Ajali na magonjwa ya afya ya akili vimetajwa kuwa sehemu ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs).
Ni katika kongamano la nne la kisayansi la magonjwa yasiyoambukiza lililofanyika jana jijini Mwanza.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa kongamano hilo, Profesa Paschal Ruggajo, mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Tiba katika Wizara ya Afya alisema ajali zinagharimu maisha ya watu wengi na ugonjwa wa afya ya akili unaathiri jamii.
“Ni vema tutambue kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanaenda sambamba na ajali na ugojwa wa afya ya akili. Ni vema kuweka mkazo kwenye kupunguza magonjwa haya bila kuyaacha nyuma ili kupata suluhu ya pamoja,” alisema Profesa Ruggajo.
Ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza limechochewa na vihatarishi vinavyorekebishika, ambavyo ni mitindo isiyofaa ya maisha kama matumizi ya tumbaku, lishe duni, matumizi ya pombe kupita kiasi, kutoushughulisha mwili au kutofanya mazoezi ya viungo mara kwa mara bila kusahau unene uliokithiri.
Alisema utafiti wa mwaka 2018 unaonyesha hapa nchini watu wazima milioni 2.6 sawa na asilimia 8.7 wanatumia tumbaku, huku utafiti wa mwaka 2012 ukionyesha matumizi ya pombe kupita kiasi ni asilimia 29.3 na kuna asilimia 34.7 ya watu wenye unene uliokithiri.
Ingawa takwimu za polisi, kitengo cha Usalama Barabarani zinaonyesha kupungua kwa ajali za barabarani 2021 licha ya madhara ya ajali hizo hususani majeruhi, hali bado ni mbaya na madhara yake kwa jamii ni makubwa.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, ajali za barabarani zilizorekodiwa zilifikia 1,864 mwaka 2021, ukilinganisha na 1,933 mwaka 2020.
Mwaka 2021 ajali hizo zilisababisha vifo vya Watanzania 1,368 na majeruhi 2,452, wakati 2020 kulikuwa na vifo 1,384 na majeruhi 2,362.
Ukiacha ajali, Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022 ilihudumia wagonjwa 28,325, kati yao 26,761 ni wagonjwa wa akili wa nje na wa ndani ni 1,564.
Wagonjwa wa msamaha waliopewa huduma walikuwa 3,985, ambao waliigharimu hospitali Sh60,2 milioni katika kipindi hicho.
Hali ikiwa hivyo, kwa ujumla magonjwa yasiyoambukiza yanazidi kuwa mzigo kwa taifa.
Agosti mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga alisema mfuko huo kwa mwaka 2021/22 ulitumia Sh99.09 bilioni kulipia huduma zilizotolewa kwa wagonjwa hao.
Kongamano kuhusu magonjwa hayo lilizinduliwa na Profesa James Mdoe, naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia aliyesisitiza juu ya umuhimu wa wanasayansi kufanya utafiti kwenye dawa za asili na endapo itathibitika kuwa ziko sawa zianze kutumika kwenye hospitali zetu.
Pia afya ya akili ikiwa ni kundi la magonjwa yasiyoambukiza, kwa takwimu za Ofisi ya Rais (Tamisemi), inakadiriwa Tanzania kuwa na wagonjwa milioni saba wenye matatizo na wengi wao wanaishi na sonona.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO zinaonyesha kuwa katika mwongo mmoja uliopita, kumekuwa na ongezeko la watu kwa asilimia 13, ambapo watu bilioni 1 wanaishi na tatizo hilo duniani.
Ajali, kundi lingine la magonjwa yasiyo ya kuambukiza, zinaelezwa na WHO kuwa kwa mwaka zinachukua uhai wa watu milioni 1.35 na wengine milioni 20 hadi 50 wakiachwa na majeraha na ulemavu wa kudumu.
Takwimu hizo zinaonyesha asilimia 74 ya watu duniani wanapoteza maisha kutokana na magonjwa yasiyoambukiza na asilimia 33 ya Watanzania wanapoteza maisha kwa magonjwa hayo ambayo idadi ya waathirika wake inaongezeka.
Katika kongamano hilo la kisayansi linalofanyika kwa wiki moja, kutakuwa na shughuli mbalimbali za kiafya zitakazohusisha upimaji wa afya bure kwenye viwanja vya CCM Kirumba.
Kongamano hilo limewaleta pamoja wadau mbalimbali wa afya zaidi ya 400 na litajadili mada mbalimbali za kitaaluma na kutoa matokeo ya tafiti mbalimbali za kiafya.
Pamoja na mada nyingine, mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza kusini mwa Jangwa la Sahara na madhara ya mabadiliko ya tabianchi itakuwa miongoni.
Mada hii itawasilishwa na Profesa Harold Renz, Profesa wa dawa katika Chuo Kikuu cha Marburg Ujerumani.
Na mada nyingine ni magonjwa yasiyoambukiza kwa watoto na vijana; asiachwe mtu nyuma, itakayowasilishwa na Profesa Francis Furia wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Muhimbili.