ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, February 28, 2026

WAZIRI MKUU ASHIRIKI MAZISHI YA KARDINALI PENGO, DAR ES SALAAM

 


Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Februari 28, 2026 ameshiriki mazishi ya Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, yaliyofanyika katika Kanisa la Hija ya Bikira Maria – Pugu, jijini Dar es Salaam.


Mazishi hayo yameongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi na kuhudhuriwa na viongozi wengine wa Serikali pamoja na viongozi wa dini mbalimbali.


VIDEO:- VIJANA 336 WAHITIMU VETA MWANZA, WANAOUZA VITENDEA KAZI WAONYWA.

 NA ALBERT G.SENGO/MWANZA

Jumla ya vijana 336 kutoka Wilaya za Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza wamehitimu mafunzo ya stadi za maisha na ufundi stadi katika fani mbalimbali, na kukabidhiwa vifaa vya kuanzia kazi ili kuwawezesha kujiajiri na kujikwamua kiuchumi. Vijana hao wamehitimu Februari 27, 2026 katika VETA Mwanza, ambapo wamekabidhiwa vyeti baada ya kupatiwa mafunzo ya uselemala, uashi, uchomeleaji, ufundi bomba, aluminium, umeme wa magari na majumbani, ufundi magari na upishi. Aidha, walipata elimu ya stadi za maisha, biashara, fedha, ujasiriamali, usawa wa kijinsia pamoja na teknolojia na TEHAMA. Wahitimu hao ni sehemu ya vijana 400 walioandikishwa katika awamu ya pili ya mradi wa Vijana Elimu, Malezi na Ajira (VEMA) unaotekelezwa na Plan International mkoani Mwanza, kwa lengo la kuwawezesha vijana kutoka familia zisizojiweza kupata ujuzi wa kujiajiri au kuajiriwa. Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiri Mkalipa, amewataka vijana hao kuendeleza ujuzi walioupata na kuvitunza vifaa walivyokabidhiwa. Ameonya kuwa yeyote atakayebainika kuuza vifaa hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.

NAMUNGO YATOA SARE 1-1 NA SINGIDA BLACK STARS RUANGWA

 

Mshambuliaji Mkenya, Elvis Baranga Rupia akishangilia baada ya kuifungia Singida Black Stars bao la kuongoza

TIMU ya Namungo FC imetoa sare ya kufungana bao 1-1 na Singida Black Stars katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.

Mkenya, Elvis Baranga Rupia alianza kuifungia Singida Black Stars dakika ya 58 kwa penalti, kabla ya mshambuliaji mwenzake, Mkongo - Fabrice Ngoy wa Ngoy kuisawazishia Namungo FC dakika ya 90’+1.

Kwa matokeo hayo, Namungo FC inafikisha pointi 21 katika mchezo wa 16 na kupanda kwa nafasi mbili hadi ya sita, wakati Singida Black Stars inafikisha pointi 16 katika mchezo wa 10 na kupanda kwa nafasi mbili pia hadi ya 10.

Friday, February 27, 2026

VIJANA 336 WAHITIMU VETA MWANZA.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiri Mkalipa
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiri Mkalipa

Jumla ya vijana 336 kutoka Wilaya za Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza wamehitimu mafunzo ya stadi za maisha na ufundi stadi katika fani mbalimbali, na kukabidhiwa vifaa vya kuanzia kazi ili kuwawezesha kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.

Vijana hao wamehitimu leo Februari 27, 2026 katika VETA Mwanza, ambapo wamekabidhiwa vyeti baada ya kupatiwa mafunzo ya uselemala, uashi, uchomeleaji, ufundi bomba, aluminium, umeme wa magari na majumbani, ufundi magari na upishi. Aidha, walipata elimu ya stadi za maisha, biashara, fedha, ujasiriamali, usawa wa kijinsia pamoja na teknolojia na TEHAMA.

Wahitimu hao ni sehemu ya vijana 400 walioandikishwa katika awamu ya pili ya mradi wa Vijana Elimu, Malezi na Ajira (VEMA) unaotekelezwa na Plan International mkoani Mwanza, kwa lengo la kuwawezesha vijana kutoka familia zisizojiweza kupata ujuzi wa kujiajiri au kuajiriwa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiri Mkalipa, amewataka vijana hao kuendeleza ujuzi walioupata na kuvitunza vifaa walivyokabidhiwa. Ameonya kuwa yeyote atakayebainika kuuza vifaa hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.

