ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, July 19, 2024

HAWA HAPA WAKALI WA ACAPELLA THE VOICE NDANI YA JEMBE FM

 NA ALBERT GSENGO/MWANZA

Kuelekea Kongamano la Kwanza la Kikanda kuhusu maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, waimbaji wa kundi la muziki The Voice wamatembelea Jembe Fm na kufanya mahojiano kisha kushare nasi utamu wa sauti zao. Kongamano hilo litaongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Dotto Biteko huku likitarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Kwa Tunza Jumamosi hii, July 20, 2024 kuanzia saa 3:00 asubuhi.

MWENYEKITI UWT KIBAHA MJI AWAKUMBUKA WANAWAKE WAJANE KATIKA FURSA ZA MIKOPO

NA VICTOR MASANGU,KIBAHA 

Mwenyekiti wa umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini amesema atahakikisha analivalia njuga suala la wanawake wajane kujiunga katika  vikundi vya ujasiriamali ili kupata fursa za mikopo.

Mgonja ameyabainisha hayo wakati akizungumza na  baadhi ya wanawake wa UWT kutoka kata za Visiga pamoja  na Misugusugu akiwa katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi yenye kuwapa ujasiri wanawake kugombea katika nafasi za uongozi.

Mwenyekiti huyo alisema kwamba katika ziara hiyo anatambua uwepo wa baadhi ya wanawake ambao ni wajane hivyo amewahimiza kujiunga katika makundi ya ujasiriamali ambayo itakuwa ni rahisi zaidi katika kupata mikopo.

"Nipo katika ziara ya kikazi katika kutembelea wanawake wa UWT kutoka kata zote 14 za Jimbo la kibaha mjini na leo nimetembelea kata ya Visiga na Misugusugu ikiwa ni kata ya kumi tangu nianze ziara yangu ,"alisema Mgonja.

Aliongeza kuwa ana imani wanawake wajane wakisapotiwa katika kupewa mitaji na mikopo wanaweza kufanya mambo makubwa na kuweza kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini.

Aliongeza kuwa kwa sasa lengo la UWT ni kuwa na siasa na uchumi hivyo atahakikisha anapambana kwa hali na mali ili kuwasaidia wajane kupata fursa za mikopo  ya asilimia 10 ambayo inatolewa na serikali.

Katika hatua nyingine alisema atahakikisha kwamba anawalinda na kuwatunza kwa hali na mali  wanawake wajane ambao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya unyanyasaji na kwamba atashirikiana na vyombo vya dola katika jambo hilo.
Kwa upande wake Katibu wa UWT kata ya Visiga alimpongeza Mwenyekiti wa  Wilaya kwa ziara yake ya kutembelea wanawake kwa ajili ya kuwahimiza kujitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya uchaguzi.

Nao baadhi ya waheshimiwa madiwani wa halmashauri ya Kibaha mjini hawakusita kuwapa ujasiri kwa wanawake hao kutoogopa kugombea katika nafasi za uongozi hasa katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Baadhi ya wanawake wajane wamesema kwamba wapo tayari kuwezeshwa mitaji pamoja na mikopo na kwamba wakiwezeshwa wanaweza kuondokana na kuwa tegemezi.



Ziara ya mwenyekiti wa umoja wa wanawake (UWT)     hadi sasa imefanyika katika kata kumi ambapo leo imefanyika katika kata ya Visiga na Viziwaviza.

Thursday, July 18, 2024

KONGAMANO LA KWANZA LA MAANDALIZI YA DIRA YA MAENDELEO YA MWAKA 2050 KUZINDULIWA MWANZA.

 NA ALBERT GSENGO/MWANZA

Kongamano la Kwanza la Kikanda kuhusumaandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050 litazinduliwa 20, mwaka huu jijini Mwanza huku wananchi wakitakiwa kujitokeza kutoa maoni yao.

