ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, May 10, 2024

MANISPAA YA IRINGA KUNOGILE YAFANYA KWELI USAFI WA MAZINGIRA KITAIFA


NA VICTOR MASANGU, KIBAHA


Manispaa ya Iringa Mkoa wa Iringa licha ya kushika nafasi ya tatu kitaifa  katika mashindano ya kampeni ya mtu ni afya awamu ya pili imeahidi kuyatekeleza maagizo ambayo yametolewa na Makamu wa Rais Dkt. Philipo Mpango kwa lengo la kuweza kuhakikisha inazingatia usafi wa mazingira ili kuweza kupambana na mlipuko wa magonjwa. 

Hayo yamebainishwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahimu Ngwada wakati akizungumza na waandishi wa bahari mara baada ya kupokea cheti na kiasi cha shilingi  milioni moja baada ya kushinda katika nafasi ya tatu kwa katika manispaa ambazo ziliweza kufanya vizuri katika suala zima la usafi wa mazingira.

Meya huyo alieleza kwamba siri kubwa ya kuweza kushika nafasi ya tatu katika nchi nzima na kwa ajili ya kuwa na utamaduni wa wananchi wa Iringa waliojiwekea katika kuweka utaratibu wa kufanya zoezi la usafi katika maeneo mbali mbali ambayo yameweza kupelekea kila mwaka kufanya vizuri katika mashindano hayo.

"Utamaduni wetu kwa watu wa manispaa ya Iringa pamoja na Mkoa mzima ni kuhakikisha kila
msimu wa mashindano hayo ya kampeni hii ya usafi tunafanya vizuri na kuwa washindi kwa hii kwa upande wangu ninawaahidi katika msimu ujao pia tutaweza kufanya vizuri kwani tutazingatia yale yote  ambayo yametolewa na Makamu wa Rais,"alisema Meya huyo.

Pia alishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kushirikiana na Wizara ya afya kwa kuanzisha kampeni hiyo ambayo imeweza kusaidia kwa kiaisi kikubwa katika kupambana na usafi wa mazingira ambao unasaidia hata kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Sambamba na hilo alibainisha kwamba mpaka kufikia hatua hiyo ya kushinda nafasi ya tatu kwa ngazi ya Taifa ni kutokana na kuweka mipango madhubuti katika maeneo mbali mbali ikiwemo kuweka sehemu maalumu kwa ajili ya kutupia taka katika kila mtaa pamoja na sehemu za kunawia mikono katika maeneo mbali mbali ya mikusanyiko kama vile mashuleni, hospitalini pamoja na kwingine ikiwa sambamba na kuzingatia taratibu  na maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu wa afya.

Katika hatua nyingine Meya huyo alitoa wito kwa wananchi wote wa Manispaa ya Iringa lengo ikiwa ni kupunguza magonjwa ya matumbo ambayo kwa sasa amesema yameshuka kwa kiwango kikubwa na kuwahimiza kuendelea kufanya usafi katika maeneo ambayo wanaishi na sehemu nyingine za biashara.

Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Iringa Dkt. Godfrey Mbangali aliongeza kuwa kwa sasa kutokana na kujipanga wamefaanikiwa kwa kisi kikubwa kupunguza magonjwa ya kuharisha ndio maana wameweza kupata ushindi huo wa nafasi ya tatu kwa nchi nzima.

"Mimia kama Mganga mkuu wa Manispaa ya Iringa tumejitahidi sana kwa hali na mali mimi pamoja na timu yangu kwa kuhakikisha kwamba tunapambana na magonjwa mbali mbali ya mlipuko ikiwemo matumbo pamoja na kuharisha na kiukweli mashidano hayo yanafanyika kisayansi zaidi na ndio maana sisi tumeshika nafasi hii ya tatu kwa kuzingatia vigezo ambavyo vinatakiwa na kwa sasa ukiangalia magonjwa ya mlipuko yamepungua sana,"alisema Mganga huyo.

Kwa upande wake Makamu wa Rais , Dkt Philipo Mpango ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alizitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha wanaweka mifumo mizuri katika maeneo yao ambayo itaweza kusaidia katika suala zima la kuboresha  usafi wa mazingira na kupambana na magonjwa ya mlipuko.

Kadhalika Waziri Mpango alipongeza makundi, taasisi, halmashauri, manispaa, pamoja na mikoa mbali mbali ambayo imeweza kufanya vizuri katika mashindano hayo na kuwataka kuendelea kushirikiana na ngazi zote pamoja na wananchi lengo ikiwa ni  kutomomeza kabisa magonjwa ya mlipuko amabayo wakati mwingine yanatokana na baadhi ya maeneo kuwa machafu.

