ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, January 30, 2026

SHABIKI KINDAKINDAKI WA MAN CITY ATUA SERENGETI

 


𝗛𝗔𝗧𝗜𝗠𝗔𝗬𝗘 ile kiu na ndoto ya kuitembelea Tanzania imetimia kwa mwanahabari wa michezo na shabiki sugu wa klabu ya Manchester City ya nchini Uingereza, Braydon Bent.

.
Akiwa katika ziara ya kitalii ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, picha na video za Braydon zimekuwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii, zikimuonesha akifurahia kwa karibu vivutio mbalimbali vya wanyamapori pamoja na mandhari ya kuvutia yanayoburudisha macho na kuigusa roho.
.


Katika safari hiyo, Braydon ameambatana na rafiki yake wa muda mrefu na mwalimu wake wa lugha ya Kiswahili, ambaye pia ni mwanahabari na mtangazaji wa kujitegemea, John Jackson maarufu kama JJ. @johnjackson_jj 
.



Kupitia ujumbe aliouandika kwenye mitandao yake ya kijamii, Braydon aliandika:-

“LIONS 🦁 & HOT AIR BALLOON IN SERENGETI 🎈🇹🇿
ASANTE SERENGETI ☀️
SERENGETI NI NOMA! 🇹🇿
DAY 2 @serengeti_national_park
.
Safari hiyo imeendelea kuonesha jinsi Tanzania inavyoendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii wa kimataifa, huku Serengeti ikiendelea kuthibitisha hadhi yake kama moja ya hifadhi bora zaidi duniani.
.
📸 Captures by @infocusstudio.tz

CC: @braydonbentpage

#visittanzani
#visitzanzibar






Thursday, January 29, 2026

SIMBA YAIKUNYUGA MASHUJAA 2-0

 


TIMU ya Simba SC imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa FC ya Kigoma katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.

Mabao ya Simba SC leo yamefungwa na winga mpya wa kushoto, Libasse Gueye (22) aliyesajiliwa mwezi huu katika dirisha dogo kutoka Teungueth FC ya kwao, Senegal dakika ya 27 na mshambuliaji Suleiman Abdallah Mwalimu 'Gomez' anayecheza kwa mkopo tangu mwanzo wa msimu kutoka Wydad Athletics dakika ya 76.

Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 16 katika mchezo wa saba na kusogea nafasi ya nne, wakati Mashujaa FC inabaki na pointi zake 13 za mechi 11 sasa nafasi ya nane.

Baada ya mchezo huo, Simba SC inarejea kambini kujiandaa na mchezo wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Espérance ya Tunisia Jumapili kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Ili kufufua matumaini ya kwenda Robo Fainali, Simba inahitaji kushinda Jumapili ikitoka kufungwa mechi zote tatu za mwanzio ikiwemo ya Jumamosi ambayo walifungwa 1-0 na Espérance Uwanja wa Hammadi Agrebi Jijini Tunis nchini Tunisia.

Bao lililoizamisha Simba SC siku hiyo lilifungwa na winga chipukizi wa umri wa miaka 19 wa Burkina Faso, Jack Diarra dakika ya 21 akimtungua kipa wa Kimataifa wa Niger, Mahamadou Tanja Djibrilla Kassali Djibo.

TFF YALIFUNGIA DIMBA LA KMC

 


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeufungia Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, maarufu kama KMC Complex, uliopo Mwenge Jijini Dar es Salaam kutotumika kwa mechi za Ligi Kuu kufuatia kupoteza sifa za kikanuni.

Taarifa ya TFF iliyotolewa leo ikiwa na saini ya Meneja Habari na Mawasiliano wa shirikisho hilo, Clifford Mario Ndimbo imezielekeza klabu zinazotumia Uwanja huo mwingine hadi hapo KMC Complex itakapofunguliwa tena baada ya mapungufu yaliyoibainika kufanyiwa marekebisho.

Mbali na wenye mali yao, KMC FC timu nyingine ambayo inatumia Uwanja huo rasmi kama wa nyumbani ni mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kwa miaka minne mfululizo, Yanga SC walioanza kuutumia msimu uliopita. 