“Huu ni mwanzo wa safari. Mmepewa elimu na vifaa vya kuanzia kazi, hatutarajii kuona mnaishia njiani. Hatutakubali kuona unauza cherehani; utakuwa hujatimiza wajibu wako,” amesema Mkalipa.

Mratibu wa mradi wa VEMA, Gadiel Kayanda, amesema shirika limetumia zaidi ya shilingi milioni 160 kulipia ada za mafunzo na kununua vifaa vya kujifunzia. Aidha, wahitimu hao wamekabidhiwa vifaa vya kuanzia kazi vyenye thamani ya shilingi milioni 69 kulingana na fani walizosoma.

Kwa mujibu wake, tayari vijana 58 kati ya walionufaika wameajiriwa, huku 30 wakijiajiri katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.

Mwakilishi wa wahitimu, Raina Revelian, mhitimu wa umeme majumbani, amesema wenzao 64 walishindwa kumaliza mafunzo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo utoro, kukosa ruhusa kutoka kwa wazazi, ujauzito, magonjwa, umbali na muda mfupi wa mafunzo.

Amesema mafunzo hayo yamewapa ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko na kuwafungua milango ya kujiajiri na kuajiriwa, akitaja siku ya mahafali kuwa ni ya kihistoria kwao.

RAIS DKT. SAMIA AKISHIRIKI MISA TAKATIFU YA KUAGA MWILI WA MWADHAMA POLYCARP KARDINALI PENGO

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisaini Kitabu cha Maombolezo kufuatia kifo cha Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo mara baada ya kuwasili katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Jijini Dar es Salaam, tarehe 27 Februari, 2026.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi mbalimbali kwenye Misa Takatifu ya kumuombea na kumuaga Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Jijini Dar es Salaam, tarehe 27 Februari, 2026.




Kengele ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph ililia kwa dakika kumi mfululizo, mara tu baada ya mwili wa Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Hayati Polycarp Kardinali Pengo, kuwasili kanisani hapo.

Na haya ni mambo machache kumuhusu;

1. Jina lake halisi ni nani? Kuna watu wanadhani Mwadhama ni jina lake? Wengine wanadhani Polycarp ni cheo chake. Jina lake ni Polycarp Pengo. Kardinali ni cheo cha Kanisa, na Mwadhama ni kivumishi cha sifa, kama ambavyo Maaskofu huitwa Mhashamu au Mbunge kuitwa Mheshimiwa.

2. Kwanini neno Kardinali lipo katikati ya majina yake na sio mwanzoni? Kwanini hakuitwa Kardinali Polycarp Pengo, akaitwa Polycarp Kardinali Pengo? Kanisa Katoliki lina utaratibu wa majina. Utaratibu huo huitwa modus titulorum ama style of titulature kwa kingereza. Kwa Makardinali wote, neno Kardinali hukaa katikati ya majina yao. Ndiyo maana Kardinali mpya anaitwa Protase Kardinali Rugambwa. Hata Papa Leo XIV kabla ya kuwa Papa aliitwa Robert Kardinali Prevost.

3. Kardinali Pengo ni miongoni mwa Maaskofu wachache kutoka Tanzania waliowekwa wakfu na Papa mwenyewe. Alipoteuliwa kuwa Askofu wa Nachingwea, aliitwa Vatican na kuwekwa wakfu na Papa John Paul II January 6, mwaka 1984 katika Basilika Kuu la Mtakatifu Petro.

4. Watu wengi wanashangaa kumbe Pengo alikuwa msomi wa kiwango cha PhD? Mbona alikuwa hajiiti Dr? Jibu ni kwamba katika Kanisa Katoliki, vyeo vya kitaaluma havipewi kipaumbele kuliko vyeo vya kiroho. Kuna doctrine ya unyenyekevu (humility) ambayo inasisitiza watawa wasijikweze kwa vyeo vya kisomi, bali wajitambulishe kwa nafasi zao za kiroho (Askofu, Kardinali, Padre etc).

Kardinali Pengo alikuwa na PhD ya Moral Theology kutoka Chuo Kikuu kinachoheshimika sana duniani cha Lateran, lakini maisha yake yote hakuwahi kujiita Dokta. Na hata pale TEC karibu Maaskofu wote ni PhD lakini huwezi kusikia wakijiita Dokta. Ni kwa sababu ya doctrine of humility.

