Kiasi cha chupa 450,000 za damu zinahitajika kwa mwaka Nchini Tanzania huku kiasi kikubwa kikitumika kuokoa maisha ya mama na watoto lakini cha kusikitisha chupa 150,000 za damu ndizo zinazopatikana na kusambazwa.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha jumla ya damu zinazotolewa kila mwaka ulimwenguni kwa utaratibu wa kujitolea ni chupa milioni 80.
Katika idadi hiyo niliyoitaja nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hutoa asilimia 38 tu idadi ambayo haiendani na asilimia 82 ya wagonjwa ambao tiba yao ina uhitaji wa damu.
Imebainishwa wagonjwa wenye uhitaji wa damu kwa wingi ni watoto chini ya miaka mitano,wanawake wajawazito,watu wanaopata ajali pamoja na wale wenye magonjwa mbalimbali yanayosababisha upungufu wa damu.
Tunaweza kuokoa vifo vinavyotokana na upungufu wa damu kwa kujitoa kuchangia damu kwani kitendo cha kuchangia damu ni kitendo cha kibinadamu kwani kinaokoa maisha ya binadamu.
Kila siku nchini Tanzania, wanawake 23 wanapoteza maisha kutokana na matazizo ya uzazi na watoto wachanga 131 hufariki dunia.
Damu salama maana yake ni ile damu ambayo haina vimelea vya maradhi ambayo yanaweza kuambukiza mtu mwingine iwapo mtu huyo ataongezewa.
Maradhi ambayo yametajwa na kuweza kuambukiza kupitia kwenye damu ni Ukimwi (HIV),Homa ya Ini (Hepatitis) pamoja na Kaswende (Syphilis) ambayo yanachunguzwa na vituo vya damu salama vilivyopo kila kanda.
Majukumu makuu ya vituo vya damu salama vinatakiwa kuhakikisha malengo ya upatikanaji wa damu salama yanafikiwa ikiwa ni pamoja na kutoa uhamasishaji kwa jamii ili kuweza kuchangia.
Lakini licha ya kuhamasisha jamii kujitoa kuchangia damu kitu muhimu kinachopaswa kufanywa na vituo vya damu salama ni kuhakikisha damu inapimwa kwa usahihi na kwa utaalamu wa hali ya juu ili kuhakikisha usalama wake.
Nikirejea katika suala la kuchangia watu wengi hawatambui umuhimu wa kujitolea kuchangia damu katika kuokoa maisha ya binadamu ili hatimaye kila mtu mwenye afya nzuri awe mchangiaji damu wa mara kwa mara.
Katika uzinduzi wa kampeni ya kuchangia damu mkoani Mara iliyofanyika Wilayani Bunda,mkurugenzi wa Shirika la (Evidence For Action) Craig Ferla linaloshughulika na kampeni ya uchangiaji wa damu Tanzania alisema vifo vya akina mama na watoto wachanga wakati wa kujifungua ni vingi hapa Nchini kuliko sehemu nyingine Duniani hivyo wanaweza kuokolewa kwa kuchangia damu.
Kila mmoja wetu anaweza kuchukua hatua katika kuokoa vifo vya mama zetu pamoja na woto wachanga wakati wa ujauzito na kujifungua ikiwa wewe ni mwanafamilia,jirani,mwanajamii,mwanamtaa,kiongozi wa dini au mtu yoyote yule unaweza kuleta mabadiliko katika kuokoa maisha ya mama na mtoto wake mchanga.
Hali hii ya akina mama na watoto wetu wachanga inatisha na kuna kila sababu ya kuchukua hatua kuweza kuokoa vifo vinavyotokana na ukosefu wa damu.
Kama tunataka akina mama na na watoto wetu wachanga wapite salama katika kipindi cha ujauzito na kujifungua ni lazima kwa pamoja tuhakikishe vituo vya tiba vinatoa huduma stahiki kwa mama zetu na pia wanawake wanaojifungulia katika vituo vya tiba vyenye wahudumu wenye ujuzi.
Inaelezwa kiwango kikubwa cha uhaba wa damu kinachangia kwa kiasi kikubwa kinapelekea akina wengi kufa wakati wa kujifunguana hata kupelekea vifo vya watoto wachanga kutokana na tatizo hilo.
Ni kuhimizana wanajamii kuchangia kutoa damu kadri inavyowezekana kutokana na ukubwa wa tatizo ambalo tayari limekwisha kuelezwa ni kubwa nchini Tanzania kuliko nchi yoyote duniani.
Kutokana na tatizo kubwa la damu,Serikali ya Tanzania kupitia Rais Jakaya Kikwete Septemba mwaka 2008 alitoa hotuba inayohimiza suala la afya ikiwemo kutanzama afya ya mama pamoja na watoto wachanga katika kuokoa maisha yao hapa namnukuu.
"
Ni lazima tuongeze kwa kiasi kikubwa mgawo wa rasilimali fedha katika afya ya mama na watoto wachanga. Ili kutimiza malengo tuliyojiwekea, inabidi tuongeze fedha katika afya ya mama na watoto wachanga kwa kiasi cha dola za kimarekani bilioni tano kila mwaka ifikapo mwaka 2010, na ongezeko la dola bilioni nane kila mwaka kufikia mwaka 2015.
Pia ni muhimu katika kuwekeza katika kuongeza idadi ya wahudumu wenye ujuzi--wauguzi, wakunga, wataalamu wa maabara na madaktari. Tunahitaji ziada ya wahudumu wenye ujuzi milioni moja kufikia mwaka 2010 ili kuhakikisha uwepo wa huduma za kuokoa maisha ya akina mama katika kipindi chote cha ujauzito na wakati wa kujifungua."
Septemba mwaka 2010, katika mkutano wa malengo ya milenia mjini New York, Tanzania ilikuwa mojawapo ya serikali zilizotoa ahadi ya “kuokoa maisha ya wanawake na watoto milioni sitini kufikia mwaka 2015.
Jitihada hizi za Serikali hazipaswi kuachiwa pekee yake bali kila mwana jamii kwa nafasi yake anaoumuhimu mkubwa wa kuona umuhimu wa kuchangia damu na kuokoa vofo vya mama wajawazito pamoja na watoto wetu wachanga wanaozaliwa na kufa kila siku kutokana na tatizo la damu.