|
RAIS wa Association of Local Government Engineers Tanzania (ALGETA) nchini, Mhandisi Ezekiel Kunyaranyara (Katikati) akizungumza leo na waandishi wa Habari (hapapo pichani), kuhusu kufanyika mkutano wao wa mwaka utakaofanyika kesho jijini Mwanza, kushoto ni Makamu wa Rais wa ALGETA, Mhandisi Gerald Matindi na kushoto ni Katibu Mkuu wa Jumuia hiyo, Mhandisi Lusekelo Mwakyami. |
NA PETER FABIAN,
GSENGO BLOG/MWANZA.
WAHANDISI 350 wa Halmashauri kutoka Mikoa 25 nchini wanachama wa Association of Local Government Engineers Tanzania (ALGETA) wanakutana kesho jijini Mwanza kwa siku mbili kujadili utoaji bora wa huduma kwa jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Mwanza, Rais wa ALGETA nchini, Mhandisi Ezekiel Kunyaranyara alisema kuwa mkutano huo wa mwaka wa wahandisi wanachama pia utajadili utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri zao za sekta ya maji, barabara na majengo.
Mhandisi Kunyaranyara alisema kuwa pia mkutano huo utajadili mfumo wa watumishi wa taaluma ya Uhandisi wa serikali wa Mitaa ili kuona kama lengo la kuwa na wahandisi wanne kila Halmashauri limefikiwa katika Idara ya Uhandisi ikiwemo wasaidizi katika Idara za maji, barabara na majengo.
“Mkutano huu utawashirikisha pia wajumbe wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Bodi ya Usajili ya Wakandarasi na Bodi ya Wasanifu na Wakadiriaji wa Majengo ili kuwezesha kujadili na kusaidia miradi ya inayotekelezwa kwenye Halmashauri kutoharibika kwa muda mfupi baada ya kukamilika kwake pamoja na kuangalia mafanikio ya miaka 8 toka kuanzishwa kwake rasmi mwaka 2007,”alisema.
Rais, Kunyaranyara alieleza kuwa katika mkutano huo wajumbe watapata fursa ya kujadili kwa kina na kushauri juu ya utekelezaji wa miradi ya maji, majengo ikiwemo ujenzi wa Vyumba vya maabara, utumiaji wa mitambo ya umeme na vifaa vya kudrufu, kusaidia wanafunzi wa kike wa sekondari kusoma masomo ya Sayansi kusaidia vitabu.
“Kupitia mkutano huu utatoa msaada wa madawati 100 kwa shule moja ya Msingi zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, kutembelea ujenzi wa miradi ya barabara za mawe za halmashauri ya Jiji la Mwanza na mgeni rasmi atakayefungua mkutano wetu wa mwaka ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Faizal Issa,”alisema.
Naye Makamu wa Rais wa ALGETA, Mhandisi Gerald Matindi, alisema mkutano huo utahudhuliwa na Wahandisi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Wilaya, Sekretarieti za Mikoa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambapo pia utekelezaji wa rasilimali watu na fedha zinavyofanikiwa.
“Mkutano huu utaishauri serikali kuhusu taratibu za manunuzi ya umma ambao umekuwa na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuchelewa kukamilika kwa wakati kutokana na sheria na taratibu za manunuzi ya umma kuwa katika Idara nyingine badala ya kuwa Uhandisi,”alisisitiza.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ALGETA, Mhandisi Lusekelo Mwakyami, alisema kuwa mkutano huo utatoa mapendekezo kwa serikali ili kuanzisha mchakato wa ujenzi wa maabara za Kanda za Uhandisi kama ilivyo kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROAD) ili kuwezesha kufanyia vipimo sampuli na malighafi za ujenzi wa miradi ili kuwa na ubora na iweze kudumu kwa muda mrefu baada.
ametoa wito kwa wanachama wote kuhudhulia mkutano huo ambao umelenga kuboresha utoaji huduma na utekelezaji bora utakaoendana na thamani ya fedha katika miradi hiyo kwenye Halmashauri zao na kuhusisha wajumbe wa ERB na CRB kutawezesha kudhibiti kwa wenye fedha kufanya ujenzi wa majengo kwa kufuata taratibu na sheria ili kutoharibu sifa ya wahandisi.