Akizungumza na wanahabari jijini Mwanza kuhusu Kongamano hilo Mkurugenzi wa Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Thobias Makoba, amesema KOngamano hilo ni sehemu ya kuongeza uelewa kwa umma kuhusu Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050

Naye Mwenyekiti wa Timu Kuu ya Kitaalamu ya Dira ya Taifa 2050 Dkt. Asha Rose Migiro amesema wameweka tahadhari kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi na mazingira kwamba ni masuala ambayo yapo yanayoepukika na yasiyoepukika nao wamejipanga kuhakikisha malengo yatakayowekwa yanatimia kwa asilimia kubwa bila kuathiriwa. ..

Aidha Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Thobias Makoba ameongeza kuwa Kongamano hilo litaongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt Dotto Biteko huku likitarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Kwa Tunza Jumamosi hii, July 20, 2024 kuanzia saa 3:00 asubuhi.

UWT KIBAHA MJI YAWAPIGA MSASA WA UCHAGUZI WANAWAKE WA KATA YA KIBAHA NA VIZIWAZIWA

 


NA VICTOR MASANGU, KIBAHA

 
Umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini imewataka wanawake kuachana na tabia ya kufanya kampeni za chini chini kabla ya muda haujafika wa kampeni  na badala yake wametakiwa kuwapa ushirikiano wa kutosha viongozi ambao wapo madarakani hadi kipindi cha muda wao utakapomalizika bila ubaguzi wowote.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini Selina Mgonja wakati akizungumza na baadhi ya wakinamama wa UWT kata za Kibaha pamoja na viziwaziwa ikiwa ni ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuzungumza na wanachama  sambamba na kuwahimiza wanawake wenye sifa na vigezo kushiriki na kujitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mgonja alisema kwamba kwa sasa ni vema  viongozi  mbali mbali ambao walichaguliwa na wananchi na wapo madarakani kwa mujibu wa sheria  wanatakiwa kuheshimiwa na kupewa ushirikiano wa kutosha  katika suala zima la utekelezaji wa Ilani ya chama  na sio kuanza kuwabeza na kuwaandaa  watu  mwingine kinyemela  kabla ya muda wake kumalizika kwani amechaguliwa kihalali.

"Katika ziara yangu lengo kubwa ni kutembelea katika kata mbali mbali ambazo zipo katika Jimbo la Kibaha mjini na kuwahimiza wanawake wenzangu kuweza kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi lakini kitu kikubwa wanatakiwa kuwaheshimu viongozi wa chama ambao bado wapo madarakani na kuachana na tabia ya kutengeneza safu ya uongozi kabla ya wakati,"alisema Mgonja.

Aidha Mwenyekiti Mgonja amebainisha kuwa lengo lingine la kufanya ziara hiyo ni kuwajengea uwezo wanawake  ili  wapate fursa ya kujiamini na kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa bila ya kuwa na uwoga wowote na kwamba wana imani ziara hiyo itaweza kuleta mabadiliko chanya  kwa wanawake kujitokeza kwa wingi.

Katika hatua nyingine aliwataka wanawake wa UWT kuendelea kumpa ushirikiano wa kutosha Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani ameweza kutenga fedha nyingi ambazo zimetumika katika miradi mbali mbali ya kimaendeleo hivyo wanawake wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kumsemea yale mazuri ambayo ameyafanya katika kipindi cha miaka mita.

 
Kwa upande wake Katibu wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini  Cesilia Ndalu alisema kwamba katika kuelekea uchagzui wa serikali za mitaa wanawake wanapaswa kuwa na uthubutu na ujasiri kwa lengo la kuweza kujitosa kuchukua fomu na kushiriki katika uchaguzi huo ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu.

Nao baadhi ya wanawake wa UWT wamempongeza Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja kwa ziara yake hiyo ya kikazi ambayo imeweza kuwapa hamasa zaidi katika kushiriki kugombea katika  uchaguzi wa serikali za mitaa.

