Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Kilimani,Gaudensia Bagoka akizungumza kwenye mahafali ya tano ya kidato cha nne cha shule hiyo jana.
Wahitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kilimani, Ilemela Irene Magesa na Ally Mohamed wakisoma risala mbele ya mgeni rasmi , Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Salum Kalli, jana.
Wahitimu wa kidato cha nne wa Shule ye Kilimani Sekondari iliyopo Ilemela wakiigiza kama maarusi wakati wa mahafali yao iliyofanyika jana shuleni hapo.
Wahitimu wa kike wa Shule ya Kilimani Sekondari, wakionyesha ubunifu wao wa mavazi ya asili wakati wa mahafali yao iliyofanyika jana.
Mkuu wa Shule ye Kilimani, Gerana Majaliwa, akitoa taarifa fupi ya mafanikio ya shule hiyo jana kwenye mahafali ya kidato cha nne mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Kilimani,Gaudensia Bagoka akisoma risala ya shule hiyo akielezea changamoto na mafanikio kwa mgeni rasmi, wakati wa mahafali ya tano ya kidato cha nne cha shule hiyo jana.
Mgeni rasmi kwenye mahafali ya kidato cha nne cha Shule ya Kilimani Sekondari, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Salum Kalli akizungumza na wazazi, walimu, wahitimu na wanafunzi jana.
Stumai Hamis, mhitimu wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Kilimani akipokea cheti kutoka kwa mgeni rasmi,baada ya kuonyesha nidhamu ya hali ya juu shuleni hapo.
Mhitimu wa kidato cha nne wa Shule wa Sekondari Kilimani, Deogratius Kadomole, akipokea moja ya vyeti kutoka kwa mgeni rasmi, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Salum Kalli wakati wa mahafali ya shule hiyo jana.Kadomole alifanya vizuri kwenye masomo ya Baiolojia, Kemia,English na Fizikia pamoja na kwenye usafi na michezo.
Mgeni rasmi wa mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kilimani, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Salum Kalli akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu waliofanya vizuri kwenye masomo yao baada ya kuwanutunu vyeti wakati wa mahafali ya shule hiyo jana.Picha zote na Baltazar Mashaka
KATIBU wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza Salum Kalli, amesema maendeleo ya nchi yanategemea vijana wasomi walioelimika na kutumia elimu yao kwa manufaa ya wengi na kuonya jamii isikubali watoto wa kike wakatishwe masomo.
Pia amewataka wazazi kufuatilia maendeleo ya elimu kwa watoto wao na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za sekta ya elimu ili kukuza taaluma shuleni.
Kalli ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya tano ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kilimani,iliyopo Manispaa ya Ilemela alitoa kauli hiyo jana.
Alisema dhamira ya serikali kutoa elimu bure kuanzia shule za awali hadi kidato cha nne inalenga kuzalisha watalaamu wasomi wa fani mbalimbali,weledi watakaotumia elimu yao kwa maslahi ya wengi na maendeleo ya nchi, hivyo wazazi na jamii wasikubali watoto hasa wa kike kukatishwa masomo kwa namna yoyote.
Pia dhamira hiyo ya serikali ya awamu ya tano inalenga kuwahudumia na kuwanufaisha watoto wa masikini na kuhakikisha wanapata elimu itakayowakomboa kwenye maisha yao.
“Nimefurahi kuona elimu inayotolewa kwenye shule hii ya kata na zingine licha ya kubezwa, imewawezesha wahitimu kuelezea changamoto na mafanikio ya shule kwa lugha ya Kiingereza.Inaonyesha jinsi walimu wanavyounga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kutoa elimu bure na wanafunzi wanafanya vizuri.Rai yangu wazazi na jamii msikubali watoto wakatishwe masomo,”alisema.
Katibu huyo wa CCM Mkoa wa Mwanza alieleza kuwa Serikali ya awamu ya nne ilijenga shule za kata ili watoto wapate elimu wakiwa karibu na mazingira ya nyumbani na kuwapunguzia baadhi ya changamoto ambapo awamu ya tano imeboresha kwa kuondoa changamoto na kero nyingi kwa kutoa elimu bure.
Aidha, Kalli alitoa sh. milioni Moja kwa ajili ya kusaidia ukamilishaji wa ujenzi wa ofisi ya walimu inayohitaji sh. milioni 3.5 pamoja na kompyuta moja itakayotumika kuandaaa kanzi data,uchapaji wa nyaraka za shule na shughuli za kitaaluma.
Awali katika risala za wahitimu hao na shule zilizosomwa na Irene Magesa na Ally Mohamed pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Gaudensia Bagoka zilielezea changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa, ukosefu wa ofisi na nyumba za walimu, mabweni ya wasichana, maktaba, kompyuta tatu, upungufu wa samani kwa ajili ya wanafunzi na walimu, huduma ya maji safi na salama.
Walisema changamoto hizo ni kikwazo cha ukuaji wa taaluma shuleni hapo na kuomba wasaidiwe ikizingatiwa ni moja ya shule bora mkoani Mwanza ambapo kwenye matokeo ya mitihani wa taifa kidato cha nne mwaka 2016, ilishika nafasi 115 kati ya shule 218 kimkoa.
Mwaka 2017 kwa mujibu wa makamu mwenyekiti wa bodi ilishika nafasi ya 138 kati ya 220 kimkoa, mwaka 2018 ilishika nafasi ya 70 kimkoa kayo ya shule 241,mafanikio ambayo ni ya kujivunia baada ya kutunukiwa cheti na ngao kutokana na kuimarika kitaaluma.
Aidha, katika hatua nyingine Kalli alisema kutokana na mafanikio ya shule hiyo, wazazi hawana budi kwenda kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura kuchagua viongozi wa serikali ya mtaa kupitia CCM wenye dhamira ya kuwaletea maendeleo.
Alisema watafanya makosa kuchagua watu wasioumizwa na maendeleo ya wananchi ambao siku zote wamebaki kulalamika huku wakiichonganisha wananchi na serikali yao kwa kubeza mafanikio yaliyopatikana. ssss