5. Kwanini hakuzikwa kijijini kwao Mwazye, Kalambo? Ukiwa Mkleri utazikwa kwa utaratibu wa Kanisa. Mkleri ni mtu aliyepokea sakramenti ya daraja Takatifu. Hata hivyo angeweza kuzikwa Jimbo Katoliki Lindi au Tunduru-Masasi alipokuwa Askofu wa kwanza wa jimbo hilo. Lakini alishajiandalia kaburi lake kule Pugu. Na alichagua Pugu kwa sababu maisha yake ya utume yamekua zaidi Dar kuliko mahali pengine. Na pia alitamani kuzikwa pamoja na Wamisionari wa kale waliozikwa Pugu.!

Chanzo:  Malisa GJ 



KAMATI YA UONGOZI WA MRADI WA JNHPP YAKAGUA MAENDELEO YA BWAWA LA JULIUS NYERERE

 

📌Yasema mradi umesimamiwa na kutekelezwa kwa ufanisi

📌Yasisitiza ni kichocheo muhimu katika za fursa za kiuchumi na kijamii

Kamati ya Uongozi wa Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), tarehe 26 Februari 2026, imekagua maendeleo ya uzalishaji wa umeme katika mradi huo na kueleza kuridhishwa na usimamizi pamoja na utekelezaji wake, uliokidhi viwango vya ubora vinavyoendana na thamani ya fedha iliyowekezwa na Serikali.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye pia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi , amesema kamati imefurahishwa na namna bwawa hilo linavyochochea ukuaji wa uchumi kwa kuongeza uzalishaji wa umeme unaosambazwa katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayochangia kuimarika kwa upatikanaji wa nishati ya umeme.

“Tumeridhishwa na jinsi mradi huu ulivyosimamiwa na kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

 Ukilinganisha na miradi mingine barani Afrika, mradi huu umejengwa kwa ubora wa hali ya juu na umeleta unafuu katika huduma ya umeme nchini. Haya ni mafanikio makubwa kwa Taifa,” alieleza Dkt. Yonazi.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Bw. Petro Lyatuu, amesema mradi huo umekamilika  kwa asilimia 100 na mchango wake tayari umeanza kuonekana. 

Amefafanua kuwa mwaka 2021, gridi ya taifa ilikuwa na jumla ya megawati 1,600, lakini kwa sasa uwezo wa uzalishaji umefikia zaidi ya megawati 4,000, zaidi ya mara mbili ya kiwango cha awali.

“Kwa sasa bwawa linazalisha umeme na tija yake imeonekana wazi. Kuongezeka kwa uzalishaji kumeimarisha gridi ya taifa na tunaendelea kuongeza nguvu katika sekta ya nishati kwa ajili ya maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi,” alisisitiza Bw. Lyatuu.

Aidha kwa hatua nyingine Kamati hiyo ilitembelea kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze, kinachopokea umeme kutoka Bwawa la Julius Nyerere na kusambaza katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji, Mhandisi Antony Mbushi, amesema kituo hicho kimekamilika na tayari kinafanya kazi.

Ameongeza kuwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma umefikia asilimia 71.58, huku mradi wa kusafirisha umeme kutoka Chalinze kupitia Kinyerezi hadi Mkuranga umefikia asilimia 59.76.

‘’Kamati imeridhishwa na maendeleo ya miradi hiyo na kusisitiza kuwa mpango uliopo ni kuendelea kuongeza uzalishaji ili kuhakikisha nishati ya umeme inakuwa ya uhakika na endelevu’,’Aliongeza Mha. Mbushi

Katika hitimisho la ziara hiyo, Kamati imeeleza kuwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya umeme unaifanya Tanzania kuwa kivutio cha uwekezaji na kitovu cha usambazaji wa umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Thursday, February 26, 2026

AZAM FC YAILAMBA MTIBWA SUGAR 3-0

 

Presha katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara inazidi kuongezeka baada ya Azam FC kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, usiku huu ni katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Azam FC yamefungwa na kiungo Feisal Salum Abdallah dakika ya tatu tu ya mchezo na mshambuliaji mpya, Jean-Jacques Ngita Kamanga raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), aliyesajiliwa dirisha dogo kutoka Aris Limassol ya Cyprus akitupia magoli mawili dakika ya 19 na 59. 

