ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, August 14, 2021

UCHAGUZI ZAMBIA:- HICHILEMA ACHUKUA UONGOZI WA MAPEMA DHIDI YA LUNGU.

 


Kiongoizi wa upinzani nchini Zambia Hakainde Hichilema amechukua ushindi wa mapema.

Matokeo ya awali yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi yanaonesha chama cha National Development kinaongoza kwa idadi ya kura dhidi ya Rais Edgar Lungu.

Mwandishi wa BBC Nomsa Maseko anasema Raia wa Zambia wanasubiri kwa hamu kujua ni nani atakuwa rais wao mpya.

Tume ya uchaguzi imekuwa ikijumuisha kura zilizopigwa Alhamisi katika uchaguzi uliyokuwa na ushindani mkali.

Matokeo ya maeneo bunge 15 kati ya zaidi ya 150 yametangazwa kufikia sasa.

Matokeo katika maeneo bunge hayo ambayo yanatajwa kuwa ni ngome za Lungu, yanaashiria kuwa Hichilema amepata uungwaji mkono mkubwa katika ngome za mpinzani wake tofauti na uchaguzi wa mwaka 2016 uliogubikwa na madai wa wizi wa kura.

Uwepo mkubwa wa wanajeshi bado unaonekana katika barabarani huku ulinzi mkali ukiwekwa katika kituo cha kutangaza matokeo.

Baadhi ya wagombea urais wamekubali kushindwa na kumpongeza Hakainde Hichilema, kiongozi wa chama cha United Party for National Development kwa kuchukua ushindi wa mapema katika uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Patrick Nshindano, amewaambia waandishi habari mjini Lusaka kuwa jumla ya kura 296,210 zilipigwa katika maeneo bunge hayo.

Matokeo ya kwanza yaliyotarajiwa kutolea jana Ijumaa yalichelewa baada ya zoezi la kuhesabu kura kuendelea hadi usiku kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura, na pia kwa sababu baadhi ya vyama vya kisiasa vilipinga matokeo yaliyotolewa na tume hiyo katika eneo bunge moja.

Kwengineko Mamlaka ya Mawasiliano na Teknolojia nchini Zambia imepelekwa mahakamani kwa kudhibiti huduma za intaneti na mitandao ya kijamii waziri wa Mamlaka tangu Alhamisi.

Mahakama kuu ya Zambia imeamuru marufuku hiyo kuondolewa mara moja.

CHANZO: BBC SWAHILI.

MBARONI KWA UHALIFU WA UTEKAJI, UBAKAJI NA KULAWITI WATOTO.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara Mark Njera.

 


Jeshi la polisi Mkoani Mtwara limemkamata Jabiri Bakari  kwa kosa la kujihusisha na uhalifu wa utekaji, ubakaji na kulawiti watoto wa kike wenye umri chini ya miaka kumi katika wilaya ya Mtwara.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara Mark Njera amewaambia waandishi wa habari leo kuwa mtuhumiwa huyo mwenye miaka 19 alikamatwa tarehe 12 August Mwaka huu  maeneo ya Mbae Manispaa ya Mtwara kufuatia msako wa jeshi la polisi uliofanywa.

Kamanda Njera amesema kabla ya kukamatwa na jeshi la polisi, mtuhumiwa aliwadanganya watoto wa kike watatu wenye umri wa miaka 8, 7 na mwingine mwenye miaka 9 ambao kwa nyakati tofauti aliwaiba sehemu mbalimbali kwa kuwalaghai kwa njia mbalimbali na kufanikiwa kuondoka nao kwenda kwenye maeneo na kuanzisha makazi ya mda akiwa na watoto hao.

Amesema mnamo tarehe 25 mwezi Juni mwaka huu mtuhumiwa alimlaghai mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 7 maeneo ya Mbae Mashariki wilaya ya Mtwara mtoto huyo akiwa anacheza na wenzake na baadae kuondoka naye ambapo mtoto huyo alipatikana baada ya siku tano akiwa amefanyiwa vitendo vya ukatili.

Mnamo tarehe 8 July maeneo ya Mbae, mtuhumiwa huyo alimchukua tena mtoto wa kike mwingine mwenye miaka 7 na kutoweka naye na kwenda kusikojulikana. Mtoto huyo alipatikana tarehe 24 Julya akiwa amefanyiwa vitendo vya kikatili.

