ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, December 16, 2023

SERIKALI YATOA BILIONI 48 KUMALIZA TATIZO SUGU LA MAJI KWA WAKAZI WA PWANI NA DAR

NA VICTOR MASANGU. PWANI

Wananchi wa kata za  Pangani, Kwala Wilayani Kibaha  pamoja na eneo la Kibada Jijini Dar es salaam wanatarajia kuondokana na changamoto sugu ya upatikanaji wa maji safi na salama baada ya Serikali kutoa  shilingi billion 48 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mitatu ya maji.

Hayo yamebainishwa  na Waziri wa maji wakati  wa  halfa ya kutiliana  saini kati ya kampuni za ujezi kutoka nchini china, na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira  Dar es salaam-Dawasa iliyofanyika mjini Kibaha huku akikemea vikali tabia ya kubambikia wananchi bili za maji.

MWANZA: Wadau wajadili mitaala ya uhandisi maji na maendeleo ya jamii

 

Wadau wa fani ya uhandisi na maendeleo ya jamii wakiwemo kutoka mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA), mamlaka ya maji vijijini (RUWASA), mamlaka ya taifa ya umwagiliaji, wakufunzi wa vyuo vya uhandisi na maendeleo ya jamii wamekutana Misungwi mkoani Mwanza kujadili mapitio ya mitaala ya programu ya uhandisi maji na maendeleo ya jamii.

Majadiliano hayo ya siku moja yamefanyika Alhamisi Desemba 14, 2023 katika ukumbi wa chuo cha maendeleo ya jamii ufundi Misungwi (Misungwi CDTTI).

Makamu Mkuu Taaluma wa chuo hicho, Dongo Nzori amesema lengo ni kupitia hiyo na kutoa maoni ya mwisho kabla ya kuwasilishwa katika Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa ajili ya kuidhinishwa.

Amesema kozi ya uhandisi maji na maendeleo ya jamii ikipitishwa na NACTVET itakuwa kozi ya pili katika vyuo vyao vya maendeleo yajamii ufundi Misungwi mkoani Mwanza na Mabughai kilichopo Lushoto mkoani Tanga ambapo itasaidia kuleta tija katika sekta ya umwagiliaji.

"Tumeamua kuleta huu mseto wa uhandisi maji na maendeleo ya jamii kwa sababu utasaidia kupunguza rasilimali watu, kuongeza ufanisi katika kusimamia miradi ya maji pamoja na kurahisisha ujenzi wa miundombinu ya maji" amesema Nzori.

Amesema kwa sasa kwenye kozi ya uhandisi ujenzi na maendeleo ya jamii ina wanafunzi zaidi ya 900 katika vyuo hivyo ambapo Misungwi kuna wanafunzi 600 na Mabughai 300 huku idadi ikitarajiwa kuongezeka baada ya kozi ya uhandisi maji na maendeleo ya majii kuanza kutolewa ambayo pia itazalisha wataalamu wanaohitajika katika soko la ajira.

Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Mabughai wilayani Lushoto, Erasmus Hipoliti amesema mtaala wa uhandisi maji na maendeleo ya jamii utasaidia vijana wengi kupata fursa za ajira kwa namna utakavyotoa wigo wa kushiriki katika masuala ya MMaendeleo ya Jamii na uhandisi maji.

Amesema bado kuna changamoto ya miradi ya maji katika jamii ndiyo maana wameanzisha kozi hiyo ili kuandaa wataalamu watakaoibua miradi ya maji hatua itakayosaidia kutatua changamoto zilizopo.

Kwa upande wake Mhandisi Willybert Bujiku kutoka MWAUWASA Kanda ya Misungwi, amesema kozi hiyo italeta manufaa makubwa kwa Serikali ambapo akiajiriwa mtu aliyesoma uhandisi maji na maendeleo ya jamii atafanya kazi kwa ufanisi mkubwa huku pia ikiongeza wigo kwa wahandisi kufanya kazi kwa weledi zaidi.

