ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, May 12, 2022

WAZIRI WA MAJI JUMAA AWESO ATINGA BUNGENI NA WAKE ZAKE WAWILI.....'HAYA NI MAHABA MAZITO SANA'


 Waziri wa Maji Jumaa Aweso, akiwa na wake zake

Waziri wa Maji Jumaa Aweso, amesema kwamba ushirikiano anaopewa na wake zake wawili hauoneshi tu kama ni mapenzi bali ni mahaba mazito na kwamba hata kuchakarika kwake kunatokana na ukaribu wao kwake.


Kauli hiyo ameitoa hii leo Mei 12, 2022, Bungeni Dodoma, wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2021, ambapo wake zake wote wawili wamehudhuria bungeni kumshuhudia.


"Leo wake zangu wote wawili wamekuja hapa kuni-support haya sio mapenzi haya ni mahaba mazito sana, mimi ninawapenda sana ukiniona nachakarika ni kwa sababu ya ukaribu wao na ushirikiano mkubwa wanaonipa, mimi Jumaa Aweso nitaendelea kuwapenda sana wake wangu," amesema Waziri Aweso

Wednesday, May 11, 2022

RC SENDIGA ATOA SIKU SABA KWA MKANDARASI PRIPAM KURUDIA UPYA UJENZI WA BARABARA YA ZIZILANG’OMBE NGEREWALA

 

Mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga akiwa kwenye ukaguzi wa barabara zaTARURA manispaa ya Iringa
Barabara ambazo mkuu wa mkoa wa Iringa alikuwa analalamikia kuwa zimejengwa chini ya kiwango
Barabara ambazo mkuu wa mkoa wa Iringa alikuwa analalamikia kuwa zimejengwa chini ya kiwango

Mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga akiwa kwenye ukaguzi wa barabara zaTARURA manispaa ya Iringa

 Na Fredy Mgunda, Iringa.

Mkuu wa mkoa wa Iringa ametoa siku saba kwa mkandarasi Pripam kurudia upya ujenzi wa barabara ya Zizilang’ombe Ngelewala kwa kujenga chini ya kiwango na kusababisha barabara hiyo kuweka nyufa mwezi mmoja tu toka kukamilika kwake.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa barabara za TARURA Manispaa ya Iringa,mkuu wa mkoa Queen Sendiga alisema kuwa hawezi kufarahishwa hata kidogo akikuta barabara imejengwa chini ya kiwango tofauti na thamani ya fedha iliyotolewa kwa mkandarasi.

Sendiga alisema kuwa haiwezekani barabara nyingi za manispaa ya Iringa zimejengwa kwa kiwango kizuri ispokuwa baarabara ya Zizilang’ombe Kitasengwa kwa kuwa imeanza kupasuka mapema jambo ambalo linaashiria kuwa barabara hiyo imejengwa chini ya kiwango.

Aliwataka wataalam Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini wilaya ya Iringa kuhakikisha wanawasimamia vilivyo wakandarasi ambao wanakuwa wamepewa tenda za ujenzi wa barabara wanajenga kwa ubora unaotakiwa kulingana na thamani ya fedha ambayo imetolewa kutoka serikalini.

Sendiga alisema kuwa baada ya siku saba atafanya ziara kukagua barabara hiyo kama imejengwa kwa kiwango kinachotakiwa kulingana na f thamani ya fedha ambayo imetolewa na serikali la sivyo mkandarasi atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Sijaridhishwa na ujenzi wa barabara inayotoka Zizi la Ng'ombe kuelekea Ngelewala Manispaa ya Iringa.Nimetoa siku saba kwa mkandarasi kuijenga upya kwa gharama zake na katika ubora unaotakiwa.” Alisema Sendiga

Aliwaambia wataalam wa TARURA wilaya ya Iringa kufanya kazi kwa weredi unaotakiwa ili kuiondolea serikali sitofahamu inayokuwa inaendelea kwenye mitandao ya kijamii juu ya ubovu wa barabara zinazojengwa katika wilaya ya Iringa.

Sendiga alimalizia kwa kuwapongeza viongozi wa TARURA Iringa kwa kazi wanayoifanya isipokuwa mradi mmoja wa barabara ya Zizilang’ombe Ngelewala ambao umeweka doa la mkoa kwa video za nyufa za barabara hiyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

 

Kwa upande wake meneja wa TARURA mkoa wa Iringa Makori George Kisare alisema kuwa wameyapokea mawazo na maagizo yote ya mkuu wa mkoa na watayafanyia kazi haraka ipasavyo kama alivyo agiza.

Akizungumzia swala la kupasuka kwa barabara ya Zizilang’ombe Ngelewala alisema kuwa mkandarasi anawajibu wa kurudia kwa gharama zake kwa kuwa yeye ndio aliyefanya kosa hilo la kiufundi.

 

Alisema kuwa watahakikisha wanamsimamia ndani ya siku hizo saba anafanya marekebisho yanayotakiwa kwenye barabara hiyo.

