ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Saturday, June 17, 2017

SIKU YA MTOTO WA AFRICA JIJINI MWANZA.

Na Zephania Mandia tarehe 16.06.2017
Jamii imetakiwa kujifunza kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ili kuhakikisha haki za watoto zinalindwa. 


Wito huo umetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishana wa Polisi Ahmed Msangi katika maadhimisho ya mtoto wa afrika mkoani Mwz.


Kutengana kwa wanandoa na ukatili dhidi ya watoto kunatajwa kuwa chanzo kikubwa cha watoto kutoroka majumbani na hatimaye kushia mitaani na wengine kuathirika kisaikolojia na hivyo kusababisha kushuka kwa taaluma.


Watoto wanaokulia mtaani wanatajwa kuwa wathirika wakubwa wa vitendo vya kikatili ikiwemo ubakaji na ulawiti. Mwenyekiti wa madereva kanda ya ziwa DEDE PETRO ni miongoni mwa watu waliokulia katika mazingira ya mtaani.


Jeshi la polisi limewataka wananchi kutumia madawati ya jinsia yaliyopo  kwenye vituo vya polisi kukomesha vitendo vya kikatili dhidi ya watoto.


Utumikishaji watoto, Mimba za utotoni,ubakaji na ulawiti kwa watoto imeelezwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili jamii kutokana na  kutotoa ushirikiano kwa jeshi la polisi na wananchi.

MAKAMU WA RAIS SAMIA AONGOZA MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA DAR.

 Watoto wakikimbia walipokuwa wakiandamana kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Kinyerezi, ambapo yalifanyika kimkoa wilayani Ilala, Dar es Salaam leo.Maadhimisho hayo yaliongozwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan. PICHA NA RICHARD MWAIKENDA;KAMANDA WA MATUKIO BLOG
 Maandamano yalielekea kwenye viwanja hivyo
 Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akiwashukuru na kuwapatia vyeti wauguzi wa kujitolea  walioshiriki kampeni kupima magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa watoto na vijana  wakati wa T
 WATOTO WAKIPIMWA UREFU
 Maandamano
 Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akiwasalimia watoto pacha Brighton na Bright Shirima alipokuwa akikagua mabanda ya tiba kwenye Tamasha la Uelimishaji na Upimaji Afya na Kinga dhidi ya Magonjwa yasiyoambukiza kwa watoto na vijana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika
 Kikundi cha hamasa cha Ilala kikihamasisha wakati wa maadhimisho hayo
 Brass Band ya Polisi ikiongoza maandamano 
 Makamu wa Rais Samia akisalimiana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangala
 Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema akihutubia 

 Kikundi cha ngoma cha Shule ya Msingi Umoja kikitumbuiza kwa ngoma ya kibati wakati wa maadhimisho hayo

 Kikundi cha Umoja kikitumbuiza kwa ngoma ya Makhirikhiri


 Makamu wa Rais, Samia akimkabidhi cheti cha shukrani DkNg'wege aliyekuwa mmoja wa madaktari walioshiriki kupma afya za watoto na vijana wakati wa maadhimisho hayo
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akihutubia katika maadhimisho hayo.Kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Dk. Kigangwala na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kote nchi kuwafichua watu wanaonyanyasa na kudhalilisha watoto kijinsia ili waweze kukamatwa na kuchukua hatua za kisheria kama hatua ya kukomesha vitendo hivyo ambayo vimeanza kushamiri katika baadhi ya jamii nchini.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo katika hotuba yake ya kuhitimisha kampeni ya kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo ilitoa huduma bure za vipimo na matibabu kwa watoto na vijana zaidi ya 1500 kampeni ambayo iliambatana na maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika katika viwanja vya Shule ya msingi Kinyerezi mkoani Dar es Salaam.