Na mnamo tarehe 6 August mtuhumiwa huyo pia alimchukua mtoto mwenye umri wa miaka tisa ambaye pia alipelekwa kusikojulikana na mtuhumiwa huyohuyo na kufanyiwa vitendo vya ukatili. Kwa muhjibu wa kamanda Njera, mtoto huyo alipatikana tarehe 7 August kufuatia msako wa jeshi hilo.

Kamanda Njera ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mtwara kuhakikisha ulinzi na usalama kwa watoto na kutambua watu wanaojihusisha na vitendo vya ukatili kwa watoto na kutoa taarifa.

SIMBA YATAMBULISHA JEMBE LINGINE KUTOKA SENEGAL

 


RASMI kikosi cha Simba leo kimemtambulisha Pape Ousmane Sakho raia wa Senegal mwenye miaka 24.

Nyota huyo anakuwa ingizo jipya la nne ndani ya Simba baada ya jana Agosti 13 kumtambulisha Duncan Nyoni aliyeungana na Peter Banda pamoja na mzawa Yusuph Mhilu.

Nyota huyo anatajwa kuwa na uwezo mkubwa ndani ya uwanja pale anapopata nafasi akiwa ni kiungo mshambuliaji kinda aliyefanya vizuri kwenye ligi ya Senegal.  

Rekodi zinaonyesha kwamba alitupia mabao 8 na pasi 10 alitoa, pia ndiye mchezaji aliyeng'ara wakati timu ya Teungueth ikiitoa timu ya Raja Casablanca ya Morocco msimu ulioisha na kufuzu hatua ya makundi ya Caf Champions League.

Kwenye kambi nchini Morocco ambapo Simba wapo kwa sasa atajumuishwa na wengine ili kuendelea na maandalizi ya msimu ujao wa 2021/22.

Friday, August 13, 2021

YANGA YATAMBULISHA WAWILI - Djuma wa AS Vita NA Jesus Moloko

Shaban Djuma.

 

UONGOZI wa Yanga leo Agosti 13 umewatambulisha nyota wao wawili ambao watakuwa ndani ya kikoi hicho kwa msimu wa 2021/22.


Djuma ni beki ambaye anapewa nafasi ya kufanya vizuri msimu ujao kwa kuwa uzoefu wake unambeba na amecheza timu kubwa ya AS Vita ya Congo.

Ni Shaban Djuma ingizo jipya kutoka AS Vita pamoja na Jesus Moloko.

Jesus Moloko.


Moloko anakuwa mbadala wa Tuisila Kisinda ambaye anakwenda kujiunga na Klabu ya RS Berkane ya Morocco.

Moloko amebainisha kuwa hajawahi kufeli katika kazi ambazo huwa anafanya hivyo anaamini kwamba atafanya vizuri ndani ya kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi.

GARI LAKWAMISHA MBOWE KUPELEKWA MAHAKAMANI

 


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu, wameshindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kile kilichoelezwa ni changamoto ya usafiri wa gari la magereza.

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita yakiweno ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi, katika kesi ya Uhujumu Uchumi namba 63/2020.

Mashtaka mengine ni kula njama za kutenda makosa, kukutwa na silaha aina ya bastola, risasi pamoja na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kinyume cha sheria.

Mbali na Mbowe, ambaye ni mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo, wengine ni Halfan Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya.

SIMBA YATHIBITISHA CHAMA KUONDOKA.

 


Kaimu Afisa habari wa Simba SC Ezekiel Kamwaga amethibitisha kuwa Kiungo wa kimataifa wa Zambia Cloutous Chama (30) amejiunga na Club ya RS Berkane ya Morocco akisaini mkataba wa miaka mitatu.

Chama amesaini mkataba huo unaotajwa kuwa umeigharimu RS Berkane ada ya uhamisho ya Tsh Bilioni 1.5 kwenda Simba SC na kuongezewa mshahara mara nne ya aliokuwa analipwa Simba SC.

Chama ambae ameonekana kwenye mazoezi ya RS Berkane akiwa na Tuisila Kisinda wa Yanga, alijiunga na Simba SC mwaka 2018 akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia.

TANZANIA: UKATILI DHIDI YA WATOTO WAONGEZEKA, POLISI.

 

Ripoti ya jeshi la polisi nchini Tanzania inaonesha ongezeko la asilimia 25.95 la ukatili dhidi ya watoto. Katika mwaka 2020 visa 7388 viliripotiwa kote nchini tofauti na mwaka 2015 ambapo matukio 5,803 yaliripotiwa.

Watetezi wa masuala ya haki za watoto wametaja imani za kishirikina na utandawazi kuwa miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa matukio hayo. 