Kwa ushindi huo, Azam FC wanafikisha pointi 22 katika mchezo wa 10 na kupanda kwa nafasi tatu hadi ya tano, wakati Mtibwa Sugar inabaki na pointi zake 21 za mechi 16 nafasi ya nne. 

CCM YATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA ASKOFU MKUU RUWA’ICHI KUFUATIA KIFO CHA KADINALI PENGO

 

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa salamu za rambirambi kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddeus Ruwa’ichi OFMCap, kufuatia kifo cha Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo hilo, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo, aliyefariki dunia Februari 19, 2026, katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alipokuwa akipatiwa matibabu.


Akizungumza Februari 26, 2026 baada ya kusaini kitabu cha maombolezo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam, Katibu Mkuu CCM, Dkt. Asha-Rose Migiro, alisema amewasilisha salamu za rambirambi kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Migiro alisema marehemu Kadinali Pengo atakumbukwa kama mchungaji wa faraja na tumaini, kiongozi wa kiroho mwenye hekima, unyenyekevu na msimamo thabiti wa maadili.

Alijipambanua si tu kwa huduma ya Kanisa, bali pia kwa mchango wake katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa, maadili ya jamii, malezi ya vijana na uwajibikaji wa viongozi.


“Kadinali Pengo ameacha alama inayodumu ya utumishi wa Mungu, utumishi wa Taifa na utumishi wa jamii. Maisha na mafundisho yake yataendelea kuwa dira kwa vizazi vijavyo,” alisema Dkt. Migiro.

CCM imesema inaliombea Kanisa Katoliki na waumini wote wapate faraja katika kipindi hiki cha maombolezo na Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.

Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi, mwili wa marehemu utawasili Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Februari 27, 2026 kwa ajili ya waumini kutoa heshima zao za mwisho, na Ibada ya Misa ya Mazishi itafanyika Februari 28, 2026 katika Kituo cha Hija Pugu, Dar es Salaam.



MBOZI WAFANYA UCHAGUZI MWINGINE BAADA YA DIWANI ALIYEKUWEPO KUJIUWA.

 


ZOEZI la upigaji kura katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Shiwinga, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, linaendelea leo Februari 26, 2026, huku wananchi wakijitokeza kwa wingi.

Uchaguzi huo umeitishwa kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Lusekelo Mwalukomo, kilichotokea Novemba 26, 2025, baada ya kunywa maji ya betri, zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo.

Kwa mujibu wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi katika kata hiyo, Selestin Luambano, jumla ya wapiga kura 6,854 wanatarajiwa kushiriki zoezi hilo katika vituo 19 vilivyotengwa kwa ajili ya kupigia kura.

Amesema jumla ya vyama nane vya siasa vimesimamisha wagombea kuwania nafasi hiyo.

Wagombea hao ni Menati Mzumbwe (CCM), Matias Dulle (ADC), Elly Shitindi (ADA-TADEA), Mary Daud (UPDP), Neema Abadallah (UMD), Emily Siwale (SAU), Mussa Dulle (Chama-Makin) na Cosam Mwakyusa (TLP).

BARABARA MLIMA KITONGA KUPANULIWA NA KUWA NJIA NNE

news

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema serikali iko katika hatua za mwisho za kuanza upanuzi wa barabara inayopita Mlima Kitonga mkoani Iringa ambayo sasa itakuwa ya njia nne na yenye taa za barabarani.

Amesema hatua hiyo ni uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan ili kupunguza foleni na kuboresha usalama wa watumiaji wa barabara katika njia hiyo inayotumiwa na magari mengi. 

Akizungumza jana baada ya kutembelea eneo hilo, Waziri Ulega, alisema barabara hiyo ni ya kimkakati kwa uchumi wa nchi kwa sababu inatumiwa pia na magari yanayokwenda katika nchi zinazotumia bandari ya Dar wa Salaam kubeba mizigo yao. 

Akitoa picha ya ongezeko la uhitaji wa upanuzi wa barabara hiyo, Waziri Ulega alisema idadi ya magari yanayopita katika Barabara Kuu ya TANZAM imeongezeka kutoka magari 1,700 hadi 3,400 kwa siku, hali inayosababisha njia hiyo kuzidiwa.

Waziri wa Ujenzi Abdala Ulega akizungumzia upanuzi wa barabara Mlima Kitonga.

“Nimepokea mapendekezo kutoka kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Iringa ya kuhakikisha tunaondoa msongamano wa magari katika Mlima Kitonga, na nimeelekeza kwa wataalamu wetu kupanua hii barabara kwa kilometa saba. Kwa sasa hivi barabara ina njia mbili kwa hiyo tutatanua na kuwa njia nne,” alisema Ulega.