Makamu wa Rais amesema kuwa watenda maovu hao lazima vifichuliwe na wananchi, walezi pamoja na wazazi kwa kuwa watu wanaofanya vitendo hivyo vya udhalilishaji wa watoto wapo miongoni mwa jamii.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Makamu wa Rais ameviagiza vyombo vya dola kutofumbua macho vitendo hivyo bali pindi wanapopata taarifa za matukio ya udhalilishaji wa watoto wachukue hatua za haraka za kuwakamata na kuwachukulia hatua stahiki watu wanaofanya vitendo hivyo vibaya.

Makamu wa Rais pia ametoa wito maalum kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kote nchini waache kuwaficha watu wanaotendea vitendo hivyo vibaya bali wawapatie taarifa walimu wao na polisi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Amesema kwa kufanya hivyo watoto watakuwa salama katika mazingira ya nyumbani na wakiwa mashuleni kwani watu wabaya wanaofanya vitendo hivyo watawajibishwa kulingana na matendo maovu waliyokuwa wanawafanyia watoto hao.

“Mtoto anaweza kufaidika na fursa sawa iwapo tu atalindwa kwa kuwezeshwa kuwa afya bora”, Amesisitiza Makamu wa Rais.

Kuhusu kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza yameendelea kuua watu kwa kasi katika nchi zinazoendelea Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania.

Amesema ipo haja ya kuimarisha juhudi za kukabiliana na tatizo hilo kwa ushirikiano wa wadau wote kwani janga hilo linagharimu taifa na wananchi wake wakiwemo watu wazima, watoto na vijana.

“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yasipodhibitiwa yatapunguza uzalishaji mali,ufanisi mahali pa kazi na hata shughuli za ulinzi na usalama nchini mwetu na hivyo pato la taifa litapungua na taifa kuwa watu maskini kutokana na magonjwa hayo”, Alifafanua Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kuwa katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza Serikali imeweza kupanua maeneo ya kutolea huduma kwa wagonjwa wa saratani nchini kwa kujenga jengo jipya katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kuongeza majengo mapya ya huduma za saratani kwenye Hospitali za Rufaa ya kanda ya Bugando mkoani Mwanza.

Amesema Serikali pia imejenga Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambayo ni taasisi ya mfano ya kutibu maradhi ya moyo ambapo kutokana na kujengwa kwa taasisi hiyo Serikali imefanikiwa kuokoa mabilioni ya fedha ambayo yangetumika kuwagharamia wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Hamisi Kingwangala amemhakikishia Makamu wa Raia kuwa Wizara hiyo itaendelea kuweka mipango na mikakati imara ya kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini.

Dkt Kingwangala ameomba wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za kidini na wadau wengine kushirikiana na Wizara ya Afya katika kuongeza kasi ya kukabiliana na magonjwa hayo ili yasiendelee kuteketeza maisha ya watu nchini

Friday, June 16, 2017

VITA MPYA YA SIASA YAIBUKA, SAKATA LA MAKINIKIA KAMPUNI YA ACACIA YAIANGUKIA SERIKALI, MASTAA SIMBA NA YANGA WATEMWA STARS.


Vita mpya ya kisiasa yaibuka, sakata la Makinikia Kampuni ya Acacia yaiangukia serikali, Mastaa Simba na Yanga watema Stars. Habarika na dondoo hizi za magazeti ya leo hapa.

JANJA JANJA SOKO LA MIGOMBANI SENGEREMA

Wafanyabiashara  wa vitunguu katika soko la Migombani katika halmashauri ya Sengerema  mkoani Mwanza , wamelalamikia kuwepo kwa watu kujitokeza na kuwatishia  kuwafukuza katika maeneo waliopewa kufanyia biashara wakidai kuwa maeneo hayo yamepangwa kaajili ya shughuli nyingine, huku watu hao wakijichukulia mali na fedha kwa baadhi ya wafanyabiashara hao ili kuwabakiza sokoni hapo.

Jembe Fm imekuwa mkombozi kwa kulifukunyua hilo kwa kuliweka hadharani ambapo sanjari na kuzungumza na wafanyabiashara wa soko hilo pia imefanikiwa kuongea na wenyekiti wa soko. YAPI YAMEJIRI TUJIUNGE NA MWAKILISHI WETU OSCAR MWANA WA KAHUKA LIVE TOKA SENGEREMA... (SAUTI KUWAJIA HIVI PUNDE)

Thursday, June 15, 2017

KOCHA WA CHELSEA KUONDOKA?