WAFANYABIASHARA WAONYWA UPANDISHAJI BEI KIPINDI CHA RAMADHANI


Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amewataka wafanyabiashara nchini kutowaumiza Watanzania kwa kupandisha bei za bidhaa hususani kipindi hiki cha kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani pamoja na mfungo wa Kwaresma kwa kuwa nchi kwa sasa haina upungufu wa chakula.


Amesema licha ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) nchini kutangaza kuwepo kwa upungufu wa mvua katika maeneo mengi nchini lakini nchi inautoshelevu wa chakula hivyo hakuna sababu ya kupandisha bei za vyakula.


Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Januari 29, wakati akijibu swali la Nancy Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. 


Mbunge huyo alitaka kujua Serikali imejipangaje kuhakikisha nchi inakuwa na utoshelevu wa chakula na kuzuia mfumuko wa bei kuelekea kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Kwaresma.


“…Kwa sasa tuna chakula cha kutosha, mahitaji ya chakula cha akiba kwa nchi ni takribani tani 150,000 na sasa nchi ina zaidi ya tani 400,000 za akiba ya chakula rai ambayo niliitoa hata nilipokutana na wakuu wa mikoa ni kuendelea kuwahamasisha wananchi  kuzingatia ushauri wa aina ya mazao ya kupanda.”


Pia, Waziri Mkuu amewaelekeza Wakuu wa Mikoa yote nchini wawaelimishe wananchi kuendelea kutumia vizuri chakula walichonacho kutokana na tahadhari ya upungufu wa mvua iliyotolewa na TMA. 


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Afya kuzingatia viwango rasmi vya gharama za huduma na kuharakisha mpango wa kutunga sheria itakayoweka viwango vinavyofanana nchini kote, ili kuondoa hali ya baadhi ya maeneo kuwa na viwango tofauti.


Ametoa maelekezo hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani ambaye alitaka kupata kauli ya Serikali kuhusu viwango wanavyotozwa wananchi kama gharama ya kumuona daktari ambaye ni mwajiriwa na analipwa mshahara na Serikali.

Waziri Mkuu amesema kwa mujibu wa utaratibu wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote, wananchi wanahimizwa kujiunga na mifumo ya bima ili kupunguza changamoto ya kuchangia gharama wanapohitaji huduma hospitalini.

Wednesday, January 28, 2026

DEPU AFUNGA MAWILI YANGA YAICHAPA DODOMA JIJI FC 3-1 MWENGE

 


MABINGWA watetezi, Young Africans, maarufu tu kama Yanga SC wametoka nyuma na kushinda mabao 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara uliochezwa jana usiku katika  Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

Mabao Yanga SC yamefungwa na washambuliaji wake wa kigeni, Muangola Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’ mawili kwa penalti dakika ya 45’+2 na la kichwa dakika ya 60 na Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo dakika ya baada ya 66, na hiyo ilikuwa baada ya mshambuliaji mzawa, William Edgar kuanza kuifungia Dodoma Jiji FC dakika ya 41 akiwatoka kwa ustadi mkubwa mabeki wa Yanga kabla ya kumtungua kipa namba moja wa Mali, Djigui Diarra.


Kwa ushindi huo, Yanga SC wanafikisha pointi 22 katika mchezo  wa nane na kurejea kileleni ikiishushia nafasi ya pili JKT Tanzania yenye pointi 21 za mechi 12.


Kwa upande wao Dodoma Jiji baada ya kupoteza mchezo huo wanabaki na pointi 10 za mechi 10 nafasi ya 11.


Baada ya mchezo huo Yanga wanakwenda Zanzibar kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri Jumamosi ya Januari 31 Uwanja wa New Amaan Complex.


Ikumbukwe Yanga ilichapwa 2-0 na wenyeji, Al Ahly Ijumaa ya Januari 23 mabao ya winga wa kushoto, Mahmoud Ahmed Ibrahim Hassan ‘Trézéguet’ moja kila kipindi, dakika ya 45’+3 na 75 Ijumaa usiku huu Uwanja wa Borg El Arab Jijini Alexandria, Misri.