki inayodhaminiwa au kumilikiwa na Benki”, aliongezea Dokta Malewa akionyesha fursa ya kibiashara iliyopo baina ya Benki na Jeshi la Magereza.

Dokta Kimei alimhakikishia Mkuu wa Jeshi la Magereza kuwa Benki ya CRDB ipo tayari kushirikiana na Jeshi hilo katika miradi mbalimbali ambayo wamepanga kuitekeleza, huku akihaahidi kutuma timu ya wataalam kutoka Benki ya CRDB kufanya upembuzi yakinifu juu ya kuweka ATM na kufungua vito vya kutolea huduma katika maeneo ya Jeshi la Magereza ilikufikisha huduma kwa akari kwa urahisi.

Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa akieleza jambo kwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Juma Malewa (hayupo pichani) katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Magereza, jijini Dar es salaam leo.

“Matarajio yangu ni kuona uhusiano baina yetu ukikua zaidi, naihidi kuwa kupitia Wakurugenzi na Mameneja wetu wa matawi tutaweka utaratibu wa kutembelea ofisi za Magereza nchi nzima ili kuhakikisha haya tuliyokubaliana hapa yanatekelezwa”, alisema Dokta Kimei.

Mkutano huo ulimalizika kwa Benki ya CRDB na Jeshi la Magereza kutengeneza kikosi kazi cha kufuatilia utekelezaji wa maazimio ambapo Kamishna Gaston Sanga Mkurugenzi wa Utawala, fedha na Rasimali watu wa Jeshi la Magereza alichaguliwa kuwa Mwenyekiti akisaidiwa na Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wakati wa Benki ya CRDB Bi. Jesica Nyachiro. Dokta Kimei pia alimuomba Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya CRDB Bi. Tully Mwambapa kuona namna ambavyo Benki ya CRDB itaweza kuunganisha shughuli zake za misaada kwa jamii na Jeshi la Magereza.



Katika mkutano huo Benki ya CRDB iliahidi kutoa msaada wa kompyuta na vitendea kazi vingine kwa Jeshi la Magereza ili kuongeza ufanisi wa Jeshi hilo. Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi April 2018, Benki ilikuwa pia imeshafungua zaidi ya Akaunti elfu tatu (3,000) za mishahara kwa askari wa Jeshi la Magereza.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei akizungumza.
Baadhi ya Maafisa wa Benki ya CRDB, wakiwa kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (kushoto) akimkabidhi zawadi maalum, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Dkt. Juma Malewa, wakati alipomtembelea ofisini kwake, Makao Makuu wa Magereza, jijini Dar es salaam, Mei 23, 2018. Mkutano huo ulikuwa na lengo kudumisha uhusiano wa kibiashara baina ya Benki ya CRDB na Jeshi la Magereza nchini.
Picha ya pamoja.