Hakika msimu uliopita ulikuwa bora sana kwake kwani aliifanya Chelsea kucheza vizuri sana na katika msimu wake wa kwanza tu na klabu hiyo ya Uingereza kocha huyo alifanikiwa kutwaa kikombe cha ligi ya Epl.

Baada ya ligi kuisha mambo yanaonekana sio mazuri kwake kwani watu wake wa karibu wamekuwa wakidai Antonio Conte hana furaha Uingereza haswa kutokana na vyombo vya habari vinavyomuandika kocha huyo.

Wiki za karibuni kocha huyo amekuwa akiandikwa sana katika vichwa vya habari vya magazeti na mitandao mbalimbali baada ya kuibuka tuhuma za kumtumia Diego Costa ujumbe mfupi kwenye simu akimuambia hamtaki.

Inafahamika kwamba tangu Conte akiwa nchini Italia anapenda maisha ya kutotokea sana katika vyombo vya habari lakini hali inayotokea Uingereza inamsumbua sana kichwa na imekuwa ikimkosesha raha.

Roman Abromovich.

Lakini pia taarifa zinadai mmiliki wa klabu ya Chelsea Roman Abromovich umekuwa tatizo sasa na ndio sababu hadi sasa Chelsea hawajasajili kwani tajiri pesa aliyotoa ya usajili ni ndogo kuweza kununua wachezaji wakubwa.

Antonio Conte ana ndoto za kubeba kombe kubwa la Champions League lakini tayari ameona bajeti ndogo ya usajili aliyopewa inaweza kuwa kikwazo kwake kuchukua kombe hilo na hii imemfanya kukosa raha.

Ripoti zinasema Conte sasa amechukia zaidi kwani amekuwa akiahidiwa tu kuhusu kununua wachezaji lakini pesa hapewi na sasa anataka kuonana moja kwa moja na Roman Abromovich au Marina Granovaskia ambae ni kati ya wafanya waamuzi wakuu wa Chelsea.

Conte pia anakosa raha kutokana na kukosa control ya academy ya soka ya Chelsea na mambo yote hayo yanamfanya kuanza kuwaza kuondoka lakini bado kuna nafasi kubwa ya kubaki kwani Roman anafuatilia kwa karibu kutaka kununua majina makubwa ikiwemo Lukaku na Morata.

aaaaWARSHA YA KARIKACHA & VIBONZO YAMALIZIKA, YAFUNGWA NA BALOZI ARTHUR MATTLI


Photo 1

Balozi na Mwakilishi wa Uswisi Afrika Mashariki, Arthur Mattli, akimkabidhi cheti cha ushiriki wa “Warsha ya Uchoraji Karikacha & Vibonzo,” Saidi Michael maarufu kama “Wakudata” hivi karibuni baada ya kushiriki mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoendeshwa na asasi ya Nathan Mpangala Foundation (NMF) na kufadhiliwa na Ubalozi wa Uswisi nchini. Katikati ni Mwenyekiti wa NMF, Nathan Mpangala.

Photo 2
Mchora vibonzo Musa Ngarango aka “Masikio Mchongoko”, akilamba ganda lake.
  
Photo 3
Mchora vibonzo chipukizi, Brenda Kibakaya alidhihirisha kuwa uchoraji vibonzo si kwa wanaume tu.

Photo 4
Magret Liwembe akimkabidhi zawadi mgeni rasmi (karikacha cha mke wa balozi iliyonakshiwa kwa saini za washiriki) kwa niaba ya washiriki wenzake.

Photo 5
Mchora vibonzo Simon Regis akitoa neno la shukrani kabla ya kukabidhiwa vyeti.

Photo 6
Baadhi ya karikacha zilizochorwa wakati wa mafunzo hayo.