Ripoti hii ya Jeshi la Polisi inakuja katika kipindi hiki ambacho wazazi na walezi wengi wanatajwa kutokuwa karibu na watoto wao, wengi wakijihusisha na kusaka maisha bora ili kukidhi mahitaji ya msingi ya watoto huku wakiwapora haki ya kuwasikiliza.

Ripoti ya jeshi la polisi inataja miongoni mwa ukatili dhidi ya watoto ulioripotiwa kwa kiwango kikubwa kuwa dhuluma za kingono ambapo katika mwaka wa 2020 kuliripotiwa visa 7263 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na mwaka 2015 ambapo vilirikodiwa visa 5803, hii ikiwa ni sawa na visa 615 kwa mwezi jambo ambalo linatajwa kuwa linahatarisha mustakabali wa ustawi kwa watoto nchini humo.

Takwimu hizo zinarandana vilivyo na zile zilizotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania, katika ripoti yake ya hali ya haki nchini humo mapema mwaka huu, ambayo ilionesha kuongezeka kwa kiwango cha kutisha kwa matukio ya aina hiyo dhidi ya watoto.

Wanaharakati: Imani za kishirikina zachangia ukatili dhidi ya watoto Tanzania

Anna Henga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania, amesema ongezeko hilo ni kutokana na kukithiri kwa imani za kishirikina miongoni mwa wanajamii wanaotaka kusaka utajiri huku maeneo yaliyomulikwa zaidi ni upande wa Kanda ya Ziwa,

Aidha, ripoti zote mbili zimekwenda mbele zaidi na kuonesha kwa mwaka 2020 kulikuwa pia na wasiwasi juu ya ukatili juu ya watoto unaofanywa na watoto wenyewe, hasa matukio ya watoto kulawitiana katika shule za msingi na sekondari, matukio ambayo vyombo vya habari vilihusika kuyaripoti kwa asilimia 87.

Utandamazi na mmomonyoko wa maadili walaumiwa

Sophia Temba Afisa Program Jukwaa la Utu wa Mtoto, Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto. Amesema Mmomonyoko wa maadili na kutamalaki kwa utandawazi ndani ya jamii ni miongoni mwa sababu zinazoongeza kasi ya matukio hayo, lakini kuna haja ya kutengwa bajeti ya kutosha kutekeleza mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kunahitajika sasa.

Baadhi ya wazazi na walezi waliozungumza na JEMBE FM wanasema kwamba kuongezeka kwa rekodi ya matukio haya ni matokeo chanya, kwani ni kunatokana na kushamiri kwa elimu kwenye jamii ambapo hapo kabla yalitokea na watu waliyamaliza katika ngazi ya familia wakihofia sheria kuchukua mkondo wake, uhasama baina ya ndugu na visasi huku wakisahau afya za waathirika.

Thursday, August 12, 2021

HUU HAPA MCHONGO KWA WANAOTAMANI KUSOMA NJE YA NCHI.

 


Wengi hudhani ili mtu apate scholarships au nafasi ya kwenda kusoma nje ya nchi kwa mataifa kama Marekani, Ufaransa, Ubelgiji, Urusi, India na maeneo mengine ina kulazimu kuwa na fedha nyingi za mamilioni kwa mamilioni, lakini hivi unajua ukiwa na mtaji wa fedha kuanzia milioni mbili unaweza kwenda kusoma nchi yoyote unayotamani?

Ili kurahisisha upatikanaji na namna ya kujiunga na vyuo mbalimbali ulimwenguni Global link imeandaa orodha ya vyuo ambamo kuna fursa za kujiunga na masomo ya juu kwa wanafunzi kimataifa ndani ya nchi na nje ya nchi. Fuatilia mazungumzo haya kuzitambua fursa hizo na namna ya kuzifanyia kazi.

STEVE NYERERE ALA SHAVU UBALOZI WA UVIKO -19

 


Msanii maarufu nchini na Mwenyekiti wa Jukwaa la Mama Ongea na Mwanao, Steven Mengele 'Steve Nyerere' ameteuliwa kuwa Balozi wa harakati za kupambana na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (Uviko 19).

Steve ameteuliwa leo Alhamisi Agosti 12 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, jijini Dar es Salaam.

Pamoja na Steve, wengine walioteuliwa ni Mwanaharakati wa Kutetea Haki za Wanawake nchini, Joyce Kiria na Mbunge wa Viti Maalumu, Neema.

Tangu janga la Uviko 19 liibuke tena nchini mwaka huu, Steve ameonyesha kupambana na janga hilo huku akihamasisha Watanzania kupata chanjo ili kujikinga dhidi ya ugonjwa huo hatari duniani.

PETER BANDA APEWA JEZI YA MIQUISSONE

 


Mchezaji mpya wa klabu ya Simba Peter Banda amekabidhiwa jezi namba 11 ambayo hapo awali ilikuwa ikitumiwa na Luis Miquissone ambaye anahusishwa kujiunga na miamba ya soka barani Afrika klabu ya Al Ahly ya huko Misri. 

Banda alijiunga na wekundu wa Msimbazi mwezi Agosti 3 mwaka huu akitokea Nyasa Big Bullets ya nchini Malawi kwa mkataba wa miaka mitatu.

 Mabingwa hao wa Tanzania hivi sasa wapo nchini Morocco ambako wameweka kambi yao kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya ujao.

MADIWANI HALMASHAURI YA WILAYA YA BABATI WALIA UBAKAJI, ULAWITI.



Na John Walter-Babati.

Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Babati mkoani Manyara, wamekemea vikali vitendo vya matukio ya ubakaji na ulawiti vinavyotokea  katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na kuitaka jamii kufichua watu wanaojihusisha na uovu huo.

Hayo yamejiri katika baraza la madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Babati, ambapo Diwani wa kata ya Dareda  Eluthery Joseph Burra amesema kuwa vitendo  hivyo vinapaswa kukemewa vikali kwani kwa hivi sasa vitendo hivyo vimekithiri katika kata yake.

Burra amesema katika kata yake ya Dareda na maeneo jirani sio watoto pekee yao hata wanaume  nao wanakumbwa na vitendo hivyo.

“Kwa Dareda sasaivi tuna kesi ambazo aidha zimeripotiwa polisi au ambazo zipo mafichoni,kuna kesi zaidi ya tatu ndani ya muda mfupi”alisema Burra

Amewataka maafisa ustawi wa jamii kufanya mikutano na wananchi mara kwa mara kutoa elimu kwani wamechoka kusikia malalamiko ya wananchi kuhusu ubakaji na ulawiti.

Diwani wa viti maalum Mariamu Kwimba  amesema Ukatili wa kijinsia umezidi kushika kasi haswa katika kata za Dareda,Dabil,Magugu na Galapo na linafanywa na wanaume ambapo wahanga ni watoto na wanawake huku watoto wa kiume wakilawitiwa.

Amesema wajibu wao kama viongozi  ni kutoa elimu katika maeneo yao kupitia vikao na mikutano ya hadhara ili kukomesha ukatili huo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Babati John Noya amesema mikutano ya hadhara itafanyika ka kushirikisha maafisa ustawi,viongozi wengine na  polisi kata wa eneo husika.

Amesema jamii ielimishwe juu ya athari ya vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia pamoja na kuwatumia wazee wa kimila katika kutokomeza vitendo hivyo.

RAIS WA MADAGASCAR ALIVUNJA BARAZA LA MAWAZIRI

 

 Rais wa Madagascar Andry Rajoelina amelivunjilia mbali baraza lake la mawaziri.

Ofisi yake haikutoa sababu, lakini Jumapili Bw Rajoelina alisema kutakuwa na hali ya kushindwa ndani ya serikali - "kama katika timu ya mpira wa miguu" - mabadiliko yangehitajika.

Kufutwa kwa baraza hilo kumekuja baada ya ripoti za njama iliyofeli ya kumuua rais ambaye ni kiongozi wa zamani wa mapinduzi huko Madagascar.

Zaidi ya washukiwa 20 - wakiwemo 12 kutoka kwenye jeshi - wamekamatwa. Bwana Rajoelina alikua rais wa kisiwa hicho miaka miwili iliyopita - baada ya mzozo wa kisheria uliogubika uchaguzi huo.

Tuesday, August 10, 2021

UTEUZI WA WANASHERIA WA KUSIKILIZA KESI YA DHULUMA ZA KINGONO DHIDI YA MSANII R.KELLY WAANZA.

 

Msanii wa R&B R. Kelly amefika mahakamani mjini New York,huku uteuzi wa wanasheria katika kesi ya dhulma za kingono dhidi yake ukianza.

Inajiri zaidi ya miaka miwili baada ya msanii huyo kushtakiwa kwa unyanyasaji wa wanawake na wasichana wadogo kwa karibu miongo miwili.

Mwimbaji huyo aliyeshinda Tuzo ya Grammy anakabiliwa na mashtaka ya unyanasaji wa kingono dhidi ya watoto, ujambazi na rushwa. Amekanusha mashtaka

Wanasheria wanaotarajiwa kuongoza kesi hiyo wanahojiwa ikiwa wanaweza kuwa na mawazo huru katika kesi hiyo.

Baada ya majaji kuteuliwa, kesi inatarajiwa kuanza Agost18 na huenda ikaendelea kwa wiki kadhaa.Msanii huyo mwenye umri wa miaka 54 akipatikana na hatia huenda akafungwa jela kwa miongo kadhaa.

Kesi dhidi yake pia imewasilishwa katika mahakama ya Illinois na Minnesota.

Alipoulizwa jinsi anavyojihisi,wakili wa Kelly,Deveraux Cannick aliliambia shirika la Habari la AFP: "Ni sawa na Jumatatu nyingine."

Kelly, mmoja wa wasanii nyota wa miondoko ya R&B miaka ya1990, amekuwa akizuiliwa tangu Julai mwaka 2019.

Kesi ya New Yorki inamtuhumu mwimbaji huyo–ambaye jina lake halisi ni Robert Kelly –kwa kuongoza kundi la mameneja , walinzi wa kibinafsi na wengine ambao waliwaanda wanawake na wasichana kwa ajili ya kufanya ngono.

Waendesha mashtaka wanasema wahasiriwa waliteuliwa katika matamasha na maeneo mengine.

DEREVA ALIYEUWA WANAFUNZI WAWILI AAGIZWA KUJISALIMISHA.

 


Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limemtaka dereva aliyesababisha ajali iliyoua wanafunzi wawili katika barabara ya Bagamoyo, maeneo ya Afrikana stendi ya daladala, Wilaya ya Kinondoni kujisalimisha haraka iwezekanavyo kituo chochote cha Polisi kilichopo karibu naye.


Ajali hiyo iliyotokea leo Agosti 9, 2021, majira ya saa 11:15 alfajiri, ambapo gari yenye namba za usajili T 274 CBX liliwagonga wanfunzi waliofahamika kwa majina ya Collins Obed Ngowi (15) Mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya Sekondari Makongo na Salvina Odoro Otieno Mwanafunzi wa darasa saba Shule ya Msingi Mount Sery wote wawili walifariki dunia, huku mwanafunzi Ashura wa kidato cha tano shule ya Sekondari Al-haramain akipata majeraha sehemu za mwili na alikimbizwa hospitalini.


Jeshi la Polisi limeeleza kuwa dereva huyo alikimbia mara baada ya tukio kutokea hivyo kumtaka ajisalimishe kwani hana uwezo wa kujificha zaidi ya muda wa saa 48.


Hata hivyo chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa gari hilo lililohusika katika ajali.

SIMBA KUWEKA KAMBI MOROCCO

 


 Klabu ya Simba itakwea pipa kuelekea nchini Morocco kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya 2021/22
 

"Morocco ndio nchi ambayo mabingwa wa nchi tutaweka kambi kujiandaa na msimu mpya wa 2021/22" Simba SC

Simba na Yanga zote zitakuwa ndani ya Morocco kujiandaa na msimu mpya wa mashindano ya klabu bingwa na kuliwinda kombe la Ligi Kuu, Simba akitaka kuweka historia ya kunyakuwa kombe hilo mara 5 mfululizo na Yanga wenye hasira ya kulikosa kombe hilo mara 4 mfululizo.

KISA CHA KWANZA CHA KIRUSI CHA MARBURG CHAGUNDULIKA GUINEA.

 


Guinea imethibitisha kisa cha ugonjwa wa Marburg, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kirusi hicho hatari kinachohusiana na Ebola kutokea Afrika Magharibi. 
 
Kama tu ilivyo kwa ugonjwa wa COVID-19, kirusi hicho kinatoka kwa mnyama na kuingia kwa binaadamu. Shirika la Afya Ulimwenguni - WHO limesema kirusi hicho kinabebwa na popo na kina kiwango cha vifo cha hadi asilimia 88, kilipatikana kwenye sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa mgonjwa mmoja aliyefariki Agosti 2 katika eneo la kusini mwa Guinea la Gueckedou. 
 
Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika Matshidiso Moeti amesema uwezekano wa kirusi cha Marburg kusambaa hadi maeneo ya mbali una maana wanahitaji kukizuia mapema. 
 
Ugunduzi huo unakuja miezi miwili tu baada ya WHO kutangaza kumalizika kwa mripuko wa pili wa Ebola nchini Guinea, ambao ulianza mwaka jana na kuwauwa watu 12.