Awali akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju ameshauri maboresho ya mitaala ya uhandisi maji na maendeleo ya jamii kusaidia kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na weledi utakaosaoidia kuchochea maendeleo katika jamii.
Makamu Mkuu Taaluma Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Misungwi CDTTI, Dongo Nzori akizungumza kwenye warsha ya wadau kujadili mitaala ya programu za uhandisi maji na maendeleo ya majii iliyofanyika katika chuo hicho.
Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Mabughai mkoani Tanga, Erasmus Hipoliti akizungumza wakati wa warsha hiyo.
Wadau wa maji na maendeleo ya jamii wakiwa kwenye majadiliano ya mitaala ya programu ya uhandisi na maendeleo ya jamii.
Wadau wakiwa kwenye majadiliano.
Wadau wakiwa kwenye majadiliano.
Wadau wakiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju (katikati waliokaa).
Wadau wakiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju (katikati waliokaa).
PIA SOMA>>> HABARI ZAIDI HAPA

ASA WATEKELEZA KWA VITENDO AGIZO LA WAZIRI MKUU

 WAZIRI wa Kilimo Hussein Bashe kulia akimgaia mche wa Mbegu ya Mchikichi zinazozalishwa na Shamba la Wakala wa Mbegu Asa Mkinga Mkulima wakati wa halfa ya ugawaji miche hiyo shamba la Mwele lililopo wilaya ya MkingaWAZIRI wa Kilimo Husein Bashe katika akionyeshwa maeneo mbalimbali yeye miche ya Michikichi kwenye Shamba la Wakala wa Mbegu Asa lililopo wilayani Mkinga wakati wa ziara yake kulia ni Mtendaji Mkuu wa Asa Sophia Kashenge na kushoto ni mkulima aliyepewa miche shamba la Mwele lililopo wilaya ya Mkinga


Waziri wa Kilimo Husein Bashe katikati akitembelea Shamba la Wakala wa Mbegu ASA wilaya ya Mkinga wakati wa ziara yake shamba la Mwele lililopo wilaya ya Mkinga kulia ni Mtendaji Mkuu wa ASA Sophia Kashenge akisisitiza jambo

 Mtendaji mkuu wa wakala wa Mbegu (ASA) Sophia Kashenge kushoto akimueleza jambo Waziri wa Kilimo Husein Bashe wakati alipotembelea wakati huo kugawa miche kwa wakulima

Mtendaji mkuu wa wakala wa Mbegu (ASA) Sophia Kashenge wa pili kutoka kulia akimuonyesha kitu Waziri wa Kilimo Husein Bashe wakati wa ziara yake kwenye Shamba hilo

Waziri wa Kilimo Husein Bashe akizungumza na wakulima wa wilaya ya Mkinga wakati wa ziara yake ya kutembelea Shamba la Mwele lililopo wilayani Mkinga

Mkurugenzi wa Bodi ya  Mkonge Tanzania (TSB) Saady Kambona akiwa na viongozi wengine wakifuatilia kwa umakini maelekezo ya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe

Watumishi wa Wakala wa mbegu za kilimo nchini (ASA) katika shamba la Mwele lililopo wilaya ya Mkinga wakiwa na viongozi wengine wakimsikiliza kwa umakini Waziri wa Kilimo Husein Bashe




Na Oscar Assenga,MKINGA

WAKALA wa mbegu za kilimo nchini (ASA) katika shamba la Mwele lililopo wilaya ya Mkinga mkoani Tanga wamezindua zoezi la ugawaji wa mbegu za michikichi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu la kutaka zao hilo litumike ipasavyo kuongeza uzalishaji wa mafuta hapa nchini.

Hatua ya utekelezaji huo imekuwa na mafanikio makubwa naa kwa sasa wana michikichi elfu 88 na lengo ni kutoa michikichi laki mbili kwa wakulima ambao wataipanda katika maeneo mbalimbali na hivyo kuwezesha kilimo cha zao kuwa na tija

Akizungumza wakati akikabidhi Miche ya Michikichi kwa Wakulima wwa zao hilo lengo likiwa ni kukabidhi michikichi laki mbili katika wilaya ya Mkinga mkoani Tanga,Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisema wananchi wanaopewa miche hiyo lazima wajaze fomu na kusaini ikiwemo kubaki na kumbukumbu ambazo zitapelekewa Halmashauri.