 Naye Diwani wa viti maalumu Halmashauri ya mji Kibaha Selina Wilson amewakumbusha wanawake hao kutumia ujuzi na maarifa waliyonayo katika kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kugombea nafasi za uwenyekiti katika uchaguzi wa serikali za mtaa mbao unatarajiwa kufanyika mwaka huu.

Ziara ya Mwenyekiti wa umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha mjini imelenga kupita katika kata zote 14 za Jimbo la Kibaha mjini ambapo kwa  leo ziara imefanyika katika kata mbili  za Kibaha pamoja na kata ya Viziwaziwa ambayo ni ya nane kufikiwa siku ya leo kwa lengo la kuwahimiza wanawake kujitokeza kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Wednesday, July 17, 2024

WILLIAM RUTO KUBUNI OFISI YA JENERALI MKUU WA KUCHUNGUZA VIFO.


Nairobi - Wizara ya Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa imefichua mipango ya kubuniwa kwa Ofisi ya Mkuu wa Uchunguzi wa Vifo. 

Katika taarifa siku ya Jumanne, Julai 16, wizara hiyo ilieleza kuwa ofisi hiyo itabuniwa chini ya Sheria ya Kitaifa ya Huduma ya Wachunguzi wa Vifo 2017. 

Wizara hiyo ilifichua kuwa ilimshauri Rais William Ruto kuunda afisi ambayo itachunguza mauaji yanayohusishwa na ukatili wa polisi. 

Kulingana na wizara hiyo, afisi hiyo itahakikisha uwajibikaji na uwazi katika visa vya vifo vinavyoshukiwa. 

 “Wizara imependekeza kwa Mheshimiwa Rais aanzishe mchakato wa uanzishaji wa Ofisi ya Mchunguzi Mkuu wa Vifo kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya Wachunguzi wa Kitaifa ya mwaka 2017 ili kuchunguza vifo vikiwemo vilivyotokana na polisi, Ofisi ya Mchunguzi Mkuu pia itahakikisha uwajibikaji na uwazi katika visa vya vifo vinavyoshukiwa," ilisoma taarifa hiyo kwa sehemu.

Ni onyo gani ilitolewa kwa polisi? Wizara hiyo pia iliwataka polisi kujizuia wanapokabiliana na waandamanaji kote nchini, ikisisitiza kujitolea kwake kuheshimu utakatifu wa maisha ya binadamu. 

Hata hivyo, polisi wamepewa mwanga wa kijani wa kutumia nguvu zinazofaa wakati vitendo vya uhalifu vinaposhinda maandamano ya amani. 

 “Polisi wanaweza kulazimika kutumia nguvu ya kuridhisha pale wanapojitenga na matukio mahususi ya maandamano yanapofikia vitendo vya uhalifu, vikiwemo fujo, uporaji, uchomaji wa mali, uvunjifu wa magari,” ilisema wizara hiyo. 

Maafisa wa polisi pia wamepewa notisi kwamba kukamatwa kunategemea Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ambayo inaeleza jinsi ukamataji hutekelezwa na kuwekwa kizuizini na kufikishwa mahakamani kwa washukiwa. 

Serikali ilitoa wito kwa wafanyabiashara na wamiliki wa majengo binafsi wanaolinda mali zao kuwasiliana na mamlaka ili kusimamia usalama kwa utaratibu 

WASHUKIWA WAWILI ZAIDI WAKAMATWA HUKU MSHUKIWA MKUU AKIZUILIWA KWA SIKU 30

Collins Khalusha alizuiliwa kwa siku 30 kutokana na mauaji ya Kware. 

Nairobi - Maafisa wa upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wamewatia mbaroni washukiwa wawili zaidi wanaohusishwa na mauaji ya kinyama katika eneo la Kware, mtaa wa mabanda wa Mukuru kwa Njenga jijini Nairobi. 