Kwa upande wake Waziri wa afya Mhe. Ummy Mwalimu alisema kwamba serikali ilishaanza kuchukua hatua mbali mbali kwa ajili ya kudhibiti na kuboresha huduma za afya nchini na kufanikiwa kupunguza na kutokomeza baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Alisema alieleza kwamba kupitia kampeni hiyo ya mtu ni afya awamu ya pili benki ya dunia imetoa isi cha shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya utekelezaji huo ambao utafanyika kwa awamu kwa kipindi cha miaka saba.

Waziri Ummy katika hatua nyingine hakusita kuupongeza kwa dhati Mkoa wa Iringa ambao umeweza kuibuka mshindi wa kwanza katika mashindano ya usafi wa mazingira na matumizi  mazuri ya vyoo bora na kuweza kukabilina na magonjwa ya mlipuko na kuongeza kuwa Mkoa huo ndio umeshika nafasi ya kwanza kwa nchi nzima na kukabidhiwa zawadi mbali mbali ikiwemo gari mpya aina ya Land crucer.
 
Manispaa ya Iringa  iliyopo Mkoa wa Iringa imeweza kushika nafasi ya tatu kitaifa katika mashindano hayo ya usafi ya mazingira kwa kipengele cha Manispaa  huku Mkoa wa Iringa ukiibuka kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza nchi nzima kwa kipengele cha utunzani wa  mazingira matumizi bora ya vyoo.

Wednesday, May 8, 2024

MWENGE WA UHURU WARIDHISHWA NA MIRADI 26 YA MAENDELEO MKOA WA PWANI WAMPA KONGOLE RC KUNENGE

 


NA VICTOR MASANGU,DAR 

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka wa 2024 Godfrey Msava amewapongeza kwa dhati viongozi mbali mbali wa Mkoa wa Pwani kwa kuweza kuwa kitu kimoja katika kusimamia miradi mbali mbali ya maendeleo ambayo imempelekea kuridhishwa na  kuipitisha miradi 26 kati ya 28 iliyotembelewa.

Kiongozi huyo alibainisha kwamba amefurahishwa kuona ushirikiano mzuri alionao Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge pamoja na timu yake nzima ya wakuu wa Wilaya,wakurugenzi pamoja viongozi wengine kwa kuwapa ushirikiano katika kipindi chote walipokuwa katika kutembelea miradi mbali mbali.
"Tumetembelea miradi mbali mbali ya maendeleo katika Mkoa wa Pwani na nimefarijika kuona idadi kubwa tumeweza kuifungua na mingine kuiwekea mawe ya msingi lengo kubwa ni wananchi wetu waweze kupata huduma stahiki kwani Rais wetu anatoa fedha kwa ajili hiyo,"alisema Mzava.

Mzava aliyabainisha hayo leo wakati wa halfa fupi ya makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru ambao ulikuwa unatokea Wilayani Mafia na kukabidhiwa rasmi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.

"Nawashukuru sana kwa dhati viongozi wote wa Mkoa wa Pwani kwa kututunza tangu siku ya kwanza hadi hii leo hatuna budi kuondoka lakini kiukweli mmefanya kazi kubwa katika miradi yenu kwa hiyo niwapongeze sana Mkuu wa Mkoa na timu yako yote,"alisema Mzava.

Pia alisema katika Mkoa wa Pwani tangu wapokelewa wameweza kupata fursa ya kutembelea,kugagua na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo ambayo imeweza kugusa katika nyanja mbali mbali.

Pia aliwaomba viongozi kuendelea kusimamia fedha ambazo zinatolewa na Rais wa awamu ya sita na katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kuwakumbusha kuifanyia kazi miradi ambayo imeonekana kuwa na dosari.

 Awali Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge akisoma taarifa kwa kiongozi huyo alibainisha kwamba mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa zimeweza kukimbizwa katika Halmashauri tisa zilizopo katika Wilaya saba za Mkoa wa Pwani.

Kunenge alibainishwa kwamba katika Mbio hizo zimeweza kupita katika miradi 28 ambayo kati ya hiyo miradi 26 ya maendeleo  imeweza kupitishwa na miradi miwili haikuweza kupitishwa kutokana na kuwepo kwa baadhi ya  dosari  katika miradi miwili ambayo nayo itasimamiwa na kufanyiwa kazi.

Kadhalika Kunenge alifafanua kwamba miradi yote ambayo imepitiwa na mbio za Mwenge wa uhuru ina jumla ya thamani ya kiasi cha shilingi trilioni 8.5.