Alisema zitapelekwa huko ili maafisa kilimo wapewe taarifa kwenye vijiji vyao ambavyo wananchi wamepewa miche ili wawafuatilie kwa ukaribu wanapopata matatizo waone namna ya kuyapatia ufumbuzi huko huko vijijini.

Waziri Bashe alisema kwa sababu wamekuwa bahati mbaya wakigawa miche lakini mingi inaishia njiani haikui na wananchi wanapoteza muda na kuweka nguvu zao hivyo ni muhimu uwepo wa ufuatiliaji huo

“Leo tunagawa miche ya Michikichi wilaya ya Mkinga na wananchi ambao wamepewa watajaza fomu kusaini na kubaki na kumbukumbu ambazo baadae zitapelekwa Halmashauri pia maafisa Kilimo wapewa Taarufa kwenye Vijiji vyao kwa lengo la kuwa na ufuatiliaji wa karibu watakakukumbana na matatizo waweze kuyapatia ufumbuzi”Alisema

Hata hivyo Waziri huyo alisema wataanzisha mashamba makubwa ya pamoja ambao amesema miongoni mwa wafaidika watakuwa wananchi wa maeneo husika huku akisisitiza umuhimu wa maafisa kilimo wakae vijijini.

“Kama walimu wanakaa vijijini na maafisa kilimo nao wakate vijiji lakini pia mikutano ya Serikali za vijiji ifanye kazi ya kujadili maafisa Kilimo maeneo hayo kama hawatimizi wajibu wao kama hawafanyi hivyo serikali za vijiji ziandike taarifa kwenye mustasari zipelekewe kwenye WDC halafu ziende Halmshauri”Alisema

Waziri huyo alisema kwamba katikaa taarifa hiyo waeleze Afisa kilimo walionae hajawahi kuwatembelea wakulima hata siku moja kwani Serikali imegawa pikipiki na sasa wanawapa vishkambie na wamepekea vipima afya vya udongo ili wanapopima shamba wawaambie kama shamba linafaa kulima mashina au na huduma hiyo ni bure.

Katika hatua nyengine Waziri Bashe amemuagiza Mkurugenzi wa Asa Sophia Kashenge waanze shughuli za kuzalisha miche ya minazi kwenye kituo hichgo kama wanavyozalisha mice ya mazao mengine ili wananchi waweze kupata m iche ya minazi kutoka kwenye kituo hicho,

Awali akizungumza katika Mtendaji mkuu wa wakala wa Mbegu (ASA) Sophia Kashenge alisema kwa sasa wana michikichi elfu 88 na lengo ni kutoa michikichi laki mbili kwa wakulima.

Sophia alisema kwamba wamefarijika sana kuona Waziri kufika katika shamba hilo ambalo kipindi cha nyuma lilikuwa limetekelezwa lakini nguvu ya Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu imeonekana na wameweza kulifufua.

Alisema kwamba huwezi kufanya uzalishaji bila kuwa na miuondombinu ya umwagiliaji na hivyo lengo lao wataendelea kuongeza uzalishaji wa mbegu jambo ambalo ni kipaumbele cha nchi.

“Suala la Uzalishaji wa Mbegu za Michikichi ni Agizo la Waziri Mkuu tokea 2018 na sisi tumeitika vizuri tuna mashamba matatu ya ASA na la Mkinga ni la pili kwa uzalishaji wa michikichi na tunaamini kazi tunayoifanya ni kumuongezea mwananchi kipato”Alisema

Naye kwa upande wake Mkulima wa zao la Michikichi Mtarajiwa wilayani Mkinga Maaono Mkangwa alisema serikasli imechukua uamuzi mzuri kuwaletea kilimo hicho ambacho wanaamani kitawainua kiuchumi.

Mpango wa serikali ni kupunguza kiwango kikubwa cha kuingiza mafuta kutoka nje ya nchi wakati mafuta hayo yanaweza kuzalishwa na wakulima hapa nchini.

Wednesday, December 13, 2023

"UKIONA MAHALI POPOTE MTU ANAFANYA KAZI VIZURI BASI KUNA WATIA MOYO NYUMA YAKE" NAIBU W. MKUU BITEKO

 NA ALABERT G. SENGO

DKT. BITEKO ASHIRIKI MKUTANO MKUU WA CCM CHATO, GEITA.