Kwa nini Amos Momanyi Mogusu alikamatwa? Mnamo Jumapili, Julai 14, miili kadhaa iliyokatwakatwa ilipatikana katika eneo la kutupa taka na umma. Katika taarifa, DCI ilifichua kukamatwa kwa Amos Momanyi Mogusu, ambaye alinaswa katika eneo la City Cabanas. 

Kulingana na maafisa hao wa upelelezi, Momanyi alipatikana akiwa na simu ya mmoja wa waathiriwa, Roselyn Akoth Ogongo, ambaye mabaki yake yalitambuliwa na jamaa zake katika Makafani ya Nairobi. 

Ni vitu gani vya waathiriwa wa mauaji ya Kware vilipatikana? Baada ya kuhojiwa, Momanyi aliongoza maafisa wa upelelezi kwa mshukiwa wa tatu aliyejulikana kwa jina la Moses Ogembo ambaye anasemekana alimuuzia simu hiyo ya rununu. 

Katika nyumba ya Ogembo, wapelelezi walipata simu 154 za mitumba, na alikiri kuwa alinunua simu zilizotumika kutoka kwa mshukiwa mkuu, Collins Khalusha. "Baada ya kukamatwa kwa Amos Momanyl Mogusu katika mtaa wa Cabanas na kupatikana kwa simu ya rununu jana, aliongoza wapelelezi hadi kwa nyumba ya Ogembo iliyoko Mukuru kwa Reuben, ambaye alipatikana na jumla ya simu 154 zilizotumika zimefichwa nyumbani kwake," DCI ilisema. 

Wakati huo huo, makachero hao walipewa siku 30 kuendelea kumzuilia Khalusha ili kukamilisha uchunguzi wa madai ya mauaji hayo. 

Je, Collins Khalusha alilazimishwa kukiri makosa ya mauaji ya Kware? Huku hayo yakijiri, Khalusha, mshukiwa wa mauaji ya takriban wanawake 42 na kuwatupa kwenye machimbo eneo la Kware, aliwashutumu polisi kwa ukatili. 

Kupitia kwa wakili wake, John Maina Ndegwa, Khalusha alidai aliteswa hadi kukiri mauaji hayo. Akiwa amefikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Irene Gichobi katika Mahakama ya Makadara, Ndegwa aliomba mahakama imruhusu kutafuta matibabu, akiongeza kuwa madai dhidi yake ni ya kuchekesha. 

UWT KIBAHA MJI YAZIDI KUCHANJA MBUGA KUHAMASISHA WANAWAKE KUSHIRIKI UCHAGUZI


NA VICTOR MASANGU,KIBAHA 


Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya ya Kibaha mjini Elina Mgonja amewataka wanawake kuachana na tabia ya kukaa vijiweni na badala yake wanapaswa kubadilika na kujiunga na vikundi vya ujasiriamali ili kuweza kujikwamua kiuchumi.

Elina ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanawake wa UWT Kata ya picha ya ndege wakati wa mwendelezo wa  ziara yake ya kikazi ya kuweza kujionea uhai wa chama pamoja na kuwahimiza kujitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi za uongozi.

Mwenyekiti huyo alibainisha kwamba wanawake wanatakiwa kujituma kwa bidii katika kufanya kazi mbali mbali ambazo zitaweza kuwasaidia kuondokana na wimbi la umasikini na kuondokana na kuwa tegemezi.


"Wanawake mnapaswa kuwa wajasiri katika kushiriki katika kazi mbali mbali ikiwa ni pamoja na kujiunga katika vikundi mbali mbali vya ujasiriamali ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuondokana na kuwa tegemezi,"alisema Mgonga.

Pia aliwataka wanawake kuhakikisha wanatengeneza mahusiano mazuri na viongozi mbali mbali wa chama cha mapinduzi na viongozi wa serikali katika shughuli mbali mbali za utekelezaji wa maendeleo.

Aidha aliwahimiza wanawake kuwa mstari wa mbele katika kumuunga mkono Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

Kadhalika Elina alisema kwamba wanawaje wa UWT wanatakiwa kuwa na umoja na mshikamano hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa lengo ikiwa ni kushinda katika mitaa yote.

Kwa upande wake Katibu wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini  Cesilia Ndalu amesema wanawake wanatakiwa kuwa na ushirikiano na upendo kwa lengo la kuweza kukijenga na kukiimarisha chama cha mapinduzi.

Ziara ya Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini ina lengo la kutembelea wanawawake wa UWT katika kata mbali mbali ili kuona uhai wa chama sambamba na kuhimiza wanawake kujitokeza kuchukua fomu za kuwania uongozi.

Tuesday, July 16, 2024

UWT KIBAHA MJI YAWAHIMIZA WANAWAKE KATA YA TUMBI NA SOFU KUJITOSA NAFASI ZA UONGOZI

 


NA VICTOR MASANGU, KIBAHA

Jumuiya  ya umoja wa wanawake  (UWT) Wilaya  ya Kibaha mjini imewahimiza wakinamama  kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi  kuchukua fomu bila ya uwoga wowote  kwa ajili ya kugombea nafasi mbali mbali za uongozi  hasusan katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa  ambao unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa UWT Elina Mgonja wakati wa ziara yake ya kikazi  katika Kata ya tumbi na Sofu yenye lengo la kuweza kuangalia uhai wa chama pamoja na kuwahimiza wanawake kushiriki  kikamilifu katika nafasi mbalimbali za uongozi.




Mwenyekiti huyo aliongeza kwamba lengo lake kubwa la  kufanya ziara hiyo ni kuwatembelea wanawake katika kata zote 14 za Jimbo la Kibaha mjini ikiwa sambamba na kuangalia mwenendo mzima wa zoezi la uandikishaji wa wanachama kujisajili  kwa mfumo wa kisasa  kwa njia  ya  kieletroniki.

"Kwa kweli nimefarijika sana nimeamua kufanya ziara yangu ya kikazi ya kutembelea  kata mbali mbali ambazo zipo katika Jimbo la Kibaha mjini na lengo lake kubwa ni kuweza kuangalia uhai wa chama jinsi ulivyo ikiwa sambamba na kuona namna ya zoezi zima la wanachama kujiandikisha kwa njia ya Kieletroniki,"alisema Mgonja.

Kadhalika aliwaomba wanawake wa Kata ya Tumbi  pamoja na kata ya Sofu kuendelea kumpa ushirikiano wa kutosha Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwa sambaamba na kumuheshimisha katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kupiga kura kwa wingi ili kushinda kwa kishindo kikubwa na kuchukua mitaa yote bila kupoteza.

Kwa uapnde wake  Diwani wa viti maalumu Selina Wilson amewahimiza wakinamama kutorudi nyuma katika kugombea katika nafasi mbali mbali ikiwa sambamba na kuchukua fomu  kwa ajili ya kuwania nafasi mbali mbali za uongoz ikiwa sambamba na kuchangamkia fursa za mikopo zilizopo ambazo zitawasaidia katika kujikwamua kiuchumi.

Naye Diwani wa viti maalumu Shufaa Bashili amewataka wakina mama pindi wanapopata mikopo kuhakikisha kwamba wanaifanyia kazi pamoja na kuirejesha ikiwa sambamba na kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Diwani wa viti maalumu wa Kibaha mjini Lidya Mgaya alisema kwamba wanawake wanapaswa wasiogope na kwamba wataendelea kumuunga mkono Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan katika masuala mbali mbali ya kimaendeleo.

 Mwenyekiti wa UWT Wilaya yaKibaha mjini amefanya ziara yake ya kikazi  katika kata mbili za Tumbi pamoja na kata ya Sofu ambapo ameambatana na baadhi ya madiwani wa viti maalumu pamoja na  wajumbe wa  kamati ya utekelezaji sambamba na viongozi wa chama cha mapinduzi CCM. 




Monday, July 15, 2024

MAONI UCHAGUZI MKUU RWANDA

 NA FLORENCIA PETER/ KIGALI/RWANDA

Baada ya Uchaguzi kufanyika Nchini Rwanda je Wananchi niyapi Matarajio yao ? Kama anavyoeleza Bi Nshimimana Tatu Mkaazi wa Wilaya ya Nyamilambo Mkoa wa Nyarugenge Mjini Kigali Nchini Rwanda alipokutana na Mic ya Jembe Fm #rwandaupdate #rwandatoday #uchaguzimkuu_rwanda

UWT KIBAHA MJI YAFANYA KWELI YATEMBELEA MATAWI 14 KUHIMIZA ZOEZI LA KUJISAJILI

 


NA VICTOR MASANGU,KIBAHA 


Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Wilaya ya Kibaha mjini (UWT) Elina Mgonja  katika kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa amefanya ziara ya kikazi na kufanikiwa  kuyatembelea jumla ya  matawi 14  kwa lengo la kuweza  kujionea hali halisi ya uandikishaji kwa njia ya kieletroniki.

Ziara hiyo ambayo imefanyika katika kata mbili za Tangini na Maili moja pia ilikuwa na lengo la kuwahimiza wanawake kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Akizungumza katika ziara hiyo ya kikazi Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja amesema kwamba ameamua kufanya ziara hiyo akiwa na wajumbe wa kamati ya utekelezaji ili kujionea mwenendo mzima wa zoezi la uandikishaji wa wanachama wa CCM  kwa njia ya kieletroniki.


Pia Mgonja alibainisha kwamba wamebaini kuwepo kwa mwamko mkubwa kwa wanawake kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo la kujisajili kwa njia ya kisasa kwa ajili ya kuweza kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unatarajjwa kufanyika mwaka huu.

"Mimi kama Mwenyekiti nimeambatana na wajumbe wa kamati ya UWT na tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutembelea matawi 14 ambayo yapo katika kata ya Tangini pamoja na kata ya maili moja na tumekuta idadi kubwa ya wanawake wamejisajili kwa mfumo wa kieletroniki,"alisema Mgonja.


Mgonja amesema kwamba lengo ni kuhakikisha wanakuwa na wanachama wengi wa CCM ambao wamesajiliwa kwa njia ya kisasa pamoja na kujiandikisha katika daktari la wapiga kura lengo ikiwa ni kufanya vizuri na kushinda kwa kishindo katika uchaguzi wa serikali za mitaa. 


Kadhalika Mgonja amewahimiza makundi mbali mbali ya wakinamama,vijana,wazee pamoja na wanachama wote kujiandikisha katika daftari la kupiga kura pamoja na kuboresha taarifa zao ili waweze kupata fursa ya kushiriki katika uchaguzi huo.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amempongeza kwa dhati Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suhuhu Hassan kwa kuweza kutoa fedha kwa ajiili ya utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo  ikiwemo katika  sekta ya afya.maji,elimu,pamoja na miundombinu ya barabara. 


Mgonja amemshukuru kwa dhati Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka pamoja na mke wake Mama Selina Koka  kwa kuweza kushirikiana kwa hali na mali katika kuwasaidia wanawake katika suala zima la kuleta maendeleo chanya katika nyanja mbali mbali.

Kwa upande wake Katibu wa UWT Kibaha mjini Cecilia Ndaru amewahimiza wanachama kuweka misingi mizuri ya kupendana na kuwa na umoja hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguguzi wa serikali za mitaa.

 Katika ziara hiyo ya UWT Mwenyekiti huyo ameambatana na viongozi mbali mbali wa chama cha mapinduzi  wakiwemo baadhi ya madiwani wa kuchaguliwa pamoja na wale madiwani wengine wa viti maalumu sambamba na viongozi wengine wa UWT.