Pia Kunenge alimpongezs Rais wa awamu ya sita Dkt..
Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutafuta fedha mbali mbali pamoja na kushirikisha wadau kwa lengo la kuweza kuwaletea wananchi maendeleo.

Mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa ukiwa katika Mkoa wa Pwani umeweza kukagua,kuzindua,kuweka mawe ya msingi pamoja na kupitia miradi mbali mbali za maendeleo ikiwemo  afya,elimu, maji,barabara,rushwa,ukimwi,madawa ya kulevya,shughuli za kimaendeleo na mambo mengine ya kijamii.

Tuesday, May 7, 2024

MWENYEKITI WA CCM KIBAHA MJINI ASHUSHA NONDO KWA WENYEVITI NA MAKATIBU WA KATA


NA VICTOR MASANGU,KIBAHA 


Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha mjini Mwalimu Mwajuma Nyamka amewataka viongozi wa chama  kuhakikisha wanaweka misingi ya  kuwaheshimu  viongozi wote  waliopo madarakani na kuachana kabisa  na tabia ya  kutengeneza safu mpya  ya viongozi wapya  kabla ya muda kufika.

Mwalimu Nyamka ameyasema hayo wakati wa kikao kazi ambacho kiliweza kuwakutanisha Wenyeviti pamoja na makatibu wote wa CCM ngazi ya Kata  kutoka kata zote 14 za Halmashauri ya Kibaha mji lengo ikiwa kujadili mambo mbali mbali ikiwemo kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.

Alisema kwamba viongozi wq chama  wanapaswa kuwapa ushirikiano wa kutosha viongozi wote waliopo madarakani kuanzia ngazi za chini hadi za juu ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo bila ya kusumbuliwa kwani bado wapo madarakani.

"Tumekutana katika kikao kazi hiki na nimewakutanisha wenyeviti wa ccm ngazi ya kata pamoja na makatibu wa Ccm ngazi ya kata  lengo lake kubwa ni kuweka mikakati madhubuti ya kukijenga chama chetu kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa,"

"Pamoja na kuwa katika maandalizi ya  kujiandaa na  kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa ni lazima tukawaheshimu viongozi ambao wapo madarakani na tusianze kupanga safu za viongozi wengine kabla ya muda wake hii haitakiwi kabisa,"alibainisha Mwenyekiti Nyamka.

Kadhalika aliongeza kuwa viongozi wa chama ambao wapo madarakani wanastahili kupewa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza Ilani ya chama kwa vitendo na sio kuwavunja moyo pindi wakiwa bado madarakani.

Kadhlika alisema kwamba lengo lubwa la chama ni kuweka mipango madhubuti ambayo itasaidia kushiriki kikamilifu na hatimaye kushinda kwa kishindo katika chaguzi mbali mbali ikiwemo wa serikali za mitaa ambao utafanyika mwaka huu.


Katika hatua  nyingine Mwenyekiti huyo aliwakumbusha viongozi hao kuweka misingi ya kuwa  na umoja na mshikamano ili kuweza  kukiimarisha chama kuanzia ngazi za mashina,matawi,kata hadi ngazi za juu hali ambayo itasaidia kukijenga chama.


 Katika hatua nyingine Nyamka alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka kwa kuweza kushirikiana bega kwa bega na wananchi katika kutekeleza miradi mbali mbali ya kimaendeleo.

Pia Mwalimu Nyamka hakusita kumshukuru kwa dhati Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutenga fedha ambazo zimeweza kusaidia kwa kiasi kukubwa katika kukamilisha miradi mbali mbali ya maendeleo.

Aliongeza kuwa Rais Samia ameweza kuteleza Ilani ya chama kwa vitendo ambayo imepelekea baadhi ya maeneo kuwaondolea adha changamoto ya  wanakinamama kutembea umbari mrefu kwa ajili ya kufuata huduma maji safi na salama.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya ya Kibaha mji Issack Kalleiya amewakumbusha viongozi kuwasajili  wanachama kwa mfumo wa kisasa wa kidigitali ambao utasaidia katika kutambua wanachama wake.

Jengo la makao makuu Benki ya CDRB lapewa cheti cha kimataifa cha kutunza mazingira

 

 
Dar es Salaam. Tarehe 6 Mei 2024: Benki ya CRDB imeandika historia nyingine kwa kupokea cheti cha kimataifa cha masuala ya mazingira baada ya jengo lake la Makao Makuu kukidhi vigezo vya kimataifa vya majengo yenye kuzingatia uhifadhi wa mazingira.

Cheti hicho cha kwanza kutolewa kwa majengo ya hapa nchini, kinatolewa na taasisi ya International Finance Corporation (IFC) ambayo ni kampuni tanzu ya Benki ya Dunia chini ya programu yake ya EDGE (Excellence in Design for Greater Efficiencies).