DKT. SAMIA NI MUUMINI NAMBA MOJA WA MARIDHIANO NCHINI- DKT. BITEKO



📌Asema anaishi na Kutenda Maridhiano

📌Awataka Viongozi Kufanya Kazi na Makundi mbalimbali ya  Wananchi

📌Askofu Bagonza atoa salam za pole kwa Serikali kufuatia Vifo na Majeruhi Hanang

Kagera

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.  Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa ni Muumini namba Moja wa maridhiano nchini na haishii katika kusema tu bali anatekeleza kwa vitendo huku nia ikiwa ni kuhakikisha kunakuwa na umoja na amani nchini.


Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 10 Disemba, 2023 wakati wa Misa Maalum ya Kutabaruku Kanisa Kuu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ( KKKT) Lukajange, Dayosisi ya Karagwe iliyofanyika wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera. Misa hiyo maalum imehudhuriwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ( CCM), Bara, Komredi Abdulrahman Kinana , Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa.


"Rais,  Dkt. Samia anasema kila mara kuwa hii nchi ni yetu sote, anatuasa mara nyingi kuwa wewe kama ni CCM mpende Mpinzani, na Mpinzani mpende CCM, tuungane pamoja tusukume nchi yetu mbele, na hakuishia hapo tu, akaunda Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano ambayo  imejumuisha makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa kutoka Vyama mbalimbali na viongozi wa dini ili kuwe na muafaka nchini, tujenge Tanzania bora kwa ajili yetu na vizazi vijavyo." Amesisitiza Dkt. Biteko

Ameongeza kuwa, Rais, Dkt. Samia amekuwa muumini wa maridhiano si kwa kuigiza bali kwa dhati ya moyo wake na ameonesha mifano mbalimbali ya maridhiano ikiwemo kuwa Mgeni rasmi katika Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA) wilayani Moshi na hicho ni kiashirikia kikubwa cha kuonesha kuwa anataka umoja na amani nchini.


vilevile, Dkt. Biteko ameendeelea kusisitiza kuwa, Serikali inaunga mkono madhehebu ya dini na shughuli za kidini nchini na ndiyo maana imeendelea kutoa uhuru wa kuabudu kwa kila mtanzania.

Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko ametaka viongozi mbalimbali nchini kufanya kazi  na watu wanaowaunga mkono na wasiowaunga mkono kwani wajibu wao ni kuwahudumia wananchi wote.


Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo amesema kuwa, miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa katika Sekta mbalimbali ikiwemo za  Nishati, Miundombinu, Afya ili kuelekea katika Tanzania tunayoitaka.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Komredi Abdulrahman Kinana amempongeza Askofu Benson Bagonza kwa uongozi mzuri katika Dayosisi ya Karagwe na ujenzi wa Kanisa Kuu jipya katika Dayosisi hiyo. Pia amewapongeza Mashemasi Watano katika Dayosisi hiyo ambao wamepata Uchungaji.

Waziri wa Ujenzi, ambaye pia ni Mbunge wa Karagwe, Mhe. Innocent Bashungwa  amepongeza pia kwa ujenzi wa Kanisa hilo Kuu na pia amempongeza Askofu Benson  Bagonza kwa kufanya kanisa katika Dayosisi hiyo kuzidi kusonga mbele.  Pia ameahidi kushirikiana nao katika kujenga Dayosisi hiyo.


Kwa upande wake, Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia  suala la maridhiano kwa makundi yanayoonesha kukinzana huku akisema kuwa upatanisho huo anaousimamia una baraka za Mungu na amemtia moyo wa kuendelea kusimamia maridhiano kwani ni Afya ya Taifa.


Aidha, amemshukuru Rais, Dkt. Samia, pamoja na  viongozi mbalimbali wa Serikali waliochangia ujenzi wa Kanisa Kuu la KKKT, Dayosisi ya Karagwe pamoja na waumini na wadau mbalimbali.



Pia, Askofu Bagonza ametoa pole kwa Serikali na Wananchi kufuatia vifo na majeruhi vilivyotokana na janga la kiasili wilayani Hanang, mkoani Manyara.


