ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, December 29, 2021

ALIYEJENGA KABURI BARABARANI APEWA SIKU 45 KULIONDOA.

 


Baraza la Ardhi la Kata ya King’ori wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, limemtaka mkazi wa kijiji cha King’ori, John Peter Nanyaro anayedaiwa kujenga kaburi katikati ya barabara kuliondoa ndani ya siku 45.


Baraza hilo limefikia hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa eneo hilo alilojenga kaburi si mali yake, bali alivamia eneo la barabara ya umma inayotumiwa pia na wananchi wengine tangu mwaka 1991.


Malalamiko hayo waliwasilishwa na Amani Urio na baraza kusikiliza mashahidi na baadaye kutembelea eneo lenye mgogoro na kujiridhisha kuwa Nanyaro amekiuka sheria.


Uamuzi huo ulisomwa na Mwenyekiti wa baraza hilo,Gabriel Nderingo Ayo akiwa na wajumbe ambao ni Efrahim Akyoo,Grace Nnko, Eliamani Nassari, Rosemary Mbise na Katibu wa baraza hilo, Charles Mbise.


Baada ya kupokea ushahidi na vielelezo na kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, baraza limethibitisha kuwa eneo hilo lilikuwa limetolewa kwa Wilfred Urio ambaye ni wa mzazi wa Amani kwa kufuata taratibu zote za kisheria.


Ayo alieleza kuwa kabla ya uamuzi baraza lilitoa fursa ya mlalamikiwa na mlalamikaji kulimaliza shauri hilo kwa mazungumzo, lakini ilishindikana kupatikana muafaka na kila upande kutakiwa kuleta mashahidi.


Baraza lilitaka kila upande kupeleka mashahidi na mlalamikaji alikuwa na mashahidi sita akiwemo mwenyekiti wa kijiji, Elipokea Samson Nanyaro na muhtasari wa kutolewa eneo hilo na vikao vya ukoo ulikabidhiwa kama ushahidi.


Kwa upande wake, mlalamikiwa Nanyaro alipeleka mashahidi watano. Hata hivyo, wanne wote walikiri kulikuwepo na barabara katika eneo lenye mgogoro.


“Baada ya kupokea ushahidi, baraza limetoa uamuzi kuwa eneo lenye mgogoro ni mali ya mlakamikaji na hivyo mlalamikiwa anapaswa kuondoa kuta za kaburi alilojeng. Pia kutombugudhi na wengine kutumia barabara hiyo,” alisema.


Alisema baraza hilo limempa siku 45 kukata rufaa iwapo hakubaliani na uamuzi huo.


“Baraza pia limejiridhisha sehemu iliyojengwa msingi hakuna kaburi na kwa kuzingatia hata maamuzi ya familia waliotembelea eneo hilo na kujirisha kuwa hakuna mtu aliyezikwa katika kaburi hilo,” alisema mwenyekiti huyo.