Photo 7
Mwezeshaji na mwenyekiti wa NMF akiwa na washiriki wakati wa mafunzo hayo kabla ya mgeni rasmi kuwasili. Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wachora vibonzo wa “kizazi cha tatu,” yalijikiti katika misingi ya uchoraji karikacha na katuni za maoni.

Photo 8
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.

AJIBU ATUA RASMI YANGA.

YANGA imempa mkataba wa miaka miwili mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu wenye thamani ya Sh50 milioni na gari lakini Simba wao wamesema kwamba hawakuwa na mpango naye na tayari Kamati ya Usajili ilikata jina lake.

Ajibu ni miongoni mwa wachezaji wa Simba ambao wamemaliza mikataba ndani ya klabu hiyo ingawa mkataba wake unamalizika ramsi mwezi ujao lakini watani zao Yanga tayari wamembana na mkataba mpya.

Yanga walianza mazungumzo na Ajibu kabla hata ya kumalizika kwa msimu wa ligi ambao umewapa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo huku Simba nao wakitafuta mbinu za kumwongeza mkataba mpya lakini mchezaji huyo alikuwa akiwasumbua kila walipohitaji kukutana ili kufanya mazungumzo upya.

Habari za uhakika ni kwamba Ajibu amemalizana na Yanga mchana wa leo Alhamisi, na tangu Jumatatu ya wiki hii alikuwa akikutana na viongozi wa Yanga ili kuweka mambo sawa na leo wamekamilisha dili hilo.

Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema kuwa Ajibu hawatakuwa naye tena  na wanafahamu kwamba watani zao Yanga wanamuhitaji hivyo Kamati ya Usajili iliamua kuondoa jina lake kwenye mipango ya msimu ujao.

IRAN YAFUZU FAINALI KUCHEZA KOMBE LA DUNIA 2018 RUSSIA.

Timu ya soka ya taifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa timu ya pili kujikatia tiketi ya michuano ya kombe la dunia hapo mwakani huko nchini Russia baada ya kuigaragaza timu ya Uzbekstan mbao 2 kwa nunge.

Mabao kutoka kwa Sardar Azmoun na Mehdi Taremi yalihakikisha Iran, ambayo mkufunzi wake ni Carlos Queiroz, itarejea tena kucheza Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfululizo ikiwa ni mara ya kwanza kupata mafanikio hayo.

Ushindi wao uliwawezesha kufungua mwanya wa alama nane kati yao na wapinzani wao, ambao wamo nafasi ya tatu kwenye jedwali.
 
Wachezaji wa timu ya soka ya taifa ya Iran wakishangilia baada ya mechi.
 Mabingwa mara tano Brazil walikuwa taifa la kwanza kujiunga na wenyeji Urusi katika kufuzu kwa michuano hiyo ya mwaka ujao nchini Russia.

Timu mbili za kwanza katika kila kundi, kati ya makundi mawili ya kufuzu katika bara Asia zitafuzu, nazo timu zitakazomaliza nafasi ya tatu kila kundi zikutane katika mechi ya muondoano ya kufuzu.

MAGAIDI WA AL SHAHBAB WAUA WATU 17 MOGADISHU.

Magaidi wa kundi la Al Shabab nchini Somalia wamewaua watu 17 katika hoteli moja katika mji mkuu Mogadishu.

Maafisa wa usalama wanasema magaidi waligongesha gari lilokuwa limesheheni mabomu katika hoteli ya kifahari ya Posh jana Jumatano na kisha kuvamia mgahawa wa Pizza House pembizoni mwa hoteli hiyo.

Taarifa zinasema magaidi hao walikuwa wamechukua mateka watu 10 katika mgahawa huo kabla ya kuokolewa na maafisa wa usalama.

Aidha maafisa wa usalama wamesema magaidi wawili wameuawa na hadi kufikia Alhamisi asubuhi duru zilikuwa zinadokeza kuwa baadhi ya magaidi bado walikuwa wamejificha ndani ya jengo hilo. Magaidi hao walikuwa wamevalia sare za kijeshi wakati wa hujuma hiyo.
 
Kati ya waliouawa ni raia mmoja wa Syria huku wafanyakazi Wahindi, Waethiopia na Wakenya wakiokolewa baada ya kutekwa nyara na magaidi.
 
Umoja wa Afrika umetuma kikosi chake katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Kikosi hicho cha AMISOM kina wanajeshi kutoka Uganda, Kenya, Burundi na Ethiopia. Askari zaidi ya 22 elfu wanaunda kikosi hicho cha AU kwa ajili ya kupambana na kundi la al Shabab huko Somalia.

Ingawa kundi la al Shabab limefurushwa katika miji yote mikubwa na maeneo muhimu ya Somalia, lakini bado lina wanamgambo wake katika baadhi ya vijiji na miji na hufanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia na maafisa wa Serikali.

MBUNGE ATAKA MAWAZIRI WAFANYIWE ‘INTERVIEW’ KABLA YA KUTEULIWA.

Dodoma. Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Msukuma, ametaka mawaziri kufanyiwa usahili kabla ya  kuteuliwa kushika  nafasi hizo kutokana na baadhi yao kuwa na elimu ya juu, lakini wanashindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Akichangia katika hotuba ya Bajeti Kuu leo Alhamisi bungeni mjini hapa, Msukuma amesema walioaminiwa na kupewa nafasi hizo wamekuwa wakitajwa kwenye kashfa kubwa.

"Wengine wamegushi vyeti, tukiangalia wana madigrii huenda wengine wana uwezo mdogo wanazidiwa na makaratasi makubwa,"amesema.

UTAFITI WA TAASISI YA TWAWEZA ULIOTOKA LEO NINI MAONI YAKO.

Dar es Salaam. Utafiti mpya uliofanywa na Taasisi ya Twaweza umebaini kuwa kukubalika kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumeporomoka kutoka asilimia 32 mwaka 2013 hadi asilimia 17 mwaka huu.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza leo Alhamisi, katika utafiti wake uitwao ‘Matarajio na matokeo; Vipaumbele, utendaji na siasa nchini Tanzania.’

Utafiti umebaini kuwa Chadema kinakubalika zaidi miongoni mwa vijana, wanaume, watu matajiri na wenye kiwango kikubwa cha elimu.

Kadhalika utafiti huo ulibaini kuwa CCM imeendelea kuimarika kwa kukubalika kwa kati ya asilimia 54 na 64 kati ya mwaka 2012 na 2017.

“Mwaka 2013 na 2014 kiwango cha kukubalika kilishuka na kilifikia asilimia 54 kutoka asilimia 65 ya 2012. Kukubalika kwa CCM kumeendelea kubaki katika kiwango hicho hicho cha asilimia 62 tangu uchaguzi wa mwaka 2015 na asilimia 63 mwaka 2017,” umesema utafiti huo.

Utafiti huo ulibaini, CCM inakubalika zaidi miongoni mwa wazee (asilimia 80), ukilinganisha na asilimia 55 ya vijana. Wanawake (asilimia 68) wanaikubali CCM kuliko wanaume (asilimia 58), maeneo ya vijijini (asilimia 66) kuliko maeneo ya mijini (asilimia 57), na wananchi masikini (asilimia 69) kuliko matajiri (asilimia 53).

Wananchi wenye elimu ya sekondari, elimu ya ufundi au elimu ya juu wanaikubali CCM kwa asilimia 46.


NINI MAONI YAKO KWA UTAFITI HUU?

MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA YATUMIA TEHAMA KUBORESHA UTOAJI HUDUMA KWA UMMA.


Serikali Mtandao inarahisisha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa umma.  
Usikose kuangalia kipindi hiki cha Seikali Mtandao katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) uone jinsi wanavyotumia mifumo mbalimbali ya TEHAMA katika kazi zao za kila siku.

WATAALAMU WASISITIZA MAZINGIRA SAFI, LISHE BORA

 Mratibu wa kampeni ya kitaifa Bw. Anyitike Mwakitalima akizungumza wakati wa mkutano kujadili uhusiano kati ya usafi wa mazingira na lishe bora kwa watoto jijini Dar es Salaam juzi.
 Dkt Generose Mulokozi (kulia) kutoka shirika la IMA World Health akisema ‘Nipo Tayari’ kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira kwa lengo la kuzuia magonjwa ya kuhara kama vile kipindupindu yanayogharimu maisha ya Watanzania.
Mtaalamu wa lishe wa Unicef Mauro Brero akitoa ishara ya kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira yenye kauli mbiu ya Nipo Tayari ikiwa na lengo la kuzuia magonjwa ya kuhara kama vile kipindupindu yanayogharimu maisha ya Watanzania.


Washirika wa maendeleo nchini wamekutana jijini Dar es Salaam leo kujadili, pamoja na mambo mengine, umuhimu wa usafi wa mazingira katika lishe bora kwa watoto na kuunga mkono kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira yenye kauli mbiu ya “Nipo Tayari”.

Kampeni hiyo inayoratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Njisia, Wazee na Watoto imejikita katika kuhamasisha watu, mijini na vijijini, kujenga utamaduni wa kuwa na vyoo na kuvitumia kikamilifu na kunawa mikono na sabuni mara baada ya kutoka chooni.

“Bila kuzingatia usafi wa mazingira, lishe bora kwa mtoto inaweza kuathiriwa na magonjwa ya kuhara kama vile kipindupindu, hivyo kuondoa virutubisho vyote mwilini. Ndio maana usafi wa mazingira na lishe bora kwa watoto ni vitu vinavyotakiwa kwenda pamoja”, anasema Dkt Generose Mulokozi kutoka shirika la IMA World Health.

Akizungumza katika mkutano huo, Mratibu wa kampeni hiyo ya kitaifa Bw. Anyitike Mwakitalima alisema: “Mazingira machafu na ukosefu wa vyoo umethibitika kuwa chanzo kikubwa kinachosababisha kudumaa kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano. Takwimu zinaonyesha kwamba asilimia 34 ya watoto wa umri huo nchini wamedumaa kutokana na kuishi katika mazingira yasiyokuwa na vyoo na kutozingatia kanuni za afya.

Alisema kuwa ukosefu wa lise bora pia hupunguza kinga ya mwili kwa watoto hivyo kuugua mara kwa mara na kuwafanya kushindwa kukua vizuri kimwili na kiakili.

Utafiti wa afya uliofanywa nchini Tanzania 2015-16 umeonyesha mafanikio ambapo namba ya watoto waliodumaa imepungua hadi asilimia 34 ikilinganishwa na mwaka 1992 wakati nusu ya watoto walikuwa wamedumaa.

Utafiti mwingine uliofanyika nchini hivi karibuni umeonyesha kuwa madhara ya udumavu kwa watoto hauishii utotoni bali huwa na matokeo hasi kwa watu wazima na kuathiri kipato chao kwa asilimia 20. Hii inarudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Inatarajiwa kuwa asilima 75 ya Watanzania watakuwa wanaishi katika mazingira safi ifikapo mwaka 2025 na asilimia 100 mwaka 2030. Mafanikio hayo makumbwa yatafikiwa ikiwa serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na washirika wa kimaendeleo wa kimataifa kufanikisha mpango huo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau wa maendeleo kutoka Action against Hunger, Aga Khan Foundation-Tanzania, Catholic Relief Services, Child Investment Fund Foundation, Department for International Development, Doctors with Africa CUAMM, Embassy of Switzerland, Feed the Children na Global Affairs Canada.

Wengine ni Global Alliance for Improved Nutrition, Ifakara Health Institute, IMA World Health, Institute of International Programs Johns Hopkins University, and International Fund for Agricultural Development, International Potato Center, United Nation Children Fund, UN World Food Program, United States Agency for International Development, World Bank, World Health Organization na World Vision International.

TURKISH AIRLINES YAANDAA IFTAR KWA WATEJA WAKE DAR ES SALAAM

Mkurugenzi wa Shirika la ndege la Turkish Airlines nchini Tanzania, Ahmet Sahin, akiwakaribisha wageni waliohudhuria Iftar iliyoandaliwa kwa ajili ya wageni na wadau mbalimbali iliyofanyika jana katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wageni waalikwa wakipakua na kupata chakula cha futari iliyoandaliwa na shirika la ndege la Turkish Airlines. Wageni na wadau mbali mbali wakipata Iftar iliyoandaliwa na Shirika la ndege la Turkish Airlines nchini Tanzania iliyofanyika jana katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Wageni waalikwa wakibadirishana mawazo katika hafla hiyo.  Baadhi ya wageni waalikwa wakiongea na Mkurugenzi wa Shirika la ndege la Turkish Airlines Tanzania, Ahmet Sahin.

Wednesday, June 14, 2017

KIRANJA WA BUNGE LA MAREKANI APIGWA RISASI.

Kiranja wa walio wengi katika Bunge la Congress nchini Marekani Steve Scalise, amepigwa risasi na kujeruhiwa alipokuwa akihudhuria mazoezi ya mchezo wa baseball miongoni mwa wabunge.

Yamkini watu wawili wamejeruhiwa, katika kile mashuhuda wanasema kuwa kisa cha umiminunaji wa risasi katika jimbo la Virginia mapema leo Jumatano.

Seneta wa Republican, Rand Paul, anasema kuwa alisikia mlio wa risasi ya kwanza, kisha ikafuatiwa na milio ya risasi.

Walinda usalama walijibu mashambulio hayo.

Bwana Scalise ambaye ni mwanachama wa chama cha Republican, anasemekana alipigwa risasi kwenye makalio, huku ikisemekana kuwa afya yake haimo hatarini kwani amefikishwa hospitalini kwa matibabu pamoja na walinzi wake ambao pia walijeruhiwa na mshambuliaji.

Idara ya Polisi huko Virginia, inasema kuwa imemtia mbaroni mshambuliaji.

Rais Donald Trump amesema kuwa: "Tumetamaushwa mno na janga hilo."

Katibu wa mawasiliano wa Ikulu ya White House , Sean Spicerameandika katika mtandao wa kijamii wa tweeter kuwa Rais Donald Trump anajulishwa kuhusiana na shambulio hilo.

JEMBE FM YAPOKEA UGENI TOKA BARAZA LA HABARI TANZANIA.


Kutoka kwa Mkuu wa vipindi @jembefm Timetheo Ngalula @mbabavc "Leo ni Furaha kubwa kwa Kituo Chetu cha @jembefm kimepokea Ugeni kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT)na Ulikuwa ni ujio wa Katibu mkuu wa Baraza hilo Mr Kajubi Mukajanga, Amepata fursa ya kutembelea ofisi zetu pia amesema anaridhishwa na utendaji wa Kituo Chetu, Vijana wetu na namna tunavyoendelea kuwa kituo bora nchini na kuwa tishio kwa Vituo vingine, Pia amempongeza C. E. O wa #JembeMediaGroup Dr Sebastian Ndege @jembenijembe kwa Uwekezaji alioufanya namna anavyotoa ajira kwa vijana na kwatengenezea mazingira mazuri ya Kazi vijana.

 "Shukrani sana kwenu MCT hakika hatutawaangusha, @jembenijembe @mbabavc @gsengo

#VyumaVimekaza #Amshaaa


BARRICK YAMUAHIDI JPM KUJENGA MTAMBO WA KUCHENJUA DHAHABU.

Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick ya Canada Profesa John L. Thorton Ikulu jijini Dar es salaam. 

Katika mkutano huo, uliohudhuriwa pia na Waziri wa Sheria na Katiba Profesa Paramagamba Kabudi na Balozi wa Canada hapa nchini, Ian Myles umemalizika kwa mafanikio makubwa ambapo pande zote zimekubaliana kukaa meza moja kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali katika sekta ya madini.

Kwa upande wake Rais Magufuli amesema Serikali inakaribisha mazungumzo hayo na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano na kampuni ya Barrick Gold Corporation ili kufikia makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa na namna kampuni hiyo itakavyoendesha shughuli zake nchini maslahi ya pande zote mbili.

Mazungumzo kati ya wawili hao yalihudhuriwa na Balozi wa Canada nchini Tanzania Ian Myles na Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba Kabudi.
 
Rais Magufuli amesema pamoja na kukubali kulipa fedha zinazodaiwa Prof. Thornton amekubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu nchini humo.
 

 

Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick ya Canada Profesa John L. Thorton akiongea Ikulu jijini Dar es salaam baada ya mkutano wake na Rais Dkt John Magufuli. Katika mkutano huo, uliohudhuriwa pia na Waziri wa Sheria na Katiba Profesa Paramagamba Kabudi na Balozi wa Canada hapa nchini, Ian Myles

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold ya Canada, Profesa John Thornton amesema atashirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu hapa nchini (smelter).
 
Profesa Thornton amesema hayo hii leo (Jumatano) Ikulu  alipokutana na Rais John Magufuli kwa ajili ya kujadiliana kuhusu sakata la mchanga wa madini.

Pia, Profesa Thornton amesema kampuni yake ipo tayari kufanya mazungumzo na Tanzania yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili na pia ipo tayari kulipa fedha zote ambazo inapaswa kulipa kwa Tanzania.


UWT YAUNGA MKONO UAMUZI YA RAIS KUHUSU MAKANIKIA NA MIKATABA YA MADINI.

UWT YAUNGA MKONO UAMUZI YA RAIS KUHUSU MAKANIKIA NA MIKATABA YA MADINI.
Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) inaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt John Pombe Magufuli na kupongeza jitihada zake za kupambana na aina zote za ubadhirifu, dhulma na unyonyaji uliobainika kwenye mikataba ya uchimbaji na usafirishaji madini, na hivyo kuhakikisha maliasili za Taifa zinatumika kwa manufaa ya watanzania wote.

Pia, Umoja wa Wanawake Tanzania unatoa pongezi kwa wajumbe wa Kamati kwa weledi, uzalendo na ujasiri mkubwa wa kubainisha hasara kubwa iliyopatikana kwa Taifa letu kutokana na usafirishaji wa makanikia, na hivyo UWT inakubaliana na kuunga mkono mapendekezo yote ya Kamati na uamuzi wa Mheshimiwa Rais Dkt John Pombe Magufuli wa kutaka kurekebisha mikataba na sheria za usimamizi na uchimbaji wa madini nchini.

Aidha UWT inapongeza hatua za awali za mazungumzo yaliyofanywa leo tarehe 14/06/2017 baina ya Mhe Rais Dkt Magufuli na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambao ni wamiliki wa Kampuni ya Acacia Mining Limited Prof. John L. Thornton na kukubaliana kuhusu malipo ya fedha zilizopotea na kushirikiana katika ujenzi wa mtambo wa kuchenjulia dhahabu (smelter) hapa nchini.

Kufanikiwa kwa mazungumzo hayo, na marekebisho ya sheria na mikataba ya madini kutawezesha Watanzania kupiga hatua ya kujikomboa na umasikini, hususani Wanawake ambao wameendelea kukosa huduma za msingi za kijamii ikiwemo afya, elimu, maji na malazi bora. Wanawake wengi wanahangaika kwa kukosa mitaji ya biashara na mikopo ya wajasiriamali wadogo huku wakisumbuliwa kulipa tozo, ushuru na kodi za kero.

UWT inatoa rai kwa wananchi wote kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kujivunia utanzania wetu. Tunamuombea Mhe Magufuli, MwenyeziMungu azidi kumpa afya njema, moyo wa ujasiri, uzalendo na upendo kwa watanzania.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

AMINA MAKILAGI (MB)
KATIBU MKUU
JUMUIYA YA UMOJA WA WANAWAKE TANZANIA.
14/06/2017