Dayosisi ya Karagwe ilizinduliwa mwaka 1979 ambapo ujenzi wa Kanisa hilo kuu ulianza mwezi Februari 24, 2023 na kukamilika mwezi Novemba 2023. Ujenzi wa Kanisa hilo umegharimu  Shilingi milioni 400.

Monday, December 11, 2023

RC Chalamila apongeza Jeshi la polisi na Barrick kwa kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa vitendo

 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila akiongea katika hafla hiyo
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila (katikati) akikabidhi cheti cha shukrani kwa Afisa Mawasiliano wa Barrick,Abella Mutiganzi na Meneja Mawasiliano (Corporate Communications and Country Liaison Manager) wa Barrick, Georgia Mutagahywa (Kulia) kutokana na kampuni hiyo kufadhili mafunzo ya utambuzi wa masuala ya jinsia yaliyoendeshwa na Jeshi la Polisi katika katika hafla ya kuhitimisha maadhimisho ya siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia iliyofanyika katika Chuo Cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (kushoto) ni Mkuu wa Chuo hicho, SACP Dk.Lazaro Mambosasa
Meneja Mawasiliano (Corporate Communications and Country Liaison Manager) wa Barrick, Georgia Mutagahywa, akiongea katika hafla ya kuhitimisha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa jinsia iliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi cha Dar es Salaam.Mwaka huu Barrick ilishirikiana na Jeshi la Polisi katika maadhimisho hayo.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akikabidhi cheti kwa Mratibu wa madawati ya kijinsia kwenye vyuo vya kati na vya juu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Gift Msowoya,
Baadhi ya wageni waalikwa wakifuatilia matukio katika hafla hiyo
Wanafunzi wa shule ya msingi Mgulani wakiimba wimbo kuhusu ukatili wa kijinsia katika hafla hiyo

Na Mwandishi Wetu

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Barrick kuadhimisha siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili kwa kijinsia kwa vitendo, ambapo limeweza kutoa elimu ya utambuzi wa vitendo hivyo na hatua za kuchukua wahanga wa vitendo hivyo katika shule za msingi,sekondari , kwenye maeneo ya biashara jijini Dar es Salaam.

Chalamila, alitoa pongezi hizo wakati wa hafla ya kufunga maadhimisho hayo iliyofanyika katika Chuo Cha Polisi cha Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka taasisi za kupinga vitendo hivyo.

Alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika siku 16 kwa kufikisha elimu ya utambuzi wa vitendo hivyo bado kunahitajika nguvu ya pamoja kuendeleakuongeza ushawishi,kuhamasisha,kukemea na kuelimisha jamii ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo matatizo ya kisaikolojia yanaopelekea wananchi wengi kuelewa tatizo hilo na kujikuta vitendo hivi vinaongezeka kwa kasi hususani katika miji mikubwa kama Dar es Salaam.

“Natoa Pongezi kwa Jeshi la Polisi na Barrick, kwa kuungana pamoja kuhakikisha mnapeleka elimu ya utambuzi wa elimu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.Natoa wito kuwa muendeleze ushirikiano huu katika kampeni mbalimbali zenye lengo la kuleta mabadiliko chanya kama ambavyo mmefanya katika maadhimisho haya.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Cha Polisi cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam,SACP Dk.Lazaro Mambosasa,alisema kuwa jeshi la polisi kwa kutumia wataalamu wake waliopo katika madawati ya kijinsia yaliyosambaa katika mtandao mkubwa wa vituo vyake litaendelea kutoa elimu na kusaidia wahanga wa vitendo sambamba ba kuhakikisha wanaofanya vitendo hivyo wanafikishwa haraka kwenye vyombo vya sheria.

Naye Meneja Mawasiliano (Corporate Communications and Country Liaison Manager) wa Barrick, Georgia Mutagahywa, alisema kuwa,Barrick Imekuwa mstari wa mbele kukabiliana na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu hivyo siku zote itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika vita vya kupambana kutokomeza vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia chini.

Awali akitoa taarifa ya kampeni hiyo kwa mgeni rasmi, Mratibu wa madawati ya kijinsia kwenye vyuo vya kati na vya juu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Gift Msowoya, alisema kuwa katika kipindi cha kampeni wameweza kufikia shule zaidi ya 10 za msingi na sekondari katika wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam,Kwenye masoko na mikusanyiko ya watu pia kupitia vipindi vya televisheni na vyombo vingine vya habari, elimu hiyo imeweza kuwafikia watanzania wengi.

Msowoya, pia alisema kuwa katika kipindi hicho cha kampeni waliweza kutembelea gereza la Segerea kupeleka elimu hiyo sambamba na kufanya matendo ya huruma ambapo waliweza kutoa msaada wa vifaa mbalimbali katika gereza hilo.

Maadhimisho ya siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ambayo huadhimishwa duniani kote na hapa nchini kuadhimishwa na taasisis mbalimbali na wadau wa masuala ya kijinsia mwaka huu yalianza tarehe 25 Novemba na kuhitimishwa tarehe 10,mwezi huu.

Sunday, December 10, 2023

Mradi wa kuzuia kuzama maji Ziwa Victoria watambulishwa Mwanza

 

Shirika la mazingira na maendeleo EMEDO limeutambulisha mradi wa kuzuia watu kuzama maji katika Ziwa Victoria kwa wadau mbalimbali wa uvuvi mkoani Mwanza.

Afisa Mradi huo, Arthur Mgema amesema lengo ni kuzuia vifo vitokanavyo watu kuzama maji katika Ziwa Victoria hasa wavuvi, watoto na wanawake wachakataji wa mazao ya samaki/ dagaa ambao wako kwenye hatari zaidi.

Akifungua kikao cha kuutambulisha mradi huo, Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya amesema matukio ya watu kuzama maji yanazuilika endapo kila mmoja atatimiza wajibu wake.

Amesema kwa Mkoa Mwanza Serikali inatekelezeka mpango wa BBT (Building Better Tomorrow) katika sekta ya ufugaji na uvuvi hivyo mradi wa kuzuia kuzama maji katika Ziwa Victoria utasaidia kutoa elimu ili kuzuia vifo zitokanavyo na kuzama maji.

Mradi wa kuzuia kuzama maji katika Ziwa Victoria unatekelezwa na shirika la EMEDO katika mikoa ya Mwanza, Mara na Kagera katika kipindi cha miaka mitatu hadi mwaka 2025 kwa ufadhili wa taasisi ya RLNI- Life Boats ya nchini Uingereza.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Afisa Mradi wa kuzuia kuzama maji Ziwa Victoria, Arthur Mgema (kulia) akimkabidhi Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya (kushoto) ripoti ya utafiti uliofanywa na shirika la EMEDO mwaka 2021 kuhusu sababu za wavuvi kuzama maji pamoja na rasimu ya uvuvi salama iliyoandaliwa katika mwalo wa Busekera mkoani Mara.
Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Elikana Balandya akifungua kikao cha kuutambulisha mradi wa kuzuia kuzama maji katika Ziwa Victoria kilichowakutanisha wadau jijini Mwanza.
Afisa Mradi wa kuzuia kuzama maji Ziwa Victoria, Arthur Mgema akieleza kuhusu mradi huo ambao umelenga kutoa elimu kwa jamii ya wavuvi ili kuchukua tahadhari za kuzuia kuzama maji.
Kaimu Afisa Maendeleo Mkoa Mwanza, Rehema Mkinze akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kuutambulisha mradi wa kuzuia kuzama maji Ziwa Victoria.
Wadau mbalimbali mkoani Mwanza wakifuatilia kikao cha kuutambulisha mradi wa kuzuia kuzama maji katika Ziwa Victoria.
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO) watu 236,000 hupoteza maisha kwa kuzama maji. Hata hivyo bado kuna changamoto ya upatikanaji wa takwimu za watu wanaofariki kwa kuzama maji katika mataifa mbalimbali duniani, Tanzania ikiwemo hivyo pamoja na mambo mengine, pia mradi wa kuzuia kuzama maji Ziwa Victoria utasaidia upatikanaji wa takwimu hizo.
SOMA PIA>>> HABARI ZAIDI HAPA