Akikabidhi tuzo hiyo, Mkuu wa Idara ya Majengo Yanayolinda Mazingira wa IFC, Dennis Quansah amesema ulinzi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja na ni muhimu kuangalia kila kitu kinachochangia uchafuzi wa mazingira yanayoleta mabadiliko ya tabianchi na athari nyingine kwa viumbe viishivyo duniani.
“Ni furaha kwa IFC kulithibitisha jengo lenu kwamba linatunza mazingira. Hili ni jengo la kwanza kwa Tanzania. Cheti hiki tunachowapa ni utambulisho kwa taassisi na mashirika ya kimataifa yanayohamasisha utunzaji wa mazingira. Matumizi ya maji, nishati na vifaa vya ujenzi ni kati ya vigezo muhimu vinavyotumika kulitathmini jengo kabla ya kulithibitisha,” amesema Quansah.

Mkuu huyo amesisitiza kwamba Benki ya CRDB imeweka mfano unaopaswa kuigwa na taasisi nyingine nchini ili kuyaboresha majengo yao na kuunga mkono juhudi za kulinda mazingira na kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi. 

Cheti hicho ni uthibitisho wa juhudi za Benki ya CRDB sio tu yenyewe kulinda mazingira bali kuwezesha juhudi zinazofanywa na watu wengine kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa kufadhili miradi yenye mrengo wa kulinda mazingira.
Sekta ya makazi ni kati ya maeneo yanayochangia uchafuzi wa mazingira kutokana na aina ya vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi wa nyumba, matumizi ya maji pamoja na nishati.

Akipokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema cheti hiki kinadhihirisha safari  waliyoianza miaka mingi iliyopita hata wakawa taasisi ya kwanza ya fedha ukanda wa kusini na mashariki mwa Afrika kutambuliwa na Mfuko wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (GCF) Novemba 2019.
“Kwa niaba ya menejimenti na wafanyakazi wa Benki ya CRDB, ninafurahi kupokea tuzo hii ya kulitambua jengo letu la makao makuu kwamba linatunza mazingira tukikidhi vigezo kwenye vipengele vyote vitatu vinavyozingatiwa na IFC kabla ya kutoa cheti. 
 
Tumepunguza matumizi ya nishati kwa asilimia 21 na matumizi ya maji kwa asilimia 27. Vifaa tulivyovitumia kwenye ujenzi navyo vinapunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa asilimia 28 hivyo kutufanya kuwa juu ya kiwango cha chini kinachokubalika,” amesema Nsekela.

Akifafanua kuhusu vigezo hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Programu Endelevu wa Benki ya CRDB, Ramla Msuya amesema katika jengo la Benki ya CRDB, taa huzima zenyewe kama hakuna mtu ofisini na maji hayatoki iwapo hakuna mtu anayetaka kuyatumia.
“Taa zinatakiwa ziwake tu iwapo kuna mtu anahitaji mwanga na maji iwe maliwatoni au jikoni, yatatoka iwapo yanahitajika. Huwezi kukuta maji yanamwagika kwa kigezo kwamba mtu kasahau kufunga bomba, hapa kwetu bomba linajifunga lenyewe kama hakuna anayelitumia, hizi ni sifa ambazo hazipo kwenye majengo mengi nchini. 
 
Vifaa vilivyotumika kweny eujenzi wa jengo hili ambalo Rais Samia Suluhu Hassan alilisifia wakati analizindua pia vinajali mazingira. Taka zote zinazokusanywa humu ndani zinarejelezwa, huwezi kuon ataka zimezagaa popote,” amefafanua Ramla.

Ili kuziwezesha taasisi na watu wengine wanaotaka kuyaboresha majengo yao yaendane na vigezo vya kimataifa vya kutunza mazingira, Nsekela amesema Benki ya CRDB inatoa mikopo inayoendana na malengo hayo.
“Tunao wabia zaidi ya 200 tunaoshirikiana nao kufanikisha uwezeshaji huu. Benki ya CRDB peke yake inaweza kukopesha mpaka dola milioni 107 za Marekani na ikishirikiana na GCF mkopo unafika dola milioni 250 na hakuna kikomo tukishirikiana na wabia wetu wengine. 
 
Tunafanya hivi ili Tanzania nayo iwe miongoni mwa mataifa yenye miradi inayolinda mazingira.  Mwaka jana tulitoa Hatifungai ya Kijani na kukusanya fedha nyingi kwa ajili ya miradi hii. Tunamkaribisha kila mwenye wazo au mradi wa kulinda mazingira,” amesema Nsekela.