MSIGWA-SERIKALI IPO KWENYE MAZUNGUMZO NA WAWEKEZAJI JUU YA UJENZI WA BANDARI YA BAGAMOYO

 

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo,Gerson Msigwa akizungumza  wakati wa ziara ya Maafisa Habari wa Wizara na Taasisi za Umma nchini  katika Bandari ya Tanga ambao wapo Jijini Tanga wakiendelea na kikao chao
Sehemu ya Maafisa Habari wa Wizara na Taasisi za Umma wakiwa kwenye Bandari ya Tanga wakati wa ziara hiyo

NA OSCAR ASSENGA,TANGA.

SERIKALI ipo na mazungumzo na  wawekezaji juu ya mpango wa ujenzi wa Bandari mpya ya Bagamoyo  mkoani Pwani ili kusogeza huduma karibu na wananchi na hivyo kuchangia kukuza pato la Taifa na wananchi kwa ujumla.

Hayo yalisemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo,Gerson Msigwa wakati wa ziara ya Maafisa Habari wa Wizara na Taasisi za Umma nchini  katika Bandari ya Tanga ambao wapo Jijini Tanga wakiendelea na kikao chao

Alisema kwa sasa wamerejesha mazungumzo hayo baada ya Rais Samia Suluhu kupitia serikali yake ya awamu ya sita kuona ni vyema wakarejesha mazungumzo hayo na kukubaliana maeneo serikali itayoona ina maslahi nayo pamoja na wawekezaji ili wautekeleze mradi huo. 

Alisema huo mradi huo ni mkubwa na wakifanikiwa kuutekeleza  utasaidia kuchochea kasi ya maendeleo na hivyo kuchangia pato la wananchi na Taifa kwa ujumla ikiwemo kufungua milango ya uwekezaji hapa nchini. 

Alisema sio Bandari bali patajengwa Viwanda, kwasababu eneo hilo wanakusudia kulifanya liwe kanda maalumu ya kiuchumi ya Bagamoyo  pale panajengwa bandari, Viwanda, eneo la makazi ,maduka makubwa na sehemu nyingi za kibiashara ikiwemo ujenzi wa viwanda takribani 1000 na hivyo itawezesha kuwa kanda maalumu ya viwanda. 

Akizungumzia ujenzi wa Bandari unaoendelea katika Mikoa ya Dar es Salaam,  Tanga na Mtwara Msigwa alisema wamewapeleka maafisa habari wa serikali ili waone kazi kubwa inayotekelezwa na serikali ili wananchi wanapotaka kujua nini serikali inafanya katika fursa ya uchumi wa bluu  ili wajue kwamba kuna kazi kubwa inayofanyika. 

"Niwaambie kwamba hii moja kati ya kazi kubwa ambazo zinafanyika hapa Tanga lakini pia tunafanya kazi kama hizi kwenye maziwa yetu ikiwemo Kigoma, Kalema kule kwenye ziwa Tanganyika,  Ziwa Victoria pia pale Mwanza tumejenga cholezo kubwa na ujenzi wa meli unaendelea kule kwa hiyo kuna kazi nyingi serikali inafanya,kwenye maeneo haya na tungependa maafisa habari wetu wajionee wao wenyewe na kupeleka huu ujumbe mzuri kwa wananchi, "Alibainisha Msigwa. 

Akizungumzia miundombinu ya reli Msigwa alisema serikali imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha treni zinarejea Mkoani Tanga mpaka Arusha ambapo hivi sasa kazi inayokwenda kufanyika ni ya kuimarisha miundombinu hiyo na kuona namna bora ya kuja na reli nzuri zaidi. 

Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo,Mhandisi wa bandari ya Tanga Hamis Omari Kipalo amesema kwa upande wa ujenzi wa gati namba moja na namba mbili katika bandari hiyo umefikia asilimia 45 mpaka sasa. 

Mhandisi huyo alisema mradi wao kimkataba unatakiwa kukamilika tarehe 16 mwezi octoba mwaka huu. 

Baadhi ya maafisa habari waliotembelea bandarini hapo wamesema ziara hiyo imewasaidia kuona namna serikali ilivyojizatiti kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo. 

David Mwaipaja ni Afisa mahusiano na mauzo kutoka Watumishi Housing Investment amesema kuwa serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika bandari zetu ambazo zipo kwenye miradi ya kimkakati jambo ambalo litakuwa chachu kwa maafisa habari kuchukua na kwenda kuisemea serikali kwa wananchi ili mambo yasiyoonekana kiurahisi kwa wananchi basi yaweze kuwafikia sawasawa na serikali inavyofanya. 

Upanuzi wa ujenzi wa mradi wa gati za kisasa katika bandari nchini unatarajiwa kufungua fursa za kibiashara ambapo ujenzi huo umefanyika katika Mikoa ya Tanga,  Mtwara na Daresalaam. 

Kwa upande wa bandari ya Daresalaam jumla ya shilingi trilioni moja nukta mbili zinatarajiwa kutumika kwajili ya ujenzi wa gati sambamba na kununua vifaa vitakavyorahisisha utoaji wa huduma ikiwemo upakuaji wa shehena.