Waziri Ulega aliongeza kuwa ni maelekezo ya Rais Samia kwamba kila mradi wa barabara uende sambamba na uwekaji wa taa za barabarani ili kuhakikisha usalama wa watumiaji ikiwemo wananchi, wafanyabiashara na madereva pamoja na kuweka kingo pembezoni mwa barabara ili kuzuia magari yasianguke kwenye makorongo.

“Ninaagiza manunuzi yaanze mara moja ili kuhakikisha kwamba barabara hii inatanuliwa kwani ina umuhimu mkubwa katika uchumi wa nchi hivyo hatuwezi kuiacha katika hali hii na kutimiza pia maelekezo ya rais kutatua changamoto zote,” alisema Ulega. 

Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Ritha Kabati, alisema barabara hiyo ni ya uchumi wa kimataifa hivyo ikitengenezwa itainua zaidi uchumi wa Mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla pamoja na kuwasaidia wananchi ambao hupata changamoto ya kufuata huduma za kijamii ikiwemo matibabu Iringa mjini. 

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa Eng. Yudas Msangi alisema gharama ya upanuzi wa kilometa saba kwa njia mbili katika barabara hiyo ni bilioni 59.2 na ukarabati wa njia mbili zilizopo ni bilioni 16.2.

Wednesday, February 25, 2026

SIMBA YAKWAA KISIKI DODOMA

 


TIMU ya Simba SC imetoa sare ya bila kufungana na wenyeji, Dodoma Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Kwa matokeo hayo, Simba SC inafikisha pointi 23 katika mchezo wa 10 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya tatu, wakati Dodoma Jiji FC inafikisha pointi 21 katika mchezo wa 16, ingawa inabaki nafasi ya sita. 

YANGA YATUMA SALAMU KWA 'KUIGAGADUA' JKT GOLI TANO MTUNGI

 


MABINGWA watetezi, Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

Mabao ya Yanga SC yamefungwa na beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ dakika ya saba, mshambuliaji Muangola Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Depu’ dakika ya 60, kiungo Mudathir Yahya Abbas dakika ya 63, mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Mpumelelo Dube dakika ya 84 na kiungo Shekhan Ibrahim Khamis dakika ya 89.

Kwa ushindi huo, Yanga wanafikisha pointi 28 katika mchezo wa 10 na kupanda kileleni ikiizidi tu wastani wa mabao JKT Tanzania, ambayo pia imecheza mechi saba zaidi. 

Mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo Dube ndiye Mchezaji Bora wa Mechi leo

STAMICO, PLANTCOR WASAINI UBIA UTAFITI NA UCHIMBAJI MADINI BUKOMBE

 NA ALBERT G.SENGO/BUKOMBE/GEITA

Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imeingia makubaliano ya ushirikiano na kampuni ya uchimbaji madini ya Plantcor ya Afrika Kusini kwa lengo la kufanya utafiti na baadaye uchimbaji wa madini katika Pori na Hifadhi ya Msitu wa Kigosi, wilayani Bukombe mkoani Geita. Makubaliano hayo yamesainiwa Jumanne, Februari 24, 2026 katika Ukumbi wa CCM Bukombe, hafla iliyohudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini, Steven Kiruswa kama mgeni rasmi. Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kiruswa amesisitiza umuhimu wa mwekezaji kuhakikisha kuwa zoezi la utafiti, litakalotumia teknolojia ya kisasa ya ndege nyuki (drones) kabla ya kuanza rasmi uchimbaji wa dhahabu, linafanyika kwa uwazi na kwa kutoa taarifa sahihi kwa wananchi ili waweze kushirikishwa na kunufaika na matokeo ya utafiti huo. Aidha, amemtaka mwekezaji huyo kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya eneo husika, hususan barabara, kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ili kurahisisha upatikanaji wa maeneo ya uchimbaji kwa wachimbaji wadogo. Ameeleza kuwa hali ya miundombinu ilivyo sasa hairidhishi na inahitaji maboresho ya haraka. Mradi huo unatarajiwa kuwa chachu ya uchumi katika wilaya hiyo kupitia kodi za mirabaha, uboreshaji wa miundombinu na huduma za kijamii kwa wananchi pamoja na ajira za muda mfupi na mrefu zipatazo 2,000.