ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, August 12, 2021

MADIWANI HALMASHAURI YA WILAYA YA BABATI WALIA UBAKAJI, ULAWITI.



Na John Walter-Babati.

Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Babati mkoani Manyara, wamekemea vikali vitendo vya matukio ya ubakaji na ulawiti vinavyotokea  katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na kuitaka jamii kufichua watu wanaojihusisha na uovu huo.

Hayo yamejiri katika baraza la madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Babati, ambapo Diwani wa kata ya Dareda  Eluthery Joseph Burra amesema kuwa vitendo  hivyo vinapaswa kukemewa vikali kwani kwa hivi sasa vitendo hivyo vimekithiri katika kata yake.

Burra amesema katika kata yake ya Dareda na maeneo jirani sio watoto pekee yao hata wanaume  nao wanakumbwa na vitendo hivyo.

“Kwa Dareda sasaivi tuna kesi ambazo aidha zimeripotiwa polisi au ambazo zipo mafichoni,kuna kesi zaidi ya tatu ndani ya muda mfupi”alisema Burra

Amewataka maafisa ustawi wa jamii kufanya mikutano na wananchi mara kwa mara kutoa elimu kwani wamechoka kusikia malalamiko ya wananchi kuhusu ubakaji na ulawiti.

Diwani wa viti maalum Mariamu Kwimba  amesema Ukatili wa kijinsia umezidi kushika kasi haswa katika kata za Dareda,Dabil,Magugu na Galapo na linafanywa na wanaume ambapo wahanga ni watoto na wanawake huku watoto wa kiume wakilawitiwa.

Amesema wajibu wao kama viongozi  ni kutoa elimu katika maeneo yao kupitia vikao na mikutano ya hadhara ili kukomesha ukatili huo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Babati John Noya amesema mikutano ya hadhara itafanyika ka kushirikisha maafisa ustawi,viongozi wengine na  polisi kata wa eneo husika.

Amesema jamii ielimishwe juu ya athari ya vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia pamoja na kuwatumia wazee wa kimila katika kutokomeza